Serikali inachochea migogoro ya kidini

Gurtu

JF-Expert Member
May 15, 2010
1,237
1,500
Nileongea na padri mmoja huko Sumbawanga kuhusu suala la waamini waliotengwa. Alinieleza kosa lililofanywa na waamini hao lilikuwa kushabikia suala la Utatu Mtakatifu kutumika katika kufananisha na nafasi za uongozi zilizogombewa katika uchaguzi wa Oktoba 31 mwaka huu. Kuhusu dadi ya waliotengwa, kadiri ya maelezo yake idadi ya waliotengwa haifikii hata watu 15 na katika waliotengwa au wanakusudia kutengwa hakuna Padre yeyote ambaye yupo katika kundi hilo.

Jambo la ajabu ni jinsi gazeti la serikali lilivyokuwa likiripoti habari hizo na tena kwa mtindo wa kichochezi. sijui habari hii ina maslahi gani na kwanini gazeti la serikali ndiyo inaandika habari hii kwa mtindo huu. moja ya hatari iliyo katika habari hii ni kule kuhusisha kutengwa kwa waumini hao na suala la kushabikia CCM badala ya kuhusisha suala hilo na ukweli kuwa waumini hao kwenda kinyume na mafundisho ya imania yao.
Soma habarileo ya leo

Imeandikwa na Peti Siyame, Sumbawanga; Tarehe: 11th December 2010

UPEPO sasa unaelekea kuwageukia baadhi ya mapadri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Sumbawanga ambao nao wanadaiwa kuwa ‘wasaliti' kwa kukaidi maagizo ya kanisa hilo kwa kushindwa kuwaadhibu waumini wanaodaiwa kuisaliti imani yao katika Uchaguzi Mkuu wa Octoba mwaka huu.

Uamuzi huo utakuwa mwendelezo wa adhabu za kanisa, baada ya wiki iliyopita gazeti hili kuripoti juu ya kutengwa na kanisa hilo waumini ambao ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zaidi ya 400 kutokana na ushabiki wa waziwazi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka huu.

Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka ndani ya kanisa hilo, Jumapili hii, Kanisa Katoliki Parokia ya Familia Takatifu linakusudia kuyatangaza majina ya waumini 20 zaidi wa Parokia hiyo ambao wameisaliti imani yao na hivyo watapewa adhabu ya kutengwa na Kanisa hilo hadi hapo watakapotubu.

Taarifa zaidi iliyopatikana kutoka ndani ya Kanisa hilo inaeleza kuwa kwa sasa wameorodhesha majina ya baadhi ya mapadri wa kanisa hilo jimboni hapa ambao
wanashutumiwa kukaidi maagizo ya Kanisa hilo ambapo mapadri wote walikubaliana kuwatambua na kuwaadhibu kwa kuwasimamisha, kuwatenga na kuwafukuza waumini wote wanaodaiwa kuisaliti imani ya Kanisa wakati wa kampeni na hatimaye uchaguzi wa mwaka
huu.

Inadaiwa kuwa, katika orodha ya majina ya mapadri hao ‘wasaliti' wapo ambao wataonywa na kuendelea na uongozi wa kiroho, lakini pia wapo ambao wataadhibiwa kwa kutengwa hadi hapo watakapokuwa tayari kutubu.

Majina hayo yatatangazwa hadharani hivi karibuni.

Uchunguzi uliofanywa na HABARILEO Jumapili umebainisha kuwa Mhashamu Baba Askofu Damian Kyaruzi Jimbo la Sumbawanga, amebariki hatua nzima ya kufukuzwa kwa waumini wanaodaiwa kuisaliti imani yao kuhudhuria Ibada za Misa Takatifu na kufungiwa Sakramenti zote kwa kile anachodai kuyathamini maamuzi ya wengi hata hivyo hayuko tayari kulizungumzia jambo hili hadharani.

Mwandishi wa habari hizi, licha ya kuomba miadi kwa takribani wiki nzima na baadaye kukubaliwa, siku ya miadi (juzi) alishindwa kuonana na kiongozi huyo wa kiroho jimboni humo ili kuzungumzia suala hili, ikidaiwa kuwa ana orodha ndefu ya watu anaopaswa kuonana nao ambapo wengi wao walikuwa ni mapadri wake.

Mgongano huo wa kiimani unaolihusisha Kanisa hilo na baadhi ya waumini wao ambao wengi wao ni wana CCM ambao wanakadiriwa kuwa zaidi ya 400, umechochewa na kile Kanisa hilo kinachoeleza kauli za kufuru dhidi ya Utatu Mtakatifu pale ambapo Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini, Aeish Hilaly wa CCM katika moja ya mikutano yake ya kugombea nafasi hiyo anadaiwa kuikufuru imani ya Kanisa hilo kwa kujifananisha na Yesu Kristo mwana wa Mungu katika dhana zima ya mafiga matatu.

Mgongano huo wa kiimani ulioanza wakati wa mchakato wa uchaguzi wa kura za maoni za CCM na kuendelea baada ya hapo, ndipo kwa mara ya kwanza baadhi ya makatekista kadhaa walipovuliwa na Kanisa nyadhifa zao hizo wakituhumiwa kuishabikia CCM hususani mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM ambaye ni Muislamu.

Mmoja wa makatekista hao akizungumza kwa njia ya simu na kujitambulisha kwa jina la Deusdeus Mwakalunde ambaye alikuwa katekista wa Parokia ya Familia Takatifu lililopo Isesa alikiri kuvuliwa wadhifa wake huo akishutumiwa kuisaliti imani yake kwa
kuishabikia CCM wakati wa uchaguzi mkuu mwaka huu .

"Nasema hivi ni kweli mimi ni mmoja wa makatekista wa Kanisa Katoliki Jimbo la Sumbawanga tuliovuliwa nyadhifa zetu hizo tuko wengi idadi kamili siikumbuki kwa sasa hata hivyo kwa sasa kanisa hilo halina tena mpango wa kuturudisha …. Kwanza mie ni Katibu wa CCM Kata ya Mollo imekuwa ni vigumu kwangu, " alisema.

Kwa mujibu wa katekista huyo ‘msaliti' waumini wa Parokia hiyo kupitia katekista wao ambaye jina lake limehifadhiwa wameshataarifiwa kuwa waumini wa parokia hiyo ambao ni wana CCM wapatao 20 majina yao yatatangazwa kwenye Misa Takatifu ya Jumapili (leo) kuwa watengwe na kufukuzwa kwa usaliti.

Hali ikiwa tete hivyo, baadhi ya waumini waliohojiwa na gazeti hili baadhi yao wameunga mkono kuadhibiwa kwa baadhi ya mapadri "wasaliti' hao wakidai kuwa nao pia wanastahili adhabu kama walizopewa baadhi ya waumini wenzao ambapo baadhi yao wanalilaumu Kanisa hilo kuwaadhibu waumini wenzao bila hata kuwapatia fursa ya kujitetea kwenye Mahakama ya Kanisa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei wa Kanisa Kuu mjini hapa, Kanoni Kanyengele alilieleza gazeti hili kuwa kama kweli kuna mapadri waliosaliti imani basi wanastahili adhabu na wanapaswa kutubu.

" Sheria ni Msumeno haibagui wadhifa wa muumini au kiongozi wa kiroho, " alisisitiza. Lakini baadhi ya waumini waliotengwa na Kanisa wanadai kuwa waliwasiliana na Mbunge Aeshy Hilaly na kumweleza masahibu yaliyowapata kwa kumshabikia na kwamba walitaka awasaidie kumaliza dhahama hii.

"Ndipo alipotueleza kuwa kama tumetengwa, basi tutafute kiwanja mjini hapa na akatuahidi kuwa atatujengea kanisa kwenye kiwanja hicho," alisema mmoja wao.

Hata hivyo mwanasiasa huyo alitakiwa na gazeti hili aeleze kama kiwanja hicho kimepatikana alikana kuwa hajawahi kukutana na wana CCM hao waliotengwa na kusema. "Hizi ni mbinu za kunichafua kisiasa siwezi kutoa ahadi kama hiyo. "

Hata hivyo kabla ya hapo akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana alikana kuikufuru imani ya Kanisa Katoliki kwa kujifananisha na Yesu Kristo Mwana wa Mungu.

"Nilichowaeleza wapiga kura wangu ni dhana nzima ya mafiga matatu … labda ulimi
uliniponza ila nilisema kuwa hata Serikali ya Mungu mbinguni inaongozwa kwa mfumo wa mafiga matatu basi nikaishia hapo kwa kuwa CCM ilikuwa inaamini kuhusu mafiga matatu kuwa lazima achaguliwe rais, mbunge na diwani kutoka CCM na si vinginevyo."

Mbunge huyo alisema kutokana na sakata hilo sasa yuko tayari kuonana na Baba Askofu Kyaruzi wa Jimbo la Sumbawanga na Uongozi wa juu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) ili kueleza ukweli wa suala hilo.

"Niliwasisitizia wapiga kura wangu ambao wengi wao ni Wakatoliki ambao ni asilimia 95 ya wapiga kura wote jimboni umuhimu wa mafiga matatu ambapo nilisema kuwa hata Serikali yaMungu mbinguni inaongozwa kwa misingi ya mafiga matatu... ndiyo nilivyosema, " alisisitiza.

Hata hivyo baadhi ya viongozi wa Kanisa hilo jimboni humo wamekuwa wakimtuhumu gombea huyo wa CCM kwamba alifananisha mafiga matatu na Utatu Mtakatifu kwa kumfananisha mgombea urais wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kama Mungu Baba, yeye mgombea ubunge kama Yesu Kristo mwana wa Mungu na wagombea udiwani sawa na Roho Mtakatifu.

Mbunge huyo alisema ana imani kuwa Mhashamu Baba Askofu Kyaruzi na hata Baraza la Maaskofu wamedanganywa kwamba ni wana CCM 10 waliotengwa na Kanisa wakati ukweli ni kwamba ni wengi wanazidi hata ile idadi iliyoripotiwa hivi karibuni ya wana CCM 400.

"Nimestushwa na habari iliyochapishwa hivi karibuni kwenye moja ya gazeti linalochapishwa kila siku, si HABARILEO kwamba msemaji wa Baraza hilo la Maaskofu Tanzania aliponukuliwa akisema kuwa ni wana CCM 10 tu ndio waliotengwa au kufukuzwa makanisani.

Akifafanua alisema kwamba hadi sasa wanachama wa vikundi vya burudani zaidi ya 40 ambavyo ni vya CCM , wanachama wake ambao wengi wao ni waumini wa Kanisa hilo wamesimamishwa na baadhi ya matekista nao pia wamevuliwa nyadhifa zao.

Wakati huo huo baadhi ya waumini waliotengwa wanakusudia kutubu makanisani ambapo baadhi yao bado wanashikilia misimamo yao ya kutokuwa na utayari huo wa kutubu na kufuatia hali hiyo hivi karibuni kilifanyika kikao cha ndani kilichowakutanisha waumini waliotengwa na Kanisa hilo ili kujadili mustakabali wao.

Kikao hicho kilifanyika kwenye ukumbi wa CCM Viwanja vya Sabasaba mjini hapa ambapo kilihudhuriwa na wana CCM anakadiriwa kuwa zaidi ya 40 ambao wengi wao walikuwa wamevalia fulana za chama chao.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Rukwa, Hipolitus Matete, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sumbawanga Mjini, Charles Kabanga, Katibu wa CCM Mkoa, Fratern Kiwango na Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini.

Hata hivyo kikao hicho kililazimika kusimama kwa muda pale Katibu wa CCM Mkoa, Kiwango alipobaini kuwepo kwa mwandishi wa habari hizi ukumbini humo na mara moja aliwambia wajumbe: "Naomba tutambuane wale wote ambao hawakualikwa hawastahili kuhudhuria na miongoni mwetu yupo huyu mwandishi naye atoke nje," alisisitiza.

Kauli hiyo ilileta taharuki miongoni mwa wajumbe wa kikao hicho ambao mmoja wao aliomba aoneshwe huyo mwandishi ili amtoe kwa nguvu ndipo alipojitokeza Mbunge Aeish na kutuliza tafrani hiyo pale alipofanikiwa kumtoa nje mwandishi huyo kwa ustaarabu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Daniel Ole Njoolay aliliambia gazeti hili leo ofisini kwake kwa kukiri kuwa mgogoro huu umewagawanya hata hivyo alisisitiza kuwa anaamini kuwa mgogoro huu si wa kudumu wakati ukifika utaisha wenyewe.

"Hapa ni suala la muda ni kama kimbunga muda ukifika kitatulia chenyewe lakini nasema ipo haja na waumini wenyewe wawe watiifu kwa viongozi wao wa Kanisa pale
wanapopewa maagizo ni kuyatekeleza na si vingnevyo," alisisitiza.
 

Kamakabuzi

JF-Expert Member
Dec 3, 2007
2,404
2,000
Gazeti hilo limepotosha ukweli kwa maksudi mazima:
Waliosimamishwa si kwa sababu ni wana CCM bali wale wote waliokufuru utatu mtakatifu.
Wenyewe walishabikia eti utatu mtakatifu: Mungu baba (ni Kikwete), Mungu mwana (ni mbunge) na Mungu roho mtakatifu (ni diwani).
Hakika hata wangekuwa waislamu wameelezwa eti Kikwete ndiye Mungu na Mbunge ndiye mtume SAW, hao wote ambao wangeshabikia hilo wangeshapitishiwa amri ya 'fatwa' - wangekuwa wamejificha sasa hivi maana vichwa vyao vingekuwa tunavitafuta!
Kweli tusichezee imani za watu eti, na ndiyo maana nasema siasa iwe siasa na dini iwe dini; na hapa watu tuelewe dini ikikemea maovu ya wanasiasa inakuwa inatetea waumini siyo kwamba inaingilia siasa.
Kibaya zaidi Habarileo ni gazeti la serikali!
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom