Willy Gamba 1
JF-Expert Member
- Jan 5, 2015
- 352
- 377
RISASI 4
na richard MWAMBE
Joseph Rutashobya anashuhudia mauaji
mabaya ya wazazi wake, hali hiyo inamwacha
yatima, anaishi maisha ya tabu mpaka
anakuwa mtu mzima.
Sasa Joseph Rutashobya 'JORU' analipiza
kisasi kwa wale waliofanya hayo. Kwa nini
Risasi 4?
fuatilia kisa hiki kinachokurudiaha nyuma.
SEHEMU YA 01
KAMBI YA JESHI MTUKULA-
August 1998
Mguu pande! Mwiliiiiiiii legeza!
ilikuwa ni sautinya amri kutoka kwa
kiongozi wa gwaride maalumu la
vijana wa JW lililokuwa likifanyika
katika kambi ya Mtukula, karibu
kabisa na mpaka wa Tanzania na Uganda.
Askari wote waliweka mguu pande na
kulegeza miili yao huku wakitazama mbele.
Jua kali lilikuwa likiwaka katika uwanja
huo, vumbi lilikuwa likitimuliwa na kaupepo
hafifu.
Wakiwa katika mistari minne yenye askari
kumi na mbili kila mmoja, James Rutashobya
alikuwa na mawazo lukuki, kijasho chepesi
kikitiririka kutoka katika katika kofia lake la
chuma na kuishia kidevuni.....
Upepo tulivu ulikuwa ukiendelea kuvuma,
kila mtu alikuwa ametulia katika uwanja
ule. Ndugu jamaa na marafiki walikuwa
wakitazama vijana wao wakakamavu wakiwa
uwanjani.
Joseph Rutashobya Joru kama walivyokuwa
akiitwa na kuruta wenzake wa kombania moja
lakini service man wake alipenda kumwita
'Nyoka wa kijani' , alikuwa kijana mpole asiye na
maneno mengi lakini aliyejawa na vitendo zaidi,
alijiamini, aliamini uamuzi wowote uinaokuja
kichwani mwake, tangu aanze mafunzo ya
kijeshi katika kambi hiyo miezi sita iliyopita
wanaomjua wanadai alikuwa haongei maneno
zaidi ya hamsini kwa siku. Hakuna aliyekuwa
akijua kwa nini kijana huyu yuko hivyo, daima
alipenda kukaa peke yake kila apatapo nafasi
akyaruhusu mawazo yake kupita hapa na pale,
kujenga hili na lile. Daima alirudishwa mbali
kifikra na hali hii.
Akiwa mguu pande, aliinama kichwa chake na
kuangalia bunduki lake aliloliinamisha kwa
mbele, likimtazama kwa huruma, likitanguliwa
na singe linalong'aa kwa jua la saa nne asubuhi
huku kitako cha mti usiooza kikiwa kwenye
vumbi la ardhi hiyo kavu. Aliitazama kwa
uchungu na kukumbuka aina hiyo ya bunduki
ilipomuacha katika hali duni akiwa mtoto wa
miaka kumi tu, likambakisha yatima, bila
msaada wowote na kumsukuma katika maisha
magumu ambayo hakuyategemea wala
hakuwahi kuyafikiri, maisha ya shida na taabu,
maisha ya kutokuwa na baba wala mama.
Aliendelea kutazama singe lile ambalo nyuma
yake kulikuwa na tundu dogo lenye kutoa risasi
pindi tu liamurishwapo. Alilitazama tena na tena
bila kuchoka moyoni akliambia.
Ni wewe nakukumbuka sana kwa sura yako,
mdomo wako mdogo ulipiga kelele za kutisha
nikamshuhudia mama yangu akianguka chini
huku akilia kwa uchungu, ni wewe ambaye
baadae ulifanya vilevile na kumuacha baba
yangu akiwa hana uhai, sasa naelewa tukio
ulilofanya miaka ile, usihofu, hukuwa wewe ila
umefanana naye,
Joru alijikuta ndani ya kumbukumbu nzito,
akiongea moyoni kwa uchungu huku akiitazama
ile 'rifle' bunduki aliyoishika mkononi mwake.
Alilolitarajia likatokea, uchungu ukatawala hisia
zake, hasira zikapanda kama moshi wa tanuru,
Joru akarudishwa kihisia katika kumbukumbu
mbaya iliyomrudisha miaka 21 nyuma, chozi
likatoka katika jicho lake na kuning'inia chini ya
kidevu chake, likajiachia na kudondoka ardhini,
kishindo kikubwa kilisikika moyoni mwa Joru,
vumbi lisilo la kawaida lilitimka na kumfanya
mapigo yake ya Moyo kuongeza kasi, damu
kwenda mbio, pumzi kutoka kwa nguvu.
Kesho na keshokutwa utakua kijana mwanangu,
hakikisha unalipa kisasi kwa damu hii
inayomwagika, damu ya familia yako, damu ya
wazazi wako,
Sauti ya baba yake ilijirudia kwa mwangwi wa
ajabu kichwani mwake ikitanguliwa na kile
kishindo cha lile chozi kufika ardhini, yote hayo
hakuna aliyeyahisi wala kuyasikia isipokuwa
Joru peke yake.
Gwarideeeeee!!!! ilikuwa amri nyingine
iliyomgutusha kutoka katika ulimwengu wa
mbali, aliinua kichwa akatazama mbele.
Silaha beganiiiiii weka! amri iliendelea kutoka
kwa kiongozi wa gwaride. Kishindo kimoja
kikasikika, bunduki zile zikishikwa kwa
ukakamavu wa mikono ya wale wana wa jeshi,
wanaomaliza mafunzo, zikapandishwa begani na
miguu kuwekwa sawa kisha ukimya ukatawala.
Muziki maalumu wa tarumbeta ulisikika ukitoka
katika kikundi cha bendi ya jeshi kilichokuwa
kikisindikiza vijana hao, muziki huo uliashiria
kuwa mgeni wa siku hiyo alikuwa akiwasili.
Baada ya dakika chache mgeni yule alipanda
katika kibanda maalumu, alikuwa ni amiri jeshi
mkuu, mkuu wa nchi, juu ya kibanda kile
maalum alisimama akiwatazama wale vijana
waliokuwa ndani ya mavazi adhimu ya kijeshi
yaliokuwa na mabaka, yaliyowapamba
wakapambika, walikuwa ni vijana kutoka kambi
zote za mafunzo za kanda ya ziwa
wakihitimisha mafunzo yao kwa pamoja, hakika
ilikuwa sherehe kubwa. Wakati wengine
wakifikiria kukutana na ndugu na jamaa zao
baada ya gwaride hili, wakiwapongeza kwa
kuhitimisha mafunzo hayo magumu, haikuwa
hivyo kwa Joseph Rutashobya, hakuwa na mtu
wa kuja kumlaki wala kumwambia hongera
katika shughuli hiyo, hali hii ilimpa uchungu
sana lakini hakuweza kupingana na ukweli halisi
uliopo, hana ndugu, hata wale waliopo hawajui
kama siku hiyo anamaliza mafunzo yake ya
jeshi kwa maana ni miaka mingi imepita hata
hawakujua kijana huyo yuko wapi, walilia
wakanyamaza, wakajua kama hajafa basi
amepotea kimazingara.
Kiongozi wa gwaride akatoa amri nyingine, sasa
ilikuwa ya kutoa heshima kwa Amiri jeshi mkuu;
kama kawaida, zile bunduki zikatolewa
mabegani na kushikwa mikononi kwa umahiri
mkubwa.
Wimbo wa Taifa kombozi la Tanzania ulirindima,
wapigaji walipiga kwa umahiri mkubwa, wimbo
wa Taifa la Tanzania ambao kutokana na
maneno yenye ujumbe mzito na melodi ya
kupendeza mataifa kama Zambia na Afrika ya
kusini yaliufanya kuwa wimbo wao wa Taifa
vilevile, na ingependeza kama Africa nzima
ingekuwa na wimbo huu mmoja kwa kila Taifa
wenye maneno matamu Mungu ibariki Afrika,
wabariki viongozi wake na watoto wake pia.
Joru alitulia kwa ukakamavu hisia zake
zikatekwa tena na wimbo huo ambao alijifunza
alipokuwa shule ya vidudu na ile ya msingi
madarasa mawili tu aliyoyasoma, chozi lingine
likadondoka ardhini na kufanya kishindo kilekile
moyoni mwake, mara sauti ya kilio kikali ikapita
mawazoni mwake...
'Aaaaaaaaaagggggghhhhh, kimbia Jose kimbia,
usitazame nyuma,'
Aliikumbuka sauti hii ya mama yake kipenzi
ikimjia katika hisia kali na nzito, Joru alijikuta
akilia kwa kumbukumbu hizo. Alimtazama mgeni
rasmi, mkuu wa nchi aliyetulia juu ya kibanda
kile akiwa ndani ya suti safi ya kimaghalibi,
hakuwa mbali kutoka katika kibanda kile.
Joru alikuwa katika gadi ya pili ambayo kwa
mpangilio wao ilikuwa mbele kushoto ilikuwa
gadi ya kwanza na kulia ilikuwa gadi ya tatu,
katika gwaride hilo kulikuwa na gadi kumi na
tano.
Joru alimtazama kwa makini mgeni rasmi
moyoni akmwambia,
Hujaubeba Uafrika, kama ungeubeba basi
ungevaa vazi nadhifu la kitenge ama cha
Sunguratex, Kilitex, au Mwatex.
Wimbo wa Taifa bado ulikuwa ukiendelea,
Heshima umoja na amani, hizi ni ngao zetu,
Africa na watu wake, maneno haya yalimpa
uchungu Joru, akaitazama Africa kwa mapana
yake,
Afrika bara zuri, bara aliloishi mwanadamu wa
kale, lilokuwa na umoja mkubwa,
Afrika, kwa nini tunapigana Afrka?
Kwa nini tunakosa upendo Afrika?
Kwanini tumepoteza thamani ya maisha hadimu
ya kiafrika yenye tunu zisizo kifani? Umoja,
mshikamano, upendo na ujamaa, unapotea kati
ya Waafrika? Chuki, ubabe, ubinafsi vimeiteka
Afrika, vimeingia mioyoni mwa Waafrika na
viongozi wake. Watu wa kale waliita bara hili
bara la giza lakini sasa tunastahili kuliita bara
jekundu kutokana na damu inayomwagika siku
hadi siku.
Wimbo ule mtukufu ulipotelea katika mawingu,
mawingu ya anga la Mtukula, mawingu safi
meupe yaliyopendezesha anga hilo, ndege aina
ya mbayuwayu waliokuwa wakiruka hapa na
pale walifanya nyimbo nyingine tamu mara tu
baada ya kuisha ule wimbo hadhimu. Joru
alikuwa bado katika hali ya ukakamavu mpaka
amri nyingine ilipotolewa.
Mgeni rasmi alishuka kutoka katika kibanda
chake na kuongozwa na askari maalum
alieandaliwa kwa shughuli hiyo ya ukaguzi wa
gwaride. Pamoja nae mkuu wa majeshi mkoa wa
Kagera aliomsindikiza, brigedia Shibagenda.
Walipita mbele ya mistari ya vikosi hivyo kwa
mwendo wa madaa wakiongozwa na wimbo
maarufu wa enzi zile,
Tanzania Tanzania, nakupenda kwa moyo wote,
Tanzania Tanzania jina lako ni tamu sana...
Joru alitulia bila hata ya kutikisika, akisikiliza
muziki ule wa uliokuwa ukipigwa na bendi ileile
huku hisia zake zikiimba pamoja na melodi
hiyo.
'Nilalapo na kuota wewe, niamkapo ni heri
mama we...'
Ni siku hii Joru alipogundua umaana na uzito
wa wimbo huo, picha za mauaji ya wazazi wake
zilimrudia na kumsumbua kichwa. Machozi
yalimtoka kijana huyu mkakamavu mwenye
tambo la mtu anayenyanyua vyuma au kufanya
mazoezi ya vitu vizito.
Mgeni rasmi alipomfikia alisimama na
kumtazama Joru ambaye alisimama
kiukakamavu; ukiacha machozi yaliyokuwa
yakitoka machoni pake na kumwagika kwa fujo
huku kelele nyingi za vilio zikimrudia, akiwaona
askari wa Uganda chini ya kiongozi wao Mali ya
Mungu wakitesa na kuua wanakijiji ndani ya
mpaka wa Tanzania na Uganda, kipande cha
ardhi ambacho Uganda ilidai kuwa ni chao,
ubabe na utemi vilitawala.
ITAENDELEA