RIWAYA: Ripoti kamili

mzaramo

JF-Expert Member
Sep 4, 2006
6,371
5,183
IMEANDIKWA NA: George Iron Mosenya

SEHEMU YA 1

Nimejifunza mengi katika maisha yangu, nimejifunza kuliweka wazi sikio langu kumsikiliza kila mtu iwe anazungumza upuuzi ama anajenga hoja chanya na madhubuti!!
Lakini yote juu ya yote, nafanya hivi lakini naweka maanani kitu kimoja tu. Ninakuruhusuni kunieleza lolote mnaloweza, ninakuruhusuni kunishauri lolote mnaloona linafaa kunishauri lakini aidha kuxchukua ushauri wenu na kuufanyia kazi hii inabaki juu yangu mimi na akili zangu!!!
Sio kila mtakalosema nitalifanyia kazi...
Hakuna gharama yoyote katika kusikiliza ila kuna gharama katika kufanyia kazi hayo uliyoyasikiliza.

HII NI SEHEMU YA KWANZA.....

KUNA Nyakati ambazo huwa najiuliza hawa wanawake ni viumbe dhaifu kupita vyote duniani ama ni viumbe majasiri kulikoni vyote??
Nikifikiria uchungu wanaopitia katika kutubeba katika matumbo yao na kisha kutuzaa napiga goti na kuwavulia kofia ya heshima lakini kuna mengine lukuki nikiyafikiria najikuta kichwa kinaniuma sana.
Ningeweza kuyasema nusunusu tena kwa mifano isokuwa hai lakini hii inaweza kupelekea nawe ukakosa neno sahihi la kunieleza, basi kwa misingi hiyo ninaileta kwenu ripoti kamili.
Kwa majina naitwa Mjuni Kalisti.
Nilizaliwa miaka thelathini na mbili iliyopita, sikubahatika kupata elimu kubwa sana lakini najua kusoma na kuandika na leo hii ninakuandikia wewe haya nikiwa na akili zangu timamu.
MAPENZI..... Mapenzi... mapenzi..... bila mapenzi nisingekuwa na cha kukuandikia leo.
Siwalaumu wazazi wangu, bwana na bibi Kalisti kwa sababu walikuwa na uwezo wa kunichagulia msichana wa kuja kuwa mke wangu lakini kwa hekima zao na kuepuka lawama zozote zile iwapo mambo yataniharibikia walinibariki kwa mikono yao miwili tena bila mimi kuwalazimisha wakampokea Tina binti ambaye kwangu mimi niliona ni mwanamke sahihi wa kumuoa na kisha anizalie watoto.
Nakumbuka mama aliniuliza kitu kimoja tu.
“Mjuni... umepata muda wa kumsoma mwenzako??”
Sikumbuki kama niliwahi kumjibu badala yake nilitabasamu tu.
Ndio, nilitabasamu kwa sababu nilitambua kuwa mama hajui lolote kuhusiana na Tina. Yule alikuwa ni binti wa aina yake kwangu, kwanza alinikuta nikiwa ninatabia ya kuvuta sigara, tabia ambayo hata wazazi wangu walikuwa hawaijui kwa sababu nilikuwa navuta kwa kujifichaficha sana, Tina aliniweka katika mapaja yake akinipapasa kichwa changu huku akinisihi kuachana na mambo yasiyokuwa na manufaa katika mwili wangu zaidi ya hasara tupu.
Nilijitetea na kumueleza kuwa sigara inanisaidia sana kuchangamka hasahasa mtu akinikwaza na pia wakati wa baridi inanifaa kunipasha mwili wangu joto.
Tina akatabasamu na kisha akanieleza kuwa sasa amejitokeza yeye na atakuwa sigara yangu, watu wakiniletea makwazo atanilaza katika kifua chake na kuniliwaza na pakiwa na baridi atanipa joto nibnalotaka.
Ilianza kama utani na hatimaye nikaachana na sigara hadi leo hii ninapokuandikia ripoti hii sivuti sigara.
Alinikuta nikiwa kijana mkubwa tu lakini suala la usafi likiwa limenipita kando, hakuniambia kwa maneno lakini alianza kuninunulia nguo za ndani na kuziandika majina, moja ikiandikwa jumatatu nyingine inaandikwa jumanne, hivyohivyo kwa siku zote saba za juma.
Na hapa akaniambia kuwa akinikuta nimevaa nguo ya ndani iliyoandikwa jumanne siku ya ijkumaa tunagombana.
Kwa sababu nilikuwa nimemzoea sikutaka kumkosa, nikawa nabadilisha kila siku......
Kwa njia ile akawa amenifunza usafi...
Looh!! Tina, nikijitazama nilivyo na kasumba ya usafi kwa sasa namkumbuka sana. Na ninapatwa na mchanganyikio wa hisia.......

Naam! Mazoea yakajenga tabia, nikawa siwezi tena kuwa mbali na Tina, hapo hata marafiki wakapungua kwa sababu sikuwa nashinda tena vijiweni kama ilivyokuwa awali. Muda wa vijiweni nitakuwa mahali na Tina.
Hakuwa mtoto wa kitajiri bali maisha ya kawaida kama ilivyokuwa kwangu tu.
Kule kujifichaficha kukatuchosha na hatimaye nikavunja ukimya nikamweleza nia yangu ya kuoana naye, Tina hakupinga akanipokea kwa mikono yake miwili.
Ikawa uchumba, hatimaye ikawa ndoa ya kiasili. Nikakabidhiwa Tina wangu, wazazi wa pande zote mbili pamoja na ndugu na jamaa waliotoa zawadi zao hatimaye nikayaanza maisha yangu na Tina.

Isikie ndoa kwa masikio yako na usipuuzie kujifunza kwa wale waliopitia maisha haya, iwe ndoa halali ya kanisani ama msikitini ama ndoa ya kiserikali ama kimila. Cha msingi kuishi na mwanamke kama ubavu wako.
Na ninakusihi sana ripoti hii usiipuuzie.
Maisha yalikuwa ya kupendeza sana, chumba chetu kimoja pamoja na sebule vilitutosha sana. Nikafanya kazi kwa bidii na Tina naye akawa anafanya kazi zake, tukahama katika maisha yale na kuhamia katika nyumba kubwa kiasi, vyumba viwili pamoja na sebule.
Ukiwa na vyumba viwili na sebule jiandae kupata wageni, maana chumba cha kulala kipo. Ujue mgeni akija na kuishia kulazwa sebuleni, siku ya kwanza na ya pili atavumilia ila zaidi ya hapo ataona aibu na kujiondokea. Ile toa meza na makochi na kutandika godoro chini inakera japokuwa kuna ndugu na marafiki mshipa wa aibu hawana wao bora liende tu.
Ilikuwa hivyo na kwetu baada ya kuwa na vyumba viwili, ndugu wema walianza kututembelea na kulala palepale.
Walianza ndugu zangu, mara ndugu wa Tina mke wangu, wanakuja na kuondoka, hii ilikuwa inapendeza sana.
Kati ya ndugu wa Tina ambao nilikuwa sipendi sanaujio wao pale nyumbani kwangu ni dada yake mkubwa kwa mama mwingine lakini baba mmoja, alikuwa anaitwa Stela. Huyu nilimchukia kuanzia kipindi kile nipo katika harakati za kumsaka kimapenzi Tina, dada huyu alikuwa akinisema waziwazi kuwa mimi ni mchafu, mara anitolee kashfa kuwa sina hadhi ya kuwa na dada yake. Na alinifanyia haya kwa sababu tu yeye mwenzangu alikuwa amesoma kiasi fulani alikuwa na diploma sijui hata ya mambo gani lakini ndo hivyo kiingereza cha kunitukana mjinga kama mimi alikuwanacho na alikitumia ipasavyo.
Lakini kwa sababu sikuwa najua kama ni matusi na kejeli ni sawasawa alikuwa anajitukana mwenyewe tu na kiingereza chake.
Ajabu sasa yeye mwenzangu akayasahau yote aliyokuwa akinifanyia, maisha yakaendelea.
Ninachioshukuru alikuwa akija nyumbani kwangu mara moja na kama akilala ni usiku mmoja tu kesho yake anaondoka.
Hii ilikuwa ahueni sana kwangu. Sipendi kabisa kuishi na wanafiki!!!
Mwaka wa kwanza ukakatika nikaketi na mke wangu na kumueleza kuwa sasa tutafute mtoto, kwa sababu maisha kwa kiasi fulani hayakuwa mabaya kwa kuongeza familia.
Tina mke wangu alikuwa msikivu na muelewa sana, kama akilipinga jambo atapinga kiakili na kama ni la haki wala hakawii kukubali.
Hata hili lilikuwa la haki akakubali!!!

Lakini jambo lililokuja kuniacha kinywa wazi ni siku nne baada ya kuwa nimemueleza mke wangu juu ya azimio lile, yule dada Stela alitutembelea na kisha kwa sababu yeye anajifanya msomi na ni mkubwaq kwetu kiumri akatuweka mezani na kutueleza kuwa lipo jambo anahitaji kutushirikisha na kutushauri.
Mara akatutajia umri wake jinsui anavyotuzidi mara elimu yake namwisho akatueleza kuwa tusiharakie maisha na kutaka kupata mtoto wakati huu.
Moyo wangu ulipiga kwa kasi sana, nilipatwa na hasira, huyu Tina mke wangu anaendaje kumshirikisha dada yake mambo yangu na yeye.
Nilijipa moyo wa subira na sikusema neno lolote lile. Akaendelea kuyachambua maisha yetu kwa kina na kutueleza kuwa tujipange zaidi ili tusije kumfanya mtoto wetu aishi katika mazingira magumu.
Kwakweli sikumuelewa kabisa Shemeji yangu yule.... nilichoshauri ni kwamba atupe muda wa kulifikiria hilo.
“Sawa mtanipa jibu lenu...” alisema huku akibetua midomo yake.
Daah! Nilichoka yaani dada mtu anataka baadaye mimi na ndevu zangu nimtumie taarifa iwapo nina mpango wa kupata mtoto ama nimeusikiliza ushauri wake na sitahangaika kutafuta mtoto.
Moyo uliniuma sana na nilijiona nikiwa nimedhalilishwa nyumbani kwangu katika namna inayoweza kufananishwa na kuvuliwa nguo zangu mbele ya watoto.
Nilipanga kuzungumza na mke wangu chumbani usiku huo lakini nikajionya kuwa nyumba yetu haijazibwa kwa juu hivyo shemeji anaweza kutusikia, nikaitunza hasira yangu hadi siku inayofuata dada mtu akiondoka zake.
 
Huwa inakera sana pale mtu ambaye anakuita wewe ni rafiki kwake, hakutafuti hadi siku anapopatwa na shida tu nd’o anakumbuka uwepo wako.
Hakika hii inawakera wengi...
Lakini je? Umewahi kujiuliza juu ya mshumaa, umeme unapokatika na hauna mshumaa ndani.. unatembea mita nyingi kwenda kuutafuta ili tu ukusaidie kuleta mwanga??
Je! Unaona ni kiasi gani mshumaa ulivyo kitu cha muhimu katika shida ya mwanga??
Naam! Hivyo hivyo kwako, usijisikie vibaya mtu akija kwako wakati wa shida... wewe ni mtu muhimu sana katika kutatua shida... na usijisikie fadhaa kwa marafiki wa namna hii....

HII NI SEHEMU YA PILI.....

Niliuona usiku mrefu sana, lakini hatimaye palikucha na shemeji akaniaga akaondoka ila alinitia kichefuchefu alipokumbushia lile jambo la kumtumia taarifa tukishajadiliana.
Nilimsindikiza kwa macho, luile umbo ambalo zamani nililiona likiwa zuri kuwa kwake sasa niliona ni mfano wa dudu washa kubwa linalotembea kwa kujikunjakunja likiwa halina umbo linaloeleweka, na kichwa chake kile chenye nywele nzuri za kisasa nilikiona mfano wa mzimu. Kwa kifupi alikera kumtazama...
Tina akanivuta mkono tukaingia ndani.....
Sikutaka tufike chumbani alkini alinisihi, tulipofika akanieleza kuwa anajua wazi kuwa nimechukia mno kwa yote yaliyotokea lakini akaniomba radhi kuwa ni yeye mwenye makosa kwa kumshirikisha dada yake.
“Lakini mume wangu, sikumfikishia taarifa nilimwambia tu... jiandae kuitwa mama mkubwa!! Hivyo tu, sijui yeye hayo aliyoyaleta kayatoa wapi!!” alizungumza nami Tina huku akizikunja na kuzikunjua ndevu zangu, jamani! Tina alikuwa mwabnamke mwenye ushawishi.... na kama wewe hujawahi kupendwa ama kupenda nashindwa hata kukusimulia ni hisia gani huja pale unapojua kuwa unapendwa halafu anayekupenda anakubembembeleza hivi.
Na kama wewe unayeisoma ripoti hii upo katika ndoa, tafadhali shika usemi huu... kama macho yako yanamuona mke ama mumeo anavutia basi piga goti na umshukuru Mungu kwa sababu kuna watu wengi sana wanamuona huyo uliyenaye anavutia na wanatamani kuwa naye lakini tazama unaye wewe na anakupenda!!!
Hii ilikuwa kwangu pia, tulijadiliana na Tina na kwa pamoja tukaamua kumpuuzia dada yake na kile ambacho alikuja kutushauri. Na kisha tukakubaliana kuwa hatutaacha kumjibu kwa sababu hii itamfanya aje kutuuliza bali tutamjibu kuwa tuliamua wawili kuoana na tumeamua wawili kuwa tunataka mtoto na si wakati mwingine bali ni sasa, nia ndo hiyo tunayo na uwezo wa kumlea mtoto tunao tunachoomba ni kudra tu za mwenyezi Mungu tuwe na uwezo pia wa kumpata mtoto.
Nikamuagiza Tina alifikishe jibu lile.
Mimi nikaondoka na kwenda kazini.

Nilirejea saa mbili usiku, nikapokelewa na harufu ya maakuli, mate yakaniruka kooni kwa sababu fujo za Tina nilikuwa nazijua. Na njaa nayo ikaamka....
Nikaingia nikawakuta wakiwa wawili, dada mtu na Tina. Njaa ikakimbia...
Jamani nilikuwa simpendi yule dada yake Tina.....
Stela akasimamana kunisalimia kwa furaha akanipa pole ya kutwa nzima na kisha Tina akanipokea kifurushi changu na kukipeleka chumbani.
Jikoni akamuacha dada yake akiendeleza mapishi, akaniandalia maji ya kuoga, akanipatia na taulo halafu kama ilivyokawaida yake akanisindikiza hadi bafuni.
Mapenzi haya, acha yaitwe mapenzi na ndo maana hata hakuna anayeweza kuelezea nini maana ya mapenzi.
Huduma na ukaribu wake ukaniliwaza, akanisubiri mlangoni hadi nikamaliza kuoga tukaondoka wote akinibebea ndoo.
“Mnapendeza wenyewe looh! Wivu wanishika mie...” stella alitutania tulipompita, nikatioa tabasamu nikapita.

SAA tatu kasoro dakika kadhaa tukiwa tunakula, Stela alituomba radhi kisha akatueleza kuiwa siku ile alikuwa kidogo amelewa na kuvurugwa na mambo yake, akatuomba radhi kwa kuingilia mambo yetu ya ndani sana yasiyokuwa yanamuhusu.
Nikamweleza asijali yeye ni dada kwetu na pia kukosea tumeumbiwa wanadamu.
Akashukuru sana na kisha akaingiza utani wa hapa na pale mwishowe akasema yeye anataka mtoto wa kike, Tina akasema anataka wa kiume mimi nikasema nataka mapacha kabisa.
Tukacheka cheko moja kubwa halafu maakuli yakaendelea kushambuliwa.

Baada ya mwezi mmoja, Tina alikuwa amekamata mimba!!
Ilikuwa furaha tele sana kwetu na hata wazazi wa pande zote mbili walifurahia, walitamani kumbeba mjukuu wao.
Mimba ya Tina ikaja na madeko, nakiri kuwa kuna muda ilikuwa inakera lakini sikuwahi kumwonyesha Tina kuwa nakerwa na hali ile.
Kuna siku anagoma kulala na mimi kitandani, anataka tulale chini, siku nyingine anataka nimpikie ugali na mlenda, nikishaivisha anagoma kul;a anataka nimkaanfgie mayai na niweke chumvi nyingi.
Nikiivisha anakula kidogo anasema ameshiba!!
Ninachoshukuru ni kwamba mwajiri wangu katiika kampuni ile ya pamba alikuwa ni swahiba wangu hivyo hata siku nikichelewa kazini alikuwa ananielewa.
Tina akaendelea na visa vyake na hapa nikaanza kukutana na taarifa mbaya kutoka kwa marafiki na sasa naziunganisha katika ripoti yangu kamili.
Rafiki yangu mmoja aliwahi kunivuta kando na kunieleza kuwa eti aliwahi kumuona dada yake Tina akiingia pale nyumbani kwangu na mama mmoja aliyekuwa na gari kisha yeye akabaki ndani ya nyumba yule mama akatoka na Tina hadi garini.
Akaniuliza iwapo namjua mama huyo, nikamweleza hapana simfahamu mtu yeyote ambaye anamiliki gari na ni rafiki yangu ama ndugu wa Tina.
Yule bwana akaniambia kuwa basi huenda ni rafiki tu!! Akaniacha hivyo..
Lakini hapohapo nikakumbuka kuwa kuna siku ambayo niliwahi kukuta uwanja umefagiliwa jioni katika halui isiyokuwa ya kawaida.
Nikajiuliza inamaana sasa walifagia ili kufuta alama za matairi ya gari?? Na kama ni kweli walifuta ni kitu gani cha siri wanaficha??
Nilikosa majibu na kamwe sikumuuliza mke wangu, bali nikaandika katika kitabu changu cha siri, na leo hi nanukuu kutoka katika kitabu changu cha siri na ninakuletea wewe msikilizaji ripoti hii kamili usikilize kisha ujifunze!!!
Mimi yalinitokea lakini kwako iwe darasa huru.....
 
Iliwahi kuwa mijadala ya kawaida tu wakati wa maisha yangu kijiweni, tulikuwa tunajiuliza ni umri gani sahihi kabisa kwa mwanaume kuoa ama mwanamke kuolewa?
Kuna waliosema miaka 30, wengine wakasema ndoa haijalishi umri cha msingi umpate wa kukupenda na wewe umpende.....
Lakini kuna mmoja alisema kuwa kumpata anayekupenda na wewe ukampenda ni ngumu sana kutokea katika maisha halisi, akasema kuwa ukishampata ambaye wewe unampenda basi mfundishe na yeye kukupenda na hapo mtaenda sawa!!!

HII NI SEHEMU YA TATU.

Baada ya yale maneno ya rafiki yangu kuwa kuna mgeni asiyekuwa wa kawaida aliwahi kufika pale nyumbani kwangu, na ile kumbukumbu ya uwanja kufagiliwa jioni katika hali isiyokuwa ya kawaisda nilipanga kufanya uchunguzi mdogo kabla sijamuuliza jambo lolote mke wangu.
Lakini baada ya kufika nyumbani na kuoga niligundua kuwa fikra zangu zilikuwa za kipuuzi sana, yaani nianze kufanya uchunguzi juu ya mwanamke aliyekuja kuzungumza na mwabnamke.
Hapana!!
Halikuwa jambo sahihi kwangu hata kidogo, niliona ni heri ya wanawake nikawaachia wanawake. Angekuwa mwanaume hapo sawa ningetakiwa kupata mashaka.
Nikaamua kuachana na mashaka haya, na yale maneno ya marafiki nikayasahau nikaendelea kumtumikia mke wangu yule aliyekuwa mjamzito.
Miezi ya ujauzito ule ilipofika minne, mke wangu akiwa na kisilani chake kilekile aliniletea hoja kuwa anahitaji kwenda kumsalimia bibi yake ambaye naye anaitwa Christina na huku ndipo alipolipata hilo jina la Tina.
Nilipojaribu kumueleza kuwa atateseka akienda huko kwa sababu ni mimi pekee ambaye naweza kumuelewa katika hali ile aliyonayo, hapo sasa ikawa kesi akanuna akagoma kula na kisha akanifukuza chumbani eti niwe nalala sebuleni.
Nilibaki kucheka tu huku nikiamini kuwa ni ile mimba yake imekuja na mauzauza yale ya kunichukia. Na hii ipo hivyo kuna wakati mwanamke akibeba mimba anakupenda sana lakini mara nyingi hujenga chuki na kisilani kisichokuwa na maana, hata atakapojifungua na ujaribu kumueleza ataruka maili mia akikataa kabisa kuwa si yeye aliyekuwa anafanya hayo!!
Kuliko kukubaliana na mambo ya kulala sebuleni huku mke wangu amenuna kitandani nikaamua kumruhusu kwenda kwa bibi yake huenda ni huyu ambaye ujauzito ule ulikuwa umempenda.
Akaniaga akaondoka baada ya siku mbili!!
Alipokuwa huko mambo yakabadilika, kila mara ananipigia simu, na alikuwa mwenye furaha sana. Hali hii ilinifanya niwe nacheka mwenyewe tu kwa sababu ilikuwa ni kama kituko.
Tulipanga majina ya kumuita mtoto akiwa wa kiume ama akiwa wa kike....

Niliendelea kuishi peke yangu, kuna marafiki walinishangaa sana kumruhusu mke wangu kuwa mbali na mimi huku akiwa na hali ile, niliwapuuza kwa sababu niliamini kabisa kuwa yanayotokea ndani wao hawajui. Hata mama yangu mzazi alisema kuwa si jambo la heri, ilikuwa mapema sana kumwacha mke wangu kuwa mbali na mimi, nilijaribu kumgusia mama juu ya hali ilipokuwa imefikia.
Akaguna na kisha akasema ya kwetu anatuachia sisi, lakini niwe makini sana na mke wangu maana wao wanawake wanajijua wenyewe.
“Yaani hata sisi kwa sisi hatujuani vizuri, sembuse nyie wanaume kutujua sasa..... ila sina maana mbaya mwanangu, nakusihi tu!!” mama alinieleza tulipokuwa tunazungumzia lile jambo.
Maneno haya ya mama yaliyokuwa katika mfumo wa fumbo ndiyo yaliiamsha akili yangu na kuamua kufikiria mara mbilimbili.
“Mama yangu ananipenda sana hawezi kuniambia jambo lisilokuwa na mantiki...” nilijionya na hapo nikachukua hatua thabiti.
Nilijionya sana nikiwa peke yangu ndani kuwa kwa lolote lile nitakalokuta kuwa haliendi sawa basi moyo wangu na uwe na subira kuu.
Nadhani ni onyo hilo ambalo liliniwezesha kuwa imara sana.
Nauli ya kwenda nyumbani kwa bibi yake Tina kwa daladala ilikuwa shilingi mia tano na kwa pikipiki ilikuwa shilingi elfu sita.
Nilitenga bajeti kwa ajili ya ripoti hii!!
Kwa sababu ilikuwa ni ripoti kamili... ripoti niliyoifuatilia kwa muda wa mwaka mmoja na nusu bila kuchoka, wakati huo moyo wangu ulikuwa wa baridi sana.......
Naam! Hatimaye ikawa ripoti kamili!!!
Ni ripoti ambayo ningekuletea wewe pekee isingekuwa na maana, badala yake ripoti hii nilimsomea muhusika mkuu.

ILIKUWA Imepita miezi mitano tangu Tina mtulivu kabisa awe amejifungua mtoto wa kike, mrembo ambaye alidai kuwa amefanana kila kitu na bibi yake.
Ndugu msomaji na msikilizaji, kumbe ukiamua kuuamrisha moyo upoe unapoa tu..... Watu wengi huwa wanaumizwa na hisia za mapenzi kwa sababu hawana amri kuu katika mioyo yao, unamkuta mwanamke anagundua kabisa mpenzi aliyenaye anamsaliti mara kwa mara. Kila akigundua hili anaishia kulia na kukonda kwa mawazo, uamrishe moyo wako sasa uambie imetosha sitaki uwe mjinga mjinga ewe moyo wangu!! Moyo utatii amri yako....

Wakati huu moyo wangu ulikuwa umepoa sana na nilikuwa tayari kuisoma ripoti kamili.
Siku hii nilimchukua mke wangu pamoja na mtoto wangu kwa ajili ya mtoko wa kawaida tu ambao ungeweza kufanyika siku ya mapumziko aidha jumamosi ama jumapili lakini mimi nilifanya hivi siku ya jumatano. Ikiwa ni miezi kumi na nane kamili tangu nianze utafiti wangu.
Niliondoka na mke wangu mbali kabisa na wilaya niliyokuwa naishi, kuna mahali nyumba ya kulala wageni nilikuwa nimechukua chumba kikubwa kabisa kilichotutosheleza.
“Umepajuaje huku?” aliniuliza mke wangu akiwa amembeba mtoto..... nilimtazama na kumweleza kuwa kuna rafiki yangu alinielekeza na aliwahi kuja naye hapo siku ya fungate lake.
Tina akatikisa kichwa kukubali....
Tuliingia na kutulia, tukaagiza chakula cha mchana kwani chai tulikuwa tumekunywa nyumbani tayari.
Nilizungumza na Tina na kupanga mipango yetu mingi tu ya siku za usoni. Pia tukapanga mambo lukuki ili mwanetu aweze kuishi katiika mazingira mazuri siku zijazo.
Baada ya kuweka oda yetu ya chakula na kuwa tumepanga mambo yote hayo, niliuendea mlango na kutoa funguo bila yeye Tina kuwa na ufahamu iwapo nimefanya jambo lile.
Nilikuwa na sababu maalumu za kufanya vile.
Nikarejea kuketi kitandani wakati huo mtoto alikuwa amelala.....
Nikatoa kitabu changu kidogo cha kumbukumbu na kumueleza Tina kuwa kuna jambo dogo sana nahitaji kumueleza na anatakiwa kuwa msikivu na mwisho kabisa kama likiwepo la kuongezea anaweza kuongezea.
“Mh! Vipi ramani ya nyumba au?” alidakia huku akiwa na mshawasha wa kujua ni kitu gani nilichotaka kumweleza.
“Hapana sio ramani ya nyumba hii mke wangu, hii ni ripoti kamili.” Nilimjibu huku nikilazimisha tabasamu.
Sasa moyo wangu uliokuwa umepoa ulianza kuchafukwa na kitu nisichokijua.......
“Hee! Ripoti kamili? Zipi hizo?” aliniuliza akiwa mwenye furaha.
“Naomba uvumilivu wako sana, usiingilie nikiwa natoa ripoti hizi... nakusihi sana mke wangu...” nilimwomba huku nikipambana kuidhibiti hali ile ya kuchafukwa iliyokuwa ikinilazimisha kufanya jambo ambalo sikutaka kabisa.

“Tina kipenzi changu, mwanamke pekee ambaye nakutambua kama mke wangu na dunia nzima inajua hivyo..... mwanamke uliyenifanya hadi leo hii sijui ladha ya sigara, nimesahau mambo ya kijiweni, ni msafi kupindukia. Napenda kukueleza kuwa kabla sijaisoma ripoti hii tambua kuwa nakupenda sana.... maneno haya yamenyooka na sijalazimishwa na mtu. Nakupenda Tina.” Nilisita na kumtazama akiwa anayepoteza amani yake usoni, mikono yake nayo ikimtetemeka.


***Naam Tina anangoja kuisikiliza ripoti kamili...... usikose kusikiliza pamoja naye ripoti hii........ ni kesho tena hapahapa katika ukurasa huu...

ITAENDELEA
 
Mwanamke anaweza kuwa mama yako, anaweza kuwa mke wako, dada na hata rafiki yako. Lakini ukimpata mwanamke mmoja anayeweza kuwa kama mama yako, mke na pia awe rafiki yako basi usimuache kamwe mwanamke huyu kwa sababu wewe utakuwa ni mmoja kati ya watu wachache waliobahatika kupata bahati katika maana halisi ya bahati!!!
NA HII NI SEHEMU YA NNE...

“Tina kipenzi changu, mwanamke pekee ambaye nakutambua kama mke wangu na dunia nzima inajua hivyo..... mwanamke uliyenifanya hadi leo hii sijui ladha ya sigara, nimesahau mambo ya kijiweni, ni msafi kupindukia. Napenda kukueleza kuwa kabla sijaisoma ripoti hii tambua kuwa nakupenda sana.... maneno haya yamenyooka na sijalazimishwa na mtu. Nakupenda Tina.” Nilisita na kumtazama akiwa anayepoteza amani yake usoni, mikono yake nayo ikimtetemeka.
Nilivuta pumzi huku nikijizuia hali iliyokuwa inamkuta Tina isiweze kunikuta na mimi. Nilizibana pumzi zangu kwa sekunde kadhaa na kisha nikazishusha.......
Naam nikajisikia ahueni, lakini hii haikuwa tiba tossha.
Mpenzi msikilizaji, wataalamu wa mambo wanasema hivi, ikiwa una kitu kinakuumiza moyoni na ukajibana muda mrefu bila kukitoa wajiundia sumu kali mwilini inayokuua polepole.
Kusema kinachokusibu ni mojawapo ya tiba!!
Na huu ulikuwa wakati wa mimi kujitibu!!
Nilimtazama tena Tina wangu usoni na kisha nikakitazama kijitabu changu kidogo.. nikapaona pa kuanzia.
“Tina mke wangu....” nilimuita kwa sauti ya kawaida kabisa.
“Bee!” aliitika huku akijibinyabinya mikono yake.
“Unamkumbuka Yasinta.....” nilimuuliza, akatikisa kichwa kujibu kuwa anamkumbuka.
“Unamkumbuka kwa lipi?” nikajazia swali jingine....
“Mjuni!! Kwanini wanikumbusha juu ya Yasinta angali tumemzika miezi mingi sasa imepita, lakini sijamsahau binamu yangu hadi sasa... kwanini wanifanyia hivi...” alikuwa mkali kiasi fulani wakati ananipa jibu hili.
Sikujali juu ya ukali wake, badala yake niliendelea.
“Ni kweli Yasinta alikufa, sikoseli ilimuua yasinta. Lakini hakufa na kitu kingine ambacho unadhani alikufa nacho Tina, Yasinta hakufa na kipengele kimojawapo katika ripoti hii.....” nilisita nikamtazama usoni tena kisha nikaendelea.
“Nilipata fursa ya kuzungumza na Yasinta kabla hajafariki, lakini hata kabla sijazungumza naye kuna vitu kadhaa niliwahi kuvinukuu enzi za uzima wake... Tina Binamu yako alikuja kuishi nasi akiwa bado binti asiyeujua mji vizuri... ulimfanya ayaone mambo mazito kuliko umri wake... nachelea kusema sio sikoseli tu iliyomlaza Yasinta kaburini hata mambo makubwa aliyohifadhi katika moyo wake yalimfanya azidiwe zaidi. Na laiti kama angepata nafasi ya kunieleza mapema huenda hadi sasa angekuwa hai..... Tina waweza kunilazimisha eti nilifukue kaburi la Yasinta ili aweze kutoa ushahidi lakini haitawezekana kwa sasa wewe tambua kuwa Yasinta hakuweza kuvuta pumzi za mwisho kabla hajanieleza kuwa kuna kipindi ulidanganya kuwa unampeleka hospitali, ukadanganya kuwa amelazwa amezidiwa na wewe utalala huko lakini haikuwa hivyo, punde baada ya Yasinta kupewa madawa uliongozana naye hadi hospitali nyingine isiyokuwa rasmi ambapo sasa mgonjwa ulikuwqa ni wewe ulienda kutibiwa maradhi yako ya mahaba katika chumba kingine. Tina, sina hasira sasa na ninakusihi sana unisikilize tu muda wako wa kusema ukifika utasema.
Hii ya kwenda na Yasinta ukaona haijatosha kunifanya mimi mpumbavu, maskini mtoto wa watu Mungu amrehemu, ukaenda kumlaza sebuleni huko akang’atwa mbu huku akikusikia ukiugulia mahaba katika chumba cha mwanaume mwingine. Naona ulitumia faida ya kuona Yasinta hajazoeana sana na mimi hivyo ukaamua kufanya haya ukiamini kuwa hatakuja kunieleza.
Na si kwa Sinta tu, natambua wazi huyu mtoto aliyelala hapo... sio mara zote eti ulikuwa unampeleka hospitali ama kliniki kama ulivyopenda kusema najua hata yeye ulimtumia kama daraja la kwenda kupata huduma kwa bwana ama mabwana wengine.....” nilisita nikatabasamu na kumuita jina lake ili aendelee kuwa makini.
“Tina!! Unapoamua rasmi kujiunga na timu ya waongo jitahidi kuwaambia hao waongo wakufundishe kuwa na kumbukumbu thabiti... naona walisahau jambo hili kukufundisha.... kliniki uliyokuwa unaenda hukusita kuitaja kila siku ukaniona mimi bwege eti sitajihangaisha kufuatilia... sasa sikia kipande hiki.... kuanzia mwezi wa kwanza wa kwenda kliniki hadi leo hii ninapokusomea hii ripoti kamili uliwahi kuniaga mara kumi na mbili kuwa unaenda hospitali, lakini kiuhalisia baada ya utafiti wangu wa muda mrefu nimegundua kuwa umewahi kwenda mara tano tu Tina!! Hivi hizo mara saba ulikuwa unaenda wapi??? Sihitaji unijibu kwa sasa, ukipenda utanijibu baada ya taarifa hii ikiwa kamilifu.....
Tina! Ujue sigara ilikuwa rafiki wa kweli kwangu, sigara haikuwahi kunisaliti, nikiiwasha inawaka nikiivuta inavutika na nikizima nitaikuta kesho ikiwa palepale nilipoiweka baada ya kuizima. Ukaja Tina ukanilaghai nikaamua kuachana na rafiki huyu wa kweli..... kama hili halitoshi ukanibebesha na mzigo wa usafi. Ndio ni mzigo tu huu kwa sababu sasa nimekuwa mtumwa, nikiona doa kwenye shati nafua, nikiona vumbi nafua!!
Tina kwa sauti laini ukasema utakuwa sigara kwangu, sigara gani ya kinafiki namna hii... laiti kama sigara zingekuwa kama wewe nadhani wavutaji wote wangeacha kuvuta mara moja bidhaa hii.
Ewe Tina nikakuamini na kukupatia moyo wangu uufanye unavyotaka leo hii unanipa mtihani huu mgumu kabisa wa kukusomea ripoti hii.
Ujue nimejifikiria siku nyingi sana, sikuwa na ujasiri wa kukusomea ripoti hii lakini leo imebidi tu. Japokuwa naona ni kama ndoto.
Mke wangu Tina, unakumbuka vyema baada ya kujifungua ukanisihi sana nikufungulie biashara kwa sababu ukikaa sana nyumbani unahofia kuvimba miguu.. nikajisemea huyu sasa ndo mwanmamke wa shoka, sikia Tina simaanishi kuwa wewe si mwanamke wa shoka la! Wewe ni mwanamke shupavu haswa na ninakiri mbele yak oleo kuwa mafanikio haya niliyonayo leo ni kwa sababu nipo na wewe, umenipigania sana hakika.
Na hata uliponisihi nikusaidie ufungue biashara zako niliobna ni jambo la heri mno, tazama nikachota akiba yote na kukuanzishia biashara ya nguo, ukasema utakuwa unakopesha watu mtaa kwa mtaa. Na kweli ikawa ukaanza kuwakopesha, awali ilikuwa nguo za wanawake pekee mrtaji ukakua ukaongezea na nguo za wqkibaba.
Hapa ndipo ulipoona kukopesha nguo pekee haitoshi ukalazimika kuanza kuukopesha nma mwili wako, kwangu mimi ukifika unasema umechoka sana lakini kwa wanaokopesheka unawakopesha bila kuchoka.
Najua unashangaa sana kuwa haya yote nimeyajua vipi na kweanini sikukueleza mapema haya ili tuachane, ningeweza kufanya hivyo Tina wangu lakini nilijipa muda wa kuligundua shaka, kulitafutia jibu lake na kisha kukitafuta chanzo.
Shaka nililipata na jibu pia lakini kuna baadhi ya vyanzo sina hadi sasa. Natarajia leo hii utanieleza nini chanzo.......

“Tina hivi unajua nampenda mtoto huyu kwa kiasi gani? Hivi unajua mama yangu anampenda kiasi gani mjukuu wake na vipi kuhusu babu yake.. unawaona wanavyompenda na kumjali mtoto huyu!!!?” akatikisa kichwa kukiri kuwa ni kweli ninayosema.
“Sasa jiulize ni wanaume wangapi hapa duniani wanaweza kupenda watoto wasiokuwa damu yao huku wake zao wakiwa wamewaaminisha kuwa ni damu zao, jiulize kina babu na akina bibi wangapi wanaweza kupenda wajukuu wasiokuwa wao katika maana halisi.” Nikasita na kumtazama Tina akiwa anahaha huku na huku. Mara akashika glasi ya maji ili anywe.
“Kunywa maji Tina kisha nikueleze nilijuaje kuwa huyu si mtoto wangu....”

Naam! Ripoti ndio kwanza ukurasa wa kwanza, anasomewa Tina. Isikilize kwa makini imeambatana na mengi sana ambayo ni somo na funzo kubwa kwako........

Asante!!!
 
“Tina hivi unajua nampenda mtoto huyu kwa kiasi gani? Hivi unajua mama yangu anampenda kiasi gani mjukuu wake na vipi kuhusu babu yake.. unawaona wanavyompenda na kumjali mtoto huyu!!!?” akatikisa kichwa kukiri kuwa ni kweli ninayosema.
“Sasa jiulize ni wanaume wangapi hapa duniani wanaweza kupenda watoto wasiokuwa damu yao huku wake zao wakiwa wamewaaminisha kuwa ni damu zao, jiulize kina babu na akina bibi wangapi wanaweza kupenda wajukuu wasiokuwa wao katika maana halisi.” Nikasita na kumtazama Tina akiwa anahaha huku na huku. Mara akashika glasi ya maji ili anywe.
“Kunywa maji Tina kisha nikueleze nilijuaje kuwa huyu si mtoto wangu....”

Hata yale maji hakunywa aliishia kuinua glasi na kuitua tena mezani, alitaka kuzungumza nikawahi kumziba mdomo wake asiseme neno lolote, na sikuruhusu tabasamu litoweke katika uso wangu niliendelea kutabasamu ili Tina aidha awe na amani ama ashindwe kabisa kunisoma iwapo nipo katika hasira ama hali tu ya kawaida.
Baada ya kuwa ametulia niliendelea kusimulia.
“Tina... shem Stela hivi yupo wapi siku hizi?” Nilimuuliza lakini sikuwa namaanisha kuwa nahitaji jibu lake. Niliendelea kusimulia,
“Tina utake usitake na hata kama machoni utakataa lakini nafsi yako lazima inakusuta tu kuwa dada yako yule ni mtu mbaya sana, yaani kati ya wanawake wenye roho chafu niliowahi kukutana nao basis hem Stela yupo katika orodha tena huenda hata kumi bora yumo. Yaani kweli Tina na akili zako ukitambua wazi kuwa ninakupenda na ninakuthamini lakini bado ukawekwa kikao na kujazwa ujinga wa kitoto namna ile......” nikasita nikacheka kidogo, Tina akashtuka sana. Nikacheka tena kisha nikaendelea.
“Tina, yaani na umri wako ule ukashawishiwa na dada yako jambo la ajabu kama lile. Yaani kisa pesa kisa pesa Tina..... eti hapa nikikuuliza sababu utasema sababu ni bikra.... sawa ni yeye aliyekutoa usichana wako na kukuingiza katika ulimwengu wa mapenzi lakini hii si tija Tina. Sawa alikuwa mwanaume wako wa kwanza, kwani mimi katika kumbukumbu zangu simtambui msichana wangu wa kwanza au? Namkumbuka vizuri sana japokuwa mimi sikuwa wa kwanza kwake... lakini nilipoamua kuingia katika maisha ya ndoa nikaamua kusahau kila kitu.
Ndugu msikilizaji napenda kukusihi jambo moja la muhimu. Kamwe usilete mambo ya kabla ya ndoa katika ndoa yako, ama hata kama sio ndoa basi kwa kijana, usikubali kuleta mambo ya kabla ya mahusiano kwenye mahusiano yako ya sasa. Eti umeoana na mtu hapo kabla hamjaoana mlipenda sana kufanya starehe, leo hii mmeoana mnataka kuendelea kufanya starehe badala ya kufanya maendeleo.
Ama eti unakuwa kama Tina, kisa kabla sijamuoa kuna mwanaume wake wa kwanza aliyemtoa usichana wake na kumuingiza katika ulimwengu mpya, hadi nakuja kumuoa anaendelea mahusiano na mwanaume yule. Hili ni daraja la juu la upuuzi tafadhali liepuke.....

Tina! Ulikosa kitu gani kwangu hadi ukaamua kujiingiza katika mahusiano na bwana yule, tena mke wa mtu daah! Inauma sana Tina, hebu simama Tina wangu.. simama ujitazame jinsi ulivyokuwa msichana mwenye mvuto, jitazame ulivyokuwa msichana jasiri. Lakini ajabu eti ujasiri wako ukaishia katika dhambi hiyo, jiulize mkewe akisikia ripoti hii atajisikiaje, kwamba wewe Tina ambaye ni mke wa mtu umeenda kumbebea mimba mume wa mtu tena kwa makubaliano kabisa.
Tina ukanifanya mi mpuuzi kweli, yaani ukashirikiana na dada yako mkapanga kuwa mimi na wewe tusipate mtoto kwanza ili umzalie huyo Malaya mwenzako.
Sikia Tina, kama ulikuwa haujajua jambo moja ni kwamba katika pita pita zangu kuikamilisha ripoti hii nimegundua mambo mengi sana, dada yako alikufanya wewe daraja tu.. unatumika atakavyo lakini kuna jambo alikuwa ananufaika nalo. Yule mzazi mwenzako alikuwa akimlipia ada ya chuo. Alikuwa pia anamnunulia simu mpya kila zilivyokuwa zinatoka.
Wewe ukawa unaamini kuwa eti mapenzi ndo yalikuwa yanakuendesha, pole Tina ulikuwa mtumwa wa mapenzi.”
Nilipotaka kuendelea mara kitoto kiliamka na kuanza kulia japokuwa si kwa sauti ya juu.. nikamchukua pale kitandani na kugundua kuwa alikuwa amejikojolea. Tina akataka kumbadilisha nguo nikamsihi awe mtulivu nitafanya mimi kila kitu.
Nikambadilisha nguo zake vizuri...
Na hapohapo sikutaka kupoteza wakati nikaendelea kuzungumza kilichokuwa kinafuatia.
“Sonia mtoto wangu, mama yako ni mwanamke imara sana, nakuombea sana mwanangu hata nikifa leo basi uurithi ujasiri na uimara wa mama yako katika kupigania maisha lakini kamwe usirithi upumbavu wake hata chembe nakuombea sana mwanangu Sonia.....” nilikitazamakile kitoto kikiwa kimetulia kabisa kikiwa kinanitazama.
“Najua wewe ni malaika na haya ninayoyasema unanisikia na kuyatunza katika kichwa chako..... Sonia, mama yako ni wa ajabu sana.. alikuwa akiniongopea kuwa anaendfa kwenye mikesha kanisani huko mara kwa mara nikawa nabaki mimi na wewe nyumbani nilikuwa nakubadilisha nguo, nakubembeleza hadi unalala. Akirejea haniulizi nimeweza vipi kukubadilisha nguo, leo hii anataka anisaidie kukubadilisha nguo.. eeh afanye hivyo ili iweje sasa kwa siku ya leo??” nilikiuliza kitoto kile huku nikikitekenya mashavuni, kikacheka kidogo huku kikitupa miguu yake huku na kule.
Sasa Tina alikuwa anabubujikwa na machozi na huku kilio cha kwikwi kikimwandama. Sikujihangaisha katika kumbembeleza niliendelea kusema na Sonia.
“Mwanangu Sonia, ninakukumbusgha usijekuwa kama mama yako. Yaani kweli unatumia kivuli cha kanisa kunilaghai mimi huku unaenda kwa bwana yako, tena bwana mwenyewe ndo baba yako Sonia. Baba gani sasa huyo? Kama angekuwa baba kweli angekubali vipi kila siku aende kuonana na mama tu halafu wewe anakuacha, eeh! Sonia mimi nd’o baba yako mwanangu...... achana kabisa na huyo tapeli wa mapenzi aliyefanikiwa kumlaghai mama yako hadi akawa mjinga!!!”
Kitoto kilikuwa kimenikazia macho huku kikiendelea kutoa tabasamu lililonipendeza kulitazama na hili lilinipa faraja sana japokuwa hakuwa damu yangu nilimpenda sana Sonia.
“Sikia Sonia, eti mama yako akaenda kubeba mimba halafu akajifanya ni ya kwangu, kumbe kuna mjinga mmoja hivi anataka wazae naye eti kisa tu alikuwa mwanaume wake wa kwanza..... samahani sana Sonia nasema maneno mazito sana mbele yako, lakini nafanya hivi kwa sababu naweza nisiipate tena nafasi kama hii ya kusema nawe tena kwqa kirefu kama leo. Halafu nimekutazama Sonia nimekumbuka jambo jingine la muhimu sana lakini hili halikuhusu wewe mwanangu, wewe lala ngoja niseme na mama yako.”
Nikamtua Sonia kitandani akabaki kuchezea vidole vya mikono yake, nikamgeukia Tina ambaye aibu kubwa sana zilikuwa zikijionyesha katika uso wake. Ni mtu aliyetamani kukimbia lakini angeenda wapi wakati nimeufunga mlango, huenda alitamani pia dunia ipasuke lakini muujiza huo hauji hovyohovyo... kwa sababu iliishaandikwa kuwa mwisho wa ubaya wowote ule ni aibu!!!

***Ni kipi kingine katika ripoti ya Mujuni Kalisti. Na nini hatma ya ripoti hii na maisha yake ya baadaye yeye na familia yake.. vipi kuhusu Sonia mtoto wa kusingiziwa lakini ambaye anapendwa kwa dhati na baba yake!!!!

Usikose kufuatilia sehemu ya sita......
 
WATU wengi huikosa furaha kwa sababau hawatambui kuwa ili uipate furaha iliyokamilika huna budi na wwewe kuwapa furaha wengine wanaoihitaji..... lakini wapo wanaojitahidi kadri wawezavyo kuwapatia furaha watu wengine tena watu wao wa karibu kabisa lakini badala ya kulipwa furaha wanalipwa huzuni..... maisha ndivyo yalivyo hayana usawa siku zote!!
NA HII NI SEHEMU YA SITA.......

Nilikuwa namuonea huruma sana Tina, nilijua ni kitu gani kinafukutika katika moyo wake, alikuwa anafanania na mtu anayeomba wakati urudi nyuma aweze kurekebisha popote alipokosea lakini kamwe wakati haurudi nyuma.
Nilijizuia nisimtazame Tina kwa jicho la huruma na badala yake nikajikaza na kuendelea kutoa ripoti ile iliyonigharimu muda na pesa nyingi katika kuifanyia utafiti na kisha kuiandaa.

“Tina ulikuwa unajisikiaje ulipokuwa unaniigizia eti ile mimba ya Sonia ilikuwa imenichukia, kila kitu nikifanya kwako kinakuwa si sawa hadi ukaomba ruhusa kwenda kwa ndugu zako, eti ukiwa na macho makavu kabisa ukasema unaenda kwa bibi yako.... dada yako yule shetani aliyevikwa ngozi ya mwanadamu ili aweze kufanya vyema kazi yake na yeye akachochea kabisa huku akinibania pua.
“Yaani sisi wanawake tuache tulivyo tu... wakati mwingine mimba inakataa ukoo mzima unashangaa inawapenda marafiki. Yaani Mungu anajua mwenye we alivyotuumba!!”.....
Yaani Stela hakuona hata aibu kumtaja Mungu katika uongo huu unaofananishwa na kisu kikali, akamtaja tu hovyo kama kweli anamaanisha anachosema.
Bwege mimi nikainama na kujichekesha nikakubali ukaondoka kwenda kwa bibi, bibi mwenyewe sasa nd’o huyo mwanaume wako....... eti mwanaume aliyekutoa usichana wako!!!
Tina yaani ukawa na amani kabisa upo na huyo mwanaume wako halafu ukawa kila muda unanipigia simu, nakumbuka kuna siku ukanigombeza kabisa eti inakuwaje nimechelewa kurudi nyumbani, tena ukalalamika kabisa kuwa unahisi siku hiyo nilikuwa namwanamke mwingine, basi mjinga mim,i nikakubembeleza wee nikikuomba uniamini... kumbe kilaunapokata simu unabaki kunicheka ukiwa na huyo mpenzi wako.
Tina, hivi kweli mtu anayekupenda kabisa akubalikusikia unaongea na mwanaume mwingine usiku manenoya kimahaba???
Hakuwa akikupenda mwanaume yule.... na kukuthibitishia uchafu wake, yaani mdogo wake aliposafiri na kumwachia nyumba amlindie ndo akatuimia fursa hiyo kukualika wewe katika nyumba hiyo, we nawe ukajiona mama mwenye nyumba kweli. Unatia huruma sana Tina....
Zamani nilisikia kuwa marafiki wengi huchonganisha tu linapokuja suala la mapenzi lakini kumbe si kila rafiki ni mchonganishi, na marafiki wengine huogopa kabisa kumtoa ushauri linapokuja suala la mapenzi lakini shukrani za dhati kwa rafiki yangu aliyeamua kusema litakalokuwa na liwe lakini hawezi kuendelea kukaa kimya......
Akanieleza kuwa kuna mwanamke alikuwa anakuja nyumbani.... nilipuuzia awali lakini nilipofuatilia kwa ukaribu nikaugundua mchezo.. bwana yako alikuwa akitumia kivuli cha mwanamke kufika pale nyumbani, halafu yeye anakuwa garini. Huyo mwanamke anafika na kukuchukua mnaingia garini milango inafungwa halafu kifuatacho ni uchafu hata kusimulia.
Na inaniumiza sana nafsi kwa sababu niliuona mchezo mzima kabisa, yaani ndani ya gari moja na mwanamke mwenzako anakushuhudia uchafu unaofanya na mwanamke huyo anajua kabisa wewe ni mke wa mtu!!!
Haukuiogopa laana Tina wangu, yaani ujasiri mkubwa kiasi kile uliutoa wapi haswa.
Natarajia majibu yako itakapomalizika ripoti hii nijue ni kitu gani kikubwa ulikuwa unapata hadi kukubali kudhalilishwa huku ukinidhalilisha na mimi...” nilisita na kumtazama Tina, alikuwa anatokwa jasho, nahisi alitegemea yote lakini hakuwahi kudhani kuwa nilikuwa nalala naye kitanda kimoja huku nikiyajua machafu haya aliyokuwa ameyahifadhi katika moyo wake akiamini kuwa ni siri.
Ndugu msikilizaji mke anauma jamani...... namaanisha mkje ambaye kila anayekufahamu wewe basi anamfahamu na yeye kama ubavu wako, mwanamke unayelala naye kitanda kimoja ukimuamini kabisa kuwa ni mtu salama katika maisha yako unakuja kugundua kuwa vile anavyokukumbatia basi anamkumbatia mtu mwingine, vile anavyokuita majina ya kimapenzi basi kuna mtu mwingine pia anaitwa hivyohivyo. Ukiwa na moyo mwepesi unaweza kujikuta umefanya jambo baya sana ambalo utalijutia tena na tena.
Naomba ninaposimulia ripoti hii wewe vaa viatu vyangu na ujiulize ingelikuwa wewe ungelifanya nini......

Nilipoona Tina anazidi kutokwa jasho niliwasha pangaboi nikaweka spidi ya kutosha tu ili aweze kupa ahueni, wakati huu Sonia alikuwa amesinzia tena.
Baada ya kumpa pumziko hili nilirejea tena kwake...... kabla sijasema neno alinieleza kuwa ikiwa nina silaha yoyote ile basi nimjeruhi hadi afe ama kama nina sumu nimpe anye afe kwa sababu hana sababu hata moja ya kumuhalalisha kuishi.
Nilimsogelea na kumvuta kwangu kisha nikamueleza kuwa sitamdhuru hata chembe, kama tulivyoingia ndivyo tutakavyotoka!!!
Na hapo sikutaka upepo ubadilike na kuanza kuzungumzia hayo menghineyo nikarejea katika kijitabu changu kidogo nikafunua na kusoma alama nilizokuwa nikizitumia katia kuandika, na hapo nikapata jambo jingine la ajabu lakini kutokana na kwamba nilifanya utafiti wa kina lilibakia kuwa la ajabu lakini la kweli.
“Tina unaifahamu Doromee!!” nilimuuliza kwa utulivu kana kwamba hakuna kinachoendelea kati yetu. Akatikisa kichwa kupinga kuwa haijui..
Nikatabasamu kisha nikaendelea.
“sasa Tina mke wangu wewe hata ungeweza kutumwa kuniua bado ungeniua tu.... sawa kwa sababu hauijui Doromee mimi ninaijua na nilifahamishwa na daktari, siku ile nilipochelewa kabisa kuamka halafu nikajikuta nikiwa nina homa kali sana. Kwenda kupima hospitali nikaambiwa siumwi na chochote... Tina awali nilihisi kuwa ripoti za daktari si sahihi lakini baadaye nikagundua kuwa ni sahihi, na aliyekutuma ni huyu mwanaume wako, akakutum,a uniwengee madawa hayo ili nipatwe na usingizi mzito sana unaodumu kwa masaa yasiyopungua kumi na mbili..... kweli kabisa mke wangu na wewe ukafanya kama alivyokutuma. Jiulize sasa ingekuwa ni sumu amekudanganya ni madawa ya usingizi.. hivi na wewe ungejiliza msibani na kugalagala katika kaburi langu huku ukilalamika eti mume wangu umeniacha na nani????
Sawa uliponiwekea yale madawa ulienda kwake au mlienda wapi?” nilimuuliza, sasa nilijisikia hasira ikinipanda sa.
Huku akiwa anatetemeka vibaya mno alinijibu kuwa walienda nyumba ya kulala wageni. Nikamuuliza kuna jipya walienda kufanya ambalo hawakuwahi kulifanya siku za nyuma akasema hakuna jipya lolote walienda kuifurahisha miili yao.
Nikataka kuongea nikajizuia maana koo lilikuwa limezibwa na donge la hasira, na nilivyojaribu kulimeza donge lile mara machozi yakaanza kunitoka.
“Tina mke wangu, wewe ni wakala wa shetani!!!” nilimwambia huku nikishindwa kujizuia kulia kwa sauti....
Afadhali kwa kiasi fulani kilio kile kilinisaidia kwa kiasi fulani, koo likaachia na sasa nikakifungua kitabu kile na kuingia katiika ukurasa mwingine wa yote ambayo mke wangu aliyafanya huku mimi nikiwa sijui lolote...

#Mkasa huu bado unaendelea, kuna mengi sana katika mkasa huu lakini ombi letu kwako ni kusikiliza huku unajifunza....

Asante
 
Back
Top Bottom