Saikolojia na kujiua/ Muhtasari

Oct 5, 2015
88
476
Baada ya askari wawili wa jeshi la polisi Tanzania, Nelson Mkonda na ASP Benedict Nyamatara kujiua kwa risasi ndani ya siku moja (juzi) ni vema kuangalia angalau juujuu mambo kadhaa, hasa eneo la saikolojia.

Kwanza kabisa, nitoe rai kwa serikali kuangalia namna ya kushughulikia jambo hili tata. Kwa juu juu unaweza kuwapuuza waliojiua na kuwaona wajinga au wapumbavu, lakini ki-uhalisia, kujiua sio ujinga au upumbavu, bali ni matokeo (mara nyingi) ya maradhi ya akili. Hawa waliojiua leo ni watu waliokuwa wamekabidhiwa silaha, kwa hiyo, bila ushahidi wa wazi, lakini kwa maoni ya awali ya kitaalamu yanayohitaji kufanyiwa uchunguzi zaidi, naweza sema, serikali imekabidhi silaha za moto kwa watu ambao baadhi yao ni wagonjwa wa akili. Na hili la askari kujiua leo, linaonesha 'taswira pacha' ya vitendo vinavyofanywa na jeshi la polisi dhidi ya raia.

Kujiua.
Kwa mujibu wa shirika la afya ulimwenguni (WHO) watu milioni moja hujiua kila mwaka. Njia kuu ya kujua, kwa wanaume ni kutumia silaha za moto, ambayo ufanisi wake ni asilimia 99. Wanawake hutumia zaidi sumu.
Njia ya pili kwa kutumika ni pombe pamoja na sumu/dawa. Njia ya tatu ni kujirusha kutoka juu ya nyumba/ghorofa, au daraja au mwamba.

Njia zingine maarufu ni kujinyonga na kujitoboa eneo lenye mrija mkubwa wa damu, kama shingoni au kiganjani. Njia ningine zinazotumika kwa kiasi ni kujinyima hewa kwa kujifunga husoni mfuko wa plastiki, kuvuta hewa ya Carbon monoxide, au Nitrogen Dioxide, au Helium nk.

Hata hivyo, njia hizo za kujiua hutegemea na mtu, kazi au elimu, jinsia na tamaduni. Kwa mfano, ni rahisi kwa askari kujiua kwa silaha kuliko kujitumbukiza mtoni. Mlevi ataamua kujiua kwa kunywa pombe nyingi badala ya kujirusha kutoka ghorofani. Daktari au mtaalamu mwengine wa afya atatumia vidonge au sindano ya sumu badala ya risasi, Watoto na vijana au watu wengine wasio walevi, wasiomiliki silaha na wasio na utaalam mkubwa wa mambo, hutumia zaidi njia ya kujinyonga, au kujichoma na vifaa vyenye ncha kama kisu.

Njia hizo za kujiua hutegemea pia vihatarishi vya nyongeza. Kwa mfano, askari mwenye maradhi ya akili yanayomtuma kuua au kujiua, kihatarishi chake cha nyongeza (additional risk factor) ni silaha aliyobeba mkononi au iliyopo nyumbani.

Huyu anaweza akapata wazo la kujiua akiwa likizo lakini akashindwa kujiua kwa kukosa silaha, isipokuwa akirudi kazini akakabidhiwa silaha anaweza kujiua mara moja. Hata kitendo cha kumiliki silaha, hata kama sio askari, ni kihatarishi cha nyongeza cha kujiua au kuua.
Daktari mwenye maradhi ya akili anayetamani kujiua, kihatarishi chake cha nyongeza ni utaalamu wake unaompa ufahsmu wa njia ya kufa haraka bila maumivu.

Sababu zinazopelekea kuwa na maradhi ya akili pia hutoa mueleekeo wa mgonjwa kuamua au kutoamua kujiua. Migogoro ya mahusiano inatajwa kuwa namba moja kwa kusababisha maradhi ya akili yanayopelekea kujiua. Sababu zingine ni pamoja na maradhi ya mwili ya muda mrefu kama kansa, au maradhi mengine yanayomfanya mtu ajione si mwenye thamani duniani, na hivyo kupelekea mfadhaiko mkubwa/Sonona unaoweza kusababisha kujiua.

Sababu ingine ni ugumu wa maisha, ingawa hiyo mara nyingi huwa ni nyongeza ya sababu zingine. Mtu anaweza kuwa na maradhi ya akili yasioonekana wazi, lakini kwa sababu ya maradhi hayo akashindwa kufanya shuguli za kujikimu. Kushindwa kujikimu kunakuwa sababu ya nyongeza na kuzidisha zaidi tatizo lake.

Matumizi ya dawa za kulevya, matumizi mabaya ya pombe na vilevi vingine, pia ni sababu zinazoweza kupelekea maradhi ya akili ambayo yatapelekea kujiua.

Hata hivyo sio mara zote kwamba kujiua ni ishara ya maradhi ya akili, wala si kila maradhi ya akili yatapelekea kujiua.

Wakati mwingine kujiua huonwa kuwa tendo la ushujaa, na hapo kuna mdahalo. Kwa mfano, katika nchi zilizoendelea kiviwanda, wawanaume wanaojiua hufikiriwa kwamba wamefanya tendo gumu la kishujaa, wakati katika maeneo mengine kujiua huchukuliwa kuwa ni tendo la watu dhaifu walioshindwa kukabiliana na hisia zao wenyewe. Katika kabila la Aguarana nchini Peru, kujiua ni kitendo cha 'kike'.

Pengine, sababu zinazopelekea kujiua ndio jambo muhimu zaidi inalofaa kutafsiri tendo hilo, kama ni udhaifu au ushujaa. Samurai wa Japan (zamani) hujiua baada ya kushindwa katika mapigano dhidi ya adui. Mbinu ya kujiua ni kuchana tumbo kwa kisu na kuruhusu ogani za tumboni zitoke nje na kufa.

Njia hiyo huitwa Seppuku, na ilikuwa rasmi kwa Samurai tu kwa ajili ya heshima yake na familia anayoiacha. Njia nyingine kama kujinyonga na kujizamisha majini zilikuwa kwa ajili ya raia wengine. Samurai aliyejinyonga au kuywa sumu au njia yoyote tofauti na Seppuku, alipoteza heshima yake na heshima ya familia yake. Hakuna mtu mwingine aliyeruhusiwa kujiua kwa njia ya Seppuku zaidi ya Samurai. Je! Kwa muktadha huo wa jamii za Samurai hapo kale, kujiua ni matokeo ya maradhi ya akili? Au jamii nzima ilikuwa inaugua?

Katika Tasnia ya kijasusi, ndani ya majeshi na vikundi vyake maalum, wakati wa vita au misheni zenye sura ya kivita, wahusika hutumia 'Suicide Pill' au kidonge cha kujiua, mara nyingi sumu aina ya Cyanide, Kwa ajili ya kujiondolea uhai wanapokamatwa na kutakiwa kutoa siri. Ingawa kuna mafunzo maalum ya kuvumilia mateso makali bila kutoboa siri, lakini Suicide hurahisisha utunzaji wa siri, na kutoa tafsiri ya ushujaa kwa mateka anayeaamua kujimaliza ili kulinda siri za nchi/kundi lake.

Kujiua kwa sababu za kimahusiano;
Fikiria kwamba umezaliwa katika familia ya kawaida na wazazi wako walikupenda sana. Wazazi walikufundisha mema na mabaya na kukueleza kwamba ukiishi kwa wema utakuwa na furaha sana. Na kwamba furaha ndio jambo muhimu kuliko yote katika maisha. Wazazi na walezi walikwambia, ukiwa mtu mwema unastahili heshima na amani ya nafsi. Walikwambia wewe ni mtu maalum kuliko wengine kwa sababu una tabia nzuri na una akili darasani.

Lakini hukufundishwa kwamba maisha ni maradhi pia, na kwa hiyo hukujiandaa kwa mambo hasi. Ulipewa kanuni za kufuata ukaamini kwamba ukifuata kanuni hizo, hutashindwa, hutakosa amani.

Naam! Pamoja na mambo mengine mengi, lakini mtu aliyeishi utoto wake akielekezwa kwa namna hiyo, ni kama aliandaliwa kujiua. Na matendo mengi ya utu uzima yana chanzo chake tangu utotoni, kabla ya miaka saba.

Migogoro ya mahusiano ndio sababu kubwa (kwa ujumla) inayopelekea maradhi ya akili yanayosababisha kujiua. Wakati mwingine migogoro inaweza kuwa ni kiharakishi, au sababu ya nyongeza.

Tafiti zinaonesha kuwa pamoja na changamoto nyingi za wanandoa, lakini wanaojiua wengi ni watu walio nje ya ndoa. Pia, pamoja na kwamba kifo kinauma kuliko kuachwa, lakini wanaojiua wengi ni wale walioachana na wapenzi kuliko waliofiwa na wenza wao. Maelezo ya hili ni kwamba, kifo kinapokelewa (accepted) kwa haraka na mfiwa anakubaliana na hali hiyo ya asili kwa kuwa hana la kufanya. Pia hisia za kufiwa huwa ni za huzuni zaidi kuliko hasira, wakati kutengana na mwenza huleta hasira na aibu zaidi kuliko huzuni. Vyote, hasira na huzuni huweza kupelekea kujiua lakini hasira ina nguvu zaidi.

Pia, watu wengi wanaojiua kwa sababu ya kutengana na wapenzi wao, mara nyingi wamewahi kuonesha dalili za kufanya hivyo kabla ya kufanya kweli. Ingawa kwa lugha rahisi unaweza kusema walipenda sana, lakini kwa lugha sahihi ni kwamba 'waliugua sana'.
Wapo pia wanaojiua bila kuonesha dalili yoyote.

Pia, idadi kubwa zaidi ya wanaojiua Kwa sababu za kimahusiano ni watu waliokuwa na kanuni madhubuti katika maisha (perfectionist), watu ambao waliogopa sana kukosea mambo.

Aidha, kujiua kunaweza kusababishwa na mgogoro wa mahusiano pekee, isipokuwa kuua mtu mwingine mara nyingi kuna sababu zaidi ya mgogoro wa mahusiano. Maana yake ni kuwa, mtu anaweza kuepuka kabisa kujiua ikiwa hatakuwa na mgogoro wa mahusiano, lakini anayeua kwa sababu ya mahusiano anaweza pia kuua mtu yuleyule au mtu mwingine kwa sababu zingine.

Zuia kujiua.
Unaweza kuokoa maisha ya mtu, na sio lazima uwe naye katika mahusiano. Sio lazima umkubalie. Katika saikolojia ya mahusiano, ikiwa moyo wako kweli umemuangukia mtu, basi jambo zuri ni kuonesha kupenda kuliko kutamka. Lakini kama moyo wako hauna nafasi kwa ajili yake, ni vizuri zaidi kutamka kuliko kuonesha kwa vitendo.

Ukishaingia kwenye mgogoro wa kimahusiano na Mweza wako akatishia kujiua, usipuuzie. Hata kama hana nia hiyo, lakini kitendo cha kutamka hivyo ni kwamba amefikia. Pengine anatishia, lakini maumivu atakayopata baadae mtakapotengana yanaweza kubadili vitisho kuwa uhalisia. Na moja ya vihatarishi vikubwa cha kujiua ni lile wazo au jaribio la kujiua.

Pia, haina maana kuendelea kuwa na mahusiano na mtu usiyempenda eti kisa ametishia kujiua, au ana dalili hizo, lakini sababu za kibinadamu ni bora kuchukua hatua. Kuwashirikisha watu wake wa karibu, ndugu na ikibidi wataalam wa saikolojia.

Jambo moja la kuvutia ni kwamba, watu wenye ujuzi wa mambo ya saikolojia (wakufunzi na watu wa kawaida waliofundishwa mambo hayo, huwa na kinga fulani dhidi ya athari za kisaikolojia zinazoweza kutokea.

Mathalani, mtu anayefahamu dalili za maradhi ya akili, ni vigumu kupata maradhi ya akili kulinganisha na asiyejua dalili hizo. Kwa hiyo moja ya msaada kwa mtu anayeonesha dalili za maradhi haya, kama kufikiria kujiua au kuua, lugha chafu kila wakati, vitendo visivyo vya kawaida vinavyotishia uhai au afya ya yake na watu wengine, ni vema akapata darasa la saikolojia, endapo hajachelewa. (Muda mzuri wa kujifunza haya ni kabla ya hizo dalili).

Nitoe rai, kwa serikali na wadau wengine kuangalia namna ya kuwasaidia watumishi wa jeshi la polisi. Kuna shida kubwa kwenye vyombo hivi "adhimu".

Tukumbuke takwimu za kitaifa zilizooneshwa mtaanzania mmoja kuwa na dalili za maradhi ya akili kwa kila watanzania wanne. Tukumbuke pia, Tanzania ni moja ya nchi ambazo watu wake hawana furaha.

Hizo ni taarifa tulizopuuza na/au kuzijadili kimasihara badala ya kuchukua hatua stahiki. Tatizo la nguvu za kiume, linakuwa kubwa pengine kwa sababu ya maradhi ya akili (sababu nyingi za upungufu wa nguvu za kiume ni sababu za kisaikolojia).

Tunaweza kuokoa maisha ya wengi na kuboresha afya za wengi kama tutachukua hatua leo!

53745904-suicide-headshot.jpg
 
mada nzuri na imeeleweka.
ipo haja hii iwe kama topic ya lazima kwenye General studies kwa A Level.
ukielimisha watu wachache nao wataelimisha wa karibu yao na jamii kwa ujumlq
 
Ni kweli kabisa mtoa mada, haya mambo huwa yananzia kwenye ubongo wa mwanadamu, tatizo jamii hupingana na na ukweli kwakutaka uthibitisho wa kuona kwa macho ya kawaida while kiuhalisia watu wameathiriwa sana na magonjwa ya kisaikolojia kuliko kawaida, ila ukielezea watu wanajenga mtazamo kuwa unawadharau kwa kuwaeleza kuwa wana matatizo ya kisaikolojia na tafsiri yao huwa "Akili zangu hazipo sawa kwan me chizi?? "

Bado elimu itahitajika kuhusu haya mambo kuliko elimu ya darasani aisee
 
Back
Top Bottom