Riwaya: Ulimwengu uliooza

Riwaya: Ulimwengu uliooza

Hyungnim

JF-Expert Member
Joined
Sep 25, 2016
Posts
301
Reaction score
484
Ni majira ya usiku wa manane uliotawaliwa na giza totoro ktk kila kona ya kijiji cha Matwebe kilichopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya.Ndege aina ya bundi wanaohusishwa na imani za ulozi hapa nchini waliendelea kutoa sauti kali na milio ya kuogofya vinywani mwao iliyosindikizwa na mvua kali za masika,radi na ngurumo za kutisha.


Ulikuwa ni muda ambao watu wanaojishughulisha kazi za uchawi walikuwa 'bize' wakiwanga na kuwatesa raia wanyonge.
Jamii hii ilitawaliwa sana na imani za ulozi .Watu walijitahidi kulinda maisha yao kwa kuwatembelea waganga wa jadi ambao waliwapa hirizi maalumu zilizonuizwa kwa maneno ya kiganga huku wakichanjwachanjwa sehemu za miili yao na kutiwa ungaunga mweusi ktk eneo hilo lililotiwa 'jeraha'.

Hakuna aliyependa kupoteza uhai wake kwa walozi hao ambao yasemekana waliwageuza wanyonge hao misukule wa kuwafanyia kazi ktk mashamba ya kakao na nafaka nyingine muhimu.Na ni hapo ile sera ya kutegemeana kwa viumbe ilipodhihirika.Mganga alitoa hirizi na mazindiko,mteja alitwaa nafaka,fedha kichele,kuku na wakati mwingine ng'ombe.Biashara ikashamiri.Waganga na waaguzi wakanona,wakanawiri na nusura wapasuke matumbo kwa shibe.

Waganga hao walitakata na nyuso zao zilijaa tabasamu yakini muda wote,pindi walipojilaza kitandani usingizi wa pono uliwakumbata!wakatopea ktk kisiwa cha maraha na kuwa na siha njema.Akina pangu pakavu tia mchuzi wakazidi didimia,mifugo na nafaka zao zikatokomea mikononi mwa waaguzi.

kuna nyakati mahali fulani kijijini hapo nikiwa na vijana nilipata dokezwa ya kuwa wazee wachache waliokuwa wakikamata mvua na kuizuia isinyeshe hali iliyopelekea ukosefu wa mvua na hatimaye ukame.Mahindi na mbaazi kondeni yakanyauka huku vijito vikiacha kulia.Mifugo ikadhoofu kwa kukosa lishe bora.Jambo la ajabu ni kuwa hata hao walozi waliathiriwa na ukame huo waliousababisha.

Hali ngumu ya maisha na dhiki iliyokithiri iliwasakama wananchi na kuwafanya wakose raha.Nyuso zikanyauka na kupoteza tabasamu angavu.ufukara hutwaa majonzi na chuki kuu!

Ukata huo ulizaa choyo kwa makabwela hao.Kila mtu aliangalia kusalimika mwa nafsi yake tu.Mafundisho adhimu ya ujamaa yaliyosisitiza upendp yaliyeyuka mithili ya mshumaa uwakao uteketeavyo.

UCHOYO uliingia kwenye mishipa ya binadamu,ukasafiri hadi kwenye moyo,ukazikamata fahamu za watu na kutuama ubongoni.Mapafu yalitoa hewa ya chuki iliyofunikwa na adui choyo.

Hata ulipotimu wasaa wa kupata pochopocho lililopatikana kutokana na juhudi za wazee,watoto wasiohusika waliondolewa pasi huruma.
"nenda nyumbani toto Hamimu eeh.uje baadaye".Hapo mtoto aliondoka akiwa ktk sononeko kuu akijua kaenguliwa kijanja kwenye ulaji.Ukarimu ulifukiwa ardhini.

Waliokuwa na miguu imara na nguvu walisafiri kwingineko ktk vijiji vya mbali na kutwaa bidhaa kadha wa kadha ambazo waliziuza kwa bei ya juu .Mfumo wa ubepari taratibu ukamea na kukita mizizi kijijini.Maskini alimnyonya fukara mwenzie na kujirundikia faida.kiumbe mwenye nguvu na imara ataishi na kudumu lakini aliye dhaifu atapotea na kufa kabisa alinena Charles Darwin.

Soga zilizidi nijuza kuwa wale ambao hawakuzingatia mpango madhubuti wa wizara ya afya kuhusu uzazi wa mpango walitia huruma nyakati hizo.kulea watoto 12 halikuwa jambo la kufurahia.Hizi ndizo athari za urijali ambapo wanaume wanapaswa kupata somo.

itaendelea
 
Well done nimekuelewa mkuu....hii ni wanaofikiri sawa sawa
 
Back
Top Bottom