SEHEMU YA KUMI NA TANO
Mama aliendelea kusimamia msimamo wake uleule kuwa
hayupo tayari kuamini mtu yeyote tena. Ataandamana
na mimi kila sehemu ilimradi tu auone mwisho wangu
aidha uwe mzuri ama mbaya.
Msimamo wa mama ukasababisha liibuke wazo jipya
kutoka kwa watu wale waliokuwa wamekusudia
kutusaidia.
Wakaniuliza juu ya ndugu tuliokuwanao Dodoma,
nikamuuliza mama swali lile kwa sababu wao
waliniuliza kwa kiingereza. Mama akasema hatukuwa
na ndugu kule.
Basi kwa sababu hatukuwa na ndugu tukaona ni vyema
na haki kumpumzisha mjomba katika kijiji kile
tuwatafute wasamaria kadhaa tulichimbe kaburi na
kumpumzisha pale.
Hilo tukaliafiki kwa pamoja!!
Kweli ikawa, mjomba akalala katika ardhi isiyokuwa
yake.
Naam! Haikuwa sawa lakini tusingekuwa na la kufanya
kwa sababu mambo yalikuwa mabaya haswa!!
Baada ya hapo safari ya kuelekea jijini ikafuata.
Tulisafiri usiku na alfajiri ilitukuta tupo jijini Dar es
salaam.
Hakika mama alikuwa amemaanisha aliposema
ataandamana nami popote iwe kwa heri ama shari.
Mama hakukubali kulala chumba tofauti na mimi.
Alisema kuwa ameishi nami miaka yote akinilea
mwenyewe na sasa sina mikono linabaki kuwa jukumu
lake kunilea mimi upya hivyo ni sawa tu nitalala naye
vchumba kimoja hadi hapo hali ya hewa itakapokuwa
tulivu.
Wale wazungu hawakupinga, tukalazwa chumba kimoja
na mama akawa mtu wa mwisho kabisa kuufunga
mlango. Akanilaza kitandani na yeye akaketi katika
kochi ambalo alikuwa ameliweka mlangoni kiusalama.
Nilimuonea sana huruma mama yangu, maisha yale ya
mashaka yalimfanya akakakonda sana. Alikonda kiasi
kwamba ukimuona kwa mara ya kwanza na kuelezwa
kuwa hapo awali alikuwa ni mnene utakataa katakata.
Lakini uwepo wa mama yangu, mwanamke na
mwanadamu pekee niliyekuwa namuamini kulinitia
faraja na hata kusinzia nilisinzia vizuri.
Mama yangu alikuwa nami bega kwa bega alinifanyioa
kila kitu kasoro kuniogesha tu ndio nilisaidiwa na wale
wazungu!
Baada ya siku mbili hatimaye tukapata miadi ya kufika
shirika la kutetea haki za wanadamu lililokuwa na ofisi
zake kubwa hapohapo jijini.
Wazungu wale hakika walikuwa wameonyesha nia ya
kutusaidia.
Niliusimulia mkasaa wote katika shirika lile, kadri
nilivyokuwa nawasimulia yote niliyoyapitia wakawa
wanatoka machozi jambo hili likanifanya nijikute na
mimi nikitokwa na machozi. Nilijiuliza ikiwa hawa watu
maneno tu yalikuwa yanawaliza vipi kuhusu mimi
ambaye niliyapitia maumivu makali kabisa moja kwa
moja katika mwili wangu.
Nilimtaja hadi yule mwanasiasa kwa majina yake juu
ya hujuma aliyotaka kuifanya ili kuniua na kumfunga
bila makosa daktari aliyeniokoa ambaye hadi wakati
ule nilikuwa sijui nini hatma ya yeye na familia yake.
Nilipotaja kuhusu yule daktari. Wale watu walinizuia
kisha mmoja akanieleza jambo zito.
Yaani kumbe baada ya mkasa ule wa pale mahakamani,
waliniteka mimi lakini hawakuiacha hivihivi familia ya
daktari, familia ilikutwa imeuwawa kinyama, mama
pamoja na watoto wake.
Daktari alivyopata ushuhuda ule akarukwa na akili na
hadi wakati huo alikuwa katika hospitali ya vichaa
mirembe akipata huduma.
Nilijikuta nakuwa mkimya kwa takribani dakika mbili
nikimtafakari yule mwanasiasa na hapo nikajiuliza
swali moja la msingi. Ikiwa huyu mwanasiasa hana
uwezo wa kumpenda mtu mmoja mmoja ataanza vipi
kuipenda na kuipigania jamii yake ikiwa atapewa
madaraka.
Kufikia wakati ule hadi sasa nikajikuta naichukia sana
siasa!!
Siku mbili baadaye nilifanyiwa mahojianon katika vituo
mbalimbali vya runinga, awali niliona kama inasaidia
sana lakini kadri nilivyokuwa nikisikia taarifa za
mauaji kuendelea nilijiona kama ninayekata tamaa.
Yule mwanasiasa hakupatikana alipokuwa na familia
yake haikujulikana wapi ilipo. Nikajisemea kuwa
huenda alikufa akiwa katika jumba lile baada ya
kumngáta vibaya sana yeye na mkewe.
Hilo la kuhisi kuwa huenda alipoteza uhai
lilinifurahisha sana kwa sababu hakika alistahili.
Kumbe kule kuonekana kwangu katika runinga na
kujitambulisha kwa majina yangu yote mawili
kukayafikia masiko ya mtu mmoja. Mtu yule akampigia
mama yangu simu.
Siku hiyo baada ya mahojiano katika kituo kingine cha
runinga nilirejea mahali alipokuwa mama na kumkuta
akiwa mnyonge sana. Nilikuwa ninao mpamgo wa
kumueleza kuwa kuna mtanzania mmoja amejitolea
kunipeleka ujerumani ili niweze kuwekewa viungo vya
bandia yaani mikono na sikio, nikajikuta naghairi!!
Upesi nikajua kuna tatizo. Nikamuuliza mama ni kitu
gani kilikuwa kinatokea…. Mama alitabasamu kisha
akaniita na kunikalisha pembeni yake.
“Mwanangu kuna mtu amepiga simu hapa!!” aliniambia
kinyonge.
“Nani huyo wa kupiga simu hadi unakuwa mnyonge
kiasi hiki mama yangu …” nilimdadisi.
“Amepiga simu baba yako, amekuona kwenye
televisheni anadai ameumizwa sana na yote
yaliyokutokea na anahitaji sana kufika hapa tulipo….”
Mama alinieleza huku akibetua midomo yake.
Nilishindwa kuzungumza kitu chochote kile kila
nikijaribu kufungua kinywa changu nakosa neno
sahihi.
Hatimaye nikaweza kuzungumza.
“Mama ukimruhusu huyo shetani kukanyaga hapa
nitamuua…”
Mama alinitazama kisha akanisihi sana kuwa iwe isiwe
yule ndiye baba yangu na ana haki ya kuniona na
kunijulia hali. Alisihi sana mama lakini sikujiona kabisa
kama nilikuwa tayari kukutanisha macho yangu na
baba yangu mzazi.
Alinisaliti vibaya sana baada ya kugundua kuwa
nilizaliwa nikiwa na ulemavu wa ngozi inakuwaje sasa
hivi aonyeshe kuguswa na haya yaliyonitokea.
Kwanini basi hakuguswa zamani sana baada ya kusikia
nimezaliwa nikiwa mlemavu. Ni kwanini alinisaliti na
kunikimbia!!
Jamani duniani kuna watu wanajua kusuka mipango!!
Looh! Imeshawahi kusukwa mipango mingi lakini huu
ulikuwa hatari zaidi.
Baada ya mama kunisihin sana kuonana na mzee
wqangu, nikamweleza sawa nitaonana naye lakini
sihitaji kabisa aanze kuniita mimi mtoto wake naomba
aje kunisalimia kama muhanga wa kawaida tu!!
Mama akamweleza mzee wangu akakubali na kuahidi
kufika siku inayofuata!!
Siku aliyofika alifika na kitoto kidogo, ambacho pia
kilikuwa na ulemavu wa ngozi.
Baada ya kuwasalimia watu wote hatimaye tukaachwa
kama familia yaani mimi mama pamoja na yule mzee na
kile kitoto.
Baba akazungumza sana akadai kuwa anasikitika sana
kwa sababu alijaribu kukikimbia kiitu ambacho
aloikuwa amepangiwa.
“Mama Majaliwa nakiri kuwa nilikuwa nasumbuliwa na
ujana nikakukimbia na kukuacha na mtoto, nilikuwa
mjinga hakika. Lakini hata mwanamke wa pili
niliyempata na yeye akaishia kuzaa mlemavu wa ngozi.
Huyu unayemuona hapa ni mtoto wangu wa pili na
nimetambua kuwa Mungu alinipangia tu kumpata
mlemavu wa ngozi ili nimuonyeshe upendo wote kutoka
moyoni…. Majaliwa mwanangu huyu ni mdogo wako
anaitwa Catherine tafadhali sana naomba umpende
kama unavyompenda mama yako. Najua mimi
haunipendi hata kidogo lakini mpende mdogo wako
yaliyopita yamepita mwanangu.” Baba alinieleza yale
maneno kwa sauti iliyojaa hekima.
Dah! Sijui nd’o kurogwa ama ni kitu gani kile lakini
nikajikuta eti namuona baba kuwa yupo sawa kabisa
na kosa alilofanya ni kwa sababu ya akili za ujana tu.
Na ule uwepo wake pale na mtoto mndogo yule ambaye
anayo ngozi kama yangu kukanifanya nimpende na
kuiona familia ikiwa kubwa na yenye amani. Nikajikuta
nasimama na kumkumbatia mzee wangu na kumweleza
kuwa nimemsamehe. Mama akatabasamu tabasamu
pana kabisa bila shaka lilitoka moyoni. Siku ile baba
alikaa pale hadi usiku kabisa Cathe akapitiwa na
usingizi baba akampigia simu mama yake Cathe na
kumweleza kuwa anamuacha cathe kwa kaka yake,
mama yake akaruhusu. Na hapo baba akaaga na
kuondoka.
Ama hakika damu inabaki kuwa damu hakuna maji
yanaweza kuiziti uzito damu.
Nikajiona niliukosa upenbdo wa baba yangu kwa muda
mrefu na nikajikuta namtamkia kuwa kesho pia aje
tushinde wote pale.
Sura ya baba yangu ni sawa nilikuwa najitazama
katika kioo, sema yeye alikuwa mweusi tu!!
Tulifanana sana!!
Kweli kesho yake mapema kabisa baba akafika akiwa
na nguo za Cathe za kubadili!!
Akaniletea na zawadi kadha wa kadha na hakusita kila
mara kunikumbusha kuwa anajutia kila kitu
alichofanya enzi za ujana wake!!
Nilimwambia asijali kabisa!!
Sikujua hata ni kitu gani alikuwa anakiwaza kwa
wakati huo!!
Na hapa huwa unakuja ule usemi LAITI NINGELIJUA!!!