Riwaya:Seven day in hell 2

Riwaya:Seven day in hell 2

gyeetitus

Member
Joined
Dec 16, 2016
Posts
86
Reaction score
39
SEVEN DAY IN HELL -2
ILIBIDI nisogee mpaka kwenye maegesho ya bodaboda nikiamini
pale itakuwa rahisi kuzungumza na dereva yeyote ili aniwahishe
kabla ile ‘ambulance’ haijapotea kabisa. Nilipopiga hatua moja,
nilijiona kuwa mwepesi sana halafu tambo lilikuwa refu sana tofauti
na kawaida.
Sehemu ambayo ningetembea hata hatua ishirini, nilipiga hatua
mbili tu, nikawa nimeshafika pale kwenye bodaboda.
SASA ENDELEA…
“OYA mambo vipi mkubwa!” nilimsalimu dereva wa bodaboda
aliyekuwa pembeni yangu kwa bashasha kubwa lakini hakuniitikia,
akawa anaendelea kuifutafuta bodaboda yake.
Nilirudia kumsalimu lakini bado hakunijibu chochote na wala
hakuonyesha kama ananisikia. Nilimgusa begani lakini bado ilikuwa
ni kazi bure, aliendelea kufutafuta bodaboda yake, nikabaki
nimepigwa na butwaa.
Ilibidi nimsogelee dereva mwingine wa bodaboda, naye
nikamsalimia kwa bashasha lakini hakunijibu, nikarudia tena na tena
lakini bado hali ilikuwa ileile, nikaenda kwa watatu ambaye alikuwa
akipiga stori na wenzake, naye akaonyesha kutonisikia.
“Kwani imekuwaje? Mbona sielewi kinachoendelea?” nilijisemea
huku nikianza kutetemeka kwa hofu kubwa, mwisho niliamua
kufanya jambo moja, nilipaza sauti kwa nguvu nikiita ‘bodabodaaa!’
niliamini yeyote ambaye atakuwa wa kwanza kuniona basi
nitamchukua huyohuyo lakini wapi! Kila mmoja aliendelea na
mambo yake.
Ni hapo ndipo nilipogundua kwamba huenda nilikuwa sionekani kwa
macho ya kawaida wala sauti yangu haisikiki licha ya ukweli
kwamba mwenyewe nilikuwa najisikia vizuri tu.
“Sasa nitafanyaje?” nilisema huku nikigeuka kuitazama ile
‘ambulance’, tayari ilishapotea kwenye upeo wa macho yangu lakini
akili zangu zilinituma kuamini kwamba lazima itakuwa imeupeleka
mwili wangu Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Nataka nikashuhudie kila kitu kinachoendelea,” nilisema huku
nikianza kutafuta mbinu nyingine ya kunifikisha hospitalini hapo.
Sijui nilipata wapi akili hizo lakini nilijikuta tu nikiamua kuanza
kutimua mbio kuelekea kule ile ambulance ilikoelekea.
Nilipopiga hatua chache tu, nilijikuta nikiwa napaa angani kwa kasi
kubwa, nikawa naitazama mitaa ya jiji kutokea angani. Kuna wakati
akili zangu zilinituma kuamini kabisa kwamba nilikuwa kwenye
ndoto ya kutisha ambayo muda wowote itaisha lakini akili nyingine
zikawa zinaniambia kwamba siyo ndoto, kila kitu kilikuwa kikitokea
kwa uhalisia.
Wakati ambulance ikiwasili kwenye geti kuu la kuingilia Muhimbili,
na mimi tayari nilikuwa nimeshafika eneo hilo, geti likafunguliwa na
likaingia moja kwa moja mpaka kwenye eneo la ‘emergency’ ambalo
wagonjwa wenye hali mbaya ndipo walipokuwa wanafikia.
Milango ya ambulance ilifunguliwa, manesi waliokuwa ndani ya ile
ambulance pamoja na wengine waliokuwa pale mapokezi,
walisaidiana kuushusha mwili wangu na kukimbizwa mpaka ndani,
nikawa nashuhudia kila kitu kilichokuwa kinaendelea.
Harakaharaka nilianza kupewa huduma ya kwanza, nikamuona nesi
mmoja akichukua mkasi na kukata shati nililokuwa nimevaa,
nilipoliona jeraha lililokuwa kifuani wangu, nilisisimka mno.
Nilijiuliza iweje mtu anifanyie ukatili mkubwa kiasi hicho, tena bila
sababu ya msingi?
Japokuwa vitabu vya dini vinakataza kulipa kisasi, nilijikuta
nikipandwa na ari kubwa ya kulipa kisasi, nilikuwa nimejeruhiwa
sana. Niliwaona hata wale manesi akitetemeka kila walipokuwa
wanalitazama jeraha langu.
Kwa bahati nzuri, madaktari wa kiume waliingia, huwa naamini siku
zote kwamba sisi wanaume Mungu ametuumba na ujasiri mkubwa
kuliko wanawake. Wakaanza kunifanyia kile ambacho
kitaalamu huwa kinaitwa ‘dressing’, yaani kusafisha jeraha kabla ya
kuanza kutibiwa. Muda mfupi baadaye, tayari nilikuwa
nimesafishwa jeraha hilo, nikahamishwa na kupelekwa chumba cha
wagonjwa mahututi nikiwa bado sijitambui huku madaktari na
manesi wakiendelea kuhangaika kudhibiti damu zilizokuwa
zinaendelea kunitoka kwa wingi.
Nilipoingizwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi,
harakaharaka niliunganishwa kwenye mashine ya kunisaidia
kupumua huku dripu ikitiririka kwa kasi kuingia kwenye mishipa
yangu.
“He has lost a great deal of blood, he need an urgent
transfusion,” (Amepoteza damu nyingi sana, anahitaji kuongezewa
damu haraka iwezekanavyo) alisema daktari mmoja kwa Kiingereza,
kwa kuwa na mimi shule ilikuwepo kiasi chake kichwani,
nilimuelewa vizuri.
Niendelee kusisitiza kwamba wakati haya yote yakitokea, katika
ulimwengu wa kawaida sikuwa na fahamu hata kidogo, nilikuwa
nimefumba macho na kulala pale kitandani kama maiti, nikiwa
nimeunganishwa na mashine ya kunisaidia kupumua lakini katika
ulimwengu mwingine ambao hata sijui niuiteje, nilikuwa
nimesimama kwenye pembe moja ya ile wodi, nikishuhudia kila
kilichokuwa kinaendelea.
Kazi ya kuokoa maisha yangu iliendelea, madaktari na manesi
wakawa wanapishana huku na kule, huyu kabeba dawa, huyu
kabeba chupa ya damu, huyu mikasi na sindano, ilimradi kila mmoja
alikuwa bize.
Nilijisikia ahueni kubwa ndani ya moyo wangu kuona watu ambao
pengine hata hawakuwa wakinijua, wakipigana kuokoa maisha
yangu. Niliendelea kuwatazama wanavyohangaika, kuna wakati
machozi ya uchungu yalikuwa yakinitoka kwa sababu ya
kilichotokea, nikawa naendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa
majibu.
Nilivuta kumbukumbu ya jinsi mambo yote yalivyoanza kutokea.
***
Januari 16, 2012
Mikocheni, Dar es Salaam.
“Haloo!”
“Haloo, nani mwenzangu.”
“Mh! Kwani namba yangu hujaisevu Moses, mbona una visa wewe.”
“Samahani, utakuwa umekosea namba, mimi siitwi Moses wala
sikufahamu.”
“Ooh! Basi samahani kaka yangu nitakuwa nimechanganya namba.
Samahani sana.”
“Usijali, kuwa makini,” yalikuwa ni mazungumzo kati yangu na mtu
aliyepiga simu na kunifananisha.
Nilikata simu na kubonyeza kitufe kwenye rimoti ya runinga yangu
kubwa (flat screen) niliyokuwa nimekata sauti (mute) baada ya
kuona simu yangu inaita. Nikawa naendelea kutazama muvi kwani
miongoni mwa vitu nilivyokuwa navipenda, ilikuwa ni kutazama
muvi, kuangalia mpira na kusikiliza muziki, hasa muda ninaokuwa
nyumbani baada ya kutoka kazini.
Haukupita muda mrefu, simu yangu ikawa inaita tena, nilikasirika
kwa sababu muvi ilikuwa imefika sehemu nzuri na sikutaka inipite
hata sehemu moja, safari hii nilibonyeza kitufe cha ‘pause’
kuisimamisha ili isiendelee, nilipotazama namba ya mpigaji, ilikuwa
ni ileile ya yule mtu aliyedai kukosea namba.
“Samahani mpendwa najua nakusumbua, nimeangalia vizuri simu
yangu na kugundua kuwa ni kweli nilikosea namba wakati
nakupigia.”
“Usijali dada, tufanye yameisha.”
“Ahsante kwa kunisamehe kaka yangu, japo sikujui lakini
unaonekana mstaarabu sana. Mimi naitwa Shenaiza sijui
mwenzangu unaitwa nani.”
“Naitwa Jamal au kwa kifupi Jay,” nilimjibu kwa kifupi kwa sababu
niliona kama ananiletea stori zisizo na kichwa wala miguu.
“Ooh! Nimefurahi kukufahamu kaka Jamal. Unaishi wapi vile?”
“Mikocheni,” nilimjibu na safari hii niliamua kubonyeza tena rimoti,
muvi ikaendelea kwani niliona hana chochote cha maana cha
kuniambia, nikawa nimeiweka simu sikioni huku nikiendelea
kuangalia muvi.
“Mbona kuna kelele kwani uko wapi?” alihoji msichana huyo lakini
sikumjibu chochote, naona baadaye alijishtukia mwenyewe,
akaamua kukata simu. Nikaiweka simu pembeni na kuendelea
kutazama muvi.
Baadaye ilipoisha, nilichukua simu yangu na kugundua kuwa
kulikuwa na meseji nyingi zimeingia bila mwenyewe kushtukia,
nikaanza kuzisoma moja baada ya nyingine.
Nilishangaa kugundua kwamba ukiachilia mbali meseji mbili za rafiki
zangu, Justice na Prosper, nyingine zote zilikuwa zimetoka kwa yule
msichana aliyekosea namba ya simu, nikashusha pumzi ndefu na
kuanza kuzisoma, moja baada ya nyingine nikiwa
na shauku kubwa ya kutaka kuona ameandika nini.
Je, nini kitafuatia?
 
Back
Top Bottom