SAKATA LA UUZAJI WA UDA: Hakuna atakayesalimika

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,779
1d23274bb5fde0b0c6e9fc4cebb1be42.jpg

Na Jacob Daffi - Imechapwa 12 October 2011

KAMATI ya baraza la madiwani iliyoundwa na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi kuchunguza ubinafsishaji wa shirila la usafiri jijini (UDA), kuvunjwa kwa bodi ya shirika hilo na kuuzwa kwa mali zake, imeagiza kufikishwa kwenye mkono wa sheria aliyekuwa meneja wa shirika hilo, Victor Millanzi.

Katika ripoti ambayo MwanaHALISI imeipata, kamati imeagiza meneja huyo achunguzwe na vyombo vya dola kutokana na ushiriki wake katika kulihujumu shirika hilo.


Aidha, ripoti imesema hatua ya Masaburi kukabidhi UDA mikononi mwa muwekezaji – kampuni ya Simon Group Ltd., - ni "kinyume cha utaratibu."


Dk. Masaburi aliunda kamati hiyo Juni mwaka huu. Ripoti inatuhumu Millanzi kuuza kinyume cha taratibu rasilimali za UDA zinazohamishika na zile zisizohamishika kama sehemu ya mkakati wake wa kukabiliana na hasara.


Hata hivyo, Millanzi katika taarifa yake mbele ya wajumbe wa Kamati amekana madai yote dhidi yake na kusema, "Nilichokiteleza nilikifanya kwa mujibu wa sheria na taratibu za kuendesha UDA."


Meya hakupata ridhaa (Resolution) ya mkutano wa madiwani. Yumkini mwanahisa wa pili mkubwa, Hazina naye hakuridhia maamuzi ya kikao hicho wala wakurugenzi wa bodi ya UDA."


Kamati ya Masaburi imeeleza, "uuzaji wa rasilimali za UDA haukufuta sheria za manunuzi ya umma (PPRA) ya mwaka 2004; wala hakukufanyika tathimini ya mali zake kabla ya kuuzwa."


Hadi kufikia 30 Juni 2010, shirika hilo la umma lilikuwa likiendeshwa kwa hasara ya Sh. 1.4 bilioni.


Kamati hiyo imebaini mali zisizohamishika za shirika hilo zilizouzwa kwa kile inachoita kiholela kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2010, ni pamoja na nyumba iliyoko kiwanja Na. 10 eneo la Jangwani Beach. Nyumba hiyo imeuzwa mwaka 1997 kwa Harold John kwa thamani ya Sh. 40 milioni.


Nyumba nyingine ni ile iliyopo Na. 60 iliyoko katika eneo la Oysterbay, ambayo imeuzwa kwa Sh. 120 milioni (1997) na ile iliyoko kitalu Na. 354, eneo la Masaki, Kinondoni, ambayo imeuzwa mwaka 2001 kwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa thamani ya Sh. 600 milioni.


Katika uza uza hiyo, kimo kiwanja kilichoko kitalu Na. 261 eneo la Ubungo kilichouzwa mwaka 1998 kwa Shirila la Maendeleo la Dar es Salaam (DCC) kwa Sh. 800 milioni, viwanja Na. 1-21 vilivyoko block V, katika Manispaa ya Ilala, vilivyouzwa mwaka 2003 kwa DCC kwa Sh. 350 milioni, kiwanja Na. 38 kilichoko Oysterbay kilichouzwa mwaka 2005 kwa kampuni ya Century Properties Ltd kwa Sh. 516.2 milioni na nyumba Na. 54 iliyoko Ilala iliyouzwa 2009 kwa Trans Ocean Supplies Ltd kwa Sh 180 milioni.


Aidha, Kamati hiyo imebaini kuwapo kwa mikataba kadhaa yenye utata ya pango ya majengo na maeneo ya wazi yanayomilikiwa na UDA. Katika maeneo mengi, hata bei hicho kinachoitwa "bei ya pango," haikuzingatia ukubwa wa eneo. Vitega uchumi vingi vimeuzwa kwa bei ya kutupa.


Kwa mfano, menejimenti ya UDA, chini ya Millanzi na Bodi ya Wakurugenzi iliyokuwa chini ya Idd Simba, ilipangisha watu mbalimbali kuanzia kwenye jengo la utawala yalipo makao makuu ya UDA, Kurasini, Dar es Salaam hadi maeneo ya wazi yaliyoko katika karakana zake.


Wapangaji hao wanaiolipa kodi ya kutupwa, ni pamoja na Nagla General Shipping Services Ltd., aliyepangishwa kwenye jengo la utawala eneo lenye ukubwa mita za mraba 19 kwa Sh. 7,500 kwa mwezi.


Wengine ni F.A.Agencies (T) Ltd., anayelipa Sh 7,200 kwa mwezi, Rafad Complex Ltd (kituo cha basi kati), anayelipa Sh. 8,400 kwa mwezi na Lake Corridor Petroleum Ltd anayeendesha kantini ya UDA kwa malipo ya Sh. 7,429 kwa mwezi.

Kampuni ya Lake Corridor Petroleum Ltd imekodishwa eneo lingine la ufundi lenye ukubwa wa mita za mraba 140 ambapo inalipa Sh. 3,000 kwa mwezi.


Nyingine ni kampuni ya Mupingwa Petroleum Ltd iliyokodishiwa ofisi za UDA zilizoko bandarini kwa Sh. 4,800 kwa mwezi, Koru Freght Ltd iliyokodisha ghala la UDA kwa malipo ya Sh 2,457 kwa mwezi, huku kampuni hiyo ikiwa imepangishwa eneo la wazi katika viwanja vya makao makuu ya UDA lenye ukubwa wa mita za mraba 370 kwa Sh. 2,485 kwa mwezi.


Wapangaji wengine na kiasi wanacholipa kwa mwezi kikiwa katika mabano, ni pamoja na Seleman Keraba (Sh. 850 kwa mwezi), Mak Consult Engineering (Sh. 4,312), Macbean Sea Trading (Sh 7,200), Koru Freight Ltd (Sh. 6,000), Koru Freight pia imepanga eneo la mita za mraba 164.52 kwa Sh. 3000, Shibat Enterprises Ltd (Sh. 7,000) na Exaud Epiana aliyepewa karakana kwa kodi ya Sh. 6,000 kwa mwezi.


Kwa mujibu wa ripoti ya kamati hiyo, viwango vya soko kwa sasa vya kukodi katika maeneo ya mijini, na hasa jijini Dar es Salaam, ni kati ya dola 7 hadi 12, sawa na karibu Sh. 10,500 hadi Sh. 18,000 kwa kila mita moja ya mraba kutegemeana na eneo lilipo jengo husika linalopangishwa.


Ripoti hiyo imebainisha wazi kwamba baadhi ya wapangaji hao wa maeneo ya UDA wameyapangisha kwa makampuni mengine ambayo wao wanawatoza bei kubwa zaidi na hivyo makampuni hayo kujinufaisha zaidi kupitia mgogo wa shirika hilo.


Kampuni ya Lake Corridor Petroleum Ltd imetajwa kama mfano wa makampuni ambayo yameingia mikataba ya kukodishwa ofisi au maeneo ya wazi, lakini wakaamua kupangisha kwa watu wengine bila kupata idhini wala kibali cha UDA.


Wakati kampuni ya Koru Freight imepanga eneo la wazi lenye ukubwa wa mita za mraba 1,916, kamati imebaini kwamba kampuni hiyo imekuwa ikilipia eneo la mita za mraba 370 tu.


"UDA iliingia ubia na Africarriers tarehe 13/10/2009kuendeleza kiwanja Na 437/129 kilichopo Mtaa wa Sokoine (kilipo kituo cha mabasi cha Stesheni). Makubaliano hayo yamebainika kuwa na mapungufu kadhaa, ikiwa ni pamoja na kutokuwapo nyaraka zozote zinazoonyesha jinsi mwekezaji huyu alivyopatikana, hivyo kutia shaka iwapo sheria ya manunuzi ya mwaka 2004 na kanuni zake za mwaka 2005 zilizingatiwa," inasema sehemu ya ripoti hiyo.


Upungufu mwingine uliotajwa na ripoti hiyo katika mkataba wa ubia huo wa UDA na Africarriers, ni kampuni hiyo kutaka kwamba baada ya mradi wa ujenzi wa ghorofa ndani ya kiwanja hicho cha kituo cha Stesheni kukamilika, mwekezaji huyo atatakiwa kumiliki hisa asilimia 75 na UDA ibakiwe na hisa 25 tu.


Aliyekuwa Meneja huyo wa UDA, Millanzi, ambaye alitimuliwa na Masaburi Juni mwaka huu, kabla ya kuivunja pia Bodi ya UDA iliyokuwa chini ya Idd Simba, anadaiwa kujichotea Sh. 40,622,651.80 kama malipo ya kiinua mgongo chake hata kabla ya kumaliza mkataba wake wa kuliongoza shirika hilo.


Kwa mujibu wa ripoti ya kamati hiyo ya Masaburi, mkataba wa utumishi wa meneja huyo ulipaswa kufikia ukomo 30 Juni 2011, lakini hata kabla ya kufikia mwisho wa mkataba huo yeye alikwishajilipa tayari kiinua mgogo chake.


Malipo hayo yanaelezwa kulipwa kwa awamu tatu. Tarehe 19 Mei 2011 kupitia vocha Na 21, alijilipa Sh. 25,000,000, tarehe 25 Mei 2011, akajilipa Sh. 5,800,000 na 30 Mei 2011, ambapo amejilipa Sh. 9,822,651.80 kupitia hundi Na. 930322.


Katika utetezi wake wa maandishi mbele ya kamati kuhusu tuhuma za kujilipa mafao
kabla ya mkataba kumalizika, Milanzi alisema, "Siyo kweli. Mimi niliajiriwa UDA mwaka 2006, tarehe 1 Juni. Hivyo mkataba wangu uliisha 30 Mei 2011."


Anasema, "Nilitoa notisi ya mwezi mmoja na taratibu zetu (UDA) malipo yanafanywa kwenye mwezi wa mwisho uliotoa notisi."


Hata hivyo, nyaraka zilizopo zinaonyesha Milanzi alisaini mkataba wa ajira tarehe 29 Juni 2006, wenye Kumb. Na UDA/A.1/6. Ulipaswa kumalizika 30 Juni 2011.

Mgogoro kuhusu menejimenti nzima ya UDA uliibuka mapema Juni mwaka huu baada ya Meya Masaburi kuamuru kumfuta kazi Millanzi, pamoja na kuivunja Bodi ya UDA iliyokuwa chini ya Idd Simba kukabiliwa na tuhuma za ufujaji wa fedha zilizokuwa zimewekezwa na mwekezaji mpya ndani ya shirika hilo.


 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

1 Reactions
Reply
Top Bottom