Safari za EAC zaipaisha ATCL

elivina shambuni

JF-Expert Member
May 31, 2018
461
295
d497e61bd9942d2b0fa4f875c6a51c72.jpg

KAMPUNI ya Ndege ya Tanzania (ATCL) imesema safari zake kwa nchi za Afrika Mashariki kutoka Dar es Salaam kwenda Bujumbura, Burundi na Entebbe, Uganda, zimepata mafanikio kwa asilimia mia moja. Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi katika mahojiano na mwandishi wa gazeti hili. Alisema kuwa nafasi walizotenga kwa ajili ya nchi hizo mbili zilijaa. Safari ya Bujumbura Matindi alisema safari ya kuelekea Bujumbura kutoka Dar es Salaam inapitia katika Mkoa wa Kigoma na kurudi Dar es Salaam kupitia Kigoma.

Alisema kutokana na mahitaji ya soko la Burundi, ATCL imetenga nafasi 20 hadi kufika mjini Bujumbura. Alisema tathmini ya mwanzo ya safari hizo, imeonesha ATCL kufanikiwa kwa asilimia mia moja kutokana na kutimia na wakati mwingine kuongezeka kwa siti zinazofika Bujumbura. Matindi aliongeza kuwa viti 20 ambavyo vilipangwa kwa ajili ya Bujumbura, kwa sasa vinaonekana kuwa ni vichache, kwa sababu ya kuongezeka kwa uhitaji wa huduma katika nchi hiyo .
Safari ya Entebbe Safari hii inaanzia Dar es Salaam kwenda Entebbe kupitia Mkoa wa Kilimanjaro na kurudi Dar es Salaam kupitia Kilimanjaro. Aliweka wazi kuwa nafasi zilizotengwa kwa ajili ya Entebbe ni 20 kama ilivyo kwa Bujumbura, lakini zinaongezeka kulingana na mahitaji. Wakati mwingine huongezeka kutokana na kuwepo kwa soko kubwa nchini Uganda, ikilinganishwa na Burundi. Alisema ATCL imepata mafanikio makubwa katika kipindi hiki cha awali kutokana na nafasi zilizotengwa kwa ajili ya Entebbe kufanikiwa kwa asilimia mia moja.

Kutokana na mafanikio hayo, ATCL itaendelea kuongeza nafasi zingine kulingana na kukua kwa soko lake katika nchi hizo za Afrika Mashariki, hasa baada ya kuwasili kwa ndege zake za Airbus A220. Sababu ya kupitia Kigoma, K’njaro Alipoulizwa kwa nini safari za kuelekea katika nchi hizo sio za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam na badala yake zikapitia katika mikoa ya Kigoma na Kilimanjaro, Matindi alisema sababu kubwa ni uhitaji mkubwa uliopo katika mikoa hiyo wakati soko likiendelea kukua. Alisema wakati soko la Entebbe na Bujumbura linaendelea kukua, yameongezeka mahitaji makubwa katika mikoa ya Kilimanjaro kuelekea Entebbe kutoka Dar es Salaam; na Kigoma kuelekea Bujumbura kutokea Dar es Salaam. Matindi alisema mikoa yote hiyo, imeonesha mafanikio makubwa kutokana na soko linavyokua katika nchi za Uganda na Burundi.

Hali hiyo inaifanya ATCL kufikiria namna ya kuongeza huduma kutokana na mahitaji yanavyokua. ATCL kujitanua zaidi Baada ya kupata mafanikio katika kipindi hiki cha mwanzo wa safari za nje ya nchi, Matindi alisema ATCL inaangalia namna ya kutanua wigo wa soko lake kutoka katika nchi za Afrika Mashariki na kuenea hadi katika nchi za kusini mwa Afrika na bara la Asia. “Tayari tumeshajiwekea mpango mkakati wa miaka mitano ambao unaonesha jinsi kampuni itakavyofanya biashara na vituo tutakavyokwenda,” alisema Matindi. Alisema kwa nchi za nje, mkakati wa ATCL ni kuingia katika miji ya Johannesburg nchini Afrika Kusini, Lusaka nchini Zambia na Harare nchini Zimbabwe katika nchi za kusini mwa Afrika, Mumbai nchini India na Guangzhou nchini China katika Bara la Asia.

Matindi alisema kwa safari katika nchi za kusini mwa Afrika, ATCL itatumia ndege zake za Airbus A220 ambazo zinatarajia kufika nchini Novemba mwaka huu, tofauti na ilivyotangazwa awali kuwa zitakuja ndege za Bombardier CS300. Kutoka Bombardier hadi Airbus Mkurugenzi huyo wa ATCL alilieleza Habari- Leo kuwa awali mipango ilikuwa ni kununua ndege za Kampuni ya Bombardier CS300, ambazo ndizo zilitegemewa kufanya safari za kanda, mfano Afrika Mashariki na kusini mwa Afrika.
Alisema programu ya CS ilikuwa ni ya Bombardier, lakini kutokana na hali ya biashara ilivyo ambayo ni kuuza na kununua, Boeing wamenunua programu ya CS, hivyo ndege za Bombardier CS 300 wamezibadilisha na kuziita Airbus A220. “Ni ndege ile ile kilichobadilishwa ni umiliki kutoka kwa Bombardier (CS 300) na kumilikiwa na Boeing ambapo zimebadilishwa jina na kuwa Airbus A220 lakini ndege ni ile ile,” aliongeza Matindi.

“Sisi kwetu ni kama fahari kwa sababu hii ni ndege nzuri yenye uhitaji katika soko la sasa. Airbus walikuwa wanashindana sana na Boeing kwa ndege za aina hiyo, kwa hiyo uzuri wa hiyo ndege ndiyo uliosababisha waichukue ili kushindana na Airbus kwa ndege za sampuli hii,” alifafanua Matindi. Dreamliner Wakati ndege za Airbus A220 zikitegemewa kuwasili nchini mwishoni mwa mwaka huu na kutoa huduma katika masoko ya masafa ya kati, ndege kubwa ya Dreamliner itafanya safari zote za masafa marefu. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, ndege hii pamoja na nyingine inayotarajiwa kuwasili nchini Oktoba 2019, zitafanya masafa marefu hasa katika miji ya Guangzhou nchini China na Mumbai nchini India.
 
Back
Top Bottom