Sala za jf zaendelea kutimia


P

Pdidy

JF-Expert Member
Joined
Nov 22, 2007
Messages
39,863
Likes
8,686
Points
280
P

Pdidy

JF-Expert Member
Joined Nov 22, 2007
39,863 8,686 280
UHAI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) sasa u mikononi mwa wabunge wa chama hicho, ambao wametangaza vita dhidi ya chama chao na serikali, na kukiingiza chama tawala katika wakati mgumu pengine kuliko nyakati zote iliyowahi kuzipitia huko nyuma, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Mmeguko na migomo ya wabunge ndiyo mambo yanayozungumzwa sana wiki hii, hasa baada ya wabunge kugomea miswada miwili ya serikali, huku baadhi yao wakihusishwa na Chama Cha Jamii (CCJ) ambacho hakijapata usajili wa kudumu, lakini kimeendelea kukitikisa CCM.

Tanzania Daima Jumapili imeelezwa kuwa baadhi ya wabunge wameamua kusimama kidete kukataa mipango mbalimbali ya chama tawala bila kuhofia kuwajibishwa na chama.

Vyanzo vya habari vimedokeza kuwa kitendo cha wabunge waliohudhuria kikao cha wabunge wa CCM ambacho kilikuwa na lengo la kuweka mkakati wa pamoja wa kupitisha muswada wa gharama za uchaguzi hasa kudhibiti matumizi ya fedha, kukataa kuupitisha huku wakitoa maneno makali, kimechangia kuzidisha ufa ndani ya chama hicho kikongwe.

Kilidokeza kuwa kikao hicho kilichokuwa kikiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kilikuwa moto, huku kiongozi huyo wa serikali akielemewa na hoja za wabunge waliokuwa wakionyesha kutokubaliana na muswada huo kwa kuwa unalenga kuwamaliza kisiasa.

Aidha, tukio jingine la wabunge, hasa wa CCM, kugoma kuupitisha muswada wa Usalama wa Taifa jana bungeni, kumeelezwa kuwa ni mwendo uleule wa kuonyesha hali ya mambo si shwari ndani ya chama hicho kinachoonekana kulegalega hasa baada ya kuibuka kwa tuhuma mbalimbali za ufisadi zikiwahusisha vigogo.

Wakati hali hiyo ya kutokuwa shwari ikiwa hivyo bungeni, kuna taarifa zimevuja kutoka kamati iliyoundwa kuchunguza chanzo cha uhusiano mbaya baina ya wabunge wa chama hicho kuwa makundi mawili yanayohasimiana yamegoma kusuluhishwa.

Taarifa hizo zinaweka wazi kiongozi mmoja ambaye yuko katika kundi la wapambanaji wa ufisadi aliitwa na kamati hiyo kwa lengo la kupatanishwa na kiongozi wa kundi la pili linaloshutumiwa kushiriki katika vitendo vya ufisadi lakini makundi hayo yalishindwa kufikia muafaka.

Kiongozi wa kundi la ufisadi anadaiwa kukataa kupatanishwa kwa kuwa hakukuwa na ugomvi binafsi bali maslahi ya taifa hivyo ni vema wanaokwenda kinyume wakashughulikiwa ili chama kisianguke kuliko kuwalinda ili waendelee kukivuruga chama.

Chanzo hicho kinadai kuwa kiongozi wa kundi la pili naye alisema hana tatizo na upatanishi huo ila ni lazima kundi la wapambanaji wa ufisadi liombe radhi kwa kuwachafua katika jamii, bungeni na chamani.

Kwa mujibu wa chanzo hicho kuna dai kuwa CCM hivi sasa inazidi kumeguka kutokana na baadhi ya makada, hasa wale wanaotuhumiwa kupambana na ufisadi, kudaiwa kuingia katika majimbo ya baadhi ya wabunge hasa ya wapambanaji wa ufisadi na kuwafadhili watu wanaotaka kuwania ubunge ili wawang’oe wabunge wa sasa.

“Vita kubwa hivi sasa ni nguvu za kifedha za kundi linalotuhumiwa kwa ufisadi ambalo limekuwa likitembeza fedha ili wabunge wanaopambana na ufisadi washindwe,” kilisema chanzo hicho.

Wakati vita ya makundi ikionekana kuiyumbisha CCM, ujio wa CCJ, unaonekana kuzidisha ufa ndani ya chama hicho kikongwe ambapo viongozi wake wakubwa mara kadhaa wametoa matamshi ya kukibeza hatua inayotafsiriwa kama ni kuingiwa na hofu.

Hofu ya CCM hivi sasa inaonekana zaidi hasa baada ya taarifa za kikachero kuweka wazi kuwa CCJ ina mikono ya vigogo wasiopungua 27 kutoka chama tawala.

Taarifa hizo za kikachero ndizo zilizozidisha hofu ya kumeguka kwa chama hicho ambacho kinaelekezewa shutuma za kulinda makada wake wanaoshutumiwa kwa kujihusisha na vitendo vya kifisadi.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa, wamesema kwamba kwa hali ilivyo hivi sasa, CCM inahitaji busara za Mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete, kunusurika kisikumbwe na dhoruba ya kukimbiwa na makada wake au kuparaganyika kutokana na uhasama unaozidisha kushamiri baina ya wanachama.

Wachambuzi hao wanaonya kuwa kama Rais Kikwete ataendelea na tabia yake ya kuhofu kuchukua maamuzi makali dhidi ya watu fulani au kundi lao ndani ya chama hicho kuna kila dalili chama kikaanza kuelekea kupasuka.

Katika hatua nyingine, kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa ubunge uwe na ukomo pia imezua hofu hasa kwa baadhi ya wabunge waliokaa bungeni kwa zaidi ya vipindi vinne ambao wanaona kuna mkakati ya kuondolewa katika majimbo yao kwa kigezo cha umri.

Wabunge hao ambao ama kwa kificho au kwa kujitokeza hadharani wameonekana wakipinga kauli hiyo ya Pinda ambayo waliita ni ya kuwachonganisha na wapiga kura hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.

Kauli hiyo ya Pinda pia iliwahi kutolewa na kada maarufu wa chama hicho, Peter Kisumo, ambaye aliwataka wazee waachie ngazi ili kuwapisha vijana waweze kuongoza.

Wachambuzi wa muasala ya kisiasa wanaweka wazi kuwa kwa kauli hizo na hali ya mwenendo wa mambo CCM haiwezi kuwa moja kama ile ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kama haitokubali kuwafukuza wanachama wake wanaokiyumbisha ama kwa maneno yao au kwa vitendo vyao.

Wanabainisha kuwa katika hali ya sasa, hasa nchi ikielekea katika uchaguzi mkuu, kuna kila dalili chama hicho kupoteza viti vingi vya ubunge na udiwani endapo wapinzani watasimamisha wagombea wenye nguvu na ushawishi mkubwa katika majimbo husika.
 

Forum statistics

Threads 1,236,296
Members 475,050
Posts 29,253,223