Ripoti ya mwenendo wa vyombo vya habari vinavyoripoti uchaguzi na hali ya usalama kwa waandishi

Dotto Mnzava

R I P
Mar 6, 2014
865
427
Vyombo vya habari ni kiungo muhimu sana kipindi cha uchaguzi kati ya wananchi na wagombea/vyama. Vyombo vya habari vikisimamia misingi yao na maslahi ya Taifa vinaweza kutoa mchango mkubwa katika kusaidia raia kuchagua viongozi sahihi.

Lakini vile vile, vyombo vya habari na waandishi wasipokuwa makini na wakienda nje ya misingi ya kazi zao wanaweza kuwa sehemu ya wananchi kupata viongozi wabovu na wakati mwingine wanaweza kuchangia kuzuka kwa vurugu kipindi cha uchaguzi na pia kuhatarisha usalama wao wenyewe.

Kwa sababu hizo tajwa, Matandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) unapenda kutoa wito kwa vyombo vya habari, na wahahabari nchini kuzingatia usawa na maadili ya taaluma zao katika kuripoti kampeni za uchaguzi zinazoendelea nchini. Mtandao kipindi hichi cha uchaguzi tunafuatilia kwa karibu utendaji wa vyombo vya habari, wanahabari, Asasi za Kirai na Jeshi Polisi hasa wanapokuwa wanatekeleza majukumu yanayohusu uchaguzi.

HALI ILIVYO SASA

Kutokana na hali inavyozidi kujitoka katika vyombo vya habari Mtandao umeona ni vyema kukemea baadhi ya mambo ambayo yamejionyesha wazi katika ufuatiliaji wa awali toka tarehe 22 Agosti 2015 hadi sasa. Mtandao unafuatilia baadhi ya vyombo vya habari hasa vyombo vya habari vya umma pamoja na baadhi vyombo vya habari vinvyomilikiwa na makampuni binafsi. Mtandao unafanya uangalizi kwa kuangalia vigezo vya kimataifa vya utangazaji wa taarifa za habari za uchaguzi vilivyowekwa na shirika la kimataifa la Article 19.

Pamoja na kwamba muda wa kutoa repoti haujafika Mtandao umeona ni vyema kuyasemea mambo yafuatayo ili kulinda umoja na amani ya Taifa. Mambo ambayo tumeweza kuyabaini na yanayohitaji mabadiliko kipindi hichi cha kampeni ni kama yafuatayo:

Vyombo vya habari vya Umma vinaripoti kampeni za uchaguzi kwa kupendelea Chama Tawala (CCM) na kuvipa nafasi ndogo Vyama Vya Upinzani huku wakati mwingine kutovipa nafasi kabisa au kuripoti habari za kuvichafua peke yake. Kwa kufanya hivi Vyombo hivi vinajigeuza kuwa Vyombo vya Serikali na chama Tawala badala ya kuwa sauti ya umma. . Suala hili ndilo lilipelekea mpaka Mamlaka ya usimamizi wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwapa Televisheni ya Taifa TBC1 Barua ya karipio kuhusu tabia ya kuvibagua vyama vingine vya siasa. Kwa hili Mtandao unatoa pongezi kwa TCRA kwa kuonyesha uhuru wao katika utendaji wa majukumu yake.

Magazeti ya Umma kama vile Habari Leo na Daily News vinaonyesha wazi wazi kupendelea chama tawala kwa kuvipa nafasi kubwa ya mbele (Front Page), huku vyama vingine vikipiwa nafasi ndogo, ama kutopewa kabisa na wakati mwingine taarifa za vyama pinzani kuonekana ni zile zenye mrengo wa hasi. Matoleo mengi yanaonyesha taarifa hasi nyingi za UKAWA huku wagombea wa chama Tawala wa nafasi ya urais , mgombea mwenza wake na wanakampeni wao wakipewa nafasi kubwa na taarifa za kujenga.

Wakati huo huo, kinyume na ilivyotegemewa vyombo binafsi ndivyo vinaonekana kama vyombo vya umma kwa kuzingatia usawa katika habari zao.Hivyo Mtandao Unavipongeza Vyombo vya habari vinavyomilikiwa na watu Binafsi kwa kuweza kuzingatia usawa katika kuripoti kampeni za uchaguzi.

Kwa kutaja machache Makampuni ya IPP, AZAM na Mwananchi Communication yameonekana kutoa fursa sawa kwa vyama vyote bila kujali ni chama tawala, vyama vikubwa au vidogo. Magazeti kama ya Nipashe na Mwanachi na Televisheni za AZAM na ITV zimekuwa zikijitahidi kutoa fursa kwa vyama na wagombea wote. Ni vigumu sana kukosa taarifa zenye kujenga kwa wagombea wote hasa katika nafasi za mbele za vyombo hivi.

Pia kumekuwepo na taarifa zinazolenga kukandamiza chama au mgombea wa mrengo fulani kwa maslahi ya chama fulani. Pia vipindi vingi maalum TBC pamoja na vile vya moja kwa moja vimekuwa vikionekana kupendelea chama tawala hasa wagombea urais na timu yake ya kampeni.

Mfano Mgombea Urais wa CCM Ndugu John Magufuli alipokuwa Tabora alirushwa moja kwa moja na TBC pamoja na Rais Mtaafu Benjamin Mkapa alipokuwa Mkoani Kagera kumnadi mgombea wa CCM. Ikumbukwe kuwa chombo cha habari hasa vyombo vinavyoendeshwa na kodi za waanchi vinatakiwa kutoa fursa sawa kwa vyama vyote na kuutaarifu UMMA kwa kutoa taarifa zilizo za kweli na sio za kuangusha chama kimoja na kuinua kingine.

Pia tumeona kosa kubwa linafanywa na karibu vyombo vyote kwa kusahau kumpa mwananchi nafasi ya kusema na wagombea. Vyombo vingi vya habari vinaendeshwa na matukio na pia wanatoa taarifa nyingi za wagombea pekee na kuwasahau wapiga kura.

Magazeti mengi sasa kila kukicha ni Lowasa au Magufuli kiasi kwamba wanachi wamejenga dhana ya kuwa vyombo vya habari vipo kwa ajili ya kusemea wagombea watafanya nini na kusahau kufikisha ujumbe wa wapiga kura wanataka nini. Tunawasihi wanahabari kwa muda huu uliobaki wajaribu pia kutoa fursa kwa wananchi kusukuma ujumbe kwa wagombea kupitia vyombo vya habari juu ya Tanzaia waitakayo.

Aidha, vyombo vingine hasa vile vinavyomilikiwa na vyama kama Uhuru na vingine vinavyomilikiwa na wanasiasa kama vile Star TV na Tanzania Daima vimeendelea kuonekana zaidi kutoa taaarifa nyingi za vyama vyao na wakati mwingine taarifa hasi kwa vyama vingine.

Vyombo hivi vinapaswa kuzingatia misingi ya uandishi na kuepuka taarifa za kichonganishi hata kama wamiliki wanauhusiano wa moja kwa moja na vyama. Hata hivyo tofouti na Uhuru Tanzania Daima na Star TV kuna wakati wanajitahidi kutoa taarifa chanya za vyama visivyokuwa na mrengo na wamiliki wa vyombo hivyo ingawa kwa uchache.

HALI YA USALAMA KWA WANAHABARI

Mtandao pia unafanya ufuatiliaji wa hali ya usalama kwa wanahabari katika kipindi hichi cha uchaguzi. Tumegundua kuwa jinsi vyombo vya habari vinavyoshindwa kutoa fursa sawa kipindi cha uchaguzi ndivyo wanavyozidi kujiweka kwenye mazingira hatarishi. Mfano mwaka 2010 wanahabari wengi wanaoripoti kwenye vyombo vya Umma waliweza kupata matatizo mengi wanapokuwa katika mikutano ya siasa.

Toka kampeni za ndani na nje ya vyama Mtandao umepokea kesi za usalama kwa wanahabari zaidi ya 6 kama kwa mfano:

Tarehe 25 Julai 2015 tulipokea malalamiko ya kufungiwa kwa Radio ya jamii " Radio kyela " huko mbeya na kusemekana kwamba radio hiyo imefungiwa kwa sababu za kisiasa. Mtandao umekwisha tuma barua TCRA kupata sababu za kufungiwa lakini wamekuwa kimya mpaka sasa.

Tarehe 31 Julai 2015 kupigwa kwa mwandishi Benson Mwakalinga na baadhi ya viongozi wa CCM huko Kyela kesi imerepotiwa Polisi.

Tarehe 17 Agosti 2015 kuvamiwa na kupigwa kwa waandishi wa habari wanne huko Ruvuma wakiwa wanarepoti habari za uchaguzi, kesi imeripotiwa Polisi.

Tarehe 11 Septemba 2015 kupigwa kwa mwandishi wa Habari gazeti la Uhuru Christopher Lissa. Mwandishi huyu alipigwa na wafuasi wa UKAWA waliodai kuwa katumwa na CCM.

Mtandao unakemea vikali vitendo vya kuwavamia na kuwapiga waandishi wa habari wakiwa katika majukumu yao ya kila siku ya kuhakikisha wananchi wanapata habari. Pia tunatoa wito kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha wanalinda usalama wanahabari kipindi hiki cha uchaguzi kwani wana mchango mkubwa katika upatikani wa viongozi bora na amani ya taifa.

Pia tunapenda kutoa pongezi kwa mahakama za Tanzania kwa kuendelea kuonyesha umuhimu wa kuwa na uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata habari kwa kuliachia huru gazeti la kiuchunguzi la Mwanahalisi. Ikukumbukwe tulipinga kwa nguvu zote kuhusu matumizi mabaya ya sheria ya magazeti ya mwaka 1976 iliyotumika kulifungia gazeti hili bila makosa.

VIFAA VYA USALAMA KWA WANAHABARI

Kutokana na hali ya waandishi kuwa tete na pia kutokana na waandishi au vyombo vya habari kujipambanua na upande fulani wa wagombea, tumeona ni vyema wakatumia vifaa ambavyo havitaonyesha ni jina wala chombo anachotoka mwandishi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba waandishi wengi hasa wa vyombo vya umma kama TBC wanapata shida sana kufanya kazi na wananchi na vyama pinzani.

Vifaa vya usalama kwa wanahabari vitasaidia kutumika kama kinga kwa usalama wao tunapoelekea katika ichaguzi mkuu.

a) Tutaanza kutoa Majeketi 200 kwa PRESS CLUB 1O Tanzania, ambayo yatatumika kwa waandishi ili kuwasaidia kwenye masuala ya usalama hasa kurepoti habari za maandamano na mikutano ya kisiasa.

Mikoa hiyo ni ile yenye ushindani mkubwa kisiasa; Dar es Salaaam, Kigoma, Mwanza, Arusha, Mtwara, Kigoma, Zanzibar, Mbeya na Iringa.

b) Mwongozo wa masuala ya ulinzi na usalama kwa waandishi katika kuelekea kwenye uchaguzi mkuu utatolewa kwa wanahabari siku chache zijazo. Mwongozo huu unatoa mambo makuu kwa mwanahabari kuzingatia katika kipindi hichi ili kuwa salama.

WITO WETU

A. Kwa Vyombo vya Habari
• Tuna sisitiza vyombo vya habari kuzingatia hali ya usalama kwa waandishi wao hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi.

• Tuna visihi vyombo vya habari hasa vile vinavyoendeshwa kwa kodi za watanzania kutoa habari bila upendeleo wowote, na kutoa habari ambazo zinajenga na sio kuliingiza taifa katika machafuko.

• Tunasisitiza vyombo vya habari kuwezesha wanahabari wao ili kuweza kujitegemea na kuacha kuambatana na wanasiasa katika usafiri wao wakiwa mikoani kwani inaweza kuathiri uandishi wao kwa kupendelea vyama vinavyowapatia usafiri na misaada midogomidogo. Kwani tayari baadhi ya waandishi wa chombo fulani wameshajiondoa kwenye msafara wa mgombea fulani baada ya kunyanyasika pale aliporusha taarifa ya kweli amabayo timu ya mgombea hawakutaka irushwe.

B. Kwa Vyama vya siasa

Tunavikumbusha vyama vya siasa kuwaheshimu waandishi na kuacha kuwatumia kuripoti habari wanazotaka wao. Tunakemea tabia ya kutaka waandishi waandike mambo mazuri tu yanayojitokeza kwenye mikutano ya wagombea na kuacha madhaifu. Wananchi wanahitaji pia kujua mazuri na madhaifu ya wagombea ili wafanye maamuzi sahihi.

C. Kwa Vyombo vya usalama

Tuna visisitiza vyombo vya usalama vyote hasa Jeshi la Polisi kuwa na mahusiano mazuri na waandishi wa habari na kuzingatia usalama wao. Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama msikubali kabisa kipindi hichi kutumika na chama chochote, kwani kufanya hivyo tunaweza poteza amani ya Taifa.

D. Kwa wanahabari.

Tunawaomba wanahabari kuwa makini na usalama wao katika kipindi hichi cha uchaguzi. Tunawakumbusha waandishi kutokukubali kutumiwa na wanasiasa kwani kwa kufanya hivyo wanaweka hali ya usalama wao hatarini. Wekeni maslahi ya Taifa mbele ili kulisaidia taifa kupata viongozi bora huku tukiendelea kubaki wamoja na wenye amani katika Taifa litakalozingatia haki na usawa zaidi.

E. Kwa jamii

Tunawaomba wanajamii kuwa walinzi wa wanahabari hasa katika kipindi hichi cha uchaguzi, kwa kuwa bila wanahabari itakuwa ni vigumu kwa wao kupata habari kwa wingi na kwa wakati. Pia wanachi tutumie fursa ya uwepo wa vyombo vya habari kuwaeleza wagombea vipaumbele vyetu katika uchaguzi huu.

F. Kwa TCRA

Tunapenda kuwasihi TCRA kuendelee kuonyesha ujasiri katika kuvikemea vyombo vya habari hasa vya umma ambavyo vinaonekana wazi wazi kuvibagua vyama vingine kipindi hichi cha uchaguzi.

Onesmo Kasale Olengurumwa,
Mratibu Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania-THRDC
 
Hivi kauli kama hizi zina tija kweli? Is there any impact ? Hatua yoyote isipochukuliwa what is next?
 
Hivi kauli kama hizi zina tija kweli? Is there any impact ? Hatua yoyote isipochukuliwa what is next?
(Nadhani hayo ni maoni yao tu hayana mashiko, hayana nguvu yoyote kwani faulo za chama tawala hazijaanzia uchaguzi huu pia vyombo vya dola kutumika kisiasa sio jambo la kushangaa ni kawaida kwa Tanzania pia wamesahau kuzungumzia VITISHO vya vita baadhi ya wapiga kampeni wa ccm wanapitapita kuwatisha akina mama kwamba eti wakichagua ukawa wataleta vita, kwa hiyo wao na watoto ndo watakao athirika kwa nini wasichukuliwe hatua kali za kinidhamu? Nani wa kuleta vita anayeshinda kihalali kwa haki vita ya nini? CCM acheni wazimu tangazeni sera kama mnazo.
 
Back
Top Bottom