RIWAYA; Chozi la Mdogo wangu

Layman1122

Member
Joined
Nov 11, 2026
Posts
5
Reaction score
3
CHOZI LA MDOGO WANGU
Na Layman Donsu

UTANGULIZI...

Ijapokuwa huzuni, kitakapopita kicheko.. Umasikini ukiweka kambi katioka malango yako.. Ama pepo la uatajiri likikupitia, iwe kwa ugumba ama kwa maradhi mshukuru yeye aliye juu, kwa maana yeye ndiye anajua kwanini ananakupitisha katika hayo..

Hakuna jambo linalokuja kwa akili zako mwenyewe usijikweze…


KARIBU TUUANZE MSIMU WA PILI.

Katika msimu uliopita ndani ya mkasa huu mzuri unaoitwa CHOZI LA MDOGO WANGU tuliweza kuona mambo yakiwa siyo mambo, baada ya wachawi waliomtokea Dorini utotoni kuhitaji kumfanya awazalie mtoto ambaye angekuja kuwafaa kwenye shughuli ambazo Dorini na ndugu yake Frank walikataa kabisa kuzitekeleza. Hatimaye mtoto aliyepangwa na wachawi hao kuzaliwa anazaliwa chini ya baba feki Dani mme wa ndoa wa Dorini.
Pia tuliweza kuona Mama wa kambo Lissa akipewa talaka na kuondoka huku akiwa na mtoto mchanga wa Mr Thomas. Ingawaje alisamehewa ila hatukufahamu maisha yake yatakuwaje, vipi kuhusu yule binti wa kizungu Enjo aliyeachwa na Frank kule Marekani atafika Tanzania kupigania penzi lake? na Je itakuwaje ikiwa atakuta Frank tayari ameshaoa mke wa Kiswahili?

SURA YA KWANZA

Dorini alipigwa na bumbuwazi kwa muda huku akijiuliza imekuwaje Emanueli awepo duniani
hadi leo mbona hafi na kwanini anazidi kumtafuta licha ya ukatili wote aliomfanyia utotoni?, Akazidi kujiuliza ni kwa nini shida za wazazi wake za tangu zamani bado zinamuandama yeye peke yake, akajiona hafai tena akatamani angepotea na kwenda sehemu ambayo hataonekana akiwa na mmewe ila haikuwezekana kabisa.


Wakati amezama kwenye lindi la mawazo akijiuliza nini afanye, mara ulivuma upepo mdogo kwenye gari lake, akabakia kujiuliza huo upepo umetokea wapi na wakati vioo vya gari lake amevifunga, hata kabla hajapata jibu mara nguvu zilimuishia akabakia kujiuliza ni nini kinachoendelea ila majibu hakuyapata kabisa, wakati anaendelea kuwaza na kujiuliza maswali mengi ghafla kilitokea kiumbe mfano wa mdoli mbele yake, kiumbe hicho au sasa tuseme tu mdoli huo ulikuwa unazungumza maneno ambayo hakuelewa ila mwishoni kabla ya huo mdoli kupotea ukabadili lugha na kuongea kwa maneno ya Kiswahili ambayo Dorini aliyaelewa vema, maneno hayo yalikuwa ni haya:-

"Tunashukuru sana maana umetutimizia haja ya mioyo yetu, tulitamani sana kukupata wewe ukakataa kujiunga nasi, mdogo wako naye akakataa ila damu yenu ndiyo tuliyokuwa tukiihitaji, maana mna damu ya dhahabu, sasa ni muda wa kumchukua mwanangu akisindikizwa na huyo ambaye utamzaa kesho saa saba na nusu mchana, yaani mtoto wa kweli wa Mr. Dani"

Dorini alihisi kuchanganyikiwa baada ya kuyasikia maneno yale, akagusa tumbo lake lililokuwa kubwa sana kwani alikuwemo mtoto ambaye amekwisha timiza miezi tisa na siku kadhaa, kwa wakati huo alikuwa kwenye matarajio ya kujifungua maana hakuifahamu siku na saa ya yeye kukileta hicho kiumbe duniani, akajiuliza kwa hiyo kumbe mtoto wake wa kwanza sio mbegu ya Dani? Aliikumbuka siku ile alipobakwa na kiongozi wa wachawi kisha baada ya kumbaka wakapotea na kumuachia uhuru hakujua maana ya kubakwa kwa wakati ule ila baada ya taarifa hii hapo akawa amefahamu kumbe walihitaji damu yake iungane na damu ya mkuu wa wachawi ili atokee mtoto. Hakutaka kuamini kuwa yule mtoto anaweza kuwa mtoto wa yule mchawi maana hakuona dalili za mimba mpaka alipokuja kulala kwa mara ya kwanza na mmewe wa ndoa. Habari za

Emanueli zikafutika kichwani kwake na kuanza kufuatilia kuhusu huyo mtoto wake wa kwanza aliyezaliwa katika mazingira ya kutatanisha na aliye mpatia jina la Wilbert.

Basi Dorini aliwasha gari lake na kuwahi nyumbani haraka, alichukua unywele wa Dani bila Dani kujua na kuchukua na unywele wa mtoto wake kisha akamfuata baba yake mlezi yaani Dokta Temba, alipofika kwa Dokta Temba alimueleza yote yaliyomkuta siku hiyo na kumueleza lile tukio la kubakwa ila akasahau kueleza kama pia kakutana na barua ya Emanueli. Dokta Temba alichukua vinasaba hivyo kisha akaenda navyo kwa ajili ya vipimo zaidi, baada dakika kadhaa majibu yakaletwa.

Dorini alimuangalia sana Dokta Temba akiwa na shauku sana ya kufahamu kilichojiri baada ya kipimo hicho cha D.N.A kufanyika. Kwanza dokta Temba alisafisha koo lake kisha kusema,
"Dorini kaa hapo nikueleze kwanza”

Dorini hakusubiri kulazimishwa, haraka alikaa kwenye sofa kisha kumuangalia Dokta Temba kwa macho ya kutarajia majibu, maana alikuwa na hamu ya kufahamu majibu ya vipimo, Dokta Temba alishusha pumzi kisha akaachia tabasamu na kusema,

"Dorini wala huna haja ya kuwaza sana dawa ya yote ni kumpokea Yesu Kristo awe bwana na mwokozi wa maisha yako maana hata mimi siamini ila nahitaji wiki hii niokoke"
Dorini aliinuka kwa hasira na kufoka,

"Baba…hivi unaona raha kuushtua moyo wangu, sihitaji unihubirie, kama huyo Yesu yupo mbona alimuacha Ema akani...”

Anaushika mdomo wake kisha akamwambia,
“Nilisahau Emanueli alinitafuta na mpaka sasa ananiita mkewe yaani nahisi kuchanganyikiwa, Aaagh! mbona nateseka peke yaangu, ngoja nikaangalie kama mme wangu baba Willy yupo salama"
Baada ya Dorini kusema hayo akawa anaondoka, mara dokta Temba alimuita kusema,

"Dorini mwanangu, mambo hayabebwi hivyo kama ukitaka kuyabeba hivyo utachanganyikiwa, wewe ni mkubwa sasa hebu kuwa na akili yako kama ya utotoni, ninakukumbuka vizuri Dorini wakati ulipokuwa mdogo ulikuwa unasovu mambo mpaka wakubwa tunashangaa, sasa kwa nini ukubwani usitatue mambo mpaka dunia ishangae? Na kama unataka kuondoka je ndio huhitaji majibu ya D.N.A ya mwanao na mmeo tena? Dorini mwanangu jifunze kumeneji yote utafanikiwa sawa mama"

Dorini aligeuka akiwa amechoka sana machozi yakiwa yameutanda uso wake mpole na wenye kuvutia sana kiasi ambacho kila mwanaume ambaye angemuona binti huyu basi angependezwa na kazi ya Mungu. Dorini alisogea taratibu kurudi ndani kwa baba yake mlezi kisha kukaa kwenye sofa huku akiuinua uso wake na kusema,

"Baba, nawezaje, nawezaje mimi kuchukulia poa shida kama hizi? nawalaumu sana wazazi wangu nawalaumu kama wangelifanya mamuzi mazuri mimi leo nisingekuwa hivi, ningekuwa na amani nisingekutana na hawa wachawi na tena nisingekutana na huyu adui wa furaha yangu Emanueli, unadhani huyu Ema nitaweza kumuepuka kweli?.

Dokta Temba alimuangalia kwa macho ya upole sana mwanae wa kumlea kisha akasema,
"Najua wewe huwezi ukamuepuka Emanueli ila serikali ya Tanzania inamuweza yule...calm down my princess"
Dorini alimuangalia Dokta Temba kisha kusema,

"Unaniambiaje nitulie, wakati unajua kabisa hali niliyo nayo siyo ya kawaida, labda nikwambie kitu baba; sidhani kama kuna ukweli wowote hapo, nimeshuhudia mwenyewe huyo Ema akipita pembeni ya trafki tena bila hofu huku gari lake halina namba ila hajafanywa chochote, ok sawa tufanye serikali imeweza kumkamata huyo Ema vipi kuhusu hao wachawi? nao watakamatwa na serikali? Baba ninachokiamini pesa ndiyo inaamua wala sio serikali"

Dokta Temba huku akiendendelea kumuangalia Dorini akamwambia,
"Kama suala ni pesa hata wewe unazo"
Dorini aliachia tabasamu la usoni huku moyo wake ukikataa kabisa kukubaliana na hilo tabasamu kisha kusema,

"Natamani sana niwe na furaha ndani ya moyo muda wote lakini sasa furaha itakujaje ilhali mateso yananiandama, eti baba ni nani asiyenijua Tanzania na Afrika nzima? Wanamuziki,waigizaji marais wa nchi zote na watu maaarufu wenye hadhi zao wananifahamu haswa kupitia huu mradi wangu mpya wa kulea watoto yatima MTOTO WA AFRIKA NA DORINI (MAD) ambao upo Afrika nzima lakini bado naambiwa huyo Ema ananizidi fedha, unadhani kama ananizidi fedha, nitaweza kupambana naye kweli?”
Dokta Temba alimuangalia sana Dorini kisha akamwambia,

"Hakuna faida kama ukiwa tajiri wa mali ukakosa utajiri wa watu, labda nikuulize kama ukizidiwa kwa kuugua chumbani kwako ni nani atakuwa wa kwanza kukuhudumia?, na ni kipi kitamtegemea mwenzake kati ya hivi vitu viwili yaani watu na mali?"
Kwa Dorini jibu la hapo halikuwa gumu hata kidogo alijibu haraka kwa kujiamini akisema,

"Mali ili zisaidie zinamtegemea mwanadamu azitumie"
Dokta Temba akamwambia kuwa,

"Na wewe anautajiri wa watu ndiyo maana ukawa maarufu na wote uliowatendea wema wanakuombea kwa Mungu ufanikiwe ila huyo Ema, sidhani kama anao huo utajiri wa watu nikianza mimi na wewe tunamchukia na wale wote wanao kupenda wewe tayari wamemchukia ni lazima tutakusaidia na Mungu naye atakusaidia, sijui unanielewa mwanangu?"
Dorini alimuangalia sana Dokta Temba kisha akamwambia,
"Kwa hiyo na wewe umemuamini huyo Yesu"
"Swadakta tena namuamini sana"
alisema Dokta Temba kwa ujasiri mkubwa.
"Mmhh! sawa bwana"

"Ndiyo hivyo na wewe hao wachawi ukiona wanakuzidi nguvu njoo umpokee Yesu Kristo apambane nao"
"Kama huyo Yesu aliniacha nikabakwa, unadhani mchezo ulipofika atauweza? hebu nipatie hiyo D.N.A yangu mie nijiondokee nikapambane mwenyewe na hali yangu, huyo Yesu kaa naye mwenyewe, kwangu hana msaada".

Dokta Temba alimpatia karatasi ya DNA huku akimuhurumia maana haamini kabisa juu ya uwepo wa Yesu, na hawezi amini kuwa Yesu anaweza kumsaidia. Dorini baada ya kuisoma ile karatasi ya majibu ya D.N.A aliangua kilio kikubwa huku mwili ukimtetemeka, huku moyoni akijiuliza,
"Kwahiyo Wilbert sio mtoto wa Dani?"
wakati analia na kujilaani mara aliigia mama yake mzazi, palepale Dorini alimfuata na kumtupia ile karatasi ya DNA huku akilaumu sana kwa kumzaa, maana leo amezaa na mtu ambaye hamjui na siyo hamjui tu bali hajui hata chimbuko lake, kana kwamba haitoshi mtu huyo pia ni mchawi, kwa hakika Dorini alilaani sana na kumhoji maswali mengi mama yake eti kwa nini alimzaa kama alijua ana wivu na Mr. Thomas, akawa anamwambia eti kama kipindi kile angeamua maamuzi mazuri yote haya yasingemsibu, yanamsimu kwasababu ya maamuzi ya kipuuzi aliyoyaamua kipindi kile.
Dorini aliondoka alipofika mlangoni kabla hajatoka nje alimgeukia tena mama yake na kumwambia,

"Nyie ndiyo mmenisababishia madhila haya yote, nachokuomba mama usije kusema hukujua, maana neno sikujua ni neno la mkosaji na ni neno la mpumbavu, kwa sababu kama hukujua kwa nini ulitenda, naondoka ila kama ambavyo mlifanya juhudi kuumiza moyo wangu basi mtafanya vivyohivyo juhudi kuutengeneza".

Baada ya Dorini kusema hayo akawa ameondoka kwa hasira sana huku akilia na kuendelea kulaumu na kulaani matukio yote yaliyo mkuta kwenye maisha yake, akawa mtu wa kujiuliza kwa nini maisha yake ni ya dhiki na maumivu, tangu utotoni mpaka ukubwani mateso ni yaleyale hayapungui halafu leo anaambiwa eti kuna Mungu. Mpaka kufikia hapo Dorini akaamini kuwa hakuna Mungu maana kama Mungu angalikuwepo basi angalimsaidia na hayo matukio ya kutisha yasingalikuwa fungu lake.
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…