SEHEMU YA KUMI NA MBILI
Nikiwa nimeyafumba macho yangu huku nikitambua
fika kuwa iwe isiwe lazima tu yule bwana ataniua.
Nikajiona mzembe kufa kirahisi bila hata kuparangana
kana kwamba ni haki ya yule bwana kuniua.
Nikayafumbua macho ghafla na kumkuta akiwa
anajiandaa kunifanyia alichotaka kunifanyia. Bila
kutarajia nikajikuta nafanya kitendo cha kijasiri bila
kuwa na mikono yangu.
Ningetumia silaha gani kama sio meno yangu.
Mpenzi msikilizaji, hii sio simulizi ya kutungwa
ukalichukulia lililotokea kama jambo la kawaida.
Ni kweli yalinitokea.
Nikamrukia yule bwana nikiwa nimeyaandaa meno
yangu na kutua vyema katika shingo yake. Ikawa
bahati nzuri kwangu na mbaya zaidi kwake.
Meno yakainasa shingo ipasavyo.
Nilitumia nguvu zangu zote zilizokuwa zimebakia
mwilini kumjeruhi yule bwana, nikayaunganisha meno
yangu, kwa sikio langui moja nikakisikia kisu
alichokuwa amekuja nacho kikidondoka chini na yowe
kubwa likimtoka.
Nikazidi kumtafuna shingo yake huku nikijua kuwa ule
ndio ulikuwa mwisho wangu. Sikujali damu iliyokuwa
inaruka nilichotazama ni kwamba na yeye anaumia
kama tulivyokuwa tunaumia sisi.
Nikiwa nimemng’ang’ania yule bwana hadi sauti ikawa
imekatika. Nikasikia mtu akijaribu kunivuta kwa
nyuma, wakati huo yule bwana alilegea na kutua chini,
nikiwa nimelowa damu vibaya mno na mguu wangu
wenye lile hogo gumu kabisa, nikamtandika tege kwa
kutumia ule mguu wenye hogo.
Kimyaa!! Hakutikisika!!
Nikageuka nikakutana na mwanamke ambaye alikuwa
akijaribu kunizuia nisiendelee kumsulubu yule bwana.
Sikujali lolote sasa nilikuwa kama kichaa, nilimvaa yule
mwanamke nikaanguka nay echini.
Wakati naanguka nikakutana na picha ukutani yule
mwanamke akiwa na yule mwanasiasa.
Kumbe ni mke wake!!!
Hasira maradufu ikanipanda tena, nikaendelea
kutumia silaha ya meno. Nikamng’ata mkono wake
kwa nguvu zote akatapatapa na kunirusha huku na
kule.
Naam! Akafanikiwa kunitoa katika mkono lakini sasa
nikatua katika paja lake, bahati iliyoje. Niliingiza
meno yangu pale kwa jinsi yalivyopenya nikahisi ni kwa
namna gani alikuwa akiumia yule mama.
Na aumie tu kwa sababu nilitaka aumie sikumg’ata ili
afurahie.
Alipiga kelele kubwa sana na kisha akapoteza fahamu.
Upesi nikatoka katika chumba kile nikiwa natamani
sana kuwa ningekuwa na mkono nilichukue bisu lile na
yeyote atakayekuja mbele yangu awe halali yangu.
Lakini sikuwa na mikono tena. Nikaifungua milango
kwa kutumia miguu na mikono.
Hatimaye nikalifikia geti na huko nikakutana na
mlinzi.
Bila shaka alipagawa kuniona nikiwa nimevuja damu
kiasi kile.
Akaanza kunionya kuwa nisimsogele.
Ebwana eeh!b nikaisikia lafudhi yake, alikuwa na
lafudhi ya kabila langu.
Aikwambie mtu kuwa kabila halina thamani tafadhali
sana jifunze lugha mbalimbali jifunze makabila
mbalimbali pia ukiweza. Wakati mwingine ukizungumza
na mtu kwa kabila lake ama lugha yake anajikuta
anakusikiliza na kukupa nafasi ya kujitetea.
Palepale nikatumia faida ile ya lafudhi ya mlinzi
nikamsemesha kikabila.
“Naitwa Majaliwa mwenyeji wa Dodoma, Mgogo halisi
kabisa… ikiwa sawa kushiriki katika kuniua mimi ndugu
yako basi uniue kwa kutumia hilo gobole lakini kama si
sawa kushuhudia mimi ndugu yako nikifa tafadhali
nisaidie, nimeteseka imetosha sikuzaliwa unavyoniona
nilivyo, wamenikata viungo vyangu, tafadhali
usishiriki dhambi hii…’ nilizungumza kiujasiri sana.
Na kweli kabila likaleta uzito akaniuliza ni kipi
kimetokea hadi nimelowa damu vile. Nikamweleza kuwa
ilikuwa niuwawe. Ni Mungu tu ameniokoa.
Kweli ikawa yale ya damu nzito kuliko maji.
Akanisogelea huku akionekana kuwa na hofu
akanichukua na kunitoa nje, huko akaniambia kuwa
yeye ni mlinzi na huwa hajui ni kitu gani kinaendelea
pale.
Lakini kuna watu ambao huwa anawaona wakija eneo
lile na kuondoka. Na yale sio makazi ya mtu bali kwa
msimu tu.
Aliposema kauli hizi akanifanya nitambue kuwa eneo
lile ni la siri sana na ni maalumu kwa maovu kama
haya.
Ajabu sasa akanieleza kuwa eneo lile lilikuwqa lipo
Dodoma!!
Nilistaajabu mpenzi msikilizaji, yaani kumbe nilikuwa
nimepelekwa kufia katika ardhi yangu ya nyumbani.
Yule mlinzi akanieleza kuwa sitakiwi kuwa pale na hata
yeye pia hawezi kuwa salama ikiwa watafika watu
wengine ambao huja katika nyumba ile na kutambua
kuwa kuna kitu anakijua kilichotokea pale ndani.
Wakati anamalizia haya mara ikasikika gari iija kwa
kasi.
Akaniamrisha nipotee, na hapoi akaqongoza njia na
mimi nikimfuata nyuma.
Msikilizaji, sikio la mwanadamu hutumika katika
kubalansi mwendo, kwa jinsi nilivyosoma shuleni ni
kwamba mtu asipokuwa na masikio hawezi kuendesha
baiskeli wala hawezi kukimbia mwendo mrefu.
Sasa nilikuwa katika kuona kwa macho yangu, nilikuwa
naanguka hovyo hovyo yule mlinzi akawa
ananinyanyua na kuendelea kukimbia sikujua hata ni
wapi tulikuwa tunaenda.
Ila sikuchoka kwa sababu nilijua kuwa Mungu yu
pamoja nasi na ni yeye aliyeniokoa hadi kufikia pale
nilipokuwa.
Baadaye yule mlinzi mzee ambaye ndiye aliyekuwa
anaongoza njia alishikwa na kichomi, akaapa kuwa
hawezi kuendelea kukimbia. Nilitamani basi mimi
nimbebe lakini ningeanzaje sasa.
Akanisemesha kilugha akanisihi nikimbie tu na nikifika
kijiji cha tatu kutoka hapo niulizie kwa mzee
anayeitwa Chilongani. Nikishampata nimeweleze kila
kilichotokea na kisha yule bwana akajitambulisha kwa
jina la Gaspa.
Nikaendelea kukimbia huku nikiamini kuwa utakuwa
muujiza tu kufika salama.
Nilikimbia huku nikiendelea kuburuza mguu wangu
wenye bandeji gumu.
Ilikuwa ngumu lakini ningefanya nini, walau nilikuwa
katika ardhi niliyozaliwa huenda nilikuwa nimeikaribia
mikono salama.
Sikuwa hata naelewa ni umbali gani kukimaliza kijiji
kimoja hadi kingine lakini nilikimbia tu bila kukoma.
Hatimaye na mimi nilichoka hadi hatua ya mwisho.
Lakini bado niliendelea kutembea mwendo wa taratibu
sana.
Na hatimaye nikaamua kucheza pata potea.
Nikaiendea nyumba fulani nikaugonga mlango.
Niligonga kama mara tatu, hatimaye mlango
ulifunguliwa na mwanaume aliyekuwa na panga kali.
Akauliza kikabila, na mimi nikajibu kikabila. Nikataja
jina la Chilongani!!
Akaniuliza iwapo mimi ni mwenyeji eneo lile
nikamwambia kuwa ni mwenyeji kiasi kiasi fulani.
Akaniuliza jina la ukoo wangu, nikamjibu!!
Nilipojibu jina langu la ukoo, ghafla nikasikia kilio
kikubwa sana kutoka ndani.
Kilikuwa ni kilio cha mwanamke…..
Na mara yule mwanaume pale mlangoni akasukumwa
na kuangukia mbali na hapo nikajikuta natazamana
ana kwa ana na mama Majaliwa!!
Akanikimbilia kwa nguvu sana na kunikumbatia
tukaanguka chinbi wote.
Nilibaki tu kuita mama mama… nisijue ni kitu gani
naweza kusema.
Yaani usiku mnene kama ule nikiwa nahitaji msaada
mkubwa kabisa nakutana na mama yangu mzazi??
Nilistaajabu msikilizaji, nililia sana….
Mama yangu naye alilia sana!!
Wakati haya yakiendelea yule bwana aliyekuwa
ameanguka mbali alikuwa sasa amesimama akishangaa
kilichokuwa kinaendelea!!
Na tukiwa bado pale chini mama yangu alikoma kulia
kisha akaanza kuzungumza.
“Maiko nilikwambia ukabisha, nilikwambia mwanangu
anateseka, nilikwambia kuwa moyo wangu hauna
amani hata kidogo ukasema niache imani potofu.
Mungu alikuwa anasema na mimi, angali wamenitesea
mwanangu, angali wamemkata mikono… yaani… yaani
kweli wameniumizia mtoto wangu hivi..” mama
hakuendelea kuzungumza tena akaanza kulia kwa
sauti ya juu sana.
Sikuhitaji kuwaza juu ya nini kinachopita katika moyo
wa mama yangu. Nilijua ni misumari mikali sana
inaupasua moyo wake!! Mama yangu alikuwa anaumia
sana!!!