Mgombea mwenza wa urais, kupitia CCM Samia Suluhu Hassan.
Mgombea mwenza wa urais, kupitia CCM Samia Suluhu Hassan, amesema chama chake kikishinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, serikali ya Dk. John Magufuli, itanunua meli tano kubwa, ikiwamo ya shughuli za uvuvi katika ukanda wa kiuchumi wa Bahari ya Hindi.
Aidha, imeahidi kuingiza nchini meli nyingine nne za kisasa zitakazofanya kazi ya kutoa huduma ya usafiri kati ya kisiwa cha Mafia, Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Tanga.
Aliyasema hayo jana katika mkutano wake wa hadhara wa kampeni uliofanyika mjini hapa, akitokea mkoani Mtwara.
Alisema serikali ya awamu ya tano itakayoundwa na Dk. John Magufuli, imepanga kuimarisha usafiri wa Bahari ya Hindi ikiwamo Mafia, ambako itaelekeza nguvu kwa kununua boti tano kubwa za usafiri na uvuvi.
"Mafia mnastahili kuwezeshwa zaidi hasa baada ya kuonyesha juhudi zenu kwa kujenga kiwanda cha samaki lakini ilani yetu pia inasema tutanunua vyombo kwa ajili ya uvuvi ili kwenda katika ukanda wa kiuchumi wa bahari kuu na kuvua samaki wenye thamani kubwa. Mpango huu kwanza utakuza ajira na kufungua fursa nyingine," alisema.
Alisema katika awamu hiyo, Serikali ya CCM imejiwekea pia malengo ya kuanzisha uhifadhi wa bahari, katika kisiwa cha Mafia ili kutunza mazingira ya bahari na kufuga samaki wengi zaidi.
"Nawaomba wataalam watakapokuja Mafia, mtoe maoni yenu ili ijulikane maeneo ya kufanyiwa uhifadhi na yatakayoachwa huru kwa ajili ya shughuli za uvuvi," alisisitiza. Kuhusu kuwawezesha kiuchumi wakazi wa Mafia, Samia alisema Ilani ya CCM inaeleza kwamba itatenga Sh. 1,000,000 katika kila kijiji cha Mafia ili kuwawezesha wananchi wake kununua vyombo vikubwa vya uvuvi. Awali, mgombea ubunge wa jimbo la Mafia, Mbaraka Dau, alisema pamoja na mafanikio yaliyotekelezwa visiwani hapo na mbunge anayemaliza muda wake Abdulkarim Shaha, bado jimbo hilo lina changamoto kadhaa.
CHANZO: NIPASHE