Rushwa katika Elimu hushusha Ubora/Hadhi na kuondoa Hamasa ya Wanafunzi kupenda Masomo

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,377
8,120
Mkazi wa Chanika, Dar es Salaam, (Jina linahifadhiwa) anasema alipokwenda kumwandikisha Mtoto wake Kidato cha Kwanza katika Shule moja ya binafsi, aliambiwa inabidi atoe Fedha kidogo ili mtoto apate nafasi.

Mzazi huyo anasema alilazimika kutoa Fedha hizo ili tu mwanaye afanyiwe Usaili na kupata nafasi ya kujiunga na Shule hiyo. Anaongeza kuwa kilichomfanya atoe Fedha ni uzuri wa Shule na Matokeo mazuri ambayo Shule imekuwa ikipata.

Anase,a “Kwa kweli hiyo Shule ni nzuri kwa sababu inafaulisha na kila Mzazi anatamani kumpeleka hapo Mtoto ili apate Elimu bora. Sasa hata kabla mtoto hajafanya Usaili, wanakwambia kupata nafasi hapo ni nadra kwasababu zaidi ya Watoto 1000 wameomba nafasi na wanaohitajika ni 200 tu, utafanya nini zaidi ya kutoa rushwa?”

===============

Katika ripoti yake ya mwaka 2013 Shirika la Kimataifa linalopambana na ufisadi la Transparency International linaonyesha kuwa vitendo vya rushwa vimekithiri kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, sekta ya elimu ni miongoni mwa maeneo yenye vitendo vya rushwa kwa kiwango kikubwa.

Kwa mfano, ripoti inasema kuwa mwanafunzi mmoja katika kila wanafunzi sita, alilazimika kulipa rushwa ili apokee huduma fulani za elimu.

Ushuhuda

Mkazi wa Chanika, Dar es Salaam, Eunice Malya anasema alipokwenda kumwandikisha mtoto wake kidato cha kwanza katika shule moja binafsi jijini hapo, aliambiwa lazima atoe fedha kidogo ili mtoto apate nafasi.

“Kwa kweli hiyo shule ni nzuri kwa sababu inafaulisha na kila mtu anampeleka hapo mtoto ili apate elimu bora. Sasa hata kabla mtoto hajafanya usaili, wanakuambia kupata nafasi hapo ni nadra sana kwani wameomba nafasi watoto 1000 na wanaohitajika ni 200 tu, utafanya nini zaidi ya kutoa rushwa,” anasema.

Aina za rushwa katika elimu

Ukitoa rushwa katika udahili wa wanafunzi, vitendo vingine vya rushwa vinafanywa katika upangaji wa vituo vya kazi kwa walimu na upatikanaji wa nafasi za kusomea ualimu katika vyuo vya Serikali.

Kwa mfano, gazeti hili limebaini kuwa baadhi ya shule mijini zina walimu wengi zaidi wa kike ambao inasemekana huhangaika kufa na kupona kupata nafasi katika maeneo hayo, hasa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam.

Matokeo yake ni kuwa walimu wasiokuwa na chochote au wasiojua nini cha kufanya, hubaki vijijini maisha yao yote.

Rushwa hizo siyo za fedha tu, bali hata kujuana jambo linalotumika kama nyenzo ya kumwondoa mwalimu mmoja kutoka kituo cha kijijini na kumleta mjini.

Vilevile rushwa ipo katika mishahara, wapo walimu wanaonyimwa mishahara makusudi, ili watoe rushwa kwa mwalimu mkuu au ofisa elimu.

Inaelezwa kuwa, mwalimu aliyeanza ajira au ambaye aliwahi kufanya kosa lakini akarudishwa kazini, anaweza asiingiziwe mshahara kwa makusudi ili atoe rushwa, kinyume na hivyo ataendelea kusota.

Aidha, wapo walimu watoro wanaoweza kukacha vipindi hata kwa mwaka lakini wanaingiziwa mshahara. Hawa imebainika kuwa wanatoa rushwa kwa wakuu wa shule na maofisa elimu wa sekondari.

Uchunguzi wa gazeti umebaini pia hata kupata ruhusa ya kwenda masomoni huhitaji kutoa ‘kitu kidogo’. Hivyo basi walimu wasiotoa rushwa wanaweza kupewa visingizio mbalimbali ili tu wakose nafasi za masomo.

Rushwa nyingine inayochukua sura mbalimbali ikiwamo kujuana ni utoaji wa nafasi za walimu kwenda kusahihisha mitihani ya taifa.

Walimu katika shule mbalimbali wanakiri kuwa wapo wenzao ambao hawajawahi kupewa nafasi ya kusahahihisha mitihani hata mara moja tangu waajiriwe, lakini kuna wengine wanaokwenda kila mwaka.

Wanasema siyo kwenda kusahihisha mitihani tu, rushwa pia ipo katika kupata nafasi za kwenda kusimamia sensa au wakati wa kusimamia uchaguzi.

Chama cha Walimu

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Oluoch anakiri kuwepo kwa rushwa katika elimu, akisema vitendo hivyo vinaanzia ngazi za juu hasa kwa maofisa elimu na viongozi wengine wa Serikali.

Anatoa mfano wa wanafunzi wanaofeli darasa la saba kuingizwa katika orodha ya waliofaulu ili waingie sekondari.

Anasema walimu wakuu hukubali kufanya uovu huo kwa kuwa wanapata maelekezo kutoka kwa ofisa elimu au kiongozi wa juu kuwa mwanafunzi fulani lazima ajiunge na sekondari.

“Kwa mfano kuna kipindi fulani walimu 400 walihamishiwa Dar es Salaam kinyemela, lakini utumishi wakasema hawajahamisha walimu hao. Kumbe Ofisa Elimu alipewa agizo awahamishie hapa. Walimu wakati mwingine hutumiwa kama mbuzi wa kafara,” anasema

Kauli ya Oluoch imethibitishwa na baadhi ya walimu katika shule mbalimbali za sekondari za Serikali, waliokiri kupokea ujumbe mara kwa mara kutoka kwa Ofisa Elimu au Mkuu wa Wilaya wakiamriwa kumsajili shule mwanafunzi fulani.

Oluoch anasema, walimu hutumiwa kama mbuzi wa kafara kwa sababu ya udhaifu sheria zilizopo. Anasema sheria zinasema mkubwa akiagiza kitu kwa mdomo lazima utimize la sivyo unaweza kufukuzwa kazi.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco), Mahmoud Mringo anasema rushwa haijazigusa zaidi shule na vyuo binafsi, ingawa anakiri kuwepo kwa chembechembe hizo wakati wa udahili.

Anatoa mfano kuwa shule ina uwezo wa kusajili wanafunzi 400, lakini walioomba nafasi ni 8000. Katika mazingira hayo anasema inawezekana walimu wakapokea rushwa na hatimaye wakaingia wanafunzi wasio na sifa.

“Hilo linatusumbua hasa katika shule binafsi. Mwalimu huweza kupokea rushwa au kuomba ili mtoto apate nafasi,’’ anasema.

Ili kumaliza vitendo vya rushwa, Mringo anaomba jamii nzima kushiriki katika mapambano ya kutokomeza rushwa.

“Kila mtu awajibike na kazi yake, pia wazazi waache kuiga tamaduni za Magharibi za kusema mtoto asipigwe au asisemwe. Vilevile, wakuu wa shule na maofisa elimu watimize wajibu wao,” anabainisha.

MWANANCHI
 
Hata kupanda daraja kwa mwalimu lazima atoe rushwa. Unahisi huyu mwalimu atamtendea haki mwanafunzi ilhali mwenyewe kainunua hiyo haki yake kwa gharama kubwa!

Sasa hivi ni msimu wa mitihani ya taifa katika levels mbalimbali na kinachotokea vituoni kipindi hiki ni aibu maana kupata nafasi ya kwenda kusimamia lazima jasho la damu likutoke.

Pia sasa walimu wengi wanapamabana waende masomoni ila kinachotanyika sasa ni Mungu tu anajua.

Sensa ya mwaka jana imefanya walimu na Maafisa Elimu Kata/watendaji kata kuwa maadui wa kudumu hadi kesho.

Hayo yote yanaenda kumwathiri mwanafunzi moja kwa moja kitaaluma sababu mwalimu yeye hana cha kupoteza.
 
Back
Top Bottom