Riwaya - Moyo wa Mama!

Riwaya - Moyo wa Mama!

Joined
Aug 12, 2011
Posts
7,150
Reaction score
14,724
Moyo wa Mama!

Na Bishop Hiluka

ZAWADI, msichana mwembamba mrefu, akiwa na urefu wa futi tano na inchi kumi na mwenye umbile lililovutia mno alikuwa anatembea taratibu kando kando ya barabara ya SUA, barabara inayoelekea katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.

Zawadi alikuwa anatokea kwenye mzunguko uliokuwa unaziunganisha barabara za Sua, Madaraka na ile inayoelekea eneo la Uwanja wa Ndege katika manispaa ya Morogoro.

Kwa mwonekano tu Zawadi alionekana kuwa na umri wa miaka 25. Nywele zake zilikuwa nyeusi tii zilizotumwa vema sambamba na sura yake iliyokuwa na mvuto wa asilimia mia moja. Nyusi na kope zake zilikuwa ndefu zilizong’ara na kuyafanya macho yake yawe wazi nusu.

Pua yake ilikuwa ndogo kiasi iliyoiacha midomo yake ijidai kwa kuhifadhi meno meupe yaliyojipanga vizuri huku yakiachia kijiuwazi kidogo kwa mbele. Alikuwa mweupe mithili ya chotara, lakini si ule weupe wa mkorogo bali weupe wa asili wenye ung’avu wa kuteleza.

Alikuwa na shingo nzuri iliyokaa vyema katikati ya mabega yake ya kike mazuri na kifua chake kilibeba matiti ya wastani yaliyochongoka mbele na yaliyokuwa na hasira ya kutoboa gauni alilovaa. Tumbo lake lilikuwa flati na kiuno chake kilikuwa chembamba mithili ya dondola.

Katika muda ule wa asubuhi Zawadi alitembea taratibu huku akiwa kainamisha kichwa chake. Alionekana kuchoka sana na mwenye mawazo mengi.

Mkono wake wa kulia alikuwa amebeba kikapu kilichokuwa na bidhaa mbalimbali ndani yake alizotoka kuzinunua katika soko kuu la manispaa ya Morogoro, na mkono wake wa kushoto alikuwa kauzungusha kwa nyuma.

Zawadi alitazama huku na kule na kushusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani huku akikunja sura yake kana kwamba alihisi maumivu makali ya kichwa na kutupa macho yake kuwatazama watu wachache aliopishana nao wakiwa katika haraka za kuwahi mishemishe asubuhi ile.

Aliwatazama wale watu kwa makini, wengi walionekana ni wenye furaha katika asubuhi ile, lakini yeye alijiona kuwa mpweke na mnyonge. Hakujua ni kwa nini alijihisi upweke na nini kilikuwa kimemnyang’anya furaha yake katika asubuhi ile! Alitafakari sana lakini hakupata jibu!

Watoto wawili watatu walikuwa wanakimbizana kando kando ya barabara ile ya Sua wakicheza na kumpita. Mmoja wa watoto hao alimkumba Zawadi lakini binti yule alimwangalia tu bila kuonesha hisia zozote za kukerwa, bali aliendelea kutembea taratibu pasipo kujishughulisha na watoto hao.

Alipita jirani na Kambarage Bar and Garden iliyokuwa upande ule wa kushoto kwake kando ya barabara ya SUA na kuwatupia jicho watu wachache waliokuwa wameketi kwenye viti vya plastiki chini ya miti ya vivuli wakiwa na chupa za bia.

Nyuma ya baa hiyo ilionekana mandhali ya uwanda mpana wenye eneo kubwa lenye miti mikubwa kwa midogo na uwanja wa mpira wa Shule ya Msingi Kikundi.

Mbele ya uwanda huo mpana wenye miti kuna mto Kikundi unaokatiza katika soko la Manispaa ya Morogoro na kwenda kumwaga maji yake katika mto Mafisa.

Kwenye mandhali hiyo nzuri ya bustani katika baa ya Kambarage, kijana mmoja mtanashati alikuwa akimwita Zawadi lakini yeye hakumjali. Aliendelea kutembea taratibu pasipo kujihusisha na mtu mwingine.

Mbele kidogo ya baa ya Kambarage upande huohuo wa kushoto alilipita soko dogo la Kikundi lililo kando kando ya barabara ya Sua, soko lile lilikuwa limesambaa katika uwanda mpana wenye miti uliosambaa hadi katika mto Kikundi na Shule ya Msingi Kikundi.

Zawadi aliwapita wachuuzi kadhaa wa mboga, matunda, vitafunwa vya aina mbalimbali na bidhaa zingine kando ya eneo la soko la Kikundi, hakujihusisha nao kabisa, bali alionekana kuzama kwenye lindi mawazo.

Wakati akipita kando ya miti mikubwa aliwaona ndege wa kila aina waliokuwa wakilia kwa namna ya kuisifia asubuhi hiyo na kuifanya kuwa njema, ingawa kwake aliiona haikuwa njema kabisa. Tena ndege hao walionekana kuwa ni wenye furaha kubwa na kulipa uhai eneo lote lililoonekana tulivu mno.

Alijikuta akisimama kwa muda kuwasikiliza ndege hao kwa makini, akajaribu kubashiri nyimbo nzuri walizokuwa wakiimba, akayasikia hadi maneno yaliyotamkwa katika nyimbo hizo ambayo ki ukweli yalibeba ujumbe mzuri wa faraja. Alijikuta akishusha pumzi ndefu akionekana kufarijika kidogo.

Alitabasamu na kuanza kutembea kando kando akiifuata barabara ya Sua inayoelekea Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, safari hii aliongeza mwendo kidogo akionekana kupata nguvu mpya.

Hakwenda mbali zaidi akasita na kuyakaza macho yake kutazama mbele yake. Kundi la watu, wakubwa kwa wadogo, wake kwa waume walikuwa wakiifuata ngoma ya Vanga iliyokuwa inatokea eneo la Msufini na kuja kwenye uelekeo wake.

Kundi hilo la watu lilimvuka Zawadi huku wakitimua vumbi utadhani ni msafara wa nyumbu wanaohama kutoka mbuga ya Serengeti na kuvuka mpaka wakiingia Kenya. Walikuwa wanarukaruka na kunengua viuno kwa furaha huku wakiimba kufuatisha midundo ya ngoma kubwa iliyokuwa ikipigwa.

Kundi hilo la watu walikuwa wanachutama na kuinuka kila walipokuwa wanaimba kiitikio cha ‘Nimeokota kidude!

Itaendelea...
 
Moyo wa Mama! - 2

Kundi hilo la watu lilimvuka Zawadi huku wakitimua vumbi utadhani ni msafara wa nyumbu wanaohama kutoka mbuga ya Serengeti na kuvuka mpaka wakiingia Kenya. Walikuwa wanarukaruka na kunengua viuno kwa furaha huku wakiimba kufuatisha midundo ya ngoma kubwa iliyokuwa ikipigwa.

Kundi hilo la watu walikuwa wanachutama na kuinuka kila walipokuwa wanaimba kiitikio cha ‘Nimeokota kidude!

Zawadi aliwaangalia kwa makini huku akifunika uso wake kwa khanga kukwepa vumbi walilotimua, aliwatupia jicho na kuonekana kushtuka mno, akayakaza macho yake kumwangalia kijana mmoja shababi mwenye mwili uliojengeka kwa misuli.

Kijana huyo alikuwa katikati ya kundi la watu akipiga ngoma kubwa kwa ustadi mkubwa na mbwembwe nyingi, huku mabinti kadhaa waliojifunga kibwebwe wakinepa kufuatisha midundo ya ngoma.

Kijana huyo aliitwa Daudi, alikuwa akiishi jirani na alilokuwa akiishi Zawadi la Manzese, na alikuwa katika umri wa miaka therathini. Daudi alikuwa amevaa fulana nyekundu na kujifunga kilemba chenye nembo ya Manchester United kichwani.

Daudi alikuwa akiipiga ngoma kubwa kwa ufundi mkubwa huku akitokwa jasho. Zawadi alimtazama kwa makini na kuachia tabasamu kisha akavuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu huku akiendelea kutabasamu.

Zawadi alisimama kando akilipisha lile kundi lipite ili yeye aendelee na safari yake.

Baada ya kundi lile kupita alianza kupiga hatua bila kugeuka kokote na kuanza kuvuka barabara kuelekea upande wa pili wa barabara akitaka kuingia barabara inayoelekea katika soko la Manzese.

Alipokuwa katikati ya barabara, kabla hajavuka sauti ya msuguano wa matairi kwenye lami kutokana na breki kali na honi kali za gari vikasikika kwa pamoja na kumshtua sana Zawadi.

Zawadi alipiga yowe kwa hofu huku akijikunja na kuruka kurudi nyuma akiwa kafumba macho yake.

Magurudumu ya gari la kifahari aina ya BMW X6 xDrive 50i yalisota kwenye lami huku gari hilo likiyumba na kumgonga Zawadi na kumtupa kando ya barabara, lakini hakupata madhara.

Katika kuanguka Zawadi aliangusha kikapu chake katikati ya barabara, magurudumu ya gari yakakikanyaga na kusaga saga kila kitu kilichokuwa ndani ya kile kikapu.

Akiwa pale chini Zawadi alifungua macho yake kwa hofu kulitazama gari lililomgonga.

Gari hilo la kifahari lilisimama katikati ya barabara, dereva wa gari hiyo alikuwa mwanamama mrefu mwenye umbo kubwa lililovutia mno, likiwa limesheheni vema na kunesanesa.

Mwanamama huyo aliitwa Tabia Msimbe na alikuwa na umri wa miaka 42. Alikuwa mrefu aliyekadiriwa kuwa na futi tano na inchi kumi, na alikuwa mweupe, weupe wake siyo ule wa kujichubua bali wa asili. Kwani alikuwa chotara aliyetokana na mama Mkaguru na baba chotara wa Kigiriki na Kiluguru.

Rangi yake ilikuwa ina mng’aro wa aina yake na ilipendeza sana, ikiwa na mvuto wa pekee kiasi cha kumfanya kuonekana bado msichana mdogo tofauti na umri wake, na wala hakuhitaji kabisa vikorombwezo vya aina yoyote kuinakshi ngozi yake.

Tabia alikuwa amevaa miwani myeusi ya jua, na alipoivua miwani hiyo ndipo yalipoonekana vyema macho yake, ambayo yalikuwa ni aina ya yale macho yanayoita kwa mng’aro sadifu, yakiambatana na kope nyingi nyeusi ambazo ziliachia nafasi kwa nyusi ili zipate kujidai.

Kwa kweli Tabia hakuwa mwanamke wa kumtizama mara moja tu ukamwacha.

Alipoivua miwani alimtazama Zawadi kwa hasira iliyochanganyika na kiburi cha kujiona kwa paka, akakunja sura yake na kushuka kwenye gari huku akimkazia macho Zawadi. Macho yao yakakutana.

Tabia alisonya kwa dharau na kuzunguka upande wa pili wa gari, akalikagua kwanza gari lake kuangalia kama halijaharibika, aliporidhika ndipo akamsogelea Zawadi ambaye kwa muda ule alikuwa wima akimtazama tabia kwa wasiwasi.

Tabia alimkwida Zawadi kwa hasira na kumtingisha kwa ghadhabu huku akifoka bila kujali umati wa watu walioanza kujaa eneo hilo.

“Wewe mpumbavu sana, unavuka bila kuangalia unadhani hii ni barabara ya mama yako? Kwa nini hauko makini unapotaka kuvuka barabara?”

Zawadi alimtazama mwanamama yule kwa wasiwasi, alitaka kusema neno lakini akasita, wingu zito la huzuni lilionekana kwenye macho yake huku machozi yakianza kumlenga machoni.

”Ningekubamiza kichwa chako kwenye mti kama ungeharibu gari yangu. Unaijua thamani ya gari hii wewe? Mpumbavu mkubwa!” alifoka yule mwanamke huku akimwachia Zawadi.

Zawadi alimtazama Tabia kwa wasiwasi katika hali ya kuomba msamaha. Mikono yake yote miwili aliikunjia kifuani.

“Samahani sana, mama...”

“Samahani…! Kwanza nani mama yako hapa?” Tabia alimkata kauli Zawadi kwa hasira huku akimkazia macho yaliyokuwa yanawaka kwa hasira.

“Ufanye ujinga na kutaka kunisababishia kesi halafu unasema kirahisi rahisi tu, eti ‘samahani mama!’ Mjinga sana wewe!” alizidi kubwata yule mwanamke kwa hasira na kubana pua pale alipotamka neno ‘samahani mama’, kisha akamsukuma Zawadi kwa hasira.

Zawadi alidondoka chini na kupata michubuko kwenye kiwiko cha mkono wake wa kushoto. Hakuwa na la kusema bali aliinua uso wake kumtazama yule mwanamke na kuanza kulia kwa uchungu.

Itaendelea...
 
Moyo wa Mama! - 3

Zawadi alidondoka chini na kupata michubuko kwenye kiwiko cha mkono wake wa kushoto. Hakuwa na la kusema bali aliinua uso wake kumtazama yule mwanamke na kuanza kulia kwa uchungu.

Bila kujali kilio cha uchungu kutoka kwa Zawadi, Tabia alilizunguka gari lake na kufungua mlango, akaingia na kuketi kwenye siti kisha akapiga ngumi juu ya usukani wa lile gari kwa hasira.

Hakuondoa gari bali aliamua kujiinamia akiulalia ule kwenye usukani wa gari kwa kitambo kidogo akionekana kama aliyekuwa akilia kwa uchungu kilio cha kwikwi.

Magari mawili matatu yalikuja na kusimama nyuma ya gari la Tabia, kwa kuwa alikuwa amesimamisha gari lake katikati ya barabara wale madereva way ale magari yaliyokuwa nyuma ya gari lake waliamua kupiga honi.

Tabia alishtuka na kuinua kichwa chake, akaangalia nyuma yake kupitia kwenye kioo cha gari cha katikati, aliyaona yale magari ya nyuma yake yakimuwashia taa kumuashiria aondoke barabarani.

Macho yake yalikuwa yamewiva na kuwa mekundu kwa kulia na machozi yalikuwa yakimtoka, hivyo akatoa tishu laini kutoka kwenye kiboksi cha tishu kilichokuwa juu ya dashbodi ya gari lake na kufuta machozi bila kujali kama yale magari yalikuwa yakipiga honi kumtaka aondoe gari barabarani.

Alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kujitengeneza vizuri kisha aliliondoa gari lake. Wakati gari ikiondoka kwa kasi Tabia aligeuza shingo yake kumtazama Zawadi kwa makini.

Zawadi alikuwa bado amesimama akiwa anafuta machozi. Watu waliokuwa wamejaa eneo hilo walibaki wanashangaa na baadhi yao walikuwa wakimlaani yule mwanamke kwa tabia yake aliyoionesha kwa Zawadi.

Zawadi alijifuta vumbi na kupangusa damu kwa kanga iliyokuwa ikimtoka kwenye kiwiko chake cha mkono, akakitazama kikapu chake kilichokuwa hakitamaniki pale barabarani.

“Hakyamungu yule mama siyo mzima kabisa,” alisema kijana mmoja mtanashati aliyelishuhudia tukio akiwa mbali na kufika pale muda mfupi kabla gari la tabia halijaondoka, kisha akampa pole Zawadi.

“Pole sana dada yangu, msamehe bure tu yule mama, ana matatizo makubwa ya kisaikolojia, maana…”

“Matatizo gani bwana, hamna ya sekenolojia wala nini, kile ni kiburi tu cha pesa,” alidakia mama mmoja mchuuzi wa mboga katika soko la Kikundi, kwa uchungu.

“Hawa wenzetu wenye pesa ndivyo walivyo, wanatunyanyasa sana sisi tusiokuwa nazo, haiwezekani umgonge mtu halafu ukimbilie kuangalia gari lako kama zima bila kumjali yule uliyemgonga! Hii ni roho ya kichawi kabisa!” Aliongeza yule mama mchuuzi wa mboga kwa hasira huku akisonya.

“Yule mama ana matatizo, mimi namfahamu vizuri, ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine na amenifundisha pale SUA. Kuna wakati unaweza kumkuta analia tu bila sababu, wakati mwingine anaweza kumkasirikia kila mtu bila hata sababu…” alisema yule kijana mtanashati kwa msisitizo.

“Au laana?” aliuliza mwanamke mmoja mnene na kuongeza, “Maana nasikia aliwahi kugombana na mama yake mzazi na walikuwa hawaongei hadi mama yake amekufa.”

“Unajua kwa nini aligombana na mama yake?” yule kijana mtanashati akadakia kwa swali.

“Kwa nini?” yule mwanamke mnene akauliza kwa shauku.

“Nasikia ni kwa sababu ya mtoto…” alijibu yule kijana mtanashati. Watu wakaanza kujikusanya kusikiliza wakimzunguka yule kijana mtanashati kwa shauku.

Zawadi hakutaka kuendelea kukusimama pale, alitazama huku na huko na kuvuka barabara haraka, akaelekea upande wa pili akiifuata barabara iliyoelekea Manzese huku akiwaacha wale watu wanaendelea kumjadili Tabia.

Watu waliokuwa wamejazana eneo lile waligeuza vichwa vyao kumsindikiza Zawadi kwa macho ya huruma na wengine waliendelea kumpa pole, huku wengine wakimlaani yule mama jeuri asiye na huruma.



* * * * *



Familia ni kitu cha ajabu sana, ajabu yake ni kwamba hakuna aliyewahi kuchagua azaliwe familia fulani. Wakati mwingine ungeweza kutaka uwe kwenye familia tofauti na uliyopo, jamaa tofauti na hata marafiki tofauti, lakini bado imeendelea kuwa ni kitu ambacho hakuna mwenye uwezo huo.

Inafikia wakati mtu angetamani kumiliki vitu kama ambavyo watu wengine wanavimiliki kwa sababu tu hana kile ambacho watu wengine wanavyo.

Lakini kwa Zawadi yeye hakuwa na makuu, alitamani kitu tofauti kabisa. Yeye alikuwa miongoni mwa watu wachache ambao walikuwa wanaridhika na familia walizonazo pasipo kujali uwezo wa familia hiyo, walichokuwa wanataka wao ni upendo na familia hizo kuwajali, basi.

Zawadi alikuwa akiishi na mama yake katika eneo la Uswahilini la Manzese, kwenye nyumba moja iliyokandikwa kwa udongo na yenye mabati yaliyochoka na kubadilika rangi kutokana na kutu iliyokuwa imeyashambulia.

Ingawa waliishi maisha ya kimasikini lakini aliamini kuwa siku moja haya yote yatakuwa historia na ndoto yake itakuwa kweli siku moja.

Hakuwa na elimu kubwa lakini aliamini kuwa elimu ya kidato cha sita aliyoipata kutoka katika Shule ya Sekondari ya Morogoro ulikuwa msingi mzuri ambao ungemsaidia kufikia malengo yake.

Majira ya alasiri Zawadi alikuwa nyumbani akiwa anafua nguo zake huku akiwa anaimba. Akiwa katika kumalizia, alizisuuza kwa maji safi na kuanza kuzianika juu ya kamba iliyokuwa imefungwa pale nje ya nyumba kati ya miti miwili mikubwa.

Itaendelea...
 
Moyo wa Mama! - 4

Majira ya alasiri Zawadi alikuwa nyumbani akiwa anafua nguo zake huku akiwa anaimba. Akiwa katika kumalizia, alizisuuza kwa maji safi na kuanza kuzianika juu ya kamba iliyokuwa imefungwa pale nje ya nyumba kati ya miti miwili mikubwa.

Kitu kimoja kilichokuwa kinamsumbua Zawadi siku ile ni kuwa alikosa raha, hakuwa mchangamfu na alionekana dhaifu aliyekuwa kachoka sana.

Wakati akiendelea kuanika nguo alihisi kizunguzungu, hasa alipoinuka ili kuanika nguo ya tatu kwenye kamba.

Alifumba macho yake na kupeleka mkono wake wa kushoto kushika kamba ambayo aliitumia kujiegemeza ili asidondoke, lakini akaonekana kuyumba kidogo.

Kwa kutumia mkono wake wa kulia alikunja ngumi na kuupeleka mkono huo katika kifua chake upande wa kushoto wa kifua. Akiwa bado kafumba macho alikunja uso wake akionekana dhahiri kuhisi maumivu makali ya kifua.

Alishusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani na kukohoa. Kisha alijilazimisha kuendelea na kazi ya kuanika nguo. Alichukua gauni na kulitundika juu ya kamba, akasita na kusimama kwa muda, uso wake kaukunja akionekana kuwa katika maumivu makali.

Alishika tena kifua chake huku akiyasikilizia mapigo ya moyo wake, ambayo kwa wakati huo yalionekana kubadilika na kwenda kasi zaidi. Akaanza kuona kizunguzungu zaidi na kupiga mweleka chini.

Alijaribu kufungua mdomo wake ili kuita lakini sauti ilikuwa haitoki. Aliyakodoa macho yake lakini ukungu mwepesi ulitanda kwenye macho yake na kumfanya kuona vitu vyote kama vivuli.

Muda huo, Daudi, yule kijana aliyempita asubuhi akiwa katikati ya kundi la watu akipiga ngoma kubwa kwa ustadi mkubwa alionekana kupita katika njia iliyopita eneo la nyumba hiyo.

Daudi alikuwa na kawaida ya kupita pale na kuwajulia hali na alipenda sana utani, lakini alishangaa sana kumuona Zawadi akiwa chini akiwa anatapatapa.

Alimsogelea huku akimwita kwa wasiwasi, alishtuka sana alipomuona Zawadi akiwa ameshika kifua chake huku akiwa amefinya macho yake kuashiria kuwa alihisi maumivu makali.

Zawadi alifumbua tena mdomo wake kutaka kusema lakini maneno yalikuwa hayatoki. Hata alipofumbua macho yake kumkodolea Daudi lakini hakumuona vizuri, aliona mfano wa taswira ya mtu kwenye ukungu mzito ikiwa imemsiamamia mbele yake.

Zawadi akafungua tena kinywa chake kutaka kuzungumza lakini alijikuta akiishia kufumbua mdomo tu huku maneno yakiwa hayatoki. Alizidi kukunja uso wake huku akiugulia kwa maumivu.

Daudi alisimama akimtazama Zawadi kwa wasiwasi, alionekana kuogopa sana na kuanza kupaza sauti yake akiita huku akiangalia huku na kule kutafuta msaada.

Alizidi kuita kwa nguvu lakini hakuna aliyetokea. Eneo lile lilionekana kutawaliwa na ukimya. Akashangaa sana maana hata majirani hawakuwepo.

Daudi akamtazama tena Zawadi kwa hofu asijue kilichompata. Alionekana kuguswa sana na hali ya Zawadi. Hakusubiri zaidi, bali alikimbilia barabarani kutafuta msaada akimwacha Zawadi bado yupo chini akigaagaa kwa maumivu.

Daudi alikimbia huku na huko kutafuta msaada lakini hakukuwa na gari yoyote iliyokuwa inapita muda huo katika mtaa ule, akaamua kwenda mbele zaidi na kutokea Barabara ya Sua.

Alisimama katikati ya barabara ya Sua akiwa amekata tamaa, mara akaiona gari ndogo aina ya BMW X6 xDrive 50i ikija upande wake kwa mwendo wa kasi ikitokea Chuo Kikuu cha Sokoine.

Daudi aliendelea kusimama pale katikati ya barabara na kunyoosha juu mikono yake kupunga akimwashiria dereva wa gari hiyo, mwanamama Tabia kusimama.

Tabia hakuonekana kutaka kusimama wala kupunguza mwendo kwani aliwasha taa kubwa za mbele za gari yake kumwashiria Daudi aondoke katikati ya barabara huku akimpigia honi.

Daudi alipuuza na kuendela kusimama katikati ya barabara huku akipunga mikono yake yote miwili juu kwa nguvu zote kumtaka dereva wa gari hiyo asimame.

Baada ya juhudi za kuwasha taa na kupiga honi ili kumfanya Daudi atoke katikati ya barabara kushindwa, Tabia hakuwa na namna nyingine ya kufanya bali kusimama, hivyo alikanyaga breki kwa nguvu na gari yake ilisota na kuyumba kwenye lami huku akijaribu kumkwepa Daudi aliyekuwa bado kasimama katikati ya barabara.

Tabia akasonya kwa hasira na kukunja ngumi huku akipiga katikati ya usukani wa gari yake kwa hasira. Gari ilisimama hatua hatua chache mbele ya Daudi.

Tabia alikunja uso wake na kuitazama saa yake ya mkononi, ni saa ghali sana ya kike aina ya Swatch Skinmesh, ambayo bei yake si haba, kwani aliinunua Pauni elfu tisini za Uingereza. Tabia alipoitupia jicho saa yake alisonya tena akionekana kuwa na haraka na hakuwa na muda wa kupoteza kutokana na majukumu mazito aliyonayo.

Aliinua uso wake kumtazama Daudi kwa makini huku akionekana kukerwa na kitendo chake cha kumlazimisha kusimama. Hata hivyo aliamua kusubiri asikie kilichomfanya kijana huyo kumsimamisha pale.

Bila kujali namna alivyomtazama, Daudi aliisogelea gari hiyo karibu na kusimama kando ya kioo cha dirisha la dereva huku akimtazama mwanamama huyo kwa makini na kuachia tabasamu la urafiki.

Tabia aliendelea kubaki kimya akimtazama Daudi kwa makini bla tashwishwi na macho yake yalikuwa yameficha kiburi. Baada ya kumuona Daudi akitabasamu, naye aliminya midomo yake huku akiachia tabasamu la dharau na kuendelea kumkazia macho Daudi.

“Una wazimu au kitu gani! Ningekugonga ungekuwa na hali gani saa hizi?” Tabia alimuuliza Daudi kwa sauti tulivu mara tu Daudi aliposimama kando ya dirisha lake.

Itaendelea...
 
Moyo wa Mama! - 5

“Una wazimu au kitu gani! Ningekugonga ungekuwa na hali gani saa hizi?” Tabia alimuuliza Daudi kwa sauti tulivu mara tu Daudi aliposimama kando ya dirisha lake.
“Samahani mama, nahitaji msaada wako, kuna mgonjwa anahitaji msaada wa haraka sana wa kukimbizwa hospitali, samahani sana…”
Tabia alimtazama Daudi kwa hasira akionekana kuchukizwa mno, kisha akasonya kwa dharau.
“Mjinga kabisa wewe! Mi nilidhani umenisimamishia kitu cha maana kumbe ni huo ujinga? Uliambiwa hii ni teksi, au mimi nafanana na dereva wa teksi?”
Daudi alimtazama Tabia kwa kitambo kidogo akionekana kufikiria aseme nini, alionekana kuhuzunika sana huku machozi yakimlenga machoni. Kabla hajasema kitu, Tabia alitema mate chini kwa dharau na kuiondoa gari yake kwa fujo kutoka eneo hilo.
Daudi aliisindikiza gari ya Tabia kwa macho huku akishangaa, kisha alinyanyua mabega yake na kubetua midomo na kugeuza shingo yake kutazama huku na huko akionekana kukata tamaa.
Muda huo wingu zito la mvua likaanza kujikusanya angani, Daudi alinyanyua uso wake kutazama angani, akashika kichwa chake akionekana kuwaza mbali sana, kisha akaanza kutembea taratibu akionekana kupoteza matumaini.
Alitembea kwa muda kidogo pasipo kuona gari yoyote, na alipoanza kukata tamaa mara aliiona gari nyingine ndogo aina ya Toyota Verossa ikija katikaa eneo hilo ikitokea Chuo Kikuu cha Sokoine. Daudi alishusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani huku akipunga juu mikono yake kuisimamisha.
Ile gari ilipunguza mwendo na kusimama na dereva wa gari ile mwanamke mmoja, Dk Pamela Mwambe alishusha kioo cha gari yake na kumtazama Daudi kwa makini. Daudi alisimama akimtumbulia macho Dk Pamela kwa wasiwasi.
Dk Pamela alikuwa mnene wa wastani, hakuwa mfupi wala mrefu bali alikuwa na kimo cha wastani na rangi ya maji ya kunde iliyokuwa ina mng’aro wa aina yake.
Japo alikuwa na umri wa miaka arobaini na saba, lakini ilikuwa vigumu mno kumtofautisha na wasichana wenye umri mdogo kutokana na jinsi alivyokuwa kajitunza.
Dk Pamela alikuwa Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo hapo Morogoro.
“Unasemaje kijana?” Dk Pamela alimuuliza Daudi baada ya kumuona akiwa amesimama kwa wasiwasi.
“Samahani, mama, nilikuwa nahitaji msaada wako…”
“Ulikuwa? Kwani sasa hivi hauhitaji tena msaada wangu?” Dk Pamela alisema huku akimkazia macho Daudi aliyeonekana kubabaika kidogo.
“Bado ninahitaji… kuna mgonjwa anahitaji msaada wa haraka sana wa kukimbizwa hospitali, naomba msaada wako mama,” Daudi alisema kwa huzuni huku akimtazama yule mama kwa wasiwasi.
“Yuko wapi?” Dk Pamela aliuliza huku akimkazia macho Daudi.
“Si mbali kutoka hapa, ni hapo mtaa wa pili kama unaelekea soko la Manzese,” Daudi alisema huku akielekeza kwa kidole chake.
“Anaumwa nini?”
“Sijui, nilikuwa napita nikamkuta kaanguka chini akilalamika maumivu ya kifua, naomba tumsaidie kabla hali yake haijawa mbaya zaidi,” Daudi alisema huku machozi yakianza kumlenga.
Dk Pamela alimtazama Daudi kwa mashaka kwa kitambo huku akionekana kujishauri, akashusha pumzi za ndani kwa ndani huku akilamba midomo yake. akatingisha kichwa chake kuonesha hayuko tayari kutoa msaada.
“Ningekusaidia lakini kuna sehemu natakiwa kuwahi,” hatimaye alisema yule mama kwa huzuni huku akimtazama Daudi kwa makini zaidi.
“Tusaidie, mama, Mungu atakulipa, pia nitachangia hela ya mafuta,” Daudi alisema kwa sauti ya kukata tamaa huku machozi yakianza kumlenga machoni.
“Sijui kwa nini nashindwa kukuamini, isije ikawa janja yako ili…” Dk Pamela alisita kidogo na kumtazama kwa makini Daudi aliyeanza kulia kwa uchungu huku akiwa amekunjia mikono yake yote miwili kifuani katika namna ya kuomba msaada.
“Tafadhali, mama naomba tumsaidie kumpeleke hospitali vinginevyo atakufa, kama ni pesa nitakutafutia, mama yangu,” alisema Daudi huku akifuta machozi yaliyokuwa yakimlenga.
“Wala siyo suala la pesa, ila…” alisema akasita tena na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.
Muda huo upepo ulianza kuvuma huku ukilisukuma lile wingu kuelekea upande wa mashariki, kisha manyunyu hafifu ya mvua yakaanza kuanguka kutoka angani kulikotanda wingu zito la mvua.
Dk Pamela akashtuka na kutazama angani, alionesha kusita sana lakini akamtazama Daudi kwa muda na kushusha pumzi ndefu kisha akampa ishara Daudi apande ngani ya gari yake.
Daudi alizunguka haraka upande wa pili wa ile gari, akashika kitasa cha mlango wa mbele wa abiria na kuuvuta mlango kisha akazama ndani. Muda ule ule ile gari ikaondoka kwa spidi na kuingia barabara barabara iliyokuwa ikikatisha katikati ya makazi ya watu kuelekea soko la Manzese.
Mara mvua kubwa ikaanza kunyesha na kumtia hofu zaidi Daudi. Dk Pamela aliendesha gari kwa umakini mkubwa katika barabara ile huku akiwakwepa baadhi ya watu waliokuwa wakikimbia kujihifadhi kwenye nyumba jirani kuepuka wasinyeshewe na mvua.

* * * * *

Zawadi alikuwa amelazwa juu ya kitanda kisafi katika wodi maalumu ya wanawake kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro. Mkono wake wa kulia ulikuwa umefungwa mrija wa drip maalumu iliyochanganywa na dawa.
Zawadi alionekana kudhoofika sana huku akionekana kupumua kwa taabu kwa kutumia mashine maalumu ya kumsaidia kupumua.

Itaendelea...
 
Dah! Ngoja nitaitafuta kwenye computer yangu ili niimalizie, maana nina hadithi nyingi kiasi kwamba wakati mwingine sikumbuki. Nadhani niliikatisha kipindi ambacho computer yangu ilikufa na kufuta documents zote...
 
Dah! Ngoja nitaitafuta kwenye computer yangu ili niimalizie, maana nina hadithi nyingi kiasi kwamba wakati mwingine sikumbuki. Nadhani niliikatisha kipindi ambacho computer yangu ilikufa na kufuta documents zote...
Jitahidi kaka.
Iko vyema sana pia mkuu.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom