Riwaya: kimbia kimbia

warumi

R I P
Joined
May 6, 2013
Posts
16,213
Reaction score
18,471
MTUNZI: HUSSEIN KULINDWA SEHEMU YA KWANZA MARA
baada ya kumaliza kupata chakula cha mchana, alielekea chumbani kwake kujipumzisha.

Huko alipumzika kitandani huku akiwa amefungulia radio yake na kusikiliza mziki laini huku akisoma moja ya magazeti yaliyokuwepo hapo kitandani kabla ya kuingia kwake chumbani humo.

Na ndivyo si zaidi ya dakika arobaini, tayari alichotwa na usingizi ambao hatahivyo ulimlaza hadi majira ya jioni. Aliamka, akatoka chumbani na kuingia sebuleni ambako nduguze walikuwa wakiangalia sinema (Unfaithful); na huku akisalimiana nap, alijiunga katika utazamaji wa filamu hiyo.

Hata hivyo, hakuweza kuiangalia sana filamu hiyo; na hivyo, hakufanya kwa sababu tu ladha ya kutamani kuitazama ilichafuliwa na kule kukerwa na mazungumzo ya nduguze ambao walikuwa wakizungumzia mambo ya wanaume (pengine mabwana zao) kwa kulinganisha na sinema hiyo; bali hivyo alitokana pia na ukweli picha hiyo ilianza kumchosha sana kutokana na kuirudia kuitazama mara kadhaa huko nyuma.

Hivyo ndivyo kwa kiwango fulani alivamiwa na upweke uliopewa makucha ya kuukwaruza moyo wake kutokana na hizo zungumza za dada zake; na ndivyo hali hiyo ya kujihisi mpweke ilisababisha ajikute akiwakumbuka watoto zake mapacha ambao alikuwa hajawatia machoni kwa takriban mwezi mzima na nusu hivi. Mawazo hayo yalimchukua hadi kumfikisha katika kujiundia uamuzi ya kwenda kule mbagala ambako ndiko watoto wake walikuwa wakiishi pamoja na mama yao mzazi.

Hivyo, aliinuka na kuondoka sebuleni bila hata ya kuwaaga dada zake. Alirudi chumbani kwake na kuvua nguo na kisha alivaa bukta, akatungua taulo na kutoka kuelekea maliwatoni. Haikumchukua dakika nyingi kuoga; na alipomaliza, alitoka bafuni na kisha akarudi chumbani tayari kwa kujibodoa na kuvaa.

Mara baada ya kuvaa, aliondoka chumbani na kuelekea jikoni ambako alimkuta mama yake aliyekuwa kajituliza kitini huku msichana wa kazi akiwa amekaa mkekani akikatakata nyama.

Alisimama nyuma ya kiti hicho alichokikalia mama yake akikiegamia. Alitulia kidogo hapo kuruhusu kuzivuta pumzi; mama yake bado hakujua ingawaje msichana wa kazi alijua kwani alimuona. "Mama, nina shida.

" Mama Esta alishtuka kidogo na kisha aligeuza kichwa chake nyuma, na alipomuona sauti ndogo ya kuguna ilimtoka! Ndio, bila mama yake kumtazama ingekuwa shida kiasi kumjua kutokana na wanawe kufanana sauti, tena wakifanana na sauti yake.

Naam, huyu aliitwa Henry Kipekecho, mtoto wa pekee wa kiume katika familia yao ambaye licha ya kufanana na baba yake, alikuwa na sauti ya kike iliyokuwa nyororo kiaina! Kwamba, sura na sauti yake havikuendana kabisa, kwani ilikuwa ni sawa na kujaribu kuwafananisha paka na panya.

Hasa ukizingatia kuwa Baba Esta alikuwa na sura mbaya kiasi, basi ndivyo pia Henry alikuwa hivyo bila kujumlisha ile ‘pasi ya iliyozidi kumfanya alandane sana na baba yake .

Mama Esta aliacha tena kumtazama kabla ya kutoa jibu, "nitaongeaje na mtu mgongoni? Hiyo ni adabu?" Henry alijilamba midomo kidogo, na kisha akatoka nyuma ya kiti; alisimama mbele ya mama yake na kuanza kusema, "mama, nataka kwenda kuwaona wanangu. Sijawaona muda mrefu!" "Nani kakukataza?...kwanza tangu lini ukaniaga unaenda huko?

Wewe sema unachotaka kusema! Acha vunga za kipuuzi hapa...Mtu mzima ovyoo!" "Sasa mama....?" Henry hakumalizia usemi aliotaka kuusema; na usoni tayari mistari miwili mitatu hivi ilianza kuelekea kutaka kujitokeza. Baada ya sekunde chache aliendelea tena, "mama… yaani, unani...aah! Anyway, siyo mbaya sana kwani haya yote ni kweli ni kwa ajili ya upuuzi wangu mwenyewe."

Mama Esta hakujibu. Henry alivyoona mama yake bado hajibu, alisema tena huku akifanikiwa kuondoa ile mistari iliyojichora katika paji lake la uso, "mama, nilikuwa naomba nauli, nataka kutoka kidogo." "Aha, kumbe ulikuwa unaomba! Isipokuwa kwa sasa…baba huombi, eeh?" Mama Esta alimjibu kwa kuzungumzia puani kwa namna ya kumdhihaki na kisha aliendelea kusema, "hivi kwanini hutulii ukatulizana?

Au nyumba hii ina miba inakuchoma?" Mama Esta alitoa cheko dogo. "Sio hivyo mama!" "Sio hivyo!" Sauti ya puani ilimtoka tena mama Esta huku ikisaidiwa na mkono wake wa kushoto kubana pua zake. Zaidi alisema, "kumbe nini?" "Ahm…nataka kuwaona…nataka kwenda kuwaona watoto wangu kama nilivyokueleza."

Henry alisema huku vidole vya mkono wa kulia vikichezeachezea ndevu zake za kidevuni. ‘Kubwa jinga na kigari chako mshenzi!' Henry alihisi kuisikia sauti fulani ikimkoromea mawazoni. "Nani atakuweza kwa uongo? Hizo ndizo fix za leo, sivyo?" Mama Esta alimjibu baada ya kutoa mguno mwingine mdogo wa kebehi.

Aliendelea kusema, "we sema unataka kwenda kwa huyo mwanamke wako! Nani asiyekujua bwana!" "Mama bwana…aah!" Henry alisikitika kinamna. "Salma! Ebu nipe hiyo pochi hapo juu ya hilo jiko." msichana wa kazi, aliagizwa. Hakuwa mbali na jiko. Aliinuka na kuunyoosha kidogo mkono wake wa kulia; na kisha ndipo aliweza kuikamata pochi. Mama Esta akapewa pochi. "Haya shika."

Alipatiwa noti ya alfu kumi. Henry aliipokea noti ile ingawaje lile tabasamu lake lililokuwa limeanza kuchipuka kwa kuchezacheza hapo mdomoni mwake lilianza tena kuchuja; ndio, hakuridhishwa na kupewa kiasi kile. "Mama, huyu msimbazi ni ponyoo dhaifu, hawezi kupenyee. Niongezee angalau mdogo wake…hapo wanaweza kusaidia kuzungumza vizuri. Mama si wajua mambo ya kasi mpya ari mpya?." "Sikuelewi, wasemaje?" Mama Esta alimaka. Akijiumauma, Henry alijibu, "mama niongezee japo alfu tano hivi. Hii kumi haitoshi." "Leo hali siyo njema."

Mama Esta alisema huku akichambua noti kadhaa zilizokuwemo katika pochi yake. Baadaye, alimpatia noti tatu za alfu huku akiendelea tena kusema, "haya, kama kweli wewe ni mwanaume niletee wajukuu!" Henry hakujibu; alitumbua macho! Hata hivyo, angejibu nini na wakati kila mara husisitiziwa jambo hilo na asiweze kulitenda! Kwa upande mmoja alimuona mama yake kama aliyemkashifu, lakini; na wakati kwa upande mwingine, huko aliyaona maneno yake yakisimama ni ukweli ukumbushao hadithi tupu imuumizayo. ‘Kweli mtu na tafsiri zake!' Aliishia kujisemea. "Hivi nasema na nani hapa?" Mama yake alimkazia macho.

Alizidi kufoka tena, "Hivi wewe vipi lakini? Kwanini huwi ngangari kuwachukua watoto wako na wakati haki zote unazo? Walete watoto, tutawalea bila matatizo kama tunavyokulea wewe pamoja na uzima ovyo wako!" "Ahsante mama." Henry alijibu haraka haraka na kuanza kuondoka huku akijifanya kama yale aliyokuwa akielezwa na mama yake yalikuwa habari za utani tu; lakini ukweli ilikuwa huko kichwani mwake tayari kulikuwa kumefumuka zogo fulani! Ndio, kile kichaa cha mapenzi juu ya Brigitte ambacho ingawaje ni kweli kilikuwa kimepungua sana, lakini hatahivyo, bado kilikuwa na uwezo wa kuendelea kumvuruga akili na hata kuweza kumfikisha katika kufanya maamuzi ya kipumbavu kwa hasara zake mwenyewe.

Bado alihitaji ushauri nasaha! Ndio hili alifahamu vyema! "Mbona hunijibu?…Unadakia ahsante tu!" mama Henry aliuliza huku akitoa cheko jingine dogo ambalo dhahiri lilikuwa la kejeli; na alijua sana alimuudhi mwanawe kwa kumuuliza mambo ambayo hakuwa na ujasiri wa kuyatimiza.

Hata hivyo, alifanya kumuuliza kama vile yalikuwa ni masihara ingawaje kwa namna fulani ilikuwa ni moja ya njia zake katika kumpatia somo mwanawe wa kiume wa pekee na kitinda mimba wake. Alikuwa mtoto wa sita.

"Mama, sasa unaninyanyasa!" Henry alitunisha misuli hata tazama yake ilithibitisha. Ndio, alitupa jicho kali! Jicho la shari! "Nani akunyanyase? Wewe unafikiri ni nani atakayekuongoa kama sio sisi wazazi na nduguzo?" Mama Esta alijibu kimasihara, na kisha akafanya kama aliyekasirika na ndivyo aliingia kusema kwa ukali, "haya potea kabla sijakunyang'anya hela zangu!…ala!" Alijikuta akikimbiwa na hasira zake ambazo zilidhihiri zilikuwa ni kamasi! Alisinyaa pia akianza kujiondoa kinyongenyonge hadi mlangoni.

Aliufungua mlango taratibu, kisha aligeuka na kumtazama mama yake kwa sekunde kadhaa… Hasira zikamrejea! Akafyonza na kutoka huku akiacha kaubamiza mlango wa jikoni kwa nguvu kiasi ulilia sana! Alitoka hadi uani. Huko alipitiliza hadi ilipokuwa imepaki gari yake aina ya landrover. Alizitoa funguo mfukoni mwake na kufungua mlango wa mbele wa gari. Tena akazichomoa funguo na kuingia garini; na kisha aliiweka simu yake ya mkononi ndani ya kichumba kidogo kilichokuwa wazi chini ya radio.

Alishikashika kidogo usukani na kisha tena, akazichomeka funguo katika ‘switch' kuiwasha gari. Alijaribu kwa safari kadhaa kuiwasha gari, lakini haikuweza kuwaka! Akajaribu tena na tena lakini wapi… Haikuwaka! Alitulia kidogo kama aliyekuwa akifikiria jambo fulani, halafu alibonyeza kitufe kimoja na kisha akatoka nje hadi mbele ya gari ulipo mlango wa chumba cha injini. Akaufungua mlango huo na kuanza kutazama ndani yake huku akijaribu kushika hiki na kile na kisha aliufunga tena mlango.

Alishusha pumzi kidogo, akarejea katika mlango wa dereva, akasogeza mkono katika ‘switch' na kuzichomoa funguo na kisha aliufunga mlango. Huku akisonya aliondoka zake. Alirudi hadi chumbani, akaziweka funguo mezani na kisha alitoka. Alipofika uwani, akielekea lilipo geti la kutokea nje ya jengo, aliweza kuzisikia sauti za mama yake. "Hilo kopo si alitupe tu jalalani tujue moja!...Ooh, gari yangu, gari yangu! Wenye magari wasemeje?" Hizo zilikuwa sehemu za sauti hizo.

Hapo hasira zilimzidia, na wala hazikuwa hasira dhidi ya mama yake; bali zilikuwa dhidi ya ule uhusiano wake na Brigitte jinsi ulivyopata kumpeleka hadi kumfikisha mahala ambapo leo hii amekuwa ‘mtu mzima ovyo huku kodi ya pango ni ubora wa shikamoo zake kwa hao wambebao!' Hasira hizo zilizokuwa sasa zimeibukia mawazoni kama mtawala mwenye mamlaka, mtawala mwenye madaraka; na zilikaribia kumfanya asitishe wazo la kwenda tabata.

Ndio, tafsiri zenye ushawishi mkubwa zilimwandama na kumjulisha ilikuwa ni fedhea kubwa kwenda huko huku akijua kwa kufanya hivyo ilikuwa pia ni sawa na kumtembelea ‘mvurugaji' aliyekuwa hadi wakati huo akiishi na Brigitte. ‘Marlon isn't your friend, but an enemy within friendship! (Marlon ni adui katikati ya urafiki)' Mawazo fulani yalimzaba kwa mwendo huu.

Sauti za mama yake zilizidi kumvuta Henry hadi kujikuta akirejeshwa nyuma kimawazo kwa kukumbushwa habari za nukta chache kabla hajafikia uamuzi wa kukaribisha uundaji wa uhusiano wa kimapenzi na Brigitte. Tena hata alimkumbushwa jinsi rafiki zake walivyowahi kumuhasa juu ya hathari za kujenga uhusiano huo dhidi ya ujengaji wa bora za maisha yake ya usoni.

***Mnh, Haya...hii ndio imeanza hivi itakwendaje?
 
Huyo mama kiboko!!
Ana maneno ya fedhuli unaweza umchape makofi
 
Eeh! Binamu umeamua kutuletea hadithi sasa, usisahau kutuita kwenye umbea tu
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…