nameless girl
JF-Expert Member
- Apr 22, 2012
- 4,195
- 2,675
- 1
ALIKUWA mwanamke! Tena mwanamke wa haja! Alisimama pale, uso wake
ukiwa umeelekezwa kwangu; kama anayesubiri nifanye kazi yangu! Naapa kuwa, kwa mara ya
kwanza, katika maisha yangu ya udunguaji, nilisita kubonyeza tufe la mwanangu, AK 47 ambaye
nilimpenda kuliko wanangu wengine wote niliopata kuwatumia.
Alikuwa pale, kasimama, huku uso wake ukielekea kwangu mara kwa mara.
‘Ananisubiri!’ Niliwaza.
Sikujua kwa nini nilisita. Maelekezo yote niliyopewa yalikuwa barabara; atakua amevaa
suruali ya kitambaa, yenye rangi nyeusi na koti lake la rangi ile ile juu ya shati yenye rangi ya
bendera ya taifa. Atatoka nje ya mlango wa hoteli saa nne na robo, akiwa katikati ya Rais wa
Nchi kulia kwake na mgeni wake, bilionea wa viwanda na machimbo ya madini upande wa pili.
Pale mlangoni watasita kidogo kuagana kabla ya kuelekea kwenye hafla maalumu. Mwondoe
akiwa pale pale mlangoni.
Maelekezo yalikuwa sahihi. Muda ulikua uleule uliopangwa. Na zaidi ya yote mavazi,
yalikuwa yaleyale yaliolekezwa. Wala si hayo tu, mamilioni ya dau langu lililolipwa katika fedha
za kigeni tayari yalikuwa yamekwisha ingia kwenye akaunti yangu ya benki wiki moja iliyopita
na kuhamishiwa katika benki mbalimbali, kwa majina tofauti, kabla ya sehemu ya pesa hizo kuja
Dar es Salaam kwa matumizi yangu madogo madogo.
Purukushani za wapiga picha wa televisheni na magazeti zilikuwa nyingi. Kila mmoja
alikuwa akihangaikia kupata picha bora zaidi, ama ya Rais ama ya mgeni, au wote kwa pamoja.
Vichwa vyao na kamera zao zilipita mbele yao kwa namna iliyonifanya nipoteze shabaha. Lakini
hilo lisingenizuia. Walengwa wangu walikuwa juu ya wapiga picha kwa ngazi moja. Isitoshe,
mimi ni mtaalamu. Sekunde moja tu ya kutikisa kichwa ilitosha kabisa kumdungua muhanga
wangu bila tatizo.
Hata hivyo, nilisita kumtekenya mwanangu. - Kitu gani basi kilifanya nisite kumbonyeza kidogo tu mwanangu ili nimalize kazi hiyo na
kuendelea na ziara yangu ya kutembelea ziwa Tanganyika ambako nilikusudia kuwinda viboko
kijiji cha Buhingu na kisha kuwashuhudia sokwe wa milima ya Kasoge? Kitu gani kiliutia uzito
moyo wangu wa kishetani, ambao daima ulifurahia kuiona risasi yangu ikimpaisha mtu angani
na kisha kumdondosha chini huku akiwa tayari ametokwa na uhai wake? Kitu gani? Kitu gani?
Kitu ga…
Mara nikakumbuka. Zilikuwepo sababu nyingi, kubwa zikiwa mbili. Ya kwanza, ilikuwa
urahisi wa kazi hii. Katika maisha yangu haya, sijapata kazi rahisi kama hii, upewe hela nyingi
Zaidi ya ambazo ungeomba, upewe wajihi wa mtu unayetakiwa kumwondoa, siku, saa na vazi
atakalokuwa amevaa! Ilikuwa nyepesi mno. Natumaini ni wepesi huo ulionitia mchecheto kiasi
cha kunifanya nisite kufanya vitu vyangu.
Sababu ya pili, mhanga wangu alikuwa mwanamke, tena mzuri! Sijapata kumuua
msichana mzuri kama huyu wala kuombwa kumuondoa duniani mwanamke. Hili pia lilinikoroga
kichwa.
Kulikoni? Nilijiuliza. Kisha nikajikumbusha taratibu za kazi zetu. Ukishapokea malipo
yako, ukishaweka utaratibu madhubuti wa kumuondoa mhanga wako, kamwe usianze kujiuliza
maswali. Hiyo ni kazi ya polisi na wapelelezi na anayewajibika kujibu ni mteja wako, sio wewe.
Wazo hilo lilinifanya nimnyanyue tena mwanangu mpenzi, kumwelekeza kule
alikokusudiwa. Nikarekebisha lensi na kuzivuta nyuso zao kwangu. Ilikuwa imepita nusu dakika
tu toka niliposita kuibonyeza. Walikuwa wangali palepale mlangoni. Raisi alikuwa amegeuka
kusalimiana na mtu fulani. Ningeweza kumwondoa, kupitia kisogo chake kwa urahisi kabisa.
Kwa bahati, sikutumwa kufanya hilo. Yule bepari wa viwanda na madini naye alikuwa pale,
kaduwaaduwaa. Ningeweza kumwondoa kwa bei rahisi vile vile kupitia upande mmoja wa sikio.
Mhanga wangu alikuwa kama anayeendelea kunisubiri. Uso wake mzuri ukiwa
umeelekezwa kwangu na macho yake yalikuwa na dalili za wasiwasi na vitone vya jasho
jembamba katika paji lake la uso, paji ambalo nilililenga vizuri kana kwamba nipo katika
mazoezi ya shabaha. Nikamtekenya mwanangu. Sekunde moja, mbili, tatu… Mara mhanga
wangu alipaa kama futi moja angani na kisha kutua kama gunia miguuni mwa Rais, akiwa tayari
mzoga. ‘Mkono wa Jibril haujapata kukosea’ niliwaza nikicheka kimoyomoyo. - Purukushani iliyofuatia hapo haikuwa na kifani. Nilitamani sana kuitazama walao kwa
dakika mbili pindi wanausalama wakicharuka kama waliopigwa ufunguo. Wanne, waliokuwa
nyuma ya msafara huo; walichupa angani, mmoja akimpitia Rais kwa kumbo ambalo
lilimwangusha na kumlalia kama ngao huku wenzake wakiwavuta na kurejea ndani. Wakati
huohuo ving’ora vililia, polisi wakiivamia barabara na kufunga mitaa. Raia wa kawaida,
waandishi na wafanyakazi wengine walikuwa taabani zaidi, huyu akianguka pale, yule
akikimbilia kule kana kwamba wamepagawa. Sikuweza kujizuia kucheka.
Nilimwona mwanausalama mmoja akitazama huko na huko, kisha macho yake yakaelekea
upande wa pili wa mtaa, katika jengo nililokuwepo mimi na kutoa maelekezo kwa wenzake
ambao walianza kujipanga kulizingira jengo hilo.
Ulikuwa wakati wangu wa kuondoka. Nilimbusu mwanangu ambaye bado alikuwa na joto
la risasi ile moja aliyotema. Nikamfungua na kumkunja taratibu na kisha kumweka katika
briefcase yake vizuri. Juu yake nilirudishia vitu mbalimbali vya kudanganyia, ambavyo
vingemlaghai mtu yeyote ambaye angepata wazimu wa kuikagua.
Haikuwa kazi kubwa kuliacha jengo hilo. Watu wote walikuwa wameduwaa,
wakishangazwa na purukushani ambazo zilikuwa zikiendelea upande wa pili wa mtaa.
Nikaipuuza lifti na kufuata ngazi ambazo zilinitoa ghorofa ya tano na kunipeleka ya nne, ya tatu,
ya pili. Hapo nilipanda lifti hadi chini. Wakati nikitoka nje ya lifti hiyo watu wawili, waliovaa
suti waliingia harakaharaka, mikono yao ikiwa mifukoni.
Hatukutazamana usoni, lakini sikuhitaji kuambiwa kua hao walikuwa wana usalama
wakifuatilia uelekeo wa ilikotokea risasi. Nilitamani kuwapa pole. Nilitamani kuangua kicheko.
Lakini yote hayo sikuyafanya. Niliondoka zangu bila kuangalia nyuma nikihisi macho yao
yakilitazama umbo langu la nyuma hadi mlango wa lifti ulipojifunga.
Sikuwa na wasiwasi. Nilijua wasingenishuku kwa lolote. Nani anaweza kumshuku
msichana mrembo, aliyevaa nguo fupi na viatu vya mchuchumio huku nywele zake ndefu
kaziachia kama msichana wa Kihebeshi? Nani angepata muda wa kushuku wakati harufu ya
marashi aliyopaka yalitawala katika chumba cha lifti alichokiacha punde?
KWA ANAYEHITAJI VITABU VYA MTOBWA TUTAFUTAN KWA NAMBA 0763044459....
STORY HII ITAWAJIA KILA SIKU MPAKA ITAKAPOKWISHA...