BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,150
Posted Date::4/19/2008
Sakata ya Waziri bilionea Tanzania yazua maswali zaidi kuliko majibu
Na Mwandishi wetu
Mwananchi
SUALA la utajiri wa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, linazidi kufukuta na sasa limeacha maswali mengi ambayo mwanasiasa huyo anatakiwa kuyajibu.
Tangu Taasisi ya Kuchunguza Makosa Makubwa ya Jinai Uingereza (SFO) iibue tuhuma dhidi ya Chenge , kwamba anamiliki kiasi cha sh bilioni 1.2 katika benki moja katika Kisiwa cha Jersey nchini humo na kuzihusisha fedha hizo kuwa zinatokana na malipo ya ununuzi tata wa rada, watu wengi wamekuwa wakihoji maswali mengi bila ya kupata majibu.
Mwaka 2002 wakati fedha hizo zinawekwa katika benki hiyo, hali ya uchumi nchini ilikuwa mbaya na kwamba ni wakati huo ndio tulikuwa tukihitaji sana fedha za kigeni, swali ni je, nani aliruhusu fedha hizo kupelekwa nje ya nchi?
Jambo jingine ambalo wananchi wanajiuliza ni je, Chenge ameripoti katika tume ya maadili ya uongozi kuwa anacho kiasi hicho katika akaunti yake hiyo na kama ametaja kiasi hicho cha fedha katika fomu zake za kugombea ubunge.
Chenge amenukuliwa na gazeti la The Guardian la Uingereza akikiri kumiliki kiasi cha dola za Marekani 1 milioni, lakini akakanusha kuzipata kutokana na kashfa ya ununuzi wa rada ya kijeshi iliyonunuliwa na Tanzania mwaka 2002 kutoka kampuni ya BAE System ya Uingereza kwa gharama ya paundi 28 milioni (Sh 70 bilioni), ambayo yanaelezwa kuwa ni malipo yasiyolingana na rada hiyo kutokana na mchakato huo kuzingirwa na rushwa.
Kabla hata ya suala hili kujulikana hadharani tayari wananchi walikuwa na wasiwasi na usafi wa Chenge hadi kushangazwa na hatua ya Rais Jakaya Kikwete kumrejesha Chenge katika baraza lake jipya la mawaziri Februari mwaka huu, baada ya kulivunja lile la kwanza kutokana na kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Chenge mwenyewe baada ya kusikia maneno hayo alisema kwa majigambo kuwa umuhimu wa kuteuliwa kwake anaujua Kikwete na aulizwe yeye (Rais) aliyemteua.
Kilicho wazi ni kuwa utendaji wa Chenge ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali kwa miaka 10 katika uongozi wa serikali ya awamu ya tatu, haukuwa wa kuridhisha kutokana na mikataba mingi mibaya inayolalamikiwa na wananchi kutiwa saini wakati yeye akiiongoza ofisi hiyo nyeti ya serikali.
Kilichozidi kuwachukiza wananchi kuhusu Chenge ni kauli yake aliyoitoa wiki hii wakati aliporejea nchini akitokea China kwamba wanamtuhumu kwa vijisenti tu, kauli hiyo inachukuliwa na watu kuwa ni dharau na kwamba ana fedha nyingi zaidi ya kiasi hicho anachotuhumiwa kuchukua.
"Nafurahi kurudi nyumbani. Tulikuwa China na Rais na ametuwakilisha vizuri. Tulipokuwa China, ndio tukasikia hizo tuhuma za vijisenti," alisema Chenge.
Ingawa Chenge amekaririwa na baadhi ya magazeti hapa nchini akiomba radhi kwa kauli yake hiyo akieleza kwamba inatokana na yeye kutojua Kiswahili na kwamba haukumaanisha kwamba yeye ana fedha nyingi mno, lakini bado wananchi wanahitaji kupata majibu ya maswali waliyonayo.
Kabla ya gazeti la The Guardian kuibua tuhuma hizo, Septemba 15, mwaka jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willbrod Slaa na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, walimtaja Chenge katika orodha ya vigogo 11, wakiwamo viongozi kadhaa wa serikali nchini wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi wa mabilioni ya shilingi za walipakodi.
Baadaye, Septemba 19, Waziri Chenge aliliambia gazeti hili kuwa walioibua hoja ya ufisadi dhidi ya viongozi wa serikali kama wakipata au kama wana ushahidi, yeye binafsi anatoa ruksa waupeleke katika vyombo husika vya dola ili ufanyiwe kazi.
Hata hivyo, suala la Chenge ni mtihani mwingine kwa Rais Kikwete ambaye anapaswa sasa kuonyesha kwamba anaweza kutekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati akiingia madarakani kwamba hatasubiri kuona ushahidi bali atatumia hata ushihidi wa mazingira kumwondoa mtu madarakani iwapo atakabiliwa na tuhuma za ufisadi.
Kikwete anasubiriwa kwa hamu na wananchi kuona kama ataweza kufaulu mtihani huu wa kumwondoa Chenge madarakani ili aweze kupisha uchunguzi unaofanywa dhidi yake na SFO pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru).