Riwaya: Fedha au Risasi

25phiri12

Senior Member
Joined
Jun 19, 2021
Posts
120
Reaction score
93
RIWAYA: Fedha Au Risasi
MTUNZI: Emmanuel Phiri
NAMBA: 0758 195 890

SEHEMU YA 01

Aliamshwa toka usingizini kwa teke kali la mbavuni, akakagumia kwa maumivu makali yaliyosambaa mwili mzima kama siafu ashambuliavyo kitoweo chake. Sauti kali ya kukwaruza ililiteka anga, sauti yake ya asili ilikuwa mbali na yeye baada ya kuipoteza kwa kilio kilichokuwa kikimwandama mara kwa mara ndani ya chumba hicho cha mahabusu. Alijikunja haraka kama nyoka akidhani atapunguza ukali wa maumivu aliyokuwa akipitia lakini ilikuwa sawa na kuchukua maji ndani ya nyumba ya makazi na kuyamwaga bahari ya Hindi. Hakupata nafuu yoyote. Mpigaji hakujali hali yake, alimwagia maji ya baridi huku akiendelea kumshambulia kwa mateke, maneno ya kashfa na matusi yaliyotaja viungo vya mwili wa binadamu, hasa mwanamke.

Mpigaji hakujali alikuwa akimtesa msichana mdogo mwenye umri chini ya miaka kumi na nane. Siyo kwamba hakujua hilo, hapana, bali alikuwa akitekeleza kauli ya mkuu wake wa kazi. Hakuishia hapo, alimshika miguu binti yule akaanza kumburuza sakafuni kama kiroba cha chumvi. Hakujali binti yule alivyokuwa akilalamika kwa maumivu aliyokuwa akipitia. Kwakuwa ulikuwa usiku wa manane wenye giza totoro, binti yule hakufanikiwa kumuona mpigaji bali alitambua uwepo wake kutokana na kipigo alichokuwa akipitia. Mpigaji alimuona binti yule vizuri kwa sababu alikuwa na tochi lenye mwanga mkali uliozidisha mateso kwa mpigwaji.

Binti alibamizwa ukutani, akapasuka usoni, akaongeza idadi ya vidonda mwilini. Madonda yaliyokuwa yameacha kuvuja damu yakaanza kumwaga damu kama awali. Aliendelea kulia kama mtoto mdogo lakini hakuna msaada wowote uliopatikana. Alikuwa mwana kondoo mbele ya simba mwenye njaa. Japokuwa sauti ya kilio chake ilipaa angani na kusambaa eneo kubwa la jengo la polisi lakini hakuna aliyefika angalau kutazama nini kilichokuwa kikiendelea. Binti yule alizidi kujihakikishia kuwa, mateso yake yalikuwa ni mpango wa uongozi wa mkoa wake na baadhi ya viongozi wa juu serikali. Alimsikia mpigaji akimfokea kwa kusema

“Lazima ufie gerezani kahaba wewe, huwezi kumuua ofisa wa polisi alafu ufumbiwe maji”

Yalikuwa ni baadhi ya maneno yaliyomtoka mpigaji. Mpigaji alimpiga binti yule mpaka akachoka, jasho lilimtiririka mithili ya mtu aliyetoka kucheza mpira wa miguu. Alitoka ndani ya chumba cha mahabusu, akafunga vizuri kwa kufuri nzito la chuma kisha akatokomea kusikojulikana. Binti akaendelea kulia kama sehemu ya kuomboleza maumivu. Akajikusanya taratibu na kuelekea kwenye moja ya kona ya chumba kile akajikunyata kama kifaranga kilichokosa mama. Kichwani aliendelea kujiuliza kwanini hapelekwi mahakamani kusomewa shitaka lake?, hakupata jawabu kamili.

Ulikuwa usiku wa siku ya tano tangu aingizwe ndani ya chumba hicho cha mahabusu. Chumba kichafu kilichotapakaa damu kila kona. Harufu za kinyesi na mikojo vilikuwa ndiyo mahala pake. Chumba hicho kilichobanduka sakafu na kuacha mawe nje yakisalimia na kuwatesa watuhumiwa kilikuwa kimening`inizwa minyororo toka darini, minyororo iliyotumika kuwafunga watuhumiwa wa makosa mbalimbali. Kwenye kona moja ya chumba hicho kulikuwa na kiti cha chuma kilichounganishwa na mfumo wa umeme, kiti hicho kilitumika kuwaadhibu wahalifu hasa waliogoma kutoa ushirikiano. Hakika kwa namna chumba kile kilivyokuwa hakikustahili kuwa chumba cha mahabusu bali chumba cha mateso, tena mateso ya magaidi au wahaini wa taifa lao.

Hata hivyo, chumba hicho kilikuwa cha siri na mara nyingi mhalifu aliteswa usiku ili kuondoa uwezekano wa watu wengine kubaini usiri huo. Mahabusu wa vyumba vya jirani walitambua uwepo wa chumba hicho kwa sababu walisikia kila kilichokuwa kikiendelea. Siri ilikuwa wa raia wa nje. Kilikuwa chumba cha mwisho kabisa kati ya vyumba vya mahabusu. Kwa nje kilionekana kama chumba kisichokuwa na matumizi yoyote. Hata sauti ya mateso ikipaa ilikuwa vigumu sana kufikia makazi ya raia kwa sababu kituo hicho cha polisi kilikuwa mbali na kilikuwa na sheria nyingi na ngumu kuruhusu raia kukisogelea. Kilikuwa kituo kilichoogopwa sana mkoani Rwama Mwanzo. Na kilikuwa ni moja ya kituo kilichokuwa na sifa mbaya sana nchini Malosha, lakini hakuna kiongozi aliyekemea suala hilo. Kiliendelea kutoa huduma za mateso kila siku. Hata wale watuhumiwa waliokuwa vyumba vya jirani waliporuhusiwa na kwenda uraiani walisema kuhusu uwepo wa chumba hicho cha mateso lakini hakuna aliyejali.

Machozi yakaendelea kutengeneza mifereji katika mashavu ya binti yule baada ya kukumbuka namna alivyoshuhudia kifo cha baba yake, siku hiyo hiyo ndiyo alikamatwa na kuswekwa mahabusu na kuanza kuteswa kama gaidi aliyekamatwa ikulu. Siku ya kukamatwa kwake alishuhudia namna vijana watatu waliovaa kiraia wakiwa wamefunika sura zao kwa soksi usoni wakimuonesha baba yake kitu kupitia simu iliyokuwa imeshika na kijana aliyekuwa katikati. Hakuweza kubaini ni kitu gani. Kati ya vijana wale watatu, mmoja alikuwa ameshika begi lililokuwa zimefunguliwa zipu na kuonesha kiasi kikubwa cha fedha (dollars). Mwingine alikuwa na bastola ndoto aina ya Beretta 92 akiizungusha kidoleni kwake kama mchezo wa watoto. Wa tatu alikuwa katikati yao na ndiye aliyekuwa mzungumzaji mkuu aliyekuwa akishurutisha jambo kwa ukali sana.

Baba yake alikuwa amepiga magoti akiomba kuachwa huru lakini hakuna aliyemsikiliza. Kipindi hicho binti yake alikuwa nyuma ya mlango akichungulia kupitia tundu la kupitishia funguo. Vijana wale watatu waliona ugumu wa mzee yule kutekeleza hitaji lao. Kijana aliyekuwa katikati ya mwenzake, alianza kutembea kushoto kisha kulia. Akainua kichwa na kukishusha chini. Alikuwa akitafakari kitu cha kufanya. Akafanikiwa kupata jawabu, akarudi mbele ya mzee yule kisha akaongea kwa sauti ya juu

“Plata o Plomo”

Kauli ya kijana yule ilimaanisha kuwa mzee achague kuchukua fedha na kutekeleza hitaji lao kisha aachwe huru au apigwe risasi baada ya kugoma kutimiza matakwa yao. Hakika ilikuwa ni ‘Plata o Plomo’. Kauli ilikuwa tata mbele ya mzee, hakuielewa hata kidogo. Vijana wale walielewa kuwa mzee hakuwaelewa walichomaanisha baada ya kusikia sentensi ile yenye maneno ya asili ya America. Kijana mzungumzaji alifafanua maana ya maneno yake. Akaeleweka kwa asilimia mia, lakini mzee hakuwa tayari kuwa msaliti. Aliongea kwa sauti ya juu kama alivyoulizwa

“Sijawahi kuwa msaliti. Sipo tayari kutimiza upuuzi wenu”

Majibu yake yaliwakera sana watekaji. Kijana aliyekuwa mzungumzaji akampa amri kijana mwenye bastola mkononi afanye kazi ya kuondoa uhai wa mzee. Hazikupita hata sekunde tano, binti aliyekuwa akichungulia mkasa wa baba yake alishuhudia baba yake akiwa marehemu baada ya kupigwa risasi ya kichwa. Bastola iliyotumika kufanya mauaji haikutoa sauti yoyote, ilikuwa imefungwa kizuia sauti. Japokuwa bastola haikuwa sauti lakini binti yule alitoa sauti ya mshituko na hofu nyuma ya mlango. Sauti yake ilisafiri mpaka kwenye masikio ya vijana wale waliomuua baba yake. Wale vijana wakageuka haraka kuangalia sauti ilipotokea.

Kitendo kile kilimuongezea hofu binti yule aliyekuwa amevaa sare za shule na begi mgongoni lenye madaftari na vitabu. Alivua begi akalitupa chini kisha akaanza kutimua mbio kuelekea nje. Alifanikiwa kufika nje ya nyumba yao lakini kabla hajafanikiwa kutoka nje ya geti alisikia mngurumo wa gari nje ya mlango wa geti kisha kimya kikatawala ghafla. Alijua si jambo jema kwake, alihisi kuishiwa nguvu kwa sababu hakujua ni nani aliyesimamisha gari nje ya geti lao. Alihisi labda ni wahalifu wengine. Alipofikiria kurudi nyuma, mwili ukakataa. Akakumbuka namna alivyoshuhudia kifo cha baba yake. Akabaki amesimama kama mlingoti wa umeme huku akitetemeka na kuruhusu haja ndoto kushambulia nguo yake ya ndani.

Kipindi akitafakari jambo la kufanya alishuhudia mlango wa geti ukifunguliwa kisha wakaingia watu watatu wakiwa na silaha za moto mikononi. Hawakutofautiana hata kidogo na wale watu aliowashuhudia wakiondoa maisha ya baba yake kipenzi, nao walikuwa wameziba sura zao kwa soksi nyeusi usoni. Watu wale walipomuona binti yule walinyooshea silaha zao haraka na kumshurutisha kusimama pale pale alipokuwa. Binti yule aliweweseka kwa hofu, akili zikaenda kushoto kisha kulia. Akahisi akishindwa kuhimili mwili wake. Akaanguka chini kama gunia na kupoteza fahamu.

Alishitushwa na kelele za hapa na pale. Alipofumbua macho aligundua yupo sebuleni kwao, maiti ya baba yake ikiwa pembeni. Alizungusha macho na kuona idadi ya polisi sita, alipojaribu kuinuka akashindwa. Aligundua alikuwa amefungwa pingu mikononi. Alihamaki kwa hofu na kutoa kauli aliyoshindwa kuielewa hata yeye. Kauli yake ikayakifikia masikio ya polisi, wakageuka na kumtazama. Walikuwa na sura za hasira na visasi dhidi yake. Mmoja kati ya polisi wale aliongea kwa ukali

“Mtoto mdogo kama wewe unafanya ukatili huu! Sasa utaieleza mamlaka”

Binti yule alishangazwa na kauli ya polisi, alihisi kama alisikia vibaya lakini haikuwa hivyo. Alisikia kwa usahihi kabisa. Sauti ya polisi yule haikuwa ngeni kwake, alihisi ilifanana kabisa na sauti aliyoisikia muda mfupi uliopita. Sauti ya miongoni mwa watu waliomuua baba yake. Sauti iliyomwambia baba yake

“Plata o Plomo” (Pesa au Risasi)

Lakini aliona kitu cha tofauti, vijana waliomuua baba yake walikuwa wamevaa mavazi ya kiraia, vile vile mauaji yalifanyika chumbani kwa baba yake na siyo sebuleni alipokuwa muda huo. Akakumbuka mara ya mwisho alikuwa nje ya nyumba yao akitafuta njia ya kutoa getini kisha akawaona vijana wengine watatu wakiingia, baada ya hapo hakuna alichokumbuka. Alijitazama vizuri akagundua amevaa mavazi ya nyumbani tofauti na alivyokuwa awali na nguo za shule. Akili ikaenda mbali sana, akahisi labda yamepita masaa mengi baada ya kushuhudia kifo cha baba yake lakini alipotazama saa yake ya mkononi ikamuonesha imepita robo saa tangu ashuhudie kifo hicho. Alikumbuka alishuhudia watu watatu wakiondoa maisha ya baba yake kisha akashuhudia watu watatu wakiingia getini, na muda huo alikuwa mbele ya polisi sita. Idadi sawa ya watu aliowaona. Akabaki njia panda. Kichwa kigagoma kufikiria zaidi.

ITAENDELEA

Kitabu cha riwaya ya MATEKA kinapatikana, piga namba 0758 195 890 utumiwe mkoa wowote
 
RIWAYA: Fedha Au Risasi
MTUNZI: Emmanuel Phiri
NAMBA: 0758 195 890

SEHEMU: 02

Alijitazama vizuri akagundua amevaa mavazi ya nyumbani tofauti na alivyokuwa awali na nguo za shule. Akili ikaenda mbali sana, akahisi labda amepita masaa mengi lakini alipotazama saa yake ya mkononi ikamuonesha imepita robo saa tangu ashuhudie kifo cha baba yake. Alikumbuka walishuhudia watu watatu wakiondoa maisha ya baba yake kisha akashudia watu watatu wakiingia getini, na muda huo alikuwa mbele ya polisi sita. Akabaki njia panda. Kichwa kigagoma kufikiria.

ENDELEA

Askari polisi aliyemkaripia awali akachuchumaa, akawa uso kwa uso na binti yule, macho yake makali yaliyoathiriwa na pombe yakatazama sura ya binti kama mkaguzi. Akatabasamu kinafki kisha akampiga kibao cha nguvu. Binti akashindwa kuhimili nguvu iliyotumika na askari polisi yule. Alibamiza kichwa chini na kuvimba nundu katika paji lake la uso. Alitamani kuongea kwa lengo la kujitetea lakini askari polisi aliweka kidole chake mdomoni akimaanisha akae kimya. Binti alilia kwa kugugumia pasipo kutoa sauti yoyote. Misuli ilivimba kichwani, alikuwa akiona kama mauzauza katika maisha halisi.

Pembeni ya mwili wa baba yake aliona kisu kwenye damu kikiwa ndani ya mfuko maalumu wa kutunzia ushahidi wa mauaji. Hapo ndipo alipozidi kupata mashaka kwa sababu, yeye alishuhudia baba yake akiuliwa kwa kupigwa risasi na sio kuchomwa kisu. Kimetoka kwa wapi? Lilikuwa swali gumu sana lililomtatiza. Aliendelea kupepesa macho kutafuta unafuu wa maumivu aliyokuwa akipitia, kupepesa kwake hakukwepa bure. Alifanikiwa kuona mfuko mwingine uliotunza bastola ndani, ulifanana kabisa na mfuko uliotunza kisu chenye damu. Alijithibitishia moyoni kuwa bastola ile ndiyo iliyoondoa maisha ya baba yake kipenzi. Swali lilibaki kwenye kile kisu. Yule askari polisi alishika fulana ya yule binti kisha akamuinua juu kwa nguvu, hakujali kama anatengeneza maumivu makali. Yeye hakujali kabisa. Alimsukuma mbele huku akamwambia

“Ongoza njia muuaji mkubwa wewe? Huwezi ondoa maisha ya watu utakavyo wewe”

Kwa namna alivyosukumwa na mikononi alikuwa amefunga pingu, alishindwa kuhimili mwili wake. Aliyumba kushoto kisha kulia, akajitahidi kupambana na uzito wake lakini hakufanikiwa, akashindwa kabisa. Akajibamiza kwenye meza ndogo ya kioo iliyokuwa na maua juu yake. Ikapasuka. Alijikuta juu ya vipande vya vioo, vipande vile havikumuacha salama. Vilishambulia bega lake la kulia kwa sababu ndio upande alioangukia. Vilimchana sana, damu zikachafua fulana yake nyeupe. Wale askari polisi wenye chuki dhidi ya yule binti hawakujali chochote. Aliinuliwa juu juu pasipo kujali alivyoumia. Askari polisi wa pili aliyeonekana kuwa na sura ya upole alimkaripia

“Unajifanya mjanja kujiumiza mwenyewe ukitegemea ni njia sahihi ya kujiokoa! Songa mbele”

Kwa shida sana, yule binti akaanza kusonga mbele kama alivyoagizwa. Walifanikiwa kutoka ndani ya nyumba ile, lakini alishitushwa na kitu alichoona uwani. Aliona maiti ya kijana ikiwa pembeni ya geti lao. Kijana huyo aliyekuwa marehemu muda huo alikuwa amevaa sare za jeshi la polisi, kifuani alikuwa amechafuka kwa damu nyingi. Sasa, aliamini kumetokea mauaji ya watu wawili, yaani baba yake na huyo polisi pia. Alishangaa sana, akajikuta akisimama ghafla. Alisukumwa mbele na askari polisi pasipo kuongea chochote, akasonga mbele.

Mshangao wa binti yule ulikuwa wazi kabisa, kila mmoja aliuona lakini haukuwa na maana yoyote katika utashi wa wale askari polisi. Waliendelea kupiga hatua kuelekea getini, macho ya yule binti hayakuhama kwenye mwili wa askari polisi aliyekuwa maiti muda huo. Walifika getini, wakafungua geti na kufika nje. Binti alishangaa kumkuta mlinzi wao wa getini akiwa kwenye sura ya furaha na bashasha, tena akivuta sigara tofauti na kipindi chote cha nyuma walichofahamu hakuwa mtumiaji wa sigara wala kilevi chochote. Sasa aliamini mlinzi huyo alikuwa ni sehemu mojawapo ya kuratibu matukio yaliyokuwa yakiendelea. Mlinzi yule aliwapa ishara wale askari polisi kuwa waondoke haraka eneo lile. Askari polisi wakatii, wakazama ndani ya gari aina ya Toyota Noa lenye vioo vyeusi lililokuwa jirani ya mlango wa geti kisha safari ikaanza.

Hali ya pale nje ilikuwa shwari kabisa, hakuna jirani hata mmoja aliyefahamu kilichotokea katika nyumba ile. Njiani, safari yao iliandamwa na ukimya mkubwa, lakini ukimya ule ulikuwa kwenye sura ya nchi na siyo moyoni mwa binti yule, aliifikiria ile maiti kisha akakumbuka kisu chenye damu, sura ya mlinzi wao mcheshi ikamjia akilini. Akachanganyikiwa. Sasa alijihakikishia kile kisu ndicho kilichoondoa maisha ya askari polisi yule. Alibaki na maswali mengi kichwani

“Kwanini polisi wamuuwe polisi mwenzao? Kwanini wameondoka na kutelekeza maiti zote pamoja na kisu na bastola ambavyo vingetumika kama ushahidi?”

Hakupata jawabu lolote, bali alipata walakini kuwa wale yawezekana wakawa sio askari polisi bali wauaji waliotekeleza mauaji wakiwa wamevaa mavazi ya jeshi la polisi. Kipindi wakiendelea na safari mara ghafla gari lao liligongwa kwa nguvu kutokea nyuma. Binti alishituka sana kwa kuhofia ajali lakini polisi walitabasamu. Likagongwa tena kwa nguvu zaidi ya mara ya kwanza, mataa ya nyuma ya gari lile yakapasuka vibaya lakini bado askari polisi waliendelea kuchekelea. Vurugu zote hizo zilifanyika katika barabara ya vumbi isiyokuwa na magari mengi, hivyo kipindi matukio hayo yakiendelea hakuna shahidi wa pembeni aliyeona.

Gari lililowabeba askari polisi na yule binti likasimama kisha lile gari la nyuma lililokuwa likiwagonga nalo likasimama. Wakashuka vijana wawili wakiwa na soksi usoni, wakasogea mpaka lilipokuwa gari la polisi. Wakagonga mlango upande wa dereva, askari polisi waliokuwa na binti ndani ya gari wakafungua milango ya gari kwa umakini sana baada ya kuamini hakuna watu wengine wanaowaona tofauti na vijana wenye soksi usoni. Wakashuka wakiwa wamemshika yule binti na kumpakia kwenye gari la nyuma walilokuwa wamepanda vijana wenye soksi usoni. Lilikuwa gari maalumu la jeshi la polisi lenye mataa ya ving`ora juu yake. Ndani ya gari lile kulikuwa na vijana wawili waliofungwa pingu moja wote wawili, sura zao zilikuwa zimechakaa sana kwa kipigo. Vijana wale waliofungwa pingu moja walikuwa wamevaa mavazi yaliyofana na vijana waliovaa soksi usoni. Askari polisi wakapanda lile gari na kuwaacha vijana wenye soksi usoni wakipanda gari lao aina ya Toyota lenye vioo vyeusi.

Vijana wale wawili wenye soksi usoni wakawasha gari na kuondoka kwa mwendo kasi wakawaacha askari polisi, binti na wale vijana wawili waliochafuka sura kwa kipigo (waliovaa nguo kama zao). Askari polisi walipojihakikishia kuwa gari la wale vijana mwenye soksi usoni lipo umbali wa kilometa kadhaa kutoka walipokuwa wakaanza kulishambulia kwa risasi, wale vijana wakajibu mapigo. Kilikuwa kitendo cha kushangaza sana kwa yule binti, yaani wamebadilishana magari kwa amani na kuwaachia wale vijana wawili waliochoka kwa kipigo kisha wanashambuliana? Kwanini tena?

Polisi wakaanza kulifukuza lile gari kwa mwendo kasi, kwakuwa lile gari lilikuwa mbali na ilikuwa sehemu ya mpango wao hawakuweza kulifikia. Lilitokomea katika njia zenye vichochoro vya kutosha. Askari polisi walikuta lile gari limetelekezwa sehemu huku likiwa limezungukwa na raia wengi. Askari polisi wawili walishuka na kuongea na raia, wengine walibaki ndani wakiwa na binti pamoja na wale vijana wawili. Raia hawakufanikiwa kuziona sura za waliobaki ndani ya gari. Raia wale walisisitiza kuwaona vijana wawili wenye soksi usoni na silaha za moto mikononi wakitokomea mtaani. Walisema waliogopa kuwasogelea kwa kuhofia kifo.

Askari polisi waliwaeleza raia kuwa wao ndio walikuwa wakiwakimbiza majambazi hao na kufanikiwa kuligonga gari lao mpaka wakaliathiri mataa ya nyuma lakini kwa bahati mbaya majambazi wakafanikiwa kuwaponyoka. Kipindi polisi akiendelea kuomba ushirikiano kwa raia endapo wakifanikiwa kuwaona wale majambazi ghafla simu ya mkononi ya askari polisi aliyekuwa akiongea ikaanza kuita kwa fujo, akaichomoa kutoka mfukoni na kupokea haraka. Akahamaki kwa jazba mbele ya raia baada ya kusikia kauli ya aliyempigia

“Unasema kuna uvamizi unaendelea kwa Logan King?”

Akasikilizia sekunde kadhaa kusikia kauli ya aliyempigia. Alipohakikisha alichoambiwa alirudisha simu mfukoni kisha akamwamuru askari polisi mwenzake warudi ndani ya gari na kugeuza haraka kuelekea ilipo nyumba ya Logan King. Nyumba ya Logan King haikuwa mbali na eneo hilo, na kwakuwa Logan King alikuwa maarufu sana kila raia aliyekuwa mahali pale alishikwa na mshituko mkubwa. Gari lilipiga breki mbele ya nyumba ya Logan King, geti likafunguliwa haraka kisha gari likaingia ndani ya geti. Geti likafungwa tena. Polisi wakashuka kisha wakawaamuru vijana wenye pingu mkononi na yule binti washuke pia.

Binti alishangaa kurudishwa nyumbani kwao, alipotupa macho kutazama sehemu anapokaaga mlinzi alimuona, lakini hakuwa sawa na jinsi alivyomuona awali. Muda huo alikuwa akivuja damu katika paji la uso wake, alikuwa maiti. Pembeni yake alikuwa amesimama kijana aliyevalia sare za jeshi la polisi, binti akajihakikishia kuwa huyo ndiye aliyefungua geti na ndiye aliyemuuwa mlinzi wao. Kwanini lakini? Hakupata jawabu. Alipotazama mahali ilipokuwa maiti ya askari polisi aliyoiona awali kipindi wakitoka, hakuiona maiti ile, wala michirizi ya damu iliyokuwepo awali haikuwepo kabisa. Binti alihisi akiota ndoto angali ni mchana na yu macho angavu, au ni mazingaombwe. Hakupata jawabu.

Hofu ikazidi kutanda moyoni kwa binti yule. Hakupata wasaa wa kuendelea kushangaa. Yeye pamoja na wale vijana walihimizwa kuingia ndani ya nyumba yao. Walipofika sebuleni, binti alikuta maiti ya baba yake ikiwa imekalishwa kwenye kiti kama mtu aliye hai. Kilichodhihilisha kifo chake ni damu zilizosambaa mwilini kwake. Sakafuni akaiona maiti ya askari polisi aliyoiona awali nje ya nyumba yao. Alishangaa, kwanini imehamishiwa ndani na eneo ilipokuwa kusafishwa vizuri. Hakuelewa kwanini mazingira yalibadilishwa namna ile. Aligeuka na kuwatazama askari polisi waliokuwa nyumba yake. Walikuwa wakitabasamu, yule mwenye sura ya upole akasema

“Hatuwezi kufumbia macho mauaji uliyofanya”

Binti alizidi kuchanganyikiwa baada ya kusikia kauli ile. Japokuwa alikuwa mdogo lakini alielewa kuna mchezo mchafu unaendelea dhidi yake. Kipindi akiendelea kutafakari, alisikia kelele nyingi nje ya geti lao. Walikuwa raia wengi waliofika eneo lile kushuhudia nini kilichotokea. Simu aliyopigiwa askari polisi mbele yao ndio iliyosababisha wafike mahala pale kujihakikishia usalama wa mpendwa wao.

ITAENDELEA

Kitabu cha MATEKA kinapatikana nchi nzima, piga namba 0758 195 890
 
RIWAYA: Fedha Au Risasi
MTUNZI: Emmanuel Phiri
NAMBA: 0758 195 890

SEHEMU: 03

Japokuwa alikuwa mdogo lakini alielewa kuna mchezo mchafu unaendelea dhidi yake. Kipindi akiendelea kutafakari, alisikia kelele nyingi nje ya geti lao. Walikuwa raia wengi waliofika eneo lile kushuhudia nini kilichotokea. Simu aliyopigiwa askari polisi mbele yao ndio iliyosababisha wafike mahala pale kujihakikishia usalama wa mpendwa wao.

ENDELEA

Askari polisi hawakujali kelele za raia waliokuwa nje ya geti, waliamini hakuna raia hata mmoja atakayeruhusiwa kuingia ndani kwa sababu getini kulikuwa na askari polisi aliyedhibiti jambo hilo. Kila sekunde zilivyozidi kusogea ndivyo kelele za umati wa raia zilivyoongezeka. Kitendo kile hakikuwa salama kwa afya ya mpango uliokuwa ukisukwa, raia wangeweza kuharibu kila kitu. Kelele za raia hazikukata kwa sababu walipata hofu ya usalama wa Logan King, waliamini lazima atakuwa hatarini kwa sababu muda huo walikuwa wakiiona maiti ya mlinzi wake wa getini ndani kidogo ya geti.

Walimshurutisha askari polisi aliyekuwa getini kuwapa taarifa ya kinachoendelea ndani, na kama mpendwa wao yupo salama au kuna jambo baya limempata. Askari polisi hakutoa ushirikiano walioutaka, aliwasihi watulie mpaka wakati wa kujuzwa utakapofika. Japokuwa kelele ziliongezeka maradufu lakini walihofia kumvamia askari polisi kwa sababu alikuwa na silaha ya moto mkononi. Walilaani na kusema maneno mengi machafu yasiyostahili kusemwa hadharani. Askari polisi watatu kati ya wale sita waliokuwa ndani ya nyumba ya Logan King walitoka na kuelekea getini kwa lengo la kuongeza nguvu ya kuwasihi na kuwazuia raia kuingia ndani ya geti. Walikuwa na silaha za moto mikononi.

Japokuwa hawakuzitumiwa dhidi ya raia lakini ziliweza kuwasaidia kutengeneza hofu kwa raia. Walifika mbele ya raia na kuwajuza kuwa uchunguzi unaendelea na baada ya muda watapewa taarifa ya awali. Raia walitulia japokuwa kelele na minog`ono ya hapa na pale iliendelea. Baada ya robo saa, gari la watoa huduma za afya lilipiga breki jirani kabisa ya geti la nyumba hiyo. Wakashuka vijana wanne, watatu wanaume, wa mwisho mwanamke. Walikuwa wamebeba machela mbili. Waliongoza njia, raia wakawapisha na kuwaruhusu waingie. Hata askari polisi waliokuwa getini hawakutia neno, walisalimiama kwa ishara ya mikono kisha watoa huduma ya afya wakazama ndani ya jengo lile.

Raia walishangaa kwanini watoa huduma wale hawakuanza kuitazama maiti ya mlinzi iliyokuwa ndani ya geti. Ilisikika minong`ono ya raia wengine wakisema kuwa, watoa huduma hao waliamua kumpuuzia mlinzi kwa sababu alikuwa maiti muda huo, hivyo basi wakaamua kuingia ndani kutoa msaada wa kiafya kwa majeruhi. Yalibaki kuwa mawazo ya raia, hakuna aliyekuwa na uhakika. Baada ya dakika kadhaa watoa huduma za afya walitoka wakiwa wamebeba maiti kwenye machela walizoingia nazo. Wawili walibeba mwili mmoja, iliwahia vigumu lakini iliwapasa kufanya hivyo kutokana na uchache wao. Miili ile ilikuwa imefunikwa shuka kuanzia miguuni mpaka kichwani. Hakuna kilichoonekana. Waliongozana na askari polisi mmoja.

Macho ya raia hayakuisha kuwashangaa watoa huduma za afya kwa huzuni kubwa. Waliamini kati ya maiti zilizobebwa kwenye machela itakuwepo maiti ya mpendwa wao. Wenye roho nyepesi hasa wasichana na wanawake waliangua vilio visivyo kifani. Japokuwa vilio viliendelea lakini waliendelea kutafakari pia kuhusu maiti ya pili iliyobebwa. Atakuwa ni nani? Hakuna aliyejua. Swali hilo liliibuka kwa sababu ilikuwa imepita wiki moja tangu nyumba hiyo ya Logan King ibaki na watu watatu, yaani Logan King, mtoto wake wa kike na mlinzi wa getini. Hakuna aliyefikiria kama machela ya pili inaweza kuwa imebeba mtoto wa Logan King kwa sababu kwa namna machela zilivyokuwa zimejaa iliwapasa kuamini waliobebwa hawakuwa watoto wadogo bali watu wakubwa.

Baada ya miili ile kupakiwa kwenye gari maalumu la watoa huduma, watoa huduma za afya walishuka na kupakia mwili wa mlinzi uliotelekezwa awali. Kisha askari polisi wawili waliungana na wale watoa huduma za afya na kuondoka mahala pale. Iliaminika kuwa askari polisi wale walikuwa na kazi moja tu, kazi ya kuzichunguza maiti ili wabaini kama kuna alama za vidole vya wauaji au kama zina kitu chochote kinachoweza kusaidia katika upelelezi wao. Raia walilisindikiza gari lile mpaka likatoweka kwenye moja ya kona inayounga barabara ya mtaa wa pili.

Hazikupita hata dakika tano, walionekana askari polisi wawili wakitoka ndani ya nyumba ya Logan King wakiwa wameongozana na vijana wawili na binti wa Logan King. Kila mmoja alishangazwa na watu wale, hasa muonekano wa binti yule. Binti wa Logan King pamoja na wale vijana walikuwa wamefungwa pingu mikononi huku wakihimizwa kwa sauti kali kupiga hatua za haraka. Kila mmoja alishangaa kwanini binti yule aliyefiwa baba yake yupo kwenye hali ile. Kwanini yupo kwenye orodha ya watuhumiwa na mauaji? Mavazi ya vijana wale yaliwahukumu mbele ya raia, yalifanana kwa asilimia mia na majambazi waliotelekeza gari mtaa wa pili. Kila mmoja alifahamu walikuwa ni wale majambazi. Hakika mpango uliosukwa kuhusu vijana hao ulikamilika kwa asilimia zote.

Raia walianza kupiga kelele za kuwalaani wale vijana, vizazi vyao vilivyopita, vilivyopo na vijavyo. Kila mmoja aliamini vijana hao ndiyo waliomuua Logan King, mlinzi wake na mtu mwingine waliokuwa hawamfahamu (aliyebebwa kwenye machela). Hatua zilipigwa mpaka nje kwenye gari la polisi, wakapandishwa kisha polisi wote wakapanda. Safari ikaanza kwa mwendo wa wastani wakiwaacha raia wakiendelea kupiga kelele za kutokukubali wahalifu kuondolewa mahala pale pasipo kipigo kutoka kwao. Sio kwamba hawakuona namna vijana wale walivyokuwa wameharibika sura zao, hawakuridhishwa. Walitaka na wao wawasurubu ipasavyo. Walitaka kujichukulia sheria mikononi. Japokuwa walikuwa na shauku la kuwaadhibu wahalifu lakini hakuna raia hata mmoja aliyekuwa tayari kumgusa mtoto wa Logan King. Mtoto aliyekuwa kipenzi cha kila raia aliyemfahamu.
*****

Yalikuwa majira ya jioni, mwanga wa jua ukianza kumezwa na mawingu mazito yaliyotanda kila kona na kutengeneza mazingira ya giza. Watu waliokuwa kwenye mizunguko yao ya kujitafutia riziki walikuwa njiani wakirudi majumbani, lakini wenye shughuli za kuingia usiku walikuwa njiani kuelekea kazini. Miongoni wa watu waliokuwa njiani kurudi katika makazi yao walikuwepo wanafunzi wa shule ya sekondari iliyobeba jina la mkoa huo, shule iliyoitwa 'Rwama Mwanzo Secondary School'. Wanafunzi hao walikuwa wakitoka ziara (tour). Walikuwa wakirejea shuleni wakitoka kujifunza na kutalii mbuga ya wanyama maarufu mkoani humo, mbuga yenye vivutio vingi vya wanyama na uoto mwingine wa asili. Vicheko na furaha viliandama safari yao.

Hakuna aliyejua kama walikuwa kwenye mtego mbaya na hatari sana. mtego unaoweza kubadilisha historia ya maisha yao au maisha ya miongoni mwao. Mara kadhaa mwalimu wao aliyeambatana nao aliwasihi kupunguza kelele, walikaa kimya dakika kadhaa kisha wakajisahau na kuendelea kuongea kwa kelele kama awali. Walikuwa na furaha isiyo kifani. Gari lao lenye chapa ya shule lilishika barabara kuu ya lami ya kuelekea shuleni kwao, ulikuwa umebaki umbali wa kilomita kumi na moja kuwasili walipokuwa wakielekea. Bahati mbaya ikatokea.

Gari aina ya Toyota Noa liliwapita kwa mwendo kasi kisha likasimama ghafla mbele yao, sekunde tatu mbele vijana watatu waliovaa soksi usoni wakiwa na silaha za moto aina ya SMG walishuka na kusimama mbele ya gari la wanafunzi, silaha zao zilielekea usawa wa gari la wanafunzi. Hofu ilitanda kwa kila mmoja aliyekuwa kwenye gari lililobeba wanafunzi. Dereva akasimamisha gari haraka kama ishara ya kutii amri ya vijana wenye soksi usoni. Vijana wenye soksi usoni, kwa mwendo kasi pasipo kutia neno lolote walifungua gari la wanafunzi kisha wawili wakazama ndani, mmoja akabaki nje akilinda usalama wao. walioingia ndani ya gari walitoa amri ya kila mmoja kukaa kimya. Hakuna aliyebisha, walitimiza agizo waliloambiwa na watekaji. Kelele walizopaza baada ya mshituko wa kuvamiwa, na kelele walizokuwa wakipiga toka awali wakakatazwa na mwalimu wao lakini wakaendelea zilikata ghafla. Hakuna aliyekuwa tayari kufa. Wavamizi waliwakagua wanafunzi haraka haraka huku wakiwahimiza kila mmoja kuwatazama usoni japokuwa sura zao zilizibwa na soksi. Kuna mwanafunzi walikuwa wakimuhitaji. Walifanikiwa kumuona. Mvamizi mmoja alimnyooshea silaha ya moto kisha akamwambia kwa sauti ya hasira iliyojaa hasira

“Inuka haraka na unifuate”

Mwanafunzi aliyeelekezewa silaha ya moto alibabaika kwa hofu, alishindwa kuinuka mahala alipokuwa amekaa. Sio kwamba aligoma, la hasha, bali alichanganyikiwa kwa tukio lile. Kijana aliyetoa amri hakuwa na muda wa kuongea mara mbili. Alisogea mpaka alipokaa mwanafunzi yule kisha akampiga kitako cha bunduki kwa nguvu. Yule mwanafunzi akajibamiza kwenye gari kisha kiti alichoegemea. Akapoteza fahamu. Alibebwa juu juu kisha akapandishwa kwenye gari la watekaji, wakaondoka nae kwa mwendo.

ITAENDELEA

Hujasoma MATEKA tu. Piga namba 0758 195 890 kupata nakala yako
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…