Rwanda ya damu imeleta Mahakama ya Kimbari

Rwanda ya damu imeleta Mahakama ya Kimbari

Kashishi

JF-Expert Member
Joined
Apr 11, 2010
Posts
1,147
Reaction score
641
NASAHA ZA MIHANGWA

Rwanda ya damu imeleta Mahakama ya Kimbari

mihangwa.jpg


Joseph Mihangwa

Toleo la 321 16 Oct 2013

MIEZI kadhaa iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, alichokoza hasira ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame; alipojaribu kumpa ushauri mzuri, wa kukaa meza moja na wahasimu wake wa Kihutu, ili kumaliza umwagaji damu nchini humo.

Ushauri huu makini ndiyo silaha pekee iletayo amani duniani; kuupuuza ni “ufashisti”. Lakini kwa Jenerali Kagame, uhasama kati ya Watutsi [yeye ni Mtutsi] na Wahutu ni wa kuzaliwa uliomo ndani ya damu, hata zama hizi za dunia ya kistaarabu. Nini chimbuko la uhasama huu usiofutika unaomfanya Kagame asisikilize mawaidha ya wenye busara juu ya jambo hili? Na kwa nini Watutsi na Wahutu wameshindwa kubadilika kwenda na dunia iliyostaarabika?

Oktoba 15, 1959, kikundi cha “wanamgambo” wa kabila la Kitutsi, kilimvizia na kumpiga na kumjeruhi vibaya, Mtemi wa Kihutu na ambaye pia alikuwa mwanaharakati wa kisiasa, kama njia ya kulipiza kisasi katika hali ya uhusiano uliokuwa umeingia dosari kati ya makabila hayo mawili.

Siku iliyofuata, kwa kile kilichokuja kufahamika baadaye kama “Upepo wa Maangamizi” [Wind of destruction], makundi ya Wahutu wazururaji yenye ghadhabu, yalijikusanya na kufanya ghasia kwa kushambulia watawala/viongozi wa Kitutsi, yakachoma nyumba na kupora mali za Watutsi.

Katika tuko hilo, Watutsi kwa mamia waliuawa; na wengine wanaokadiriwa kufikia 130,000 kukimbilia katika nchi za Kongo, Burundi, Uganda na Tanganyika. Hayo ndiyo yalikuwa mauaji ya kwanza ya kimbari nchini Rwanda, na chanzo cha uhasama unaoendelea hadi leo.

Uhasama kati ya Watutsi na Wahutu nchini Rwanda, ni wa aina ya ukatili unaochafua historia ya ustaarabu wa Mwafrika, ambao, kama tutakavyoona katika makala haya, ulianzishwa na Wamisionari na Wakoloni wa Kizungu, ambao ndio hao hao leo, wameanzisha Mahakama ya Mauaji ya kimbari [mjini Arusha], katika harakati za kutaka kuzuia na kuficha aibu waliyoianzisha. Wazungu wanaingiaje katika mgogoro huu?

Falme za kale za Rwanda na Burundi, ambazo kabla ya ukoloni zilichukua nafasi kubwa eneo la Maziwa Makuu; baadaye zilitawaliwa kwa pamoja na Wabelgiji [baada ya Wajerumani] kama koloni lililojulikana kama “Rwanda - Burundi”.

Falme zote mbili zilikaliwa na makabila ya Wahutu, ambao ndio walikuwa wengi; na Watutsi ambao walikuwa wachache kwa idadi, ikilinganishwa na Wahutu; uwiano ambao umeendelea hadi sasa. Makabila haya yenye kuzungumza lugha moja, mila na desturi moja, yaliishi kwa amani na kwa pamoja katika maeneo ya milima ya falme hizo.

Katika kipindi kabla ya Ukoloni, kabila la Watutsi, ambao walikuwa wafugaji wasiozidi asilimia 15 ya Wakazi wa falme hizo mbili, lilijitambua kama tabaka la kikabaila na la kitawala, dhidi ya Wahutu ambao kwa asili walikuwa wakulima.

Kwa hali hiyo, Wahutu walitakiwa kujitoa nguvu kutumikia watawala wa Kitutsi; wakati Watutsi walisamehewa. Kwa ujumla, ubaguzi kati ya Watutsi na Wahutu, ulikuwa mtindo wa maisha ya kila siku.

Chini ya utawala wa kikoloni, kwa kuanzia na Wajerumani, kisha Wabelgiji; zilitolewa tafsiri tata juu ya watu hawa. Mnamo miaka ya 1900, Wajerumani, waliwachukulia Wahutu na Watutsi kama makabila mawili tofauti.

Na kutokana na idadi ndogo ya Maafisa wao katika koloni hilo, Wajerumani waliegemea zaidi upande wa Watutsi kama wasaidizi wa watawala [Waungwana], wakawakabidhi jukumu la kuwasimamia Wahutu, na hivyo kujikweza juu yao. Miaka ya 1920, Wabelgiji walikwenda mbali zaidi, kwa kuanzisha Vitambulisho kuonyesha kabila la kila mtu. Kwa wale ambao kabila au asili yao ilikuwa ya kutiliwa shaka, kipimo cha umiliki wa mifugo kilitumika; kwamba, mwenye ng’ombe kati ya 7-10, aliwekwa katika kundi la kabila la Watutsi, na wale wenye chini ya hapo, walihesabiwa Wahutu.

Kwa vigezo hivyo vya Vitambulisho, ilikuwa sasa vigumu kwa Mhutu kuhesabiwa Mtutsi, wala Mhutu kuwa na haki sawa na Mtutsi ya kushika madaraka na uongozi katika jamii ya Rwanda.

Wabelgiji walianzisha urasimu uliowapendelea Watutsi katika elimu, na hasa Kanisa Katoliki ambalo halikuficha nia na azima yake ya makusudi ya kuwainua zaidi Watutsi juu ya wenzao Wahutu. Askofu Mkazi wa kanisa hilo wa enzi hizo, Muadhama [Monsignor] Leone Classe, ambaye mwaka 1907 alifika Rwanda kama kasisi wa kawaida tu, alihesabiwa kama Mshauri mkuu wa kutegemewa nchini Rwanda na Serikali ya Ubelgiji. Kwa hiyo, pale Kanisa Katoliki lilipopewa mamlaka yote ya kusimamia elimu nchini miaka ya 1930, Serikali na Kanisa waliungana katika mchakato mzima wa kuwainua Watutsi juu zaidi.

Chini ya mpango huo wa kibaguzi, Watutsi walipewa nafasi nzuri ya kwanza katika elimu; wakaajiriwa kama “Wanyapara”, wasimamizi wa Vibarua wa Kihutu. Vivyo hivyo, Machifu wa Kitutsi walipewa jukumu la kusimamia amani, utulivu na nidhamu.
Kufikia mwaka 1930, Wabelgiji walikuwa wameridhia na kutekeleza sera ya ukabila kuwa ndiyo tafsiri na mwongozo wa maisha nchini Rwanda na Burundi; umoja wa falme hizi mbili, uliokuwapo hapo nyuma uliyoyoma, ukanyauka na kufa; na badala yake uhasama ukatawala.

Kupigwa kwa Mtemi na mwanaharakati huyo wa siasa wa Kihutu na wanamgambo wa Kitutsi, Novemba 15, 1959, kulitokana na mwanaharakati huyo kuendeleza mapambano ya Wahutu ya kupigania haki dhidi ya unyanyasaji waliokuwa wakitendewa na Watutsi, walipewa nguvu na Watawala wa Kikoloni.

Itikadi iliyojengeka ni kwamba, Watutsi walivamia Rwanda enzi za kabla ya Ukoloni na kuwafanya Wahutu watumwa wao. Itikadi hii ilijengwa na kupewa nguvu na Wasafiri wa Kizungu karne ya 19, kwa kuwaelezea Watutsi kama kabila la uzao wa Ki-hamiti [Hamitic], lenye utamaduni bora kuliko wa Wahutu, lililoingia Rwanda kutokea nchi za milima ya Uhabeshi; na wakati mwingine walidhaniwa ni wa uzao wa Mfalme Sulemani wa Kibiblia, kwa Malkia wa Sheba.

Kwa Wakatoliki, na kwa mujibu wa mwanahistoria, Jean - Pierre Chrestsen, katika kitabu chake “Mission in Rwanda”, itikadi hii iligeuzwa kuwa injili ya historia ya kikabila, na kuingizwa katika vitabu vya historia ili iweze kusomwa na wote.

Itikadi hii potofu ndiyo iliyozua harakati za ukombozi za Kihutu, kwa kuanza na viapo kwa kuzingatia Tamko [Manifesto] la “BaHutu” la kikundi cha Wasomi tisa wa Kihutu, waliofuzu masomo yao kwenye Seminari za Kanisa, kupinga mfumo wote wa utawala na kiuchumi nchini Rwanda. Kilichopingwa zaidi na wasomi hao kwa nguvu zote ni kuhodhiwa kwa mfumo wa siasa na uchumi na kabila moja - Watutsi; huku wakitaka juhudi za makusudi zifanywe kuwainua Wahutu.

Kufuatia Tamko hilo, Serikali ya Kibelgiji ilikubali kufuta vitambulisho vilivyotofautisha Wahutu na Watutsi, hatua iliyopingwa vikali na wanaharakati hao, wakitaka vibakie kuonyesha uwingi wa Wahutu, kuwa ndio ukweli wenyewe ili kuhalalisha dhana ya utawala wa wengi - Wahutu. Kuanzia hapo, vyama vya siasa vilianzishwa kwa misingi ya ukabila, huku Wahutu wakipga Kampeni kufutwa kwa “ufalme” na umwinyi wa Kitutsi na kuanzishwa kwa Jamhuri.

Hiyo ndiyo ilikuwa sababu mojawapo ya kitendo cha kupigwa na kuumizwa vibaya na kikundi cha Wanamgambo wa Kitutsi, kwa Mtemi na mwanaharakati huyo wa Kihutu, Oktoba 15, 1959, kilichofungua mlango kwa mauaji ya kwanza ya kimbari nchini Rwanda, kama tulivyoeleza hapo mwanzo.

Kwa matukio haya ya kutia hofu na wasi wasi kwa Wabelgiji, Serikali ya Ubelgiji iliamua kubadili mambo. Kanali Guy Logiest, Afisa wa Jeshi wa Kibelgiji, aliyeteuliwa na nchi yake kusimamia Rwanda kama “Msimamizi Mkazi maalum”, aliamua “kuzima na kufuta kabisa kiburi, majisifu na ufedhuli wa Kitutsi, kwa kuwaumbua kwa ukandamizaji na uonevu wao dhidi ya Wahutu”.

Kwa hiyo, mapema mwaka 1960, Kanali Logiest, aliwafukuza Machifu wa Kitutsi na kuteua Wahutu kuchukua nafasi zao. Na kama ilivyotarajiwa na wengi, mara Machifu hao wapya walipochukua utawala, walianzisha mateso kwa kuwaadhibu Watutsi katika Wilaya walizoongoza kwa hasira za kale, nao wakakimbilia Kongo, Burundi, Uganda na Tanganyika kwa maelfu.

Katika tukio moja, kwa mfano, wanasiasa 20 mashuhuri wa Kitutsi walizingirwa wakauawa sawia; Redio Kigali iliongeza propaganda kwamba “Magaidi wa Kitutsi walikuwa wakijikusanya kurejesha utawala wao”; Viongozi wa jadi wa Kihutu waliagizwa kuanzisha vikundi vya ulinzi vya kujihami hivi kwamba, wanamgambo wa Kihutu huko Gikongoro, waliua kila Mtutsi aliyeonekana; 5,000 waliuawa.

Huko Shigira, mpakani mwa Kongo na Rwanda, zaidi ya Watutsi 100 walijitupa mtoni wakafa kuliko kukamatwa na kuteswa na Wahutu; zaidi ya Watutsi 10,000 waliuawa.
Pamoja na mateso hayo, Watutsi, katika kambi zao za Wakimbizi, waliendeleza mipango ya kuunda vikundi vya “Waasi”, maarufu kwa jina la “Inyenza” kwa Kinyarwanda, au “Mende” [Cockroach], kwa lengo la kurejesha himaya ya utawala wao.

Katika chaguzi za Serikali za Mitaa zilizofanyika Juni na Julai, 1960 katikati ya ghasia zilizoendelea, Chama cha Wahutu cha “Hutu parti du Mouvement de Emancipation Hutu - Parmetu, kilishinda viti 2,390 vya Halmashauri kati ya viti 3,125, na hivyo Wahutu wakashika hatamu karibu kila Wilaya.

Kwa matokeo hayo utawala wa Kibelgiji, kwa “kula njama” na viongozi wa Kihutu, uliongoza kile kilichoitwa “mapinduzi halali” dhidi ya “kiburi, majivuno na ufidhuli wa Kitutsi”, kama moja ya Programu za utawala wa Kanali Guy Logiest.

Msumari wa moto na wa mwisho ulipigiliwa kichwani mwa jamii ya Watutsi, wakati Mameya [Bourgmestres] na Madiwani wapya waliochaguliwa, walipoitwa kukutana katika mji wa Gitarama, Januari 1961, mahali alipozaliwa kiongozi wa Wahutu, Gregory Kayibanda, ambako kwa kauli moja, walitangaza kukomeshwa kwa “ufalme” wa kihimaya wa Watutsi, na kuanzishwa kwa Jamhuri, na kufuatiwa na uchaguzi wa Wabunge, Septemba 1961, uliothibitisha “ukuu” wa Wahutu.

Kufikia hapo, mstakabali wa kisiasa nchini Rwanda ulianza kuchukua mkondo tete, kiasi kwamba Tume ya Udhamini ya Umoja wa Mataifa, katika Taarifa yake ya 1961, ilionya na kutahadharisha kwa maneno yafuatayo: “Matukio ya miezi 18 iliyopita, yameleta udikteta wa kibaguzi wa Chama kimoja madarakani …. Mfumo wa kikandamizaji [wa Watutsi] uliopita, umerithiwa na mfumo mwingine [wa Wahutu] wa kikandamizaji. Inawezekana kabisa kwamba, siku moja tutashududia machafuko ya kulipa kisasi kwa upande wa Watutsi”.

Rwanda ilipata uhuru Julai 1, 1962, chini ya Serikali ya ki-Jamhuri, ikiongozwa na Gregoire Kayibanda, mwanasiasa mwenye uchungu wa haki na maslahi ya Wahutu, na ambaye aliapa toka mwanzo, kuhakikisha kuwa Watutsi wanachukua nafasi ya chini katika jamii ya Kinyarwanda.

Utabiri wa Tume ya Umoja wa Mataifa haukuchukua muda kutimia, wakati hapo Desemba 1963, kikundi cha Watutsi wapatao 200 wenye silaha za pinde, mishale na bunduki zilizotengenezwa kienyeji, kilipovuka mpaka kutoka Burundi na kujiunga na Watutsi wa ndani ya nchi, na kushambulia kambi ya Jeshi na kupora silaha na magari; kisha kikaelekea mji Mkuu wa Rwanda, Kigali, kujaribu kupindua Serikali madarakani.

Ingawa waliweza kusambaratishwa na majeshi ya Kayibanda bila kuleta madhara makubwa, lakini jaribio hilo lilikuwa ni ishara tosha kwa machfuko yasiyokoma na yanayoendelea kuikumba hadi sasa Rwanda kwa misingi ya uhasama wa jadi.

Mwaka 1973, Kayibanda alipinduliwa na Mkuu wa Jeshi, Jenerali Juvenal Habyarimana, akatupwa gerezani alikofia kwa njaa. Habyarimana alianzisha utawala wa kidikteta wa Chama kimoja cha “Mouvement Revolutionnaire National pour le development” [MRND], ambapo kila raia alilazimishwa kujiunga; na kwa kila mtu kuwa na kitambulisho kuonyesha kabila lake na anakoishi.

Chini ya Habyarimana, Watutsi waliendelea kupata kadhia ile ile ya kubaguliwa kama mwanzo, ingawa hawakuteswa au kunyanyaswa kama huko nyuma.
Habyarimana, Mhutu, mzaliwa wa Rwanda Kaskazini, Wilaya ya Gisenyi, yeye akiwa mgombea pekee katika chaguzi zote, alipita kila mara kwa ushindi wa kishindo usiopungua asilimia 98 ya kura. Lakini kila mara ilipokuja kuunda Serikali, Watutsi walipewa nafasi moja ya Uwaziri, moja ya Balozi, mbili za Ubunge [wa kuteuliwa] katika Bunge la viti 70, na Wajumbe wawili kwenye Kamati Kuu ya Chama chake cha MRND.

Na katika Jeshi, ilikuwa marufuku kwa Watutsi kushika Cheo cha “Ofisa”; Wanajeshi na Askari wa Kihutu, hawakuruhusiwa kuoa wanawake wa Kitutsi ili kutochafua “nasaba” ya Wahutu.

Mzimu wa ubaguzi wa kikabila nchini Rwanda, uliopandikizwa na Wamisionari na Wakoloni wa Kibelgiji, utaendelea kuisumbua na kuitesa nchi hiyo kwa muda mrefu, licha ya kwamba Wakoloni hao hao wamerejea kuanzisha Mahakama ya Watuhumiwa wa mauaji ya kimbari, iliyopo mjini Arusha, kujaribu kwa aibu kubwa, kudhibiti Jini ambalo wao wenyewe waliruhusu litoke ndani ya chupa. Je, Afrika imelaaniwa, kwamba haiwezi kujisimamia kwa amani, ila kwa msaada wa Wazungu?

Tufuatilie mtandaoni:

- See more at: Raia Mwema - Rwanda ya damu imeleta Mahakama ya Kimbari

Chanzo: Gazeti la RaiaMwema
 
Historia imeishia kati, imekwepa kuelezea uvamizi wa Watusi (RPF) na mauaji wa Habyarimana na Raisi wa Burundi yaliyofanywa na Watusi. Imekwepa kuongelea kulipiza kisasi kwa Watusi kwa kuua maelfu ya wakimbizi wa kihutu huko DRC. Imekwepa kuongelea mfumo wa utawala wa sasa ambao mawaziri na wabunge na viongozi wote wa jeshi ni Watusi. Imekwepa kuongelea jinsi wazungu walivyowageuka wahutu kwa kuanzisha mahakama ya kimbari inayowahukumu wao kwa upendeleo upande wa watusi (Kama tu walivyowageuka watusi kipindi cha Guy Logiest)
Je, Mihangwa ameikatisha historia kwa kuwa Raia Mwema ni Gazeti la Generali Ulimwengu ambae ni Mtusi?
 
Back
Top Bottom