Ni mwendo unaotia matumaini licha ya baadhi ya watu kubeza isijekuwa kama Manchester United.
Manchester ilishinda mechi zote za kirafiki na kuzifunga hadi timu kubwa kama Real Madrid na Liverpool, lakini haijaonja ushindi wowote katika mechi nne za mashindano ilizocheza mpaka sasa. Imefikia hata hatua ya kufungwa mabao 4-0 na timu ya Daraja la Kwanza ya MK Dons.
Wakati ukiendelea kutafakari hayo, Mwanaspoti linakuletea mambo 10 yaliyojionyesha kwenye mchezo wa Simba na Gor Mahia ambapo Simba ilishinda mabao 3-0, wafungaji wakiwa Raphael Kiongera (mawili) na Ramadhani Singano ‘Messi'.
Phiri anaiwezea Simba
Kwa wiki tatu ambazo Phiri amekuwa klabuni hapo, mabadiliko makubwa yameonekana.
Msimu uliopita ilikuwa na kikosi dhaifu kilichoshindwa hata kuifunga Ashanti United iliyoshuka daraja.
Juzi iliwakosa Pierre Kwizera, Amri Kiemba, Haruna Chanongo, Saidi Ndemla, Joram Mgeveke na Amissi Tambwe waliokwenda kwenye majukumu ya kitaifa, pia ikawakosa Jonas Mkude na Issa Rashid ' Baba Ubaya' ambao ni majeruhi, lakini ilicheza kwa kiwango cha juu.
Ilikuwa zaidi ya Simba ya wiki nne zilizopita iliyochezwa dhidi ya Zesco ya Zambia wakati huo ikiwa chini ya Mcroatia Zdravko Logarusic.
Friends usipime
Ni miezi miwili tangu Kundi la Friends of Simba lichukue madaraka katika klabu hiyo chini ya Rais Evans Aveva. Usajili wa maana uliowaongeza akina Kwizera, Raphael Kiongera, Elius Maguli na Shaban Kisiga, umeimmarisha mno timu. Licha ya wachezaji hao Simba pia imewasajili kipa Hussein Sharrif ‘Casillas' na Peter Manyika Junior, beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala' na Abdi Banda ambao pia wameonyesha uwezo wa kuvutia.
Okwi ataisaidia Simba
Kesi ya mshambuliaji mpya wa Simba, Emmanuel Okwi raia wa Uganda ilitarajiwa kusikilizwa jana Jumapili kuamua kama Okwi ni halali wa Simba ama la. Endapo mambo yatakwenda vizuri kwa Simba ni dhahiri kuwa Okwi atafanya makubwa msimu ujao. Katika mchezo wa juzi Okwi alicheza kwa kiwango cha juu licha ya ukweli kwamba hajacheza mechi ya mashindano kwa muda mrefu.