Salim Ahmed Salim aliteuliwa balozi akiwa kijana mdogo wa miaka 22

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
21,898
31,969
SALIM AHMED SALIM ATEULIWA BALOZI AKIWA KIJANA MDOGO WA MIAKA 22 1964
NA
HAMZAH RIJAL
6215764e-65a5-42a4-8592-7afb7bef1afa.jpg

Salim Ahmed Salim na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere 1964​

Mara baada ya kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapo mwaka 1964, Mambo ya Nje ni moja ya mambo yaliyokubalianwa kuwa yawe ya Muungano, hivyo nafasi kama za Ubalozi katika Nchi mbalimbali Washirika na Taasisi za Kimataifa ilibidi zigawanywe kati ya Watanganyika na Wazanzibari ili dhana ya Utanzania ipate kuonekana dhahiri.

Ni katika wakati husika ndipo Rais Julius Nyerere, Kama Mkuu wa Nchi na mtu mwenye Mamlaka ya Uteuzi wa Mabalaozi alipoomba majina ya wale ambao walionekana kuwa na sifa za kuteuliwa kuwa Mabalozi kutoka Zanzibar kwa Rais Abeid Amani Karume.

Miongoni mwa majina yaliyoletwa na Sheikh Karume kwa Mwalimu Nyerere ni jina la Kijana mdogo wa miaka 22 Salim Ahmed Salim, jambo ambalo lilimfanya Mwalimu Nyerere amuulize maa ya pili Rais Karume juu ya umri wa Kijana huyo, majibu aliyopewa ni kuwa huyo ni Kijana wa Zanzibar mwenye vigezo na uwezo, apewe nafasi.

Bila hiyana, Mwalimu Nyerere akamteua Kijana huyo Salim Ahmed Salim kuwa Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Uarabu ya Misri, nafasi ambayo aliitumikia kwa muda wa Mwaka mmoja kati ya Mwaka 1964 na 1965 kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania Nchini India.

Unaweza kudhani kuwa Salim Ahmed Salim alipewa nafasi husika kwa upendeleo, au kwa kuwa Chama chake cha Ummah Party kilikuwa na mahusiano ya karibu na Chama cha ASP cha Karume.

Uwezo wa Dkt Salim Ahmed Salim katika kuieneza Diplomasia ya Tanzania kwa muda wa miaka 50 ya Muungano wetu unaonyesha dhana ya upendeleo isivyo na mashiko, lakini hata uzoefu na Ukindakindaki wake wakati akiteuliwa kushika nafasi hiyo pamoja na kuwa alikuwa na umri mdogo vinaonyesha kuwa aliistahili nafasi hiyo.

Salim hakuwa mgeni wa Siasa za Zanzibar, alichipukia katika Chama cha Zanzibar Nationalist Party, ZNP chini ya ulezi wa Komredi mahiri, Profesa Abdulrahman Mohammed Babu na bega kwa bega naye alishiriki katika kukiasisi Chama cha Kwanza chenye kufuata Mrengo wa Kijamaa katika Afrika, Chama cha Ummah Party, Chama ambacho kilishirikiana na Chama cha ASP katika kutekeleza Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yaliyomuingiza madarakani Karume.

Ni Chama hiki cha Ummah Party ndicho kilichotoa wanamapinduzi Majemedari kama Komredi Ali Sultan Issa, Kanali Ali Mahfoudh, Komredi Sharifu Ahmed Badawyi Qullatein na wengineo ambao walikuwa chachu ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kijana mdogo Salim Ahmed Salim alishirikiana na kulelewa na wote hao, jambo lililompa uzoefu, uwezo na mafunzo. Mpaka leo rekodi zinamuonyesha Dkt Salim A Salim aliyezaliwa Januari 23, 1942 kuwa ndiye Mtanzania mwenye umri mdogo zaidi kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nje ya Nchi.

Pichani ni Kijana wa Miaka 17 wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Ndugu Salim Ahmed Salim wa Chama cha ZNP akiwa pamoja na Rais wa Chama cha TANU, Ndugu Julius Kambarage Nyerere. Picha husika inaonyesha uzoefu na ushiriki wa Kijana huyu katika Siasa za Ukombozi tangu akiwa na umri mdogo tu.
 
Sikuwahi kujua, nasikitika hii ni thread ya zamani lakini naiona leo. Kwa hakika ngoja nitalii kwenye hili jukwaa. Ahsante Mohamed Said
 
Kuna kitu cha maana Mwalimu alikiona ndani ya Salim ambacho wana CCM wenzake walishindwa kukiona yeye akiwa hai hata alipokufa. Sijui kwa kuwa na yeye ni "Chotara" ndiyo maana amekuwa "akikataliwa" mara kwa mara!!??
 
Miongoni mwa majina yaliyoletwa na Sheikh Karume kwa Mwalimu Nyerere ni jina la Kijana mdogo wa miaka 22 Salim Ahmed Salim, jambo ambalo lilimfanya Mwalimu Nyerere amuulize maa ya pili Rais Karume juu ya umri wa Kijana huyo, majibu aliyopewa ni kuwa huyo ni Kijana wa Zanzibar mwenye vigezo na uwezo, apewe nafasi.

Pichani ni Kijana wa Miaka 17 wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Ndugu Salim Ahmed Salim wa Chama cha ZNP akiwa pamoja na Rais wa Chama cha TANU, Ndugu Julius Kambarage Nyerere.


...Kama nimefanya hesabu vizuri picha hii ilipigwa mwaka 1959. So, Mwl. Nyerere alimfahamu Salim kabla ya kupelekewa jina na Karume hapo mwaka 1964. Kama hivyo ni kweli, je, ilikuwaje Mwalimu alimwuliza Karume mara mbili juu ya umri wa Salim?
Nionavyo mie ni kuwa Wana harakati wa kudai uhuru Tanganyika, Zanzibar na Nchi nyingine za Afrika walikuwa wanafahamiana. Yawezekana pia kuwa picha hii ilipigwa baada ya Mkutano wa Pan Afrika wa mwaka 1958....
Nawaomba wana Historia wenye kumbukumbu sahihi wanijuze zaidi..
 
Back
Top Bottom