RIWAYA: PENZI HARAMU

RIWAYA: PENZI HARAMU

Decree Holder

JF-Expert Member
Joined
Jul 19, 2015
Posts
2,559
Reaction score
3,748
Wanabodi karibuni sana twende pamoja kwenye Riwaya hii:

JINA : PENZI HARAMU
MWANDISHi: ZAWADI B LUPELO

Karibu

SEHEMU YA KWANZA
Ndani ya ukumbi wa Black Lord Hall majira ya usiku watu wa kila aina wakiwa wamefurika, wakiwa wamechachawa waliojawa na taharuki,

“Hivi kweli Amani anamwoa Liya?” Aliuliza mmoja wa wageni waalikwa.

Hakuna aliyekuwa anaamini, katika mazingira ya sasa, katika jamii ya sasa ya kitanzania. Jamii inayoshikilia maadili, mila na desturi kama vile mtoto aliye mgongoni amshikiliavyo mama yake, ni jambo la ajabu na isingetegemewa Amani na Liya kuoana. Inawezekanaje? Na nini hatima yake? Hii ndoa itafika wapi? Maswala haya na mengine mengi yaligonga vichwa vya wageni waalikwa waliobahatika kuhudhuria harusi ile ya aina yake.

Watu walikuwa wamekaa kitako mithili ya watu wanaosubiri siku ya unyakuo wa Yesu Kristo, siku ile ambayo tunaambiwa watu wote tutaota mbawa na kupaa kama ndege. Ni watu wenye shauku kuu, furaha, huzuni, mshangao, masikitiko na kila aina ya hisia ziliwagubika wahudhuriaji kila mmoja na hisia yake. Wapo waliosema ndoa ile ni chukizo mbele za Mungu, wakasema Biblia imekataza, Koran hairuhusu, serikali haipendi! Mila zimekiukwa!. Kila mwenye lake lilimtoka kama ilivyo kawaida ya walimwengu.

Baada ya muda mfupi minong'ono ikajaa mule ukumbini sauti zikawa nyingi zikikinzana hakukuwa na shaka kuwa ilikuwa ni mijadala juu ya ile ndoa,

“Hallow! Hallow! Mabibi na mabwana” alisikika mshereheshaji wa sherehe wenyewe wanamwita MC

“Nitaomba tusimame wakati maharusi wakiwa wanaingia ukumbini”

Watu wote walisimama mwenye kigelegele chake alipiga, mwenye kusonya alisonya, mwenye kucheka alicheka mwenye kulaani hivyo hivyo. Ilikuwa ni harusi ya tofauti kwani harusi zilizo nyingi tunatengemea watu kuwa na hisia moja ya furaha na bashasha lakini harusi ya Amani na Liya ilikuwa ya tofauti sana kwani iliwagawa watu kihisia. Muziki uliwashwa kwa sauti ya juu zaidi wakati maharusi wakiwa wanaingia ukumbini. Naam! Amani na Liya wakiwa wameshikana mikono wakicheza taratibu huku wanajongea ndani kwa mwendo wa mnato

“Mabibi na mabwana vigelegele tafadhali!” alisikika mshereheshaji maarufu kwa jina la MC Oscar.

Basi vigelegele vikazidi mle ukumbini kana kwamba kila jambo lipo sawa. Amani na Liya wakiwa wameshaingia ndani walicheza taratibu kuelekea kwenye meza walizoandaliwa maharusi.

Liya alikuwa ni binti mrembo sana mwenye urefu wa wastani, mweupe si mweupe, mweusi si mweusi mwenye rangi iliyotulia. Mnene si mnene mwenye umbo la wastani, anavutia kumtazama, amepambwa akapambika. Wakati wanacheza na kujongea vilipo viti vyao macho ya Amani wakati wote yapo kwa Liya akimwangalia kwa jicho la huba, basi Liya akitabasamu ni raha tupu mithili ya watu waliopo peponi. Wanaonekana ni vijana wadogo wanaofurahia ndoa yao changa ikiwa ina masaa machache toka kufungwa kwake.
Baada ya Amani na Liya wakiwa wameshachukua nafasi na sherehe ikiwa inaendelea, MC aliruhusu burudani kidogo kutoka kwa kikundi cha vichekesho cha Negro Comedians ambao walikuwa ni vijana wanaochipukia kwenye sanaa jijini Dar es salaam chini ya kijana maarufu Amali Said. Wakati sherehe ikiendelea Amani alivitazama viti vilivyokuwa mbele yake ni vitupu ni viti walivyokuwa wameandaliwa wazazi wa maharusi yaani wazazi wa Amani na Liya au tuseme walezi. Viti vilikuwa vitupu hakuna mzazi au mlezi aliyehudhuria ukumbi ulijazwa na ndugu na jamaa na marafiki wengine. Hili jambo lilimshughulisha mno Amani akachukuliwa ghafla na mawazo akatuama mawazoni kwa muda akavuta pumzi
"kwanini lakini?” Alijiuliza Amani hakupata jibu ya maswali yote yaliyokizonga kichwa chake.
“Nimekosa nini kwa Mungu?”
“Eeh Mungu wangu niongoze mimi mwanzo” Amani alisali kimoyomoyo.

Amani akiwa ametuama mawazoni
sherehe ikiwa inaendelea zilisikika kelele zikitokea upande wa mlangoni.
“Kuna nini huko mlangoni?” aling'aka mshereheshaji.
Ilikuwa ni watu wanne waliovalia nguo za kipolisi waking'ang'ania kuingia ndani kwa ulazima. Punde si punde walifanikiwa kuingia ndani baada ya kuishinda kamati ya ulinzi ya sherehe ile pale malangoni mwa ukumbi. “ MC tunaomba maiki DJ zima muziki haraka”aliamrisha kwa ubabe na kwa sauti ya kukoroma Afande Hashimu.
MC Oscar alimkabidhi maiki na baada ya muziki kuwa umezimwa

“Huu ndiyo mwisho wa sherehe hii haramu na maharusi mpo chini ya ulinzi”
Amani alisimama na kusogea akijaribu kutaka kuongea na Hashimu “Afande naomba hao wanandoa haramu wakamatwe mara moja wapo chini ya ulinzi” aliamuru Afande Hashimu.
“Lakini…lakini…Afande…” Amani alikatishwa
“Haya mpo chini ya ulinzi maelezo yote kituoni”Aliongea Afande mmoja huku akimtia pingu Amani.
Amani na Liya walitiwa nguvuni ilikuwa ni usiku wa saa tano ndiyo kwanza sherehe imeanza kuchanganya. Polisi waliwatia pingu mikononi Amani na Liya huku wakiwakokota kama majambazi wa kutumia silaha. Waliwatoa nje na kuwapeleka kwenye gari yao ya polisi. Ndani ya ukumbi tahaluki ikazidi maneno yakawa mengi kila mtu akaongea lake,
“nilijua tu chezeya jamhuri weye hehehe heee!” Alisikika akiongea kwa kebehi moja ya mgeni mwalikwa aliyekuwa amekaa karibu na mlango wenyewe wanamwita “malkia wa kuchamba”
Shoga weee halo haloo! Teeena” alidakia jirani yake maarufu kwa jina la “mama pilikapilika”
Basi hali ndivyo ilivyokuwa mle ndani. Siku zote mambo yakikwendea kombo siyo wote watakaosikitika wengine watafurahi sana. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Amani wapo waliosema alikuwa anajidai polisi kiko wapi kakamatwa na polisi wenzie. Wengine wakatoa unabii wakisema “tulijua tu Amani na Liya hii ndoa haramu haitawaacha salama”.
Ikawa ilivyokuwa Mwenye lake alisema, mwenye kusikitika hivyo hivyo mithili ya bahari ya Hindi kila mtu anaogelea kwa namna yake.
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA PILI

Gari ya polisi iliwashwa kuelekea kituoni. Amani alionekana mtu aliyejawa na hamaki, hisia za kufedheheka zimemjaa . Mawazo yakiwa yamemtanda akamwangalia Hashimu Kwa jicho la hasira na kisirani.
"Siamini kama Hashimu ungeweza kunifanyia hivi" aliongea Amani Kwa sauti ya masikitiko
"Lakini Kwa Nini lakini Hashimu?" Alilalama
"Tatizo jinai baba" alijibu Hashimu
"Jinai? Haa! Jinai ndiyo iliyofanya uje kunikamata Kwa kunifedhehesha tena katikati ya harusi yangu? Siku muhimu katika maisha yangu? Kwanini usisubiri sherehe iishe?" Amani alizidi kulalama
"Lakini sijavunja sheria yoyote, mwosha huoshwa, Amani umesahau kwamba wewe pia ulikuwa askari? Umesahau uliyokuwa unayafanya? Wewe Amani huna uhalali wa kunifundisha mimi ustaarabu katika kazi huna?" Alijibu Hashimu huku akitoa kipisi Cha sigara katika mfuko wa shati na kukiweka mdomoni.
"Nimesema sijavunja sheria yoyote, once a criminal always a criminal" aliongeza Hashimu.
Tangu hapo Amani hakujibu chochote alijikalia kimya

Gari ilisimama kituo Cha polisi kinondoni Amani na Liya walishushwa kwenye gari na kupelekwa mahabusu Kila mtu chumba chake.
"Leo utafanyia Honeymoon humu ndani" Hashimu alimwambia Amani Kwa kejeli huku akifunga mlango wa mahabusu.

Usiku ule ulikuwa mrefu Kwa Amani na Liya. Liya alichuruzika machozi usiku kucha. Ama kweli mapenzi mashenzi, furaha yangu imegeuka huzuni, lakini ni kosa la nani? Sisi tuna kosa gani? Kosa letu ni kupendana?. Hayo ni badhi ya maswali yaliyoishughulisha akili ya Liya usiku ule. Liya alikuwa amekufa juu ya Amani wenyewe wanasema kafa kaoza, aambiwi akaambilika. Hasikii la mshauri Wala nani. Wameongea wamechoka ni kama wanampigia mbuzi gitaa vile.

Kwa upande wake Amani juu ya Liya alikuwa amefikia point of no return. Hayupo tayari kumwacha Liya. Ilifika hatua wazazi walitishia kumtenga na kumlaani kama hatamwacha Liya lakini hakukubali. Sasa swala limefikia hatua mbaya wazazi wamekuja na sababu mpya kuliharamisha penzi lao. Wazazi wanadai Amani na Liya ni mtu na dada yake yaani watoto wa mama mmoja. Mama yake Liya Bi Betina Mtingo anatajwa kuwa ndiye mama yao Liya na Amani. Swala hili halimwingii akilini Amani, haamini anachoambiwa yeye anachojua mama yake anaitwa Bi Kisa Gwankota na siyo Bi Betina.

Wazazi pande zote mbili wamelivalia njuga swala hili. Mapenzi ya wawili hawa yameingia mdudu, wazazi wanayapiga vita, harusi wazazi wameisusia, wanasema hawawezi kuhudhuria ndoa haramu ndugu wa mama mmoja kuoana si uchuro huu?. Leo hii Amani na Liya wamelazwa mahabusu kosa kubwa likiwa ndugu wa damu kuoana na kushirikiana kimapenzi wenyewe wanaita "incest" ni kosa la wanandugu kufanya mapenzi lililopo katika sheria za nchi hii.
Lakini ukweli wa tuhuma hizi hakuna haujuaye pengine mahakama peke yake ndiyo inaweza kutenda haki. Lakini wazazi wao wanaonekana wamedhamiria ni ama Nia ni kulisambaratisha penzi hili au pengine wasemacho ni Cha kweli hakuna ajuaye.

Usiku ule ulikwisha akina Amani na Liya wakiwa kituoni pale. Kukacha na makucha yake, mapambazuko yakaonekana. Siku ya pili yake Amani na Liya walichukuliwa mpaka kwenye ofisi ya Afande Daudi ambaye aliwachukua maelezo yao na kuyaandika katika karatasi. Watuhumiwa wote wawili katika maelezo yao mbele ya Afande Daudi walikana kuhusika kufanya mapenzi ya wanandugu "incest"kama kosa walilokamatiwa lilivyokuwa likijieleza. Kwa uelewa wao ni kwamba wao si ndugu Kila mtu ana wazazi wake. Liya anadai yeye ni mtoto wa Bi Betina Mtingo na Baba yake ni Andrea Mtingo. Amani anadai yeye ni mtoto wa Bi Kisa Gwankota na baba yake ni Mzee Sauli Sitande.
"Tunao ushahidi wa kutosha kuthibitisha pasi na kuacha shaka yoyote Ile kuwa nyinyi ni ndugu wa damu na mmefanya kosa la "incest" na Kwa sababu hiyo kesho tutawapandisha kizimbani Ili mkajibu mashitaka yanayowakabili". Alieleza Afande Daudi
"Kwa Sasa mtarudishwa tena ndani maana hakuna aliyekuja kuwawekeeni dhamana" aliongeza Afande Daudi
"Lakini Afande Kwa mujibu wa sheria tunatakiwa tuachiwe huru maana hairuhusiwi kutushikiria hapa zaidi ya masaa 24". Alihoji Amani Kwa werevu mkubwa.
"Amani usijifanye wewe ni mgeni na kazi hii mimi ni mtu wa kupokea amri tu" alijibu Afande Daudi
"Ina maana umepokea amri kutoka juu? Alihoji Amani huku akihamaki
"Usitake kuniharibia kazi, ninaomba urudi mahabusu". Alijibu Afande Daudi Kwa kufoka.
"Sikuharibii kazi ila ni haki yangu ya kisheria, saa 24 zinakwisha Leo hivyo Leo hii ilitakiwa tuachiwe huru ama tupandishwe kizimbani" alifafanua Amani kisheria zaidi.
"Ohoo unajitia unajua sheria siyo? Unataka kuniletea vurugu mimi? Sivyo?". Aling'aka Afande Daudi huku akinyanyuka kitini.
"Afande Nyandu na Gosha nyooni" aliita Afande Daudi

Basi wakaja Afande Nyandu na Gosha ni maafande waliojazia kidogo hivi wakawabeba mzobemzobe wakianza na Amani alijaribu kufurukuta wakamshinda nguvu, wakarudishwa mahabusu yeye na kipenzi chake Liya kusubiri siku itayofuata ambapo watapandishwa kizimbani Kwa mujibu wa Afande Daudi...

ITAENDELEA
 
Back
Top Bottom