Sakata la Richmond, Dowans: Wabunge walonga
na Mwandishi Wetu, Dodoma
Tanzania Daima
MATUKIO mawili makubwa yenye uhusiano wa karibu, lile la kurejea kwa kasi kwa mjadala wa Richmond bungeni katika siku za hivi karibuni na la kusitishwa kwa mkataba wa kuzalisha umeme wa Dowans yanaonekana kuendelea kuwagawa wabunge.
Mahojiano ya ana kwa ana yaliyofanywa na Tanzania Daima mjini Dodoma na Dar es Salaam jana yanaonyesha kuwa, wabunge wamepokea tukio la juzi la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) la kusitisha mkataba wa Dowans kwa mawazo tofauti.
Akizungumza mjini hapa jana, Mbunge wa Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi alisema watu walioingia mkataba na Kampuni ya Dowans ambao umevunjwa rasmi jana, hawapaswi kulaumiwa kutokana na hali ilivyokuwa wakati huo, kwani nchi ilikuwa imebakisha wiki mbili tu iingie gizani.
Karamagi ambaye Februari mwaka huu alilazimika kujiuzulu uwaziri wa Nishati na Madini baada ya jina lake kuhusishwa katika mkataba huo, aliyasema hayo wakati alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu uamuzi huo uliotangazwa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Idris Rashidi.
Kutokana na hali hiyo, Karamagi aliitahadharisha serikali kuwa, inapaswa kuwa makini na hatua za kujitetea zinazoweza kuchukuliwa na upande ulioathirika kutokana na maamuzi ya kusitishwa kwa mkataba huo.
Definitely (hakika) aliyeathirika atajitetea aidha, kwa kwenda mahakamani au vinginevyo
kila mkataba una vipengele vya kuuvunja na kujitetea, alisema Karamagi katika mahojiano yake na Tanzania Daima.
Alisema pia kuwa awali TANESCO ilichelea kuvunja mkataba wake na Richmond ambao ndio walioiuzia mkataba wake Dowans Oktoba 23, mwaka jana kutokana na hofu ya kuchukuliwa kwa hatua za kisheria dhidi yao.
TANESCO wenyewe waliona kuwa iwapo wangekatisha mkataba wakati ule, Richmond wangetumia vipengele kuzuia uletwaji wa majenereta mengine, hivyo nchi ingeendelea kuteseka, alisema.
Wakati Karamagi akitoa tahadhari hiyo, wabunge wengine waliohojiwa na Tanzania Daima, walisema kuwa hatua hiyo ya serikali imechelewa sana, hasa ikizingatia kuwa, nchi imelipa fedha nyingi wakati hakukuwa na mkataba halali wa kuifanya ilipe fedha hizo.
Mnataka niseme nini kuhusu hili? Maoni yangu yako open (wazi). Sisi ndio tuliishauri serikali kuwa hili ni kosa na tukatoa mapendekezo, alisema Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa (CUF), ambaye alikuwa mmoja wa wajumbe wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mchakato ulioipatia ushindi Kampuni ya Richmond katika kandarasi ya kufua umeme wa dharura.
Hata hivyo, katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Idris Rashid, alisema uamuzi wa shirika lake kuvunja mkataba huo, hauna uhusiano na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Teule ya Bunge chini ya Dk. Harrison Mwakyembe, iliyochunguza utata wa zabuni ya Richmond, iliyosababisha mbali ya Karamagi, Waziri Mkuu wakati ule Edward Lowassa na Dk. Ibrahim Msabaha (Nishati na Madini), kujiuzulu nafasi zao.
Kwa upande wake, Mnyaa alisema ripoti ya kamati yao waliyoisoma Februari mwaka huu, ilithibitisha pasipo shaka kwamba, serikali ilikuwa na uwezo wa kuagiza majenereta yaliyoletwa na Richmond kwa nusu ya bei ambayo iliyakodisha.
Unapeleka maombi yako tu, unayapata majenereta yao mwenyewe, si ya kukodi, hakuna capacity charge, alisema Mnyaa.
Alipotakiwa kueleza iwapo hatua ya serikali haiwezi kuwa na madhara, alisema hilo linategemea na vipengele vya mkataba, lakini kwa vyovyote vile, katika suala hilo, serikali ina haki.
Hatua hiyo ya serikali ilipongezwa pia na Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini ya Bunge, William Shellukindo ambaye wakati uchunguzi wa utata katika mkataba wa Richmond ukianza mwishoni mwa mwaka jana, alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Biashara na Uwezeshaji, ambayo ndiyo iliyopendekeza kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge.
Tuliieleza serikali waziwazi kuwa mkataba ni mbovu
tunafurahi kwa sababu sasa serikali inakubaliana na sisi, alisema Shellukindo.
Shellukindo ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM), alikwenda mbali zaidi kuwazungumzia watu ambao wamekuwa wakilalamika kuwa walionewa na Kamati Teule ya Bunge, na kubainisha kuwa katika suala la uchunguzi dhidi ya Richmond, hakuna mtu aliyekuwa anafuatwa binafsi.
Hakuna visa wala kusingiziana, hatukumuonea mtu
mwenye malalamiko afahamu kuwa sasa hivi hatuzungumzii Richmond tena, imemalizika.
Anayetaka (kuijadili) ajenge hoja ya kulihoji Bunge kwa sababu ripoti ile sasa si ya Mwakyembe, ni maamuzi ya Bunge zima. Hatuna haja ya kupoteza muda kuijadili tena Richmond, alisema Shellukindo.
Hata hivyo, kwa upande wake, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM) ambaye jina lake lilitajwa mara kadhaa katika ripoti ya Mwakyembe, alipohojiwa kuhusu suala hilo, hakuwa tayari kusema lolote zaidi ya kueleza kusikitishwa kwake na namna mjadala wa Richmond unavyoendelea kinyemela bungeni.
Mimi ninachoweza kusema ni kwamba, nashangazwa na hatua ya Spika kumruhusu Mwakyembe aendeleze mjadala wa Richmond bungeni hivi sasa, wakati mimi nilinyimwa fursa ya kuzungumzia suala hilo Aprili. Kwa hakika haya yanayotokea bungeni hivi sasa ni sawa na mchezo wa Ze Comedy, alisema Rostam, huku akikataa kueleza lolote zaidi.
Kwa upande wake, Dk Mwakyembe, alipofuatwa ili kutoa maoni yake kuhusu suala hilo, ikiwa ni pamoja na hatua ya serikali kusitisha mkataba wa Dowans, alikataa kusema lolote.
Naye Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP) alisema anaamini kuwa hapakuwahi kuwapo kwa mkataba halali ilhali taifa likiwa limeingia hasara kubwa kutokana na kuendelea kufanya kazi na Dowans.
Hakuna walichovunja na tayari tumeshaingia hasara kubwa, serikali iseme itawafanya nini walioingia mkataba huo usiokuwepo, alisema Cheyo na kubainisha kuwa hatua zilizochukuliwa ni kielelezo kuwa serikali imechukizwa, kama walivyokuwa wamechukizwa wananchi.
Kwa upande wake, akilitolea ufafanuzi suala hilo, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema hatua dhidi ya watu walioingia mkataba huo zipo chini ya dhamana ya Waziri Mkuu, ambaye ndiye aliyeahidi kushughulikia mapendekezo ya Bunge yaliyotokana na kamati teule.
Hata hivyo, Ngeleja alisema kwa upande wao, hiyo ni hatua ya kwanza, na hivi sasa wanatafakari hatua nyingine ya kuchukua kuhusu masuala kadhaa, ikiwamo ukweli kuwa Dowans ilizalisha umeme ambao ulitumiwa na nchi.
Tutakaa na pande zote, TANESCO na Dowans kuzungumza, lakini baada ya tarehe ya kusitisha mkataba hakuna malipo yatakayofanyika, alisema Ngeleja. Chini ya mkataba huo, TANESCO ilikuwa ikilipa sh milioni 152 kwa siku kama Capacity Charge.
Akizungumzia msingi wa kusitishwa kwa mkataba huo, Ngeleja alisema baada ya uchunguzi wa kina, serikali imejiridhisha kuwa hakukuwa na kampuni iliyosajiliwa kwa jina la Richmond Development Company LLC, ambayo ndiyo iliyoingia mkataba na serikali.
Kwa maana hiyo, kwa kuwa hakukuwa na kampuni hiyo, hata mkataba haukupaswa kuwepo kwa sababu hakuna mtu wa kuingia mkataba huo, alisema.