Riwaya: Senyenge

SEHEMU YA ISHIRINI
Dokta McBannerman alikuwa bado ameweka mgomo kutoa taarifa binafsi za wateja wake. Kwahivyo alitoa anuani ya Bwana na Bibi Hobie, lakini namba zao za simu alizing’ang’ania. Jodie hakuona kama kuna utofauti. Hakuendelea kuuliza maswali. Alishikana naye mikono ya kwaheri na kutoka nje huku Reacher akimfuata kwa nyuma.

“Hali sio nzuri,” Jodie alisema. “Umewaona wale wagonjwa waliokuwa pale mapokezi?”

“Ndiyo,” Reacher alijibu. “Nusu watu nusu wafu.”

“Baba alikuwa kwenye hiyo hali pia dakika za mwishomwisho. Halafu walikuwa wanafuatilia nini hiki ambacho kimempa mtu hasira hadi anaanza kuua watu hovyo?”

Reacher hakujibu. Waliingia kwenye Bravada yao, Jodie akikaa kiti cha abiria na Reacher akikaa nyuma ya usukani. Jodie alipiga simu kuomba taarifa. Aliambiwa namba za simu za familia ya Mzee Hobie ambaya makazi yake yalikuwa kaskazini mwa Garrison. Aliandika zile namba kwenye karatasi aliyokuwa amechana kutoka kwenye notebook yake. Alipokata simu akaziandika na kupiga. Simu ililia kwa muda kidogo kabla upande wa pili haujabonyeza kitufe cha kupokea halafu sauti ya mwanamke ikasikika.

“Abee?” Sauti ilisema.

“Mrs. Hobie?” Jodie aliuliza

“Ndiyo?” Sauti ilijibu tena. Jodie akaanza kuwaza muonekano wa Mrs. Hobie – Mwanamke mzee mwenye mvi kichwani, mwembamba na pengine amevaa nguo zinazoonekana kumvaa zilizochoka huku akiwa kashika mkonga wa simu ya kizamani kwenye sebule ya nyumba ambayo imechoka pia.

“Mrs. Hobie, ninaitwa Jodie Garbar. Ni binti yake na Leon Garbar.”

“Ndiyo?”

“Amefariki siku tano zilizopita.”

“Ndiyo, ninafahamu.” Mrs. Hobie alisema na kuongeza, “Nimesikitishwa sana na hiyo taarifa. Baba yako alikuwa anatusaidia na alikuwa mtu mzuri sana. Sijui kwanini watu wazuri wanawahi kufa. Pole sana.”

“Nashukuru,” Jodie alijibu. “Lakini sijui kama unaweza kuniambia alikuwa anawasaidia jambo gani?”

“Kwa sasa hakuna umuhimu hata nikikuambia.”

“Kwanini?”

“Kwa sababu baba yako amekwishafariki,” Mrs. Hobie alisema. “Yeye ndiye alikuwa tumaini letu la mwisho.”

Kila neno alilosema lilikuwa limemaanishwa. Sauti yake ilikuwa ya chini. Kulikuwa na mchanganyiko wa hisia za kukata tamaa mwisho wa sentensi yake, kama mtu aliyeamua liwalo na liwe sitaki tena. Jodie akaiona tena picha ya Mrs. Hobie kichwani mwake. Mwanamke mzee – mifupa bila nyama na mashavu yaliyolowa kwa machozi yaliyokuwa yanadondoka kutoka machoni.

“Pengine ninaweza kukusaidia.” Jodie alisema.

Ukimya ukapita kabla sauti ya Mrs. Hobie haijarudi tena kwenye spika za simu. “Sidhani,” Alisema. “Sidhani kama hili ni tatizo linaloweza kushughulikiwa na mwanasheria.”

“Ni tatizo la aina gani?”

“Sidhani kama kuna umuhimu wa kuliongelea tena,” Mrs. Hobie alisema.

“Hauwezi kuniambia hata kidogo tu?”

“Hapana. Nadhani kila kitu kimeshaisha.” Mrs. Hobie alisema. Sauti yake ilikuwa bado ni ya mtu aliyekata tamaa.

Ukimya ulipita kidogo. Jodie akageuza macho na kuangalia jengo la ofisi ya Dokta Mcbannerman.

“Lakini baba yangu angeweza vipi kukusaidia? Ni kwa sababu alikuwa analijua tatizo lako? Au ni kwa sababu alikuwa jeshini?”

“Ndiyo. Na ndiyo maana nahofia hauwezi kunisaidia kwa vyovyote. Inahitaji mtu wa jeshini. Hata hivyo asante kwa kujali.”

“Huyo mtu yupo,” Jodie alisema. “Na nipo naye hapa. Alikuwa anafanya kazi na baba yangu jeshini na yupo tayari kuwasaidia.”

Ukimya ukapita tena kwenye simu. Kulikuwa na muungurumo wa spika unaotengenezwa na mgongano wa mawimbi kama simu nyingi zinavyosikika watu wawili wakiwa wanaongea halafu wakae kimya. Ni kama Mrs. Hobie alikuwa anafikiria. Akubali au abadilishe mada.

“Jina lake ni Reacher,” Jodie alisema. “Pengine baba aliwahi kulitaja hilo jina? Na baba ndiye aliyemtafuta awasaidie.”

“Alimtafuta?”

“Ndiyo. Nadhani alikuwa na uhakika huyu Reacher angewasaidia.”

“Huyo mtu alikuwa ni Polisi Jeshini?”

“Ndiyo. Kwani kama alikuwa mwanajeshi wa kawaida kuna tatizo?”

“Sina hakika,” Mrs. Hobie alisema. Halafu akanyamaza. Alikuwa anahema kwa nguvu. “Anaweza kuja nyumbani?” Aliuliza hatimaye.

“Nitakuja naye,” Jodie alimwambia. “Tunaweza kuja sasa hivi?”

Ukimya tena. Kuhema. Kutafakari.

“Mume wangu amemaliza kumeza vidonge muda sio mrefu na sasa hivi amelala. Hali yake sio nzuri.”

Jodie alitikisa kichwa kukubali. “Mrs. Hobie kwani wewe hauwezi kutuambia walikuwa wanafuatilia nini?”

Ukimya tena. Kuhema. Kutafakari.

“Nitamwachia mume wangu awaambie. Nadhani maelekezo yake yamenyooka tofauti na ya kwangu. Ni hadithi ndefu kidogo.”

“OK, atakuwa ameamka saa ngapi?” Jodie aliuliza. “Au tuje baadae?”

Ukimya mwingine.

“Huwa analala sana baada ya kumeza vidonge vyake, Mwambie Rafiki yako aje kesho asubuhi.”



HOBIE ALITUMIA NCHA ya chuma lake kubonyeza kitufe cha simu yake ya mezani. Aliinama kwa mbele na kumuita yule mwanaume wa mapokezi kwa jina lake. Hii haikuwa tabia yake isipokuwa kama alikuwa na jambo linalomsumbua kichwa chake.

“Tony,” Alisema. “Tunahitaji kuongea.”

Tony alikuja na kukaa kwenye sofa lililokuwa karibu kabisa na meza ya Hobie.

“Aliyeenda Hawaii ni Garber,” Tony alisema.

“Una uhakika?” Hobie aliuliza.

Tony alitikisa kichwa kukubali. “Alipanda ndege ya American hadi Chicago na kutoka Chicago hadi Honolulu. Halafu akarudi kesho yake, Aprili kumi na sita. Alilipa kwa Amex na taarifa zote hizo zipo kwenye kompyuta zao.”

“Lakini huko alienda kufanya nini?” Hobie aliuliza.

“Hatuna uhakika.” Tony alinong’ona. “Lakini tunaweza kubashiri.”

Ukimya ukapita. Tony akayakaza macho yake kwenye uso wa Hobie upande ambao haukuwa umeliwa na lile kovu kubwa.

“Nimesikia pia fununu kutoka Hanoi,” Hobie alisema.

“Mungu wangu, lini?”

“Dakika kumi zilizopita.”

“Mungu wangu, Hanoi,” Tony alisema. “Shit, shit, shit.”

“Miaka thelathini,” Hobie alisema. “Na hatimaye mwisho umefika.”

Tony hakujibu. Baadala yake alisimama akaenda kusimama kwenye dirisha na kufungua pazia. Nje kulikuwa na jua kali ambalo liliingiza mwanga kiasi mule ndani.

“Unatakiwa kuondoka sasa hivi. Mambo yamekwishakuwa mabaya.”

Hobie hakujibu. Alikuwa analipapasa chuma lake kwa vidole vyake vya mkono wa kushoto.

“Uliniahidi,” Tony alisema. “Onyo la kwanza, Onyo la pili utaondoka na onyo zote tayari zimekuja.”

“Bado itawachukua muda,” Hobie alisema. “Kwa sasa hivi hawawezi kufanya chochote.”

Tony alitikisa kichwa kukataa. “Garbar hakuwa mwehu. Lazima kuna kitu alikuwa anafahamu. Na kama alienda hadi Hawaii lazima kuna sababu nzuri iliyokuwa imempeleka huko.”

Hobie aliutumia mkono wake wa kushoto kuliongoza chuma lake la kulia hadi lilipotua juu ya uso wake. Alianza kulikandamiza kovu lake huku akisuguasugua sehemu ya kovu lake kupunguza mwasho.

“Na huyu Reacher?” Aliuliza. “Kuna Habari gani?”

“Nilipiga simu St. Louis,” Tony alisema. “Naambiwa alikuwa polisi wa wanajeshi pia. Alihudumu na Garbar kwa muda wa miaka kumi na tatu. Na wote walikuwa wamewasiliana na Costello.”

“Kwanini?” Hobie aliuliza na kujijibu, “Familia ya Garbar iliwasiliana na Costello kumtafuta Reacher. Kwanini? Kwanini?”

“Sina uhakika,” Tony alijibu. “Ninachojua alikuwa huko Keys akichimba mabwawa ya kuogelea.”

“Polisi wa wanajeshi mchimba mabwawa?”

“Usijiulize maswali,” Tony alisema. “Unatakiwa kuondoka.”

“Hakuna kitengo sikipendi kama polisi wa wanajeshi,” Hobie alisema.

“Ninafahamu hilo.”

“Kwahivyo huyo mjinga anafanya nini huku?”

“Usijiulize sana. Unatakiwa kuondoka.” Tony alisisitiza kwa mara ya tatu.

Hobie alitikisa kichwa kukubali. “Nadhani unanijua mimi ni mtu wa kubadilika kuendana na mazingira.”

Tony aliachia pazia. Chumba kikaingiwa tena na giza. “Sijasema ubadilike. Nimesema ukae kwenye mpango tulikuwa tumepanga.”

“Mpango upo palepale, lakini siwezi kuondoka kabla sijamalizana na Stone.”

Tony alirudi kukaa kwenye sofa lake lilelile. “Ninafahamu, lakini ni hatari sana kuendelea kubakia. Maonyo yote mawili yametokea. Moja Veitnam na linguine Hawaii. Ondoka.”

“Ni kweli, lakini mipango huwa inabadilishwa kidogo.”

“Kivipi?”

Hobie aliguna na kutikisa kichwa chake. “Tutaondoka ndiyo, lakini ni baada ya kumalizana na Stone.”

Tony aliguna na kuinua mikono yake kama anayeuliza kitu. “Wiki sita ni muda mrefu sana. Garbar alikuwa amekwishaenda Hawaii na alikuwa mmoja wa majenerali. Lazima kuna kitu atakuwa anafahamu.”

Hobie alitikisa kichwa kukubali, “Unachokisema ni kweli. Lakini huyohuyo Garbar aliugua na akafa na hivyo vitu alivyokuwa anavijua vilienda naye huko kuzimu.”

“Unajaribu kusema nini?”

Hobie alilishusha chuma lake chini na kuliweka mezani. Akakigusa kidevu chake kwa vidole vya mkono wake mzuri. Aliviacha vidole visambae kwenye kovu lake. Lilikuwa ni pozi alilolitumia , bila kujua, kila mara alipotaka kuongelea mpango muhimu.

“Siwezi kuondoka na kumuacha Stone,” Alianza kueleza. “Nikimuacha hicho kitendo kitanifanya nijute hadi siku ambayo nitaingia kaburini. Kukimbia, nakubaliana na wewe, ni jambo zuri. Lakini bado ni mapema kiasi kwamba tukikimbia sasa hivi tutakuwa ni waoga, Tony.”

“Sijakuelewa bado. Unataka kusema nini?”

“Tunatakiwa kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Ni kweli wiki sita ni muda mrefu na tunatakiwa kuondoka kabla ya hizo wiki sita, lakini sio kabla hatujamalizana na Stone. Ndiyo maana inatakiwa tuharakishe mambo tufanye kila kitu harakaharaka.”

“Ok, Kivipi?”

“Ninaingiza hisa za Stone sokoni leo, sasa hivi.” Hobie alianza kueleza tena. “Haitachukua muda thamani yake itakuwa chini sana na mabenki yatashtuka. Kesho asubuhi Stone atakuja hapa jasho likiwa linamtoka. Mimi sitakuwepo. Kwahivyo wewe utamwambia sisi tunataka nini, na tutakipata vipi, na tutafanya nini kama asipotoa ushirikiano. Niamini mimi. Atatupa kila kitu chake ndani ya siku chache tu. Tutauza kila kitu halafu tunaondoka.”

“Ok, kivipi. Bado sijaelewa.”

Hobie aligeuza kichwa kuangalia kona za kwenye kile chumba.

“Wale wanaume mikia wawili hawatakuwa ni tatizo. Mmoja wao anamuua mwenzake usiku wa leo, na atakayebaki utashirikiana naye hadi tumpate Mrs. Jacob, ambapo wewe utawafuta wote. Tutauza boti, tutauza nyumba zote, tutaondoka, bila kuacha nyayo. Inaweza ikachukua wiki. Wiki moja tu. Nadhani tunaweza tukajipa wiki moja tu, sio?”

Tonny alitikisa kichwa kukubali. “Na vipi kuhusu Reacher?”

Hobie alitikisa kichwa pia, “Nina mpango tofauti kwaajili yake.”

“Hatuwezi kumpata,” Tony alisema. “Sisi tukiwa wawili tu hatuwezi kumpata ndani ya wiki moja.”

“Hakuna haja ya kumtafuta.”

Tony alitumbua macho. “Tusipompata tunaacha nyao.”

Hobie alitikisa kichwa chake. Halafu akaushusha mkono wake kutoka usoni. “Nitamshughulikia kwa makini sana. Hakuna haja ya kumaliza nguvu zangu kumtafuta. Nitamuacha anitafute. Ninajua atanitafuta na atanipata. Ni kawaida ya polisi wa wanajeshi.”

“Halafu nini.?”

Hobie alitabasamu. “Halafu ataishi maisha marefu na ya furaha,” Hobie alisema. “Pengine miaka thelathini tena.”
 
Sema port hii kitu ni habar nyingine, sema tu hapo kutenganisha tukio na tukio kwa kutumia hizi ***** ili mtiririko ueleweke kirahisi
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom