Riwaya - Gereza la Kifo

Riwaya - Gereza la Kifo

Bishop Hiluka

JF-Expert Member
Joined
Aug 12, 2011
Posts
7,147
Reaction score
14,708
Gereza la Kifo

Mtunzi - HAMISI KIBARI

UTANGULIZI

Hamisi Hussein Kibari ni mtunzi wa riwaya na mashairi, mwandishi mkongwe wa habari nchini na mtengeneza filamu. Kwa kipindi cha takribani miaka 25, amekuwa akiandika hadithi katika magazeti mbalimbali. Baadhi ya hadithi zake zilizompa umaarufu ni pamoja na Ninastahili Kifo; Nkurukumbi; Hukumu ya Kifo; Machozi ya Suzana; Mtoto wa Boksi; Maskini Mdogo Wangu; Mtoto wa RPC; Nongwa; Nioneshe Mama na kadhalika.

Baada ya utangulizi huo, sasa endelea...

WALARI Saire alinyanyuka kwenda kufungua mlango wa ofisi yake ndogo baada ya kuona mtu aliyekuwa anagonga hatokei hata baada ya kumwambia mara mbili aingie ndani kwa kuwa mlango ulikuwa wazi.

Ofisi yake hiyo ilikuwa katika mtaa wenye shughuli nyingi, katikati ya Manispaa ya Mji wa Bulibuli. Ndio maana alikuwa kasindika mlango ili kupunguza kelele wakati akiandika habari aliyokuwa anatarajia kuituma kwa mhariri wake.

Pale nje alikuta watu wawili, mtu mzima na kijana mwenye umri wa miaka kati ya 18 na 20 wakiendelea kugonga. Inawezekana walikuwa hawamsikii wakati akiwakaribisha kutokana na kelele zinazosababishwa na magari pamoja na pilika nyingine za kila siku katika eneo hilo lenye shughuli nyingi.

Walari aliwakaribisha ndani, lakini kabla ya kuingia wakauliza kama ofisi ile ilikuwa ni ya mwandishi wa habari.

Msingi wa swali hilo bila shaka ulitokana kuidharau au kuishangaa ofisi hiyo finyu na isiyo maridadi. Isitoshe hakukuwa na bango lolote.

"Ndiyo. Hii ni ofisi ya mwandishi. Karibuni. Piteni ndani," akajibu Walari ambaye alishajua kilichokuwa kinawasumbua watu hao.

Ofisi yake ilikuwa kama uchochoro na hata ukuta wake ulikuwa haujapigwa rangi. Bado alikuwa hajapata fedha kutoka makao makuu ili kukarabati ofisi hiyo ambayo awali ilikuwa ikitumiwa na mafundi viatu.

Lakini hiyo ndio ofisi ambayo waajiri wake huko makao makuu ya nchi walikuwa na uwezo wa kuilipia pango kila mwezi. Licha ya uduni wake, ofisi hiyo iliyokuwa katikati ya mji, karibu na stendi, ilikuwa ikimfaa Walari kulinganisha na ofisi za waandishi wa magazeti mengine kwani ilikuwa rahisi kwa watu kumpata.

Na kuwepo kwake hapo, kulimsaidia kupata kirahisi matukio mengi yanayotokea katikati ya mji na kuyafanyia kazi mara moja.

Sasa aliona umuhimu wa kuweka bango pale nje ya ofisi hiyo ambayo alikuwa keshaitumia kwa zaidi ya miezi minane tangu aipate.

Wale watu wenye nyuso zisizo na furaha waliingia na kuketi kwenye benchi fupi lililokuwa mbele ya meza kuukuu ya Walari iliyochongwa kwa mbao duni.

Kwa dakika kadhaa wale watu walibaki wakipepesa macho katika ofisi hiyo, na hasa majarida kadhaa yaliyokuwa juu ya meza huku wakisubiri mwenyeji wao atulie ili wamweleze kilichokuwa kimewaleta.

Kitu cha maana kilichokuwa pale juu ya meza ni kompyuta ya kizamani na printa.

Walari alipita moja kwa moja hadi kwenye kiti chake ambacho angalau kilikuwa cha kisasa kiasi, nyuma ya meza yake.

"Karibuni sana… Naweza kuwasaidia?" Aliuliza Walari akitazama saa yake. Ilikuwa inaelekea saa tano na nusu mchana. Ilibaki nusu saa kabla ya muda aliotakiwa kufika katika ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Bulibuli ili kupata taarifa kuhusu matukio mbalimbali ya uhalifu yanayotokea kila siku.

Wakati waandishi wengine wa magazeti ya kila siku ama redio walikuwa wakituma kwa wahariri wao habari hizo kama zilivyo, yeye, kutokana na kuandikia gazeti litokalo kila wiki, alikuwa akichagua habari moja anayoona ina uzito zaidi, anaifanyia uchunguzi wa kina na kisha kuituma kwa mhariri wake makao makuu ya nchi, Bandaria.

Mara nyingi Walari alikuwa anaonekana kuwaudhi polisi kwa namna alivyokuwa akifuatilia tukio wakati mwingine zaidi ya polisi na anapoliandika kwa kina wao wanaonekana kama wazembe.

Mara kadhaa alishalalamikiwa au kutishwa na polisi kwamba anawavurugia ushahidi lakini akawashinda kwa hoja. Tatizo kubwa lilikuwa uwajibikaji duni wa watumishi wengi katika sekta ya umma.

"Tumeelekezwa kwa mwandishi wa habari anayeitwa Walari Saire. Sijui ndiye wewe?" Aliuliza yule mwenye umri mkubwa.

"Ndiyo mimi, karibuni sana. Mnasemaje?"

"Bwana Mwandishi, sisi tumekuja kukuona kama mnaweza kutoa taarifa hizi kwenye vyombo vya habari, pengine itasaidia umma kuelewa matatizo wanayoyapata wenzetu wanaofungwa katika Gereza Kuu la Magamaga, hapa Bulibuli," akaanza yule mtu.

Akaendelea: "Samahani, nilisahau kwanza kujitambulisha. Mimi naitwa Ibrahim Kamba, mkazi wa kijiji cha Magoze (kilichopo nje ya mji) na huyu ni kijana wa pale kijijini, anaitwa Semba."

Yule mtu akapitisha ulimi kwenye midomo yake mikavu kisha akaendelea: "Watu wanakufa hovyo katika Gereza la Magamaga. Kuna milipuko mingi ya magonjwa. Hakuna dawa na watu wanafanywa kama wanyama. Wafungwa wamejaa sana kuliko uwezo wa vyumba hadi kulala ni taabu sana. Hivi ninavyoongea nimeshazika mwanangu mmoja na mwingine yuko chumba cha maiti, tutamzika leo.

“Walikamatwa na huyu mwenzao niliye naye hapa kwa tuhuma za wizi wa nyavu za kuvulia samaki, kosa ambalo hawakufanya kabisa. Lakini hao wenzake wamekufa wakiwa katika hili gereza kutokana na magonjwa ambayo yanaweza kutibika."

Kamba akanyamaza kidogo tena, akaendelea: “Mmoja kafariki dunia kutokana na malaria tu baada ya kukosa tiba kwa muda mrefu. Huyu ambaye tunakwenda kumchukua chumba cha maiti sasa hivi, kafa kwa kuhara damu. Naye, kama mwenziye, hakupata tiba," akasema Kamba.

Kabla Walari hajahoji kitu, Kamba akaongeza kwamba watu wanakufa kila mara gerezani lakini anashangaa waandishi hawafichui hali hiyo ili umma ujue na pengine wakubwa huko makao makuu ya nchi wakachukua hatua ili kuokoa maisha ya wananchi.

"Nasikia huko mfungwa anapokufa, askari wa gereza wanashangilia kwamba afadhali amepunguza msongamano. Huyu kijana aliyekuwa huko atakueleza zaidi. Nasikia kutokana na wafungwa kulawitiana bila kizuizi utadhani wameruhusiwa, Ukimwi nao unaua wengi huko," alimaliza kusema Kamba akimgeukia kijana aliyekuwa ameandamana naye.

"Kwa kweli, braza, hali ni mbaya sana," akaanza yule kijana aliyetambuliwa kwa jina la Semba.

"Mimi nimetoka gerezani juzi tu. Nilikuwa rumande kwa miezi sita kwa tuhuma za wizi wa nyavu za kuvulia samaki. Nimeachiwa baada ya mtu aliyekuwa akitushitaki kutofika mahakamani kila kesi inapotajwa. Kama alivyosema mzee hapa, wenzangu wawili, mtoto na mpwa wa huyu mzee wamekufa huko gerezani. Mwenzangu mwingine, kwa sababu tulikuwa wanne, yuko hoi hospitali. Tulimpeleka baada ya kutoka gerezani. Naye ana hali mbaya. Anahara damu. Amini usiamini kama wiki hii tungeendelea kuwa gerezani naye angekufa."

Akakohoa kidogo yule kijana ambaye afya yake ilikuwa inaonekana mbaya vilevile, akaendelea: "Huwezi kuamini, mule gerezani wastani wa mfungwa mmoja anakufa kila siku. Lile ni gereza la kifo. Angalia mimi mwenyewe nilivyo. Nimeota mapele na ukurutu mwili mzima hadi yamekuwa madonda. Nikikuonyesha sehemu zangu za siri namna nilivyooza utakimbia. Maji ni ya shida na matandiko ni machafu sana. Lishe ya huko usiseme, mawese yanamwagwa tu kwenye maharage, wala hayaivi. Ugali mchungu kama mwarubaini, kitoweo ni sawa na kula wadudu waliochanganywa na maharage. Natamani ungekuwa na uwezo wa kwenda huko na kujionea mwenyewe jinsi hali inavyotisha."

Kijana huyo pia alisema kwamba ukiacha mahabusu, wafungwa wamekuwa wakienda kufanya kazi sehemu za hatari kwa maslahi ya wakubwa hapo gerezani ambako pia wao huambulia labda chakula cha maana kidogo, tena baada ya kupigwa sana mijeledi. Akasema mfungwa wa Gereza la Magamaga hawezi hata siku moja akaamini kuwa gereza lile liko katika nchi huru.

itaendelea...
 
Back
Top Bottom