Simulizi: MFUASI |
14
(MWISHO)
***
|MOROGORO|
Safari ya Chox na Koplo Ponda ikawa ya kibubu bubu. Hakuna aliyemsemesha mwenzake. Mpaka wanafika katikati ya msitu wa kibungo, eneo ambalo lilikuwa kimya sana ndipo Chox akaiingiza gari pembeni na kusimama ghafla.
“Vipi?” Ponda akauliza
“Nahisi kuna tatizo naomba unisaidie kucheki tafadhali.” Chox akajibu huku akifungua dashbodi na kutoa bastola kinyemela wakati Ponda akifungua mlango wa gari kushuka.
“Afande kwani shida yako hasa nini mpaka unataka kumchunguza ndugu yangu na hayo madawa ikiwa unajua akili zake haziko sawa?” Chox akasema kwa wahka baada ya kushuka huku mikono akiwa ameificha bastola kwa nyuma. Ponda alishamstukia, akamtazama kwa makini akiwa amesimama mbele yake.
“Hilo ndilo tatizo ulilosema nikusaidie kucheki?” akamuuliza.
“Yaah tatizo ni wewe kiherehere kutaka kufatilia mambo yasiyokuhusu.” Chox akasema huku akimnyooshea Ponda mdomo wa bastola.
“Na leo ndio utakuwa mwisho na mwanzo wako kujitia mjuaji na mchunguzi kwenye mambo yasiyokuhusu! Sali sala zako za mwisho Koplo!” Akasema huku akitoa usalama wa bastola na kukiweka tayari kidole chake cha shahada kuachia risasi ambayo amekusudia kumtwanga kichwani askari aliyesimama mbele yake.
“Oooh! Kwahiyo unanithibitishia sasa kumbe wewe si mtu mwema na yule si nduguyo?” Ponda akauliza huku akinyoosha mikono hewani.
“Uko sahihi ila haina maana yoyote kwako. Kwaheri!” Chox akasema na ile anataka kufytua risasi tu akawa amechelewa!
Kwa kasi ya ajabu Koplo Ponda akarusha teke kali lililoupiga mkono wa Chox uliokuwa umeshika bastola kizembe. Chox akahamaki kutaka kuiwahi bastola ilipoangukia lakini akajikuta akiangukia mgongo kwa kupigwa ngwala ya teke mzunguko na Ponda ambaye alikuwa na uwezo mkubwa wa kupambana.
“Enhee! Je, haina maana yoyote kwangu?” Ponda akazungumza kwa kebehi akiwa amesimama huku mguu mmoja amemkanyaga Chox kifuani akiwa ametumbua macho pale chini.
Chox akajihami kwa kumputa mguu Ponda ili akabiliane naye ila ndivyo akazidi kufanya makosa. Akajikuta anabutuliwa mateke kama mpira kila alipotaka kusimama akarambishwa udongo.
Mwishowe akawa hoi akihema ulimi nje kama jibwa huku damu zikimvuja puani.
“Basi afandee… naomba tuzungumze nisamehe kaka!” Chox akatweta akiwa taabani. Ponda akamwinamia kwa hasira pale chini akamkemea zaidi.
“Nikusamehe ihali ulikuwa tayari kumuua afisa wa polisi kwa bastola?” huku akimshika kidevu akamtazama kwa ujirani. Akamgeuza na kumfunga pingu mikononi kabla hajamtupia ndani ya gari upande ule wa viti vya nyuma. Alipotazama mbele ya gari kulikuwa na gazeti, akalitumia kuikota ile bastola na kuiweka ndani ya dhashbod kisha akakamatia usukani mwenyewe akawasha gari Koplo Ponda na safari ikaendelea akiifata barabara ya mjini.
* *
Mzee Gulilo akaingia kazini kumtibu Izani kwa dawa za mitishamba. Ndani ya chumba kilichotengwa kwa ajili hiyo matibabu yakawa yanaendelea ambapo Izani baada ya kusafishwa na kupewa chakula, akalazwa kwenye ubao akiwa kama alivyozaliwa, Mzee Gulilo akaanza kumchanja na kumbandika majani aliyoyajua mwenyewe ambayo aliamini yana uwezo ya kunyonya sumu iliyosambaa kwenye damu ambayo inasababisha Izani atepete kwa Alosto. Tiba zilifanyika usiku kucha mzee Gulilo hakulala wala Tibwili hakusinzia kama Muhondogwa.
“Huyu kijana ana nyota ya bahati sana.” Mzee Gulilo akazungumza na Tibwili wakati huo Izani usingizi ulikuwa umemtuliza na mate kuacha kumtoka ovyo.
“Kwanini?” Tibwili akauliza.
“Alikuwa si wa kupona huyu mpaka sasa! Bila shaka hata aliyemtupa aliamini kashakufa.” Mzee Gulilo akasema, Tibwili akatulia kumsikiliza.
“Hii mifyonzamusu huwa inakunywa sumu taratibu kwa siku mbili mpaka tatu! lakini huyu jinsi inavyoelekea kesho tu ataanza kuwa sawa! Si unaona?” Mzee Gulilo akasisitiza huku akizidi kumkandika Izani majani aliyoyaita Mifyozamusu ambayo yalimnatia kama sumaku.
Kulipopambazuka Tibwili akajiandaa na kuchukua baiskeli akapiga pedeli kwenda eneo ambalo network ya simu ilipatikana.
Ilikuwa ni zaidi ya kilomita tano kutoka kijijini kwao. Alipofika huko mtu aliyefikiria kumpigia alikuwa mmoja tu! Zombi Zomboko ambaye aliwahi kuwa mkuu wake kipindi wakiwa kwenye kundi la Simba wasiofugwa kabla Zomboko hajaachana na mambo ya uhalifu.
Ingawa tokea hapo hawakuwa na urafiki wa karibu na Zomboko alibadili namba lakini hakuwahi kufuta namba yake wala Zomboko hakubadilisha namba yake.
Na kweli alipotulia eneo lenye mtandao baada ya kuwasha simu alipopiga namba ya Zomboko ikaita na haikuchelewa kupokewa. Tibwili mapigo ya moyo yakaongeza kasi lakini akajituliza na kuwa tayari kuzungumza punde sauti nzito ilipomwitika upande wa pili.
“Hallow..Nani?”
______***_______
| DAR ES SALAAM|
Kama ilivyokuwa destuli yake kila asubuhi Zomboko alienda uwanjani kupasha misuli kabla hajafungua saluni yake.
Na kipindi hiki akawa anatoka na mwanae Kine akimfunza ushupavu ili asiwe mwanaume mzembe kwenye maisha yake.
Baada ya tizi na kurejea nyumbani, akajiandaa na kuelekea ofisini kwake. Ilikuwa yapata saa tatu asubuhi akiwa anakaribia kufika ofisini kwake, simu iliyokuwa mfukoni ikatoa mtetemo na kuita. Akaitazama namba haikutoka na jina. Zomboko akaipokea na kuuliza anayepiga kabla ya mazungumzo zaidi.
“Ndugu yako Ze Don T naongea kaka Zomboko kwema?” Sauti ya Tibwili ikasikika upande wa pili, Zomboko akaitambua.
“Unajua lakini hatuna undugu sasa?”
“Ndio..!” Tibwili akakubali
“Haya sema shida…mida ya kazi hii!” Zomboko akaongea kibabe kwa sauti isiyotaka mazoea na mtu anayemsemesha.
“Huna habari yoyote kuhusu Izani umesikia?” Tibwili akauliza.
“Sema shida yako, sijakwambia uniulize maswali?”
“Daah! Mkubwa Zombi nina jambo muhimu lakini nataka nikwambie.”
‘Oyaa! Punguza maelezo zungumza kiume Tibwili acha kuzunguka kama shoga anayetafuta bwana.” Zomboko akasema kwa sauti kali wakati huo kashafika mbele ya saluni yake. Tibwili akasikika akishusha pumzi upande wa pili na kuzungumza.
“yule dogo wa kitaani Izani Nteze ametupwa kijijini kwetu huku ameokotwa jana akiwa hoi!”
“Eti nini, hebu rudia..” Zombko akahamaki na kushusha mzuka wake baada ya kusikia taarifa hizo. Tibwili akarudia na kuzungumza hatua zote walizochukua mpaka muda huo.
Akili ya Zomboko ikaunganisha matukio haraka akayakumbuka maswali aliyohojiwa na Markus Makata na zaidi akamtafakari dereva wa mchungaji Ndimbo Masizi kuja kunyoa saluni kwake na kwenda kunywa kwenye grocery yake, na kote huko aliwauliza watoto wake kuhusu Izani Nteze. Machale yakamcheza Zombi Zomboko akapata walakini juu ya taarifa zile za Izani Nteze.
***
|ARUSHA|
Lile Jitu la ajabu Tutu likazidi kushangaa kuona Anita haonekani kutoka ndani ya mwanahaki. Ukuta uliokuwa katikati ya nafsi ya Mwanahaki uliwazuia kuhakikisha. Mawasiliano kwa mkuu wao napo hayakuwa yamerejea. Akazidi kuhamaki kuona Mwanahaki akirejea akiwa mwingi wa simanzi wala asimuone Anita kama alivyotaraji.
Akaingia moja kwa moja na kujifungia ndani. Siku hiyo kwa mara ya kwanza Zuberi Mwanahaki akalia kama mtoto. Mpaka giza linaingia hakula chochote wala Neema hakurejea.
Kwa maumivu makubwa Zu beri akaoga na kuswaki kabla hajavaa kanzu yake na kutandika mswala na kuanza kusali huku akimlilia Mungu ampe nguvu na subira katika kipindi kile kigumu kilichomvamia moyoni mwake. Akaomba pia kama kuna nguvu ya kishetani imemwingia mkewe basi Mwenyezi Mungu amuokoe katika hilo.
“Yaa Allah nipe nguvu nishinde haya. Oooh Yaarabbi mlinde mke wangu na umuokoe na vitimbi vya kishetani ee Mungu wangu. Hakika wewe ndiye mjuzi na msikizi. Nakuomba yarabbi mimi ni mja dhaifu sijui kinachoendelea ndani ya mke wangu. Kwanini iwe hivi leo..! Kwanini anioneshe mabadiliko haya kwa kiwango hiki..! Eeeh Mwenyezi Mungu pokea dua hii umlinde huko aliko awe salama. Yaa Allah takabbar-Duaa!” Zuberi akasali na kuomba huku machozi yakimtoka. Akabaki pale kwenye mswala akiomba mpaka usingizi ukampitia.
Ndipo Malaika wa faraja alipomshukia akiwa usingizini na kumfunika kwa nuru ya mbawa yake iliyompelekea Mwanahaki kusafirishwa kwenye iliyomshangaza ambayo ilimjengea maswali ya majibu ya hatua anazopaswa kuchukua.
Zuberi Mwanahaki akajiona ndani ya ndoto akiikimbiza ile gari iliyompakia mkewe na mara akatokeza katikati ya msitu kijijini kwao Dutumi Morogoro.
“Neema…Neema…Mke wangu!” akawa anaita huku akifatilia alama za matairi ya gari ambayo mke wake alitoroshwa nayo. Alipotokeza mbele akashangaa ametokea kwenye nyumba ya Mjumbe wa kijiji chao ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa marehemu baba yake Mzee Mwanahaki.
“Vipi Zuberi… Mbona hivyo?” Mzee Siriaki akamuuliza huku akishangaa hali aliyokuwa nayo Zuberi.
“Kuna gari nilikuwa naifatilia imemteka mke wangu?”
“Hapana! Gari ile ilikuwa imemteka Izani Nteze na sasa tuko naye hapa anaendelea vizuri.” Mjumbe Siriaki akamjibu na mara akatokea Izani akiwa na kina Tibwili. Zuberi akabaki na mshangao mkubwa.
“Lakini mimi nilikuwa naifatilia gari iliyompakia mke wangu?” akauliza na ajabu Izani alipozungumza akaisikia sauti ya mkewe ndani yake.
“Mke wako atarudi ukishanichukua mimi naye utampata. Amefungwa kivuli na watu waliotumwa kumwangamiza Mfuasi wangu. Wala si yeye aliyekuwa anakujibu vile na wala yule aliyekimbia naye kwenye gari si Markus Makata wala hajawahi kuwa na mahusiano na mtu huyo. Pole sana..! Nifuate hakika ukinitoa hapa utampata mkeo.” Izani aliposema hayo mara Zuberi akashangaa kuona mazingira yanabadilika na mbele yake akamshuhudia mkewe amekamatwa na kiumbe wa ajabu.
35
“NEEEMAAA!” Akamwita huku akimkimbilia yule kiumbe na mara akastuka usingizini kabla hajamfikia. Akashangaa kuona tayari kulishakucha. Akanyanyuka na kuifata simu yake ilipokuwa akastaajabu zaidi kuona tayari majira yalisoma saa nne asubuhi.
Akiwa bado anatafakari Ndoto ile ya asubuhi mara simu ikaita mikononi mwake na alipotazama anayepiga likatokea jina ‘MY WIFE’
Mapigo ya moyo wake yakaongeza kasi akiwa bado anaiwazia ndoto iliyomkurupusha usingizi.
______***_______
| DAR ES SALAAM|
Usiku ulipoingia Zongo akamwacha Ndimbo Masizi na kuondoka kwenye anga ya jiji la Tanzania na kulifata jiji la Kenya alipotoka.
Lakini kabla hajaondoka akamwachia maneno yaliyounyong’onyesha moyo wa mchungaji Ndimbo Masizi na kuua tumaini lake la ushindi wa kile alichofikiri chepesi.
“Umekuwa mzembe kila wakati Ndimbo! Umeharibu mikakati yote dakika za mwisho. Sasa nakuacha upambane nayo mwenyewe hii vita ambayo itaanza baada ya masaa 54 kupita. Na imebaki siku moja tu ambayo ni kesho unatakiwa ufike kilingeni. Lakini kwa kukanyaga kwako mchanga wa bahari na kushindwa kumtoa mwanao wa kiume jiandae kulishuhudia anguko lako la fedheha.”
Sauti hiyo aliisikia Ndimbo pekee. Usiku huo kwake ukawa mzito kupita kawaida. Kwa mara ya kwanza mama Anita akamshuhudia mumewe akiweweseka na kusema maneno yaliyomstaajabisha usiku.
“Nitamtoa tuuu Mtumishi! Tafadhalii sitaki kufedheheka…! Ni mke wangu kaniponza… Sikukusudiaa aaah Hapanaaa! Nimekubali kazi iendelee.. Mtumishiii..Mtumishii..” Ndimbo akaweweseka kwa sauti usingizini wakati mama Anita yuko macho anamtazama kitandani.
Akajikuta anashindwa kumuamsha kwa taharuki asielewe nini maana ya maneno ya mumewe. Mwishowe akaamua kufanya maombi ambayo yakamkurupusha usingizini Ndimbo.
“Hebu acha mama Papii! Tulale mke wangu tafadhali nyamaza sijisikii vizuri usipige kelele.” Ndimbo akazungumza na kuzidi mshangaza mama Anita.
Leo hii mume wangu maombi yamekuwa kelele kwake?
Akajisemea moyoni pasipo kumwambia kwa mdomo mumewe. Ikabidi ajilazimishe kulala ingawa mashaka yaliyomzonga kichwani yakamfanya usingizi upae. Alitamani jumapili ifike haraka alifikishe tatizo la mumewe kwa wazee wa kanisa lake wapate kufanya ibada maalum ya kumrudisha mchungaji wao katika hali ya kawaida.
* *
Kwa upande wa Chikala baada ya kufatilia gari na kulipeleka gereji, akawa anatafakari vile Papii alivyokuwa anamkataa baba yake.
Watoto ni malaika kweli, yule mtoto itakuwa kuna mambo kayaona hayako sawa kwa baba yake… Daah!
Akasema moyoni mwake Chikala ambaye kutokana na mizunguko ya kutwa akashindwa kukutana tena na Kisa Kabeby.
Akiwa anarejea kutoka gereje alikopeleka gari baada ya kumaliza taratibu za kipolisi, simu yake ikaita. Alipotazama anayempigia alikuwa Chox ndipo akakumbuka kuwa hajamwambia kuhusu bosi wao mkubwa kupata ajali.
“Sema Chox umesikia chochote kuhusu bosi?” Chikala akazungumza baada ya kupokea simu.
“Hapana mkuu, bosi kafanyaje tena?”
“Amepata ajali ila yuko poa hajaumia sana.”
“Duh! Kweli ni ajabu maana na mimi nilikuwa nataka tuonane kesho kuna jambo nataka tuongee ila si kwa njia ya simu.” Chox akasema upande wa pili na kumshangaza Chikala.
“Jambo hilo lina uzito gani kama tumeweza kuzungumza kwa simu kummaliza Izani teja, je hilo ni kubwa kuliko hili?” Chikala akauliza kwa sauti ya kukereka kiasi. Chox akaomba msahama na kumhakikishia Chikala kuwa hawezi kusema kwa simu hilo jambo aliloliona ni kubwa na muhimu kuliko yale aliyozungumza naye kwa simu. Chikala akashangaa na kupata shauku ya kusikia.
“Okey sasa kesho itabidi nimsindikize mzee Nairobi. Kesho kutwa nitaika huko, na ole wako liwe jambo la kipuuzi.” Chikala akaweka onyo, na kukata simu baada ya mazungumzo.
Mpaka giza linaingia hakutoka baada ya kufika kwake akaamua kulala mapema siku hiyo huku akiwazia kujiengua kufanya kazi kwa Ndimbo Masizi.
Kunapoendea huyu mzee anaweza kuja kutuumiza hadi tuliokuwa nje ya familia. Hapana, kama pesa ninayo sasa ya kuishi mjini bila mawazo…heri niachane nae tu ayanywe mwenyewe aliyoanza kuyakoroga.
Akajisemea na kujiapiza moyoni Chikala. Usiku huo naye kwake ulikuwa wa kiutofauti mpaka kunakucha alikuwa na usingizi wa mang’amung’amu.
Kilichomwamsha asubuhi naye ni simu kutoka kwa Ndimbo Masizi akimtaka awahi mapema amsindikize Nairobi. Safari hii Chikala alikosa kisingizio akaamua kukubali kusafiri na bosi wake.
***
|MOROGORO|
Koplo Ponda aliendeesha gari mpaka makao makuu ya polisi mkoa. Njiani alikuwa akiwasiliana na aliyewahi kuwa mkuu wake wa kituo zamani ambaye naye alihamishiwa Makao makuu ya polisi Morogo akiwa kama mnadhimu wa kambi.RSM Jongo, na kumwelezea kila kitu.
“Vyema sana lilete hilo jambazi pia nazungumza na mkuu hapa aitwe mkuu wa kituo Mtamba tumuweke kizuizini leoleo. Vyema sana Sajenti…ooh No Koplo!” RSM Jongo akazungumza kwa simu na kumpongeza Ponda.
Na kweli baada ya Ponda kumfikisha mtuhumiwa akawekwa kwenye chumba maalum huku akiomba kesi ile asipewe yeyote kwakuwa ameianza mwenyewe basi aimalizie.
Kutokana na sifa zake kujulikana na makamanda wa makao makuu kuptia RSM Jongo, wakakubali wamwache Ponda amfanyie mahojiano mtuhumiwa wake aliyemleta kipindi taratibu za kumkamata mkuu wa kituo Mtamba zikiandaliwa.
Na hapo ndipo Chox akabanwa vikali na Ponda akilazimishwa kumpigia bosi wake baada ya kufunguka kuwa yeye anatumiwa tu na mtu anayeitwa Chikala Gumbo.
“Sikiliza wewe! Kwa usalama wako usiende kupotelea jela, mpigie na umwite huyo anayekutuma. Tukimkamata tutakuacha huru!” Ponda akasema kwa ushawishi ambao Chox alijua ni uongo wa polisi tu. Lakini pia hakuwa tayari kutektea mwenyewe. Akaamua kushirikiana na Polisi kumvuta Chikala Morogoro.
Na ndipo alipompigia Chikala akiwa makao makuu ya Polisi Morogoro, huku simu yake ikirekodiwa.
“Vyema sana koplo. Sasa kwakuwa huyu kashafika na tushatrack mawasiliano, tutawasiliana na wenzetu wa Dar waanze kumfatilia huyo mshenzi kesho si ndo wanasafiri na bosi wake? Lazima tuwatie kizuizini.” RSM Jongo akazungumza na Ponda baada ya kutoka kwenye chumba cha mahojiano alipofungiwa Chox.
Ponda akageuza kurejea Mtamba jioni hiyo wakati mkuu wake wa kituo akijiandaa kwenda makao makuu ya mkoa kuitika wito ambao hakujua kinachoendelea.
36
Asubuhi ya kizaa zaa ikawadia. Mkuu wa kituo cha polisi Mtamba akawekwa kitimoto na maafisa wa Taaasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) akihojiwa kwa tuhuma za kupokea rushwa iliyosababisha kumwachia mtuhumiwa aliyekutwa na dawa za kulevya.
Wakati huohuo pia Chox akabananishwa mpaka akasema alipoenda kumtupa Izani Nteze.
“Aisee! Kumbe ni yule kijana aliyekuwa anahimiza watu kupambana na dawa za kulevya nyinyi ndio mmemtenda ubaya sio? Mmeona anawaharibia biashara?” RSM Jongo akawaka vikali.
Koplo Ponda naye akawa amedamkia makao makuuya mkoa mapema kuendelea na hatua ya pili ya mahojiano na uchunguzi kwa mtuhumiwa wake. Alipofika baada ya kusalimiana na polisi wenzake akaingia ofisi ya RSM kuzungumza naye.
“Nimetoka naye mshenzi huyu kumbe kijana mwenyewe ni Izani Nteze! Hujasikia sekeseke lake mwaka jana?” Jongo akaongea na kumfanya Ponda afikiri bila kukumbuka.
“Wewe nawe hukumbuki ilivuma yule mchungaji Ndimbo Masizi aliibiwa na kijana wake aliyekuwa anarusha kipindi kwenye TV akiwasihi vijana wa mitaani kuachana na mihadarati?”
“Anhaaa! Sasa nimekumbuka mkuu. Si unajua tena toka tumepelekwa maporini habari za jiji zinatupita!”
“Sasa yule naye mshenzi, ila tushafanya mawasiliano na makao makuu inasemekana anasafiri kwenda Nairobi leo. Washatumwa askari wa kuwakamata washenzi hawa.” Jongo akaongea wakati huo msafara wa kamanda mkuu wa polisi mkoa RPC MAVUGO ulikuwa unawasili kituoni baada ya kutoka ziara ya kikazi Mvomero.
“Enhee nimesikia kuna jambazi lilitaka kumuua afisa wangu liko wapi kwanza nilione?” Ndilo lilikuwa swali la kwanza pindi RPS Mavugo alipowasili makao makuu. Moja kwa moja akaongozwa mpaka kule alipofungiwa Chox ambaye alikuwa hoi kwa mateso.
“Khaa! We kijana yaani unathubutu kuja kumnyooshea kija na wangu bastola?” Rpc akawaka na kumkata kofi Chox.
“Inspekta, nataka faili la huyu mpuuzi lije ofisini kwangu.” akatoa agizo na kutoka kwenye kile chumba.
“Sawa mkuu!” Inspekta aliyekuwa pembeni yake akaitika na kupiga saluti.
Siku hiyo ilikuwa ni ya kibano tu kwa Chox ambaye alitoa ushirikiano wa kutosha ili asiumie peke yake. Ndipo saa nne asubuhi akafungwa pingu na kupakiwa kwenye difenda iliyokuwa na zaidi ya askari nane kwenda Dutumi huko kwenye msitu alipoutupa mwili wa Izani Nteze.
______***_______
| DAR ES SALAAM|
Saa tatu asubuhi ndani ya jumba la mchungaji Ndimbo Masizi, Chikala akawasili akiwa tayari kuelekea na Ndimbo huko Nairobi.
Ndimbo siku hiyo aliamka akiwa mkimya hakuwa tayari kuzungumza na yeyote. Hata mkewe alipomsimesha hakumpa ushirikiano. Muda wote huo Anita alikuwa ndani ya Papii akiuongoza mwili wa ndugu yake usijikwae hatarini.
Alipofika Chikala na kuondoka na Ndimbo ndipo Anita naye akatoka kwenye mwili wa Papii baada ya kumwona Malaika wa taarifa akitua mbele yake.
“Salamu ewe Anita mwenye upendo. Kibali chako kimetunukiwa zawadi ya ushindi. Na habari njema katika yale masaa yaliyokuwa hatari sasa yamekuwa kinyume kwako. Adui yako anaenda kutiwa nguvuni sasa.” Malaika wa taarifa akasema maneno yaliyomfurahisha Anita.
“Na vipi kuhusu Izani?”
“Izani yuko kwenye mikono ya mkondo wa Mwanahaki ambaye naye atakuwa safarini leo pindi utapofanikisha kuiweka huru nafsi ya Neema naye utaweza kumwingia kuendeleza ushawishi wa safari hakika ataenda kumtwaa Izani.” Malaika akajibu, Anita akastaajabu zaidi.
“Je nitawezaje kuiweka huru nafsi ya mwanadamu mwenye mwili hali mwenyewe ni nafsi tupu! Niaiwezejae hiyo vita?”
“Vita yako umeirahisisha katika machaguo yako Anita. Laiti ungechagua kubaki kwa Mwanahaki ungechagua ubinafsi ambao ungekusababishia uishie kifungoni kwa mashetani yaliyokuwa yanakuandama. Lakini Mola wako amekupa tunu kwa chaguo lako la ukombozi kwa wengine naye amekufanyia ukombozi kwako. Na sasa nakujaza nguvu uende Arusha ukakikomboe kivuli cha Neema ili nafsi yake iwe huru, pia utumie nafasi hiyo kulipa kisasi kwa kumwangamiza Tutu, lile jitu la kishetani lililokunyonya damu na kuua mwili wako.”
Baada ya kusema hayo yule Malaika ikaanza kumtoka Nuru ya ajabu mithili ya moto na kumwingia Anita kisha akaondoka alipomaliza. Anita naye akajishangaa kujiona amekuwa wa kipekee ndani yake, haraka akaondoka kurudi Arusha kwenda kumwoko Neema ambaye hakuwa huru kinafsi.
* *
UWANJA WA NDEGE - DAR
ASP Mwita Mwitike akiwa na maafisa sita kutoka makao makuu wakiwa wamevaa kiraia, walikuwa tayari wameiweka shabaha yao ya kumkamata Mchungaji Ndimbo Masizi na kijana ake Chikala Gumbo ambaye waliitrack namba yake ya simu waliyotumiwa na wenzao wa Morgoro ambao kwa muda huo nao walikuwa safarini kwenda kuuchukua mwili wa kijana Izani Nteze.
“Habari zenu?” Mwita akawasabahi kina Chikala punde tu waliposhuka kwenye gari kabla hata hawajaingia uwanjani.
“Njema!” Mchungaji Ndimbo akaitika huku akiwa mwenye haraka zaidi.
“Hampaswi kwenda popote mzee kuanzia sasa mko chini ya ulinzi, mnatakiwa kuongozana nami makao makuu Posta.” ASP Mwita akasema huku akiifunua upande wa koti la suti aliyovaa na kuonesha kitambulisho chake.
Mchungaji Ndimbo almanusura aanguke kwa mshtuko, wakati Chikala alipotaka kuweka hoja tayari wakawa wametoka maafsi wengine wanne na kuwazunguka wakiwataka wajisalimishe kwa amani waongozane kabla hawajatumia nguvu kuwatoa.
“Lakini…..” Mchungaji Ndimbo akataka kutia neno.
“Hakuna cha lakini mzee, unahitajika kituoni huko ukatuambie lakini zako.” ASP Mwita akaweka mkazo wake na ndipo Mchungaji Ndimbo na Chikala Gumbo wakakamatwa kama utani.
***
|ARUSHA|
Anita akafika kwenye ile nyumba ya Mwanahaki ambapo Nafsi ya Neema ilikuwa bado kizuizini na lile jitu Tutu lililofura hasira.
Safari hii lilikuwa mwenyewe na likafanikiwa kumwona Anita na kujikuta linatabasamu. Akadharau bila kujua uwezo mpya aliokuwa nao Anita ambaye pia alikuwa na hasira kuu kuhusu lile jitu.
Akaja kwa kasi ya Kombora la Moto mpaka Tutu akashangaa na kujikuta akipasuliwa mkono aliokinga kumkamata Anita.
“AAAGHHHRRR” Likanguruma kwa hasira ya kuachwa na mkono mmoja ambao alitumia kudhibiti kivuli cha Neema. Ndipo likageuka na kwa hasira likauchomoa ulimi wake mrefu wenye ncha mbili zilizochongoka.
Sauti ya Malaika wa taarifa hakuwa mbali na Anita kumpa maelekezo namna ya kutumia nguvu zake wakati anakabiliana na lile jitu.ambalo ndilo lilikuwa shetani lililotegemewa na Dokta Zongo.
37
“Nyoosha kidole kimoja cha mwisho na cha mwanzo zungusha mara sabaaa” Anita akaisikia sauti ya Malaika wa taarifa. Naye alipofanya hivyo akashangaa mkono wa nafsi yake kugeuka panga la moto na kuukata ulimi wa jitu uliokuwa unamfata kwa kasi kila alivyokuwa anaukimbia hewani.
Safari hii Tutu akajikuta anashindwa kuhimili vishindo vya kuendelea kumzuia Neema kivuli. Akajikutaanamwacha huku likipiga kelele za maumivu na hasira.
Vile kivuli cha Neema kilivyoachiwa tu kikafunukia juu ya Anita na kutoa heshima ya shukurani kabla hakijapotea eneo lile kwa kasi kuyeyuka.
Sasa vita ikabaki kwa Neema na Tutu ambaye hakuwa na msaada wowote.
Anita akammaliza kwa kukita kichwa chake na kushuhudia damu za ajabu zikiambaa juu yake zikatokea nafsi nyingi zilizowahi kudhulumiwa miili yao na Tutu zikifurahi na kumshangilia Anita huku zikimwinamia kwa heshima.
“Hongera Anita.” Sauti ya Malaika wa taarifa ikasikika pia ikimpongeza Anita ambaye pia akafarijika kulipa kisasi kwa jitu la ajabu lililouzulumu mwili wake.
* *
Wakati Anita akilimaliza lile jitu, upande wa pili kivuli cha Neema kikarejea na kuiamsha nafsi yake iliyomtoa kwa nguvu Ngondi aliyekosa namna wala ujanja wa kuikabili.
Neema akastuka na kujikuta kwenye mtaro wa barabara. Akatazama pembeni yake na kuiona simu yake.
Mungu wangu! Mume wangu…!
Akahamaki na kunyanyuka akiwa anajishangaa kujiona pekupeku. Alipotoka kwenye mtaro ndipo akagundua alikuwa maeneo ya Daraja mbili. Akazidi kuhamaki hata asikumbuke alifikaje hapo. Ikabidi ampigie simu mume wake huku mashaka yakiwa yamemjaa kichwani.
Ndipo muda huo ambao Zuberi alishtuka usingizini baada ya kuota ndoto ya ajabu iliyomjuza cha kufanya. Akaisogelea simu yake kutazama muda tayari saa nne asubuhi, na mara simu yake ikaita.
Zuberi akastukaa kuona ni mkewe ndiye anampigia. Akaanza kwa kutamka “Bismillahi” ndipo akapokea simu ambay ikamshangaza kusikia Neema akilia upande wa pili.
“Haloow! Hallooow mke wangu.” Akaita lakini mara simu ikakatika. Alipopiga akashangaa Zuberi kusikia simu haipatikani.
Wakati huo huo Anita akamwingia Zuberi ndani yake na kumtuliza nafsi.
Oooh! Hapa sina budi kufata maelekezo ya ile ndoto. Naamini Allah atamlinda mke wangu nitamkuta salama.
Zuberi akatahayuri kwa msukumo wa Anita aliyekuwa ndani yake. Akajiandaa haraka akaoga na kuchukua vitu muhimu akaweka kwenye begi kabla hajafunga mlango na kuondoka kuwahi kituo cha mabasi Arusha.
Upande wa pili Neema akajikuta akigugumia baada ya kilio cha muda alipoisikia sauti ya mumewe. Lakini kwa bahati mbaya simu yake ikazima chaji. Hakuwa na namna tena ya kufanya zaidi ya kukodi bajaji baada ya kutembea hatua chache mbele. Alipofika akakuta tayari mumewe ameshaondoka. Uzuri kulikuwa na mahala maalum wanapoweka funguo za nyumba, ambapo alipafikia na kufungua mlango akaingia ndani na kutoka akiwa na pesa ya malipo ya nauli kwa bajaji aliyokodi. Alipomlipa dereva bajaji akarejea ndani na kuiweka kwenye chaji simu yake huku akiwa bado anatafakari mambo yalivyomwendea mpaka kujikuta amelala nje ya nyumbani kwake tena amemakia kwenye mtaro? Akaanza kulia tena mpaka moyo wake ulipotulia ndimbo akawasha simu na kuwasiliana na mumewe.
Safari hii akaweza kuzungumza vyema na akashangaa mumewe kumpokea katika hali ya kawaida bila kumsema vibaya.
“Usijali mke wangu kwakuwa umesharuddi kwako nisubiri mimi naelekea kumchukua Izani. Bila shaka mambo yote yatakuwa sawa mke wangu, najua haikuwa nia yako nami sina kinyongo kuwa na amani. Nakupenda” Zuberi akazungumza maneno yaliyompa faraja Neema na kujikuta tabasamu lake likirejea.
_____***_____
|NAIROBI|
Zongo akapiga yowe baada ya kukuta chumba chake cha sita kikinyesha mvua ya damu katikati ya mchoro wake wa kafara na juu yake ukatokea mwili wa Tutu! Ukiwa hauna kichwa wala mkono.
“Aaaaaaaaaaaaaahhhhhh Ndimbooooo! Lazima ulipeee” Akaapia na kumlilia Tutu kama mwehu. Hakika kwa mara ya kwanza hata Lululu akamuogopa Zongo vile alivyobadilika siku hiyo baada ya zoezi la jana yake kushindikana na muda huo lilikuwa limebaki lisaa limoja kwisha ule muda wa masaa hamsini na nne aliokuwa amempatia Ndimbo Masizi.
“Lululuuuu nataka Ndimbo Masizi akamatwe na ateseke kweywe kutumiaka kama Mtumwa wetu. Nataka ndani ya siku tatu aanze kutumikia haiwezekaniiii haaa! Haiwezekaniiiiii…! Tutuuuuuu!” Zongo akazidi kubwata akitoa agizo kwa mtumishi wake Lululu.
Lululu akamwinamia mkuu wake kwa heshima ya utayari wa kwenda kutimiza agizo hilo.
***
|MOROGORO|
Chox akawaongoza polisi mpaka kwenye msitu kule alipomtupa Izani siku moja iliyopita.
“Wewe liuaji? Ndio hapa?” Polisi wakamuuliza baada ya kufika eneo husika na kukuta hakuna mtu ingawa walihisi dalili za uwepo wa mtu za ya mmoja eneo lile kwa jinsi nyasi zilivyokuwa zimekanyagwa.
“Ndio hapa afandee! Ndio hapa kweli niliutupa hapa mwili na alikufa mwenyewe sijamuua mimi.” Chox akajitetea na kusema kwa kumaanisha akiwa chini ya ulinzi mkali.
Polisi wakapiga picha lile eneo na hawakuwa na budi zaidi ya kujigawa wengine wakarejea mjini na polisi wawili wenye silaha wakaachwa wafatilie njia ambayo ilionyesha kuna watu walipita kutokea pale alipohakikisha mtuhumiwa kuwa aliutupa mwili wa Izani Nteze.
Polisi walioachwa waendelee na utafutaji alikuwa ni Koplo Ponda na mwenzake kutoka makao makuu Morogoro.
Chox akapakiwa kwenye Difenda na kurudishwa mjini ambapo pia aliwafikisha polisi kule alipokuwa anaishi na kuwaonesha mzigo wa madawa uliobaki sambamba na mawasiliano yote aliyokuwa anafanya na Chikala Gumbo. Polisi wakachukua vidhibti muhimu na ile nyumba ikazungushiwa utepe na kuwa chini ya uangalizi wao.
* *
Saa kumi jioni Mwanahaki akawasili Morogoro mjini na kuamua kuchukua gari ya kukodi ili aweze kuwahi Dutumi siku hiyohiyo akiwa na lengo la kugeuza kesho yake mapema.
“Kaka kuna usalama kweli? Mbona polisi tena na bunduki porini huku?” Dereva wa gari alilokodi Mwanahaki akazungumza wakati wakiingia kwenye kijiji ambacho Zuberi alikuwa anamuelekeza. Hata yeye akashangaa kukuta askari kijijini kwao na watu wakiwa wengi kwa mjumbe.
“Usijali hapa kwetu ni salama siku zote, labda kuna mnyama pori kaua mwanakijiji.” Mwanahaki akasema kumuondoa hofu dereva.
Watu waliokuwa kwa mjumbe wote wakageuza macho kuitazama gari iliyokuwa inaingia kijijini muda huo ambao tayari ilikuwa yapata saa tatu usiku.
“Ooooh Mwanahaki mwenyewe kabisaaa.” Mzee Siriaki akamtambua Zuberi mara baada ya kushuka kwenye gari na kusogea walipokuwa. Akanyanyuka na kupeana mikono na wanakijiji waliokuwa kwa mjumbe ambao wengi walimjua mbali ya kukaa kwa muda mrefu bila kuwatembelea.
Zuberi alifanana sana na baba yake marehemu mzee Mwanahaki. Na hiyo ndio ikawa chachu ya Mzee Siriaki asimpotee machoni kijana yule.
“Kwema lakini baba yangu?” Zuberi akasema huku akikaa kwenye kigoda alichopishwa na Muhondogwa.
“Bwana kwema! Kisogo tuseme si kwema.” Mzee Siriaki akazungumza huku akiwageukia polisi wawili wenye bunduki waliokuwa wamekaa kwenye benchi.
“Jamani kina baba huyu ni kijana wangu naye ndiye msomi wa kijiji chetu anaitwa Zuberi Mwanahaki, imekuwa vyema pia amefika.” akasema na kumgeukia tena Zuberi. Akaanza kumsimulia tukio la Muhondogwa na Izani.
“...sasa huyo bwana Mungu alivyo mkubwa amekamatwa na alipofika kuonesha alipomtuma ndipo hawakukuta mtu. Na hawa polisi kwa werevu wao wameweza kufatilia mpaka wanafika kwangu na kwa maelezo yao nimwaambia mtu huyo tunajua taarifa zake na ninaye. Na ndio mara nawe unaingia…karibu sana kikao hiki kinakuhusu baba.” Mzee Siriaki alipokuwa anazungumza Mwanahaki akawa anaiona ile ndoto yake na kuzidi kuamini kweli Dunia inaendeeshwa na ulimwengu wa ndani ya ndoto zake.
“Huyo Mtu ni IZANI NTEZE?” akauliza na kumfanya Koplo Ponda na mwenzake washtuke kwa kumwangalia kwa makini na taharuki.
38
______***______
|DAR ES SALAAM|
Kwenye chumba cha mahojiano makao makuu ya jeshi la polisi, Posta mitaa ya Ohio na Ghana Avenue, mchungaji Ndimbo Masizi na dereva wake Chikala Gumbo wakawa wanahojiwa kwa zamu na ASP Mwita Mwitike ambaye alipewa agizo hilo moja kwa moja na IGP Mukan Mukazabe baada ya kujua kuwa mtuhumiwa anayefatiliwa ni mchungaji mkubwa na maarufu nchini.
“Mchungaji upo hapa kwa tuhuma za kuhusika na uuzaji wa dawa za kulevya. Kweli si kweli?” Mwitike akaanza kwa swali gumu lililomfanya Ndimbo astuke na kutumbua macho asiamini anachokisikia.
“Afande tuheshimiane tafadhali mbona unanitungia kashfa nisiyostahili? Nitakufungulia kesi kama itajuliakana unanisingizia kwa kashfa nzito ya kunichafua tafadhali…!” Mchungaji Ndimbo povu likamtoka huku akihema kwa tabu. Moyoni mwake hofu ilikuwa inamchemka lakini akawa anajaribu kuizuia machoni mwa afisa aliyekuwa anamuhoji.
ACP Mwitike akamtazama Ndimbo huku akicheka kwa kumsikitikia na kuandika maneno yake.
“Unamfahamu Izani Nteze?” Mwitike akauliza swali lililokata mazungumzo ya awali na vitisho vya Ndimbo akajikuta anajibu huku akishindwa kuizuia hofu machoni mwake.
“Izani? Nani yule mwizi..! Ndio vipi kwani?” akababaika.
Mwitike akaisoma hofu yake na kumkazia sura.
“Kwa hiyo ndo ukaagiza vijana wako wamuue na kumtupa porini?” akamchanganya kwa kugusa mulemule
“Nani? Wee afande mbo…”
“Wewe ni mchungaji muuaji au mponyaji?” Mwitike akamkamatia tena kwa juu Mhungaji Ndimbo ambaye presha ikazidi kumpanda kwa maswali yaliyomchanganya mpaka akahisi hana kichwa.
Baada ya kuchukuliwa maelezo ikawa zamu ya Chikala ambaye naye makosa yake yalifanana na Bosi wake ingawa naye alipinga kwa kukanusha.
* *
Habari ya kukamatwa mchungaji Ndimbo uwanja wa ndege ikafika kwa familia yake. Mama Anita akazidi kushangazwa na kustaajabu mauzauza yasiyokauka yanayowakuta tokea kifo cha binti yao Anita.
Akafika makao makuu kuzungumza kujua kesi inayomkabili mchungaji ndipo wote walistaajabu waliosikia. Taarifa zikasambaa kama upupu zikayawasha masikio ya kila aliyesikia kuwa Ndimbo Masizi anajihusisha na biashara za dawa za kulevya.
“Hapana jamani mbona hamumuogopi Mungu mnamsingizia mume wangu?” Mama Anita akajaribu kupinga pindi alipoambiwa na ACP Mwita kosa linalomkabili mumewe ambapo hatopewa dhamana mpaka afikishwe mahakamani kujibu mashtaka matatu yanayomkabili yakiwa na uuzaji wa madawa ya kulevya, utekaji nyara.
***
|MOROGORO|
“Unamfahamu vipi Izani Nteze?” Ponda akauliza
“Ni kijana aliyejitolea maisha yake kupambana na matumizi ya mihadarati na dawa za kulevya mitaani. Namfahamu kwakuwa nimekuwa Mfuasi wake siku zote nilimfatilia kwenye kipindi cha TV” Mwanahaki akafafanua na kuwafanya wale maafisa watazamane na kumtilia mashaka.
“Je, tunaweza kuongozana nawe kwa gari uliyokuja nayo tuwahi makao makuu muda huu, kwakuwa Izani tunaye na eneo hili mnara hausomi.” Ponda akabadili mwelekeo wa swali ambalo pia Mwanahaki akalielekea bila kusita akaliunga mkono.
“Bila shaka kwa maana lazima tumwanike shetani na matendo yake ili wanaojifunza kupitia sisi wasalimike. Duh! Mchungaji kumbe ni nyoka?” Mwanahaki akasema bila kubabaika, Koplo Ponda akaona wazi mtu yule si mtu mbaya. Anita akiwa ndani ya Mwanahaki akafurahi sana kumwona Izani ingawa Izani hadi muda huo alikuwa bado hajaanza kuzungumza ila ile alosto ilimpotea wala udenda haumtoki. .
Safari ya Zuberi Mwanahaki na kina Ponda ikafatia kwa ile gari ambayo alifika nayo baada ya kuikodi tokea Morogoro mjini. Mtu mwengine aliyejumuishwa kwenye safari hiyo ni Muhondogwa, Mzee Gulilo na mjumbe mzee Siriaki wote hao wakaenda kutoa maelezo yao ya kimaandishi kama mashahidi makao makuu ya Polisi mkoa.
Tibwili yeye alijificha tokea aliposikia kuna Polisi wamekuja kijijini kwao, hakutaka kuonekana mpaka walipoondoka usiku huo.
* *
- SIKU MBILI MBELE -
INASHANGAZA SANA! KUMBE MCHUNGAJI NDIMBO MASIZI NI ‘SHETANI MWENYE SURA YA MALAIKA’
Gumzo likateka vichwa vya habari za magazeti Tanzania. Kila mtu akastaajabu nchini kwa kesi ambayo hakuna aliyewahi kuifikiria hususani waumini wa kutupwa wa kanisa la mchungaji Ndimbo Masizi.
Siku hiyo ikawa siku ya kwanza kufikishwa Mahakamani watuhumiwa watatu wakiongozwa na mtuhumiwa Ndimbo Masizi.
Siri zake nyingi zikafichuka baada ya upekuzi wa kutosha uliofanywa na jeshi la Polisi kukuta vithibitisho vingi vya kumtia hatiani.
IGP Mukan Mukazabe akazungumza na vyombo vya habari baada ya upekuzi mkali wa vijana wake kukusanya vielelezo vya kutosha vilivyomtia hatiani Ndimbo Masizi na dereva wake Chikala Gumbo pamoja na Chox ambaye naye akahamishiwa Dar Es Salaam kuhukumiwa pamoja.
Mwanasheria Neema Hussein akaungana na mumewe kuhakikisha haki inatendeka kwa Izani Nteze, wakisimama kama wanasheria wake waliojitolea kuhakikisha naye anafaidika kupitia kesi ile baada ya kuharibiwa maisha yake na mipango yake mizuri.
Hali ya Izani ilianza kuleta matumaini baada ya kumbukumbu zake kuanza kurejea na kuweza kuzungumza kilichotokea mpaka anasingiziwa kesi ya wizi ambayo hakuitenda.
“Waliniteka…Wakanitesa…Wakanichoma sindano za madawa mara kwa mara mpaka nikawa sijikumbuki….” Izani akafunguka huku machozi yakimtoka. Mkasa wake ulimgusa mpaka muheshimiwa Rais na viongozi wengine wa serikali.
Watu walilaani baada ya kuujua ukweli ambao wengine uliwatoa machozi kumuona na kumsikia Izani akizungumza hadharani mbele ya vyombo vya habari kwa mara ya kwanza. Wengi wakakiri kweli Ndimbo Masizi ni Shetani Mwenye Sura ya Malaika. Na kila aliyekiri hilo akawa Mfuasi mpya wa Izani Nteze.
“Natoa agizo kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuhakikisha pia wanachunguzwa wachungaji wote waliokuwa na urafiki wa karibu na Ndimbo Masizi pia nawaonya viongozi wa dini zote na kuwaomba wasitumie jina la Mungu kama kivuli cha kuficha maovu yao. Serikali yangu haitatazama hilo endapo utabainika muhalifu. Nawaomba sana na kuwakumbusha jamani tumuogope Mungu.”
Nukuu hiyo ikanukuliwa kwenye akaunti ya Twitter ya Rais wa Tannzania.
Kesi ya Ndimbo ilipotajwa kwa mara ya kwanza pale mahakamani ndipo Lululu akamtokea kichawi mchungaji Ndimbo Masizi akaanza kuweweseka mbele ya halaiki.
“Msiniue tafadhaliii…Nisamehe Lululu nimeangamia…Aaah” Ndimbo akapayuka na kumshangaza hata Hakimu. Kile alichokuwa anakiona hakuna mwengine aliona.
“Umeshindwa kuwa mtiifu Ndimbo. Umesababisha matatizo na sasa utaenda kuteseka na kutumikia katika ulimwengu wetu.” Lululu akasema huku akimchoma kisu cha kishetani Ndimbo Masizi kwenye moyo na kuanza kumvuta kimazingara bila waliokuwepo kung’amua zaidi ya kumshuhudia Ndimbo akianguka kizimbani.
Mahakama ikashangaa kuona mtuhumiwa Ndimbo Masizi akianguka huku amejishika moyo baada ya kuweweseka. Ikabidi zifanyike huduma za kumsaidia haraka na kesi kuhairishwa huku watuhumiwa wengine wakirudishwa rumande.
* *
Hatimaye Mchungaji Ndimbo Masizi akafariki akiwa anakimbizwa hospitali ambapo walipompima wakagundua amekufa kutokana na mshtuko wa moyo. Ingawa katika uhalisia muda huo Ndimbo alikuwa katekwa kichawi na kufikishwa kwenye himaya ya mateso makali na kutumikia ambayo ilikuwa chini ya Dokta Zongo na magwiji wenzake wa kishetani kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu.
Msiba mwengine ukamkuta mama Anita. Msiba ambao haukuwa na mvuto wa upendo. Waandishi wa habari na polisi wakawa wengi msibani kuliko waumini wa kanisa na raia wema. Ndimbo Masizi hakuzikwa kwa heshima ile aliyojitengenezea akiwa hai. Ingawa pia katika uhalisia kilichozikwa hakuwa Ndimbo Masizi ila ni kiini macho tu! Ndimbo akabaki kwenye kifungo cha mateso ya kishetani ambapo huko alipigwa muhuri wa mateso mpaka kifo cha kweli kitapomkuta.
Kesi ya Chikala na Chox haikucheleweshwa ilipotajwa mara pili na hukumu ikatolewa baada ya ushahidi kukamilika wote wakakutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka thelathini kila mmoja.
Kisa Kabeby akakimbia na kuutelekeza Mgahawa baada ya kuhofia asije kujumuishwa kwenye kesi.
Yule Mkuu wa Kituo Mtamba akakutwa na hatia baada kuchunguzwa na Takukuru akashtakiwa kwa kosa la kupokea rushwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili bila dhamana.
Koplo Ponda akapandishwa cheo kikubwa zaidi ya mwanzo alipokuwa jijini Dar. Akaapishwa na kuvishwa nyota moja iliyomtambulisha kuwa Isnpekta Msaidizi wa Polisi na kupewa kituo cha Mtamba kuwa mkuu wake mpya.
Izani Nteze akapelekwa nje ya Nchi na ofisi ya Rais kwa matibabu zaidi wakati nafsi ya Anita ikifunguliwa rasmi milango ya ulimwengu wa nafsi na kupokewa mahala pema alipoungana na nafsi nyengine njema.
Ndoa ya Zuberi Mwanahaki na Neema Hussein ikarejea kwenye amani na utulivu wake. Mawasiliano yao na Izani aliyefikishwa Marekani kwa matibabu yakawa yanaendelea kila siku kwa njia za video calls.
Kanisa la Ndimbo Masizi likachomwa moto na watu wasiojulikana na hata mama Anita akahofia kuendelea kuishi jijini na kuamua kurejea kijijini kwao akiwa na watoto wake Papii na Doris.
Huko akaamua kujikabidhi mbele ya Kristo kwa imani akisoma biblia na kuwahimiza watoto wake waishi kwa kumtegemea Mungu wala wasije kubabaishwa na tamaa za ulimwengu watapokuwa wakubwa.
(SIKU CHACHE BAADAE)
TANDALE - DAR ES SALAAM
“Samahani kaka Zomboko. Nataka kufanya kipindi na wewe. Jina lako limeombwa na wadau wengi wa Habari za Kitaa waliokusikiliza siku ile.” Markus Makata akazungumza baada ya kufika kwa mara nyengine uwanja wa Fisi kwenye saluni ya Zombi Zomboko, ambayo sasa aliibadili jina kutoka ZOMBOKO HAIR CUTTING SALOON na kuwa MFUASI HAIR CUTTING SALOON
“Unataka kunihoji au unaomba?” Zomboko akajibu kwa sauti kavu huku akimtazama Markus ambaye siku hiyo aliongozana na timu nzima ya kipindi chake waliofika na gari yao ndogo ya ofisini.
“Ok, samahani…Naomba!” Mark akajibu huku akishusha pumzi.
“Anhaa! Sawa, Je, nawe ni shabiki wa Izani Nteze?” Zomboko akauliza.
“Hapana…” Mark akajibu
“Ila,,,,” Zomboko akasema huku akimtazama Mark na timu aliyokuja nayo ambao walisimama nje wengine wakiwa wamebeba kamera kwaajili ya kuwaonesha watu wa mitandaoni.
“Mimi ni Mfuasi wake Izani Nteze.” Markus akajitambulisha.
“Weeh Hahahahahaaa Karibu sana Mfuasi mwenzangu.” Zomboko akacheka kwa mara ya kwanza Markus naye akacheka na hata alioongozana nao wakatabasamu na amani ikanyanyuka mioyoni mwao. Wakaandaa mazingira kwaajili ya kipindi ambacho sehemu kubwa ya nchi siku hiyo waliwasha redio kumsikiliza Zombi Zomboko ambaye kwa mara ya kwanza kwenye kipindi cha siku hiyo akajitambulisha hewani huku akirekodiwa na video kuwa naye ni MFUASI wa Izani Nteze na anamsubiri kwa hamu ataporejea kuendeleza mapambano ya vita vya uraibu na utumiaji wa dawa za kulevya
MWISHO