JOTO LA MOTO
JF-Expert Member
- Apr 11, 2018
- 758
- 555
TITLE: RIPOTI YA MKAGUZI.
SEHEMU YA KWANZA.
NDANI-OFISI YA MZEE WOTA.
Mzee Wota, Bwana wa miaka 60 hivi, ameketi akiwa makini akisoma kilichopo kwenye Lap top, huku akibofya keyboard ya Lap top ile.
Mlango unagongwa, “ingia” anasema Mzee Wota huku bado akiwa amekazia macho kwenye Laptop yake.Mlango unafunguka anaingia Paul Siza, kijana mtanashati, miaka kama 35 hivi, akiwa amevalia nadhifu, anaingia na kusimama mbele ya meza ya Mzee Wota, Mzee Wota anainua kichwa kumuangalia Paul, “shikamoo Mzee” anasema Paul, “vipi mbona leo asubuhi asubuhi?” anauliza Mzee Wota, Paul anabaki kimya kwa sekunde kadhaa kisha anashusha pumzi, “Mzee kwa nini usirekebishe tu hiyo ripoti?”, anasema Paul, Mzee Wota anabaki anamuangalia Paul, “walau huu upepo upite” anaongeza Paul, Mzee wota anatoa miwani, “ndio kilichokuleta kwangu asubuhi hii Paul?” anauliza Mzee Wota kwa sauti ya chini, “Kijana huu ukaribu wetu usikufanye utake kunielekeza cha kufanya” anasema Mzee Wota huku amemkazia Paul macho,zinapita sekunde chache, Mzee Wota anavaa miwani na kurudi kuendelea kutumia lap top yake, Paul anabaki amesimama. Zinapita sekunde kadhaa, Mzee Wota anaacha anachofanya, anaifunga Lap top na kuiweka kwenye begi lililokuwa pembeni, anavua miwani na kuiweka kwenye mfuko wa koti, kisha anainuka anachukua lile begi na kuelekea mlangoni, kabla ya kuufungua mlango anageuka na kumuangalia Paul, “kijana ..mimi huwa sirudi nyuma” anasema Mzee Wota, “kawaambie waliokutuma kwangu kuwa hii ripoti itasomwa kama ilivyo..haitabadilishwa hata nukta” anaongeza Mzee Wota kisha anageuka na kufungua mlango na kutoka. Paul anabaki amesimama kwa muda kisha anatoa simu yake mfukoni na kuibofa mara kadhaa huku akielekea mlangoni na kutoka.
NJE-KWENYE PARKING-MCHANA.
Paul anaelekea ilipo Gari aina ya Rav 4 nyeupe, huku akiwa na simu sikioni, “naona Mzee bado ameshikilia msimamo wake” anasema Paul, “basi..wewe umeshamaliza kazi yako Siza..tuachie fanya mambo mengine” inasema sauti ya kwenye simu, “kupanga ni kuchagua..naona Mzee ameshachagua” inaongeza sauti ile ya kwenye simu, “lakini Enok...” anasema Paul na mara unasikika mlio wa kuashiria simu imekatika, Paul anaitoa simu sikioni, anafungua mlango wa gari, anaingia na kuondoa gari.
NJE-BARABARANI-MCHANA.
Gari aina ya Toyota Landcruiser V8 nyeupe ikiwa mwendo wa wastani inakatiza barabara ya uhuru kuelekea mtaa wa Jitegemee.Ndani ya Gari yupo Mzee Wota,na pembeni yupo Ben, kijana wa miaka 31 hivi akiwa kwenye usukani anaendesha. Wanaenda kwa muda huku wote wakiwa kimya kila mmoja akitafakari ya kwake, huku kwa mbali ikisikika sauti ya matangazo kutoka kwenye redio ya gari lile.“Mzee mimi naona kadri siku zinavyoenda na hii kazi inakuwa na mitihani” anasema Ben na kumfanya Mzee Wota ashtuke na kugeuka kumuangalia, “wamekufuata tena?” anauliza Mzee Wota, Ben anashusha pumzi “bado wananisumbua” anasema Ben, “wewe waambie kila wanachotaka kusikia..mimi sina shida Ben” anasema Mzee Wota, "usiingie matatizoni kwa ajili yangu" anaongeza Mzee Wota, “tatizo hawaniamini..wanaona kama kuna ninachowaficha” anasema Ben huku akinyonga usukani kuingia kwenye parking ya jengo moja la ghorofa mbili lililopo upande wa kushoto wa barabara, gari linafika parking na kusimama.
NJE-KWENYE PARKING YA JENGO-MCHANA.
Mita kadhaa pembeni kutoka liliposimama gari la Mzee Wota ipo Noah nyeupe yenye vioo vya giza (tinted). Mzee Wota anateremka na kisha anafungua mlango wa abiria na kubeba begi lake la Laptop, anageuka na kukutana uso kwa uso na Ziba, Bwana wa miraba minne, akiwa amevalia miwani nyeusi, “tuna shida na wewe Mzee” anatamka Ziba huku bastola ikiwa mkononi kwake, “hii ni nini tena?” anauliza Mzee Wota kwa mshtuko na mshangao huku anaangalia pembeni na kuwaona Enok na Kabwe, nao wakiwa wamevalia miwani nyeusi, “gari ile pale inakusubiri” anasema Ziba huku akielekeza kwa bastola ilipo ile Noah nyeupe.
Wakati huohuo Kabwe anafika upande ule alipo Ben “shuka chini” anaamrisha Kabwe,Ben anateremka, “twende” Kabwe anamuamrisha Ben kisha wote wanaongozana kuelekea ilipo Noah ile na kuingia.
NDANI-CHUMBA NAMBA 1-MCHANA.
Ben yupo kwenye kiti, Kabwe ameketi mita kadhaa mbele yake akiwa amekunja nne na sigara mdomoni, “nadhani tulikuelekeza wapi upeleke Gari?” anasema Kabwe, “siwezi kumsaliti Mzee Wota..yule ni kama Baba yangu” anasema Ben, “unajaribu kuwa shujaa sio?” anasema Kabwe kwa sauti ya kebehi, Ben anabaki kimya, Kabwe anapiga pafu ya sigara, “umefanya uchaguzi mmbaya sana dogo” anasema Kabwe na kupiga tena pafu moja ya sigara na kisha anakunjua miguu yake na kuketi kwa kuinamia mbele,“na vipi kuhusu hiyo nywila?” anauliza Kabwe kwa sauti ya chini na ya upole, “ukweli utakuweka huru” anaongeza Kabwe, Ben anashusha pumzi,
“hiyo ni siri yake mimi siifahamu” anasema Ben, Kabwe anashusha pumzi, anainuka na kutoa simu yake mfukoni na kuibofya, anaiweka sikioni, “itabidi twende kwenye plani B..mtafuteni Sele” anasema Kabwe na kisha anaitoa simu sikioni.
NDANI-CHUMBA NAMBA 2-MCHANA BAADAE.
Sele, Bwana wa makamo, yupo na Laptop ya Mzee Wota akibofyabofya, Mzee Wota ameketi kwenye kiti pembeni, nyuma yake amesimama Mbupu, bwana wa miraba minne akiwa ameshikilia SMG jirani na kichwa cha Mzee Wota, Enok amesimama mita chache kutoka pale, akiwa na simu sikioni, akionekana yupo makini kusikiliza simu ile, “ndio tupo hapa na mtaalamu wa mifumo tunaweka mambo sawa boss”, anasema Enok, zinapita sekunde kadhaa,“Sawa Boss nimekuelewa”, anasema Enok na kuitoa simu sikioni na kuja walipo wengine na kuketi juu ya meza anayoitumia Sele, “hivi haya yote ni kwa faida ya nani?” anauliza Mzee Wota na kumfanya Enok kugeuka na kumuangalia Mzee Wota kwa jicho korofi, “mnapoteza muda ..ipo siku ukweli wote utajulikana tu” anaongeza Mzee Wota huku bado Enok akimuangalia, kinapita kimya kifupi huku Sele akiendelea kubofya ile Laptop,“mimi naombeni nikajisaidie” anasema Mzee Wota na kukatisha ukimya ule, Enok anaangalia pembeni na kuchukua chupa kubwa tupu ya maji juu ya meza na kumrushia Mzee Wota, Mzee Wota bila kujigusa anaiacha chupa ile ikimgonga na kuanguka chini, kisha anashusha pumzi na kumuangalia Enok “walau uniheshimu kwa umri wangu basi” anasema Mzee Wota. Kimya kinaendelea huku Sele akiendelea kubofya ile Laptop.
NDANI-OFISI YA BOSS-SAA TATU USIKU.
Mzee Bosi, Mzee wa miaka 70 hivi, amesimama pembeni ya meza yake, mkononi ana glasi yenye pombe kali,Enok amesimama pembeni akiwa ameweka mikono nyuma mithili ya Mtu mtiifu sana kwa mkubwa wake, Mzee Bosi ameinamisha kichwa kama mtu anayefikiria jambo, “mmeachana nae saa ngapi?” anasema Mzee Bosi, “jioni hii..saa kumi na mbili” anasema Enok, wanabaki kimya kwa sekunde kadhaa.
“mmefanya maamuzi ya kipumbavu sana” anasema Mzee Bosi kwa sauti ya chini huku bado ameinamisha kichwa chake, “tulisubiri maelekezo yako boss” anasema Enok, “tumia akili Enok” anasema Mzee Bosi kwa ukali huku anainua kichwa kumuangalia Enok, “tutasahihisha Boss” anasema Enok,
“lini?” anauliza Mzee Bosi kwa ukali, “ndani ya saa 24” anasema Enok na kutulia, kunapita ukimya kwa sekunde kadhaa, “ondoka” anasema Mzee Bosi na kumshtua Enok, “sawa bosi” anasema Enok huku kwa haraka anageuka na kuondoka.
NDANI-NYUMBANI KWA PAUL-CHUMBANI-USIKU WA MANANE.
Miri, mwanamke wa miaka kama 30 hivi, amelala kitandani fofofo na mara anashtushwa na mguso wa kitu na kufungua macho, anainua kichwa kuangalia pembeni yake, “D” anaita Miri kwa sauti yenye mshtuko na uoga, anakuja Paul huku akiwa anavaa Sweta, “mambo yameshaharibika kule kwa Mzee Wota” anasema Paul huku akiwa anaketi na kuvaa viatu vyake vya michezo (raba), “Mungu wangu” anasema Miri kwa mshtuko, “kwa hiyo unaenda huko?” anauliza Miri, Paul bila kumjibu anainuka na kuelekea mlangoni, “nisubiri usiniache” anasema Miri huku kwa haraka akitoka pale kitandani.
....itaendelea...