Shangilieni Stars ila msisahau Buzwagi, BoT na Richmond
Mwandishi Wetu
Kutoka Gazeti la Tanzania Daima
LEO timu yetu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, inajitupa uwanjani kumenyana na timu ngumu ya soka ya taifa ya Msumbiji kuwania tiketi ya kwenda Ghana, kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika, mwakani.
Kwa mtu anayejua maana ya uzalendo, hatakuwa na pingamizi kuwashajihisha Watanzania kuishangilia timu yao ya taifa.
Kwa vile Watanzania huwa hawana uhaba wa uzalendo japo kwa wengine ni juu juu, hili halina utata kuwa, wataishangilia timu yao, tena kwa nia safi, na wengine kwa nia chafu. Kuna msemo unaosema kwenye msafara wa mamba na kenge wamo.
Kadhalika, hata kwenye mashamsham na shamrashamra za kuishangilia Stars, ambao ndio msafara hasa wa mamba, kuna mikenge tena mingi itakayotaka kuutumia mwanya huu kuficha uchafu na aibu zao.
Hapa ndipo masuala mazito na muhimu kama kuendelea kuwashikia kidedea mafisadi wetu, yanaweza kusahaulika hata kupuuziwa. Hapa mikenge itafanya kila liwezekanalo ili kushangilia Stars kunoge, hata kuwa dili ili angalau yapumue kwa muda, hata kuwasahaulisha kabisa wananchi ambao si haba wanaonekana kuanza kutoka kwenye ukondoo na blanketi la kulishwa sifa uchwara.
Kwa siku nne zilizopita, hamasa ya Watanzania iko juu mno, idadi kubwa ya magari, hata ya daladala yanapeperusha bendera ya taifa. Kwa kifupi kila kona unayopita mazungumzo ni Stars, Stars, Stars.
Kwa wanaojua kuwa kwetu michezo haina umuhimu sana kwa wanasiasa, kuna kipindi hushangaa hata kuiona Stars au hata wakimbiaji wakikaribishwa bungeni hata Ikulu.
Mara nyingi hili linapotokea, ujue kuna lengo la kutaka kuipumbaza hadhira kama ilivyotokea siku za nyuma, baada ya Stars kuishinda Burkina Faso, ambapo kashfa ya Benki Kuu (BoT) ilikuwa imepamba moto.
Kutokana na ushindi huo, wanamichezo waliitwa bungeni, kanuni ikavunjwa kuwaruhusu wachezaji na walimu wao kuingia na kushangiliwa kiasi cha kupoteza kabisa hoja ya BoT iliyoshikiwa kidedea na Mbunge wa Karatu, Dk. Willibroad Slaa (CHADEMA).
Wakati hilo likiendelea, ulitokea msiba wa mbunge Amina Chifupa. Nao kwa namna yake, uliihamisha hadhira ya kashfa hiyo kwenda kwenye majonzi, huku mafisidi angalau wakipata ahueni kwa kutomeza dawa za shinikizo la moyo.
Hata ule moto wa kumtaka Gavana wa BoT, Daudi Balali kuwajibika, bahati mbaya ulizimika ghafla, huku naye akitukoga na kutusuta kuwa yuko comfortable, na ari yake ya kazi iko juu kwa madai kuwa tuhuma dhidi yake ni uzushi na kamwe hawezi kuachia ngazi kwa uzushi wa kwenye mtandao.
Tukirejea kwenye Taifa Stars, tuliwahi kuhoji kwanini timu hii inakuwa ya maana wakati wa matukio ya kashfa au hata inapopata ushindi baada ya kuhangaishwa kimalipo? Nani asiyejua kuwa Stars mara nyingi inachangiwa na wafanyabiashara wengi, lakini baadhi yao wachafu ambao kimsingi wanapenda kuitumia ama kutangazia biashara zao au kuwa karibu na mawaziri ili wafanikishe dili zao?
Tujiulize huku tukidurusu. Je, hii pesa inayoteketea kwa kuwasamehe kodi wafanyabiashara, kwanini isipewe Taifa Stars kama kweli tunaijali na kuipenda? Maana hawa wanaoichangia ili kuitumia na kupatia umaarufu, utakuta wengi wao ni wale wale wakwepa kodi, wafanya magendo, walanguzi hata wanaosamehewa kodi.
Kwanini tuwe na pesa ya kutumia kwenye sherehe na makongamano ya kipuuzi tukose ya kuiwezesha Taifa Stars? Kwa watu makini, uwekezaji kwenye michezo unalipa kuliko mambo mengine ya kisiasa. Kama vyama vinapewa ruzuku kujiendesha, kwanini Taifa Stars nayo isipewe? Maana ni kwa ajili ya taifa sawa na asasi nyingine.
Kama kuna mtoto yatima Tanzania, basi na Taifa Stars nayo ni miongoni mwao.
Taifa Stars wamepata nafasi hii ya kuungwa mkono na wananchi, piga ua wawape wananchi raha basi.
Lakini, wakati wananchi wakipewa raha, wasilewe kiasi cha kusahau wale manyangau wanaowanyima raha kwa kuwaibia na kuwatumia kama mataahira.
Stars wapeni raha wananchi, lakini raha hiyo isiwafanye wasahau hoja nyeti kama ile iliyotolewa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, kuhusu kusainiwa mkataba wa Buzwagi.
Watanzania shangilieni Stars, lakini msilewe kiasi cha kusahau ununuzi wa rada tuliyoambiwa tutadai chenji yetu. Ununuzi wa ndege ya rais ambayo licha ya kununuliwa kwa zaidi ya sh bilioni 40, haifanyi kazi ipasavyo huku kukiwa na kashfa ya BoT, IPTL, Richmond na mauzauza mengine yenye utata.
Shangilieni Stars, lakini msisahahu usiri uliopo kwenye mikataba mingi ambayo wabunge wetu wameshindwa kuhoji, huku mkikumbuka suala la muafaka wa Zanzibar, ambao hadi sasa hakuna dalili za kufikiwa.
Stars wapeni raha Watanzania, lakini raha hiyo isiwafanye msahau umasikini unaozidi kila kukicha huku wananchi wakianikizwa kwa kauli ya maisha bora kwa kila Mtanzania.
Juzi juzi nchini Irak, imegundulika kuwa mpira unaweza kuwaunganisha watu hata wenye tofauti kubwa, ambazo zimewashinda wababe wa vita na wanadiplomasia. Nasi kwa Tanzania, tuitumie fursa hii kushikamana dhidi ya ufisadi ambao unaonekana kumshinda rais na serikali yake.
Ni michezo hii ilizaa vyama vya siasa kama TANU na ASP. Kadhalika ni michezo hii inaweza kuleta vuguvugu la kisiasa dhidi ya siasa babaishi na za kujuana na kulindana ambazo zimekuwa maafa kwa nchi yetu.
Wakati tukishangilia Taifa Stars, tujiweke sawa kuwazomea mafisadi tunaowajua, ambao wanajifanya hawasikii wala hawaoni kuwa tunajua na tunataka wawajibike bila mjadala.
Tunafahamu michezo ina mashabiki wengi kuliko siasa. Hivyo tutumie fursa hii kuzidi kuwahimiza wananchi wasilewe ushindi au fursa ya kufika tulipofika bali waamke na kudai haki ya kuwa na nchi isiyoendeshwa kimizengwe kutumiana na kudanganyana.
Tutumie fursa hii kukumbushia kurejeshwa kwa nyumba zetu, kutaja mali za maofisa wa serikali, kusuka upya na kupunguza Baraza la Mawaziri ambalo linaonekana wazi kupwaya na kukosa maana.
Wakati tukijiandalia tukio hili, tuwaambie tena wale wote wenye kashfa kuachia ngazi ili tupate watu wenye akili na adili, watuongoze badala ya kutuibia na kutufanya majuha.
Mungu ibariki Taifa Stars, Mungu ibariki Tanzania.
0713 260 071