Serikali haipendi kuona wananchi wanaonewa – PINDA | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Serikali haipendi kuona wananchi wanaonewa – PINDA

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Maxence Melo, Jun 4, 2009.

 1. Maxence Melo

  Maxence Melo JF Founder Staff Member

  #1
  Jun 4, 2009
  Joined: Feb 10, 2006
  Messages: 2,606
  Likes Received: 1,705
  Trophy Points: 280
  TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

  SERIKALI HAIPENDI KUONA WANANCHI WAONEWA – PINDA

  WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka viongozi wa dini watambue kuwa kamwe Serikali haipendi kuona wananchi wake wanaonewa wala kuwa chanzo cha mgogoro ambayo wakati mwingine husababisha mauaji.

  Ametoa kauli hilo leo asubuhi (Alhamisi, Juni 4, 2009) wakati akijibu maswali yaliyoulizwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwenye ukumbi wa Mikutano wa CCT/CTC mjini Dodoma.

  Alikuwa akijibu swali la kwanza lililoulizwa na Askofu wa KKKT - Kaskazini Mashariki, Dk. Steven Munga ambaye alitaka kujua Serikali ina msimamo gani juu ya wananchi wanaonyanyaswa au kuuawa katika maeneo ya migodi au hata kuwekewa sumu katika mito wanayoitumia kwa maji ya kunywa..

  Waziri Mkuu alisema licha ya juhudi mbalimbali ambazo Serikali imekuwa ikichukua bado matendo kama hayo yamekuwa yakifanyika iwe katika makampuni, mashamba binafsi au migodini.

  Alisema suala la migodoni alilogusia Askofu munga ni nyeti kwa sababu linagusa hisia za watu wengi na ndiyo maana Rais Jakaya Kikwete aliunda Tume ya Bomani na kuitaka ifuatilie mambo mengi ambayo yamekuwa yakinung’unikiwa na wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya migodi.

  Alisema ripoti hiyo imekwishakabidhiwa Serikalini na pindi utekelezaji wa mapendekezo yake utakapoanza, utapunguza baadhi ya mambo yaliyolalamikiwa kwenye ripoti hiyo.

  Akifafanua zaidi Waziri Mkuu aliwataka wamiliki wa migodi hiyo wawe na staha na waijali jamii inayowazunguka. “Kuna haja ya Serikali kuipitia upya sekta hii kwa sababu wanaoathirika hapa ni Watanzania, tukiwaacha na kuwapuuza haya uliyoyasema ndiyo yanajitokeza,”.

  Akijibu swali la pili lililoulizwa na Dk. Mwita Akili ambaye ni Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, aliyetaka kujua ni kwa nini Serikali inaachia wananchi wanajenga katika maeneo yaliyozuiliwa halafu inakuja kuendesha bomoabomoa wakati kuna watendaji hadi katika Serikali za Mitaa, Waziri Mkuu alisema kutokujua sheria siyo utetezi wa kisheria kwani hata kama kuna watendaji hiyo siyo dhamana kwamba watu waendelee kuvunja sheria. “Hii siyo dhamana kwamba mtu aendelee kujenga ndani ya eneo la akiba ya barabara eti kwa sababu hajaambiwa na mtendaji wakati akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria…,” alisema.

  “Hata ukiangalia ujenzi holela wa nyumba, hakuna mtu anaweza kujenga mahali bila kupangiwa. Hapa Dodoma hatuwezi kuruhusu pawe na squatters hata kidogo, kabla hujajenga nenda kaulize kwenye ofisi ya mtendaji taratibu zikoje ili ujue kama eneo hilo ni halali au la,” alisema.

  Naye Askofu Jacob Mameho ole Paulo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Morogoro alitaka kujua Serikali imejifunza nini na zoezi la kuhamisha wafugaji maeneo ya Ihefu, Ifakara ya bonde la Rukwa na kwa nini Serikali haiondoi wakulima waliovamia maeneo ya wafugaji.

  Akijibu swali hilo Waziri Mkuu alisema katika kikao cha Bunge kilichopita Serikali iliamua kusitisha zoezi la kuhamisha wafugaji kwa sababu kuwepo kwa mapungufu mengi ya kiutendaji katika zoezi hilo. Alisema mkoa wa Morogoro ndiyo unaongoza kwa idadi kubwa ya watu waliokufa kutokana na zoezi hilo.

  “Baadhi ya watendaji wamekamatwa kwa rushwa, baadhi ya wafugaji wamerudishiwa mifugo yao ukiuliza sababu hupati, baadhi ya watendaji wamenunua mifugo iliyokamtwa kwa sababu ulikuwa inauzwa kwa bei chee… na haya ndiyo masuala ya maadili ya viongozi tuliyoongelea leo… kama kiongozi, huyu mtu alipaswa asiguse hata ngombe mmoja,” alisema.

  Akifafanua, Waziri Mkuu alisema bado kuna tatizo ambalo kuhusu migogoro ya wafugaji na wakulima ambalo halijachunguzwa kwa umakini. “Bado kuna tatizo ambalo hatujalijibu, nimepanga tukimaliza Bunge la Bajeti niende mikoa ya wafugaji ya Mwanza, Shinyanga, Manyara na sehemu ndogo ya mkoa wa Singida maana huko ndiko kwenye matatizo,” alisema huku akishangiliwa.

  “Kama Serikali bado hatujakaa na wafugaji na kuainisha tatizo ni nini hasa… kama tatizo ni maji, malambo, majosho au malisho nini basi dawa yake? Inabidi tuangalie mahitaji halisi na kuamua malambo na majosho mangapi yajengwe, au eneo la malisho litengwe kwa ajili ya idadi kadhaa ya mifugo, mingine iuzwe ili inayobaki itoshe kwenye eneo lilipangwa…” alisema.

  Alisema: “Inabidi yajengwe machinjio ya kutosha ili wafugaji wauze nyama kwa faida na si kwa bei ya kutupa na kuwapa hasara kama wakati wa zoezi lililopita… changamoto ziko huko na dawa si kusafirisha mifugo hadi Rukwa kwa vile umesikia kuna bonde la malisho.”

  Akitoa mfano wa mkoa wa Dodoma, Waziri Mkuu alisema kuna machinjio ya kisasa moja tu wakati wafugaji waliopo ni wengi. “Hebu jiulize ni kwa nini hali iko hivi?” Alisema kuna haja ya kupima maeneo na kuweka mifumo ya miundombinu ambayo itawapa wafugaji uhakika wa masoko.

  Alisema katika mkutano uliomalizika jana jijini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete wa kujadili mbinu za kuinua kilimo Tanzania, washiriki walikubaliana kuweka mifumo ya uwekezaji ya kusaidia wafugaji ili kuboresha sekta hii.

  Waziri Mkuu amerejea jijini Dar es Salaam leo mchana ili kuhudhuria kikao cha Kamati Kuu ya CCM.


  IMETOLEWA NA:
  OFISI YA WAZIRI MKUU,
  DAR ES SALAAM
  ALHAMISI, JUNI 4, 2009
   
 2. Oxlade-Chamberlain

  Oxlade-Chamberlain JF-Expert Member

  #2
  Jun 4, 2009
  Joined: May 26, 2009
  Messages: 7,928
  Likes Received: 103
  Trophy Points: 160
  serikali haijui kama wananchi wanaonewa kwa vile wao ndio wanawaonea wananchi.sasa hampendi kutoana tunaonewa wakati nyinyi ndio mnatuonea hajui anachozungumza waziri mkuu.
   
 3. Z

  ZeMarcopolo JF-Expert Member

  #3
  Jun 5, 2009
  Joined: May 11, 2008
  Messages: 13,590
  Likes Received: 480
  Trophy Points: 180
  You mean clueless?
   
 4. Mchaga

  Mchaga JF-Expert Member

  #4
  Jun 5, 2009
  Joined: Apr 11, 2008
  Messages: 1,371
  Likes Received: 10
  Trophy Points: 135
  hah...hah...hah...siasa bwana!
   
 5. Juma Contena

  Juma Contena JF-Expert Member

  #5
  Jun 5, 2009
  Joined: May 21, 2009
  Messages: 1,195
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 135
  majuzi juzi tu tumesoma watu 7 wapegigwa risasi kisa wazee wa kijiji wamelalamika ardhi yao isichukuliwe ni sehemu yao kuabudu. Polisi hao wakawafunga kwanza hao wazee na watu walipoandamana kutaka wazee wao waachiliwe ndipo polisi wakaanza kupiga risasi sasa unasema upendi waonewe vipi iwapo hawana uhuru hata wa ku-protest hata kwenye vijiji
   
 6. Mzizi wa Mbuyu

  Mzizi wa Mbuyu JF-Expert Member

  #6
  Jun 5, 2009
  Joined: May 15, 2009
  Messages: 5,499
  Likes Received: 1,080
  Trophy Points: 280
  Yeye angesema hivi "Mimi Mizengo Kayanza Pinda sipendi"!
  Lakini serikali hii! lini imewaonea huruma watu wake!? hii ya JK, ambayo kila kitu inachokifanya ni kwa manufaa ya wakubwa tu!?
  Hebu angalia jinsi wakulima wetu wanavyo hangaika na kilimo cha kijima, vijana wetu wanavyokosa ajira wakimaliza elimu zao nk! hakuna mkakati wowote wa kutatua tatizo hili zaidi ya mikakati ya kisanii ili waweze kutawala tena 2010-2015!
   
Loading...