Ripoti ya Mawauji ya Arusha na kinachoendelea Bungeni juu ya ripoti ya mauwaji mengine ya waTZ.

Dec 11, 2010
3,321
6,328
Wakuu.

Naomba kunakili Maneno ya Mchungaji Msigwa wakati akiwasilisha. "Kuikosoa na kuisema vibaya serikali yako hakumaanishi kuwa huna uzalendo na nchi yako, na kuisema vizuri serikali hakumaanishi kuwa wewe ni mzalendo sana na nchi yako"

Bungeni wanajadili mauwaji yaliyotokea kwa watanzania wenzetu kupitia operation tokomeza ambayo badala ya kuleta tija imeleta madhara makubwa kwa watanzania wenzetu ikiwemo vifp , kuteswa, kubakwa kwa kina mama na kusokomezwa chupa maeneo ya siri huku wanaume nao wakilazimisha kufanya mapenzi na miti.

Tukiwa tunajiuliza hayo yote, tuone hii ripoti ambayo mpaka leo serikali imegoma kuitoa hadharani na kuamua kuificha imesababisha kina nani kuchukuliwa hatu?

1.0 UTANGULIZI:

1.1 Muhtasari wa Tukio:
Tarehe 5 Januari 2011, Jiji la Arusha lilikumbwa na machafuko
yaliyotokana na vurugu za kutawanya maandamano yaliyofanywa na Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo. Wakati Chama hiki kikidai kukamilisha
taratibu zote za maandalizi na makubaliano na jeshi la polisi, tarehe
4 Januari usiku, mkuu wa jeshi hili Inspekta Generali Saidi Mwema
aliyazuia maandamano hayo kupitia vyombo vya habari hususani luninga
za ITV na TBC katika habari za saa mbili usiku.


Uamuzi wa kuyazuia maandamano hayo na kuruhusu mkutano wa hadhara
ulidaiwa kuwa ni kutokana na sababu za ‘ki intelijensia’. Kwamba
kufanyika kwake kungeleta machafuko. Pamoja na zuio hilo, Chadema
iliendelea na, maandamano hayo wakiyaita ya amani..

Kufuatia tukio hilo, vyombo vya habari kwa maana ya magazeti, redio na
luninga vilitoa taarifa mbali mbali kuhusiana na vurugu hizo za
Januari 5, 2011 mkoani Arusha.

Miongoni mwa magazeti hayo ni Gazeti la Majira ISSN 0856 – 5086
Na.6211 Vol. II/4221 Ijumaa Januari 7, 2011, ISSN 0856 – 5086 Na.6212
Vol. II/4222 Jumamosi Januari 8, 2011 na Mwananchi ISSN 0856 – 7573
Na.03848 Ijumaa Januari 7, 2011, ISSN 0856 – 7573 Na.03849 Jumamosi
Januari 8, 2011.

Magazeti mengine yalikuwa ni Nipashe ISSN 0856 – 5414 Na.056888
Jumamosi Januari
8, 2011 na Tanzania Daima ISSN 0856 9762 Toleo Na.2226 Ijumaa Januari
7, 2011, ISSN 0856 9762 Toleo Na.2227 Jumamosi Januari 8, 2011 na ISSN
0856 9762 Toleo Na.2228 Jumapili Januari 9.

Magazeti ya kiingereza na mengineyo yaliyotoa taarifa hizi ni pamoja
na ‘The Guardian ISSN 0856 – 5422 ISSUE no. 5019 na, Daily News ISSN
0856 – 3813 no. 10240 yote ya tarehe hiyo ya ijumaa Januari 2011.



Vurugu hizo zilisababisha watu watatu (3) kuuwawa, ishirini na nane
(28) kujeruhiwa, arobaini na tisa (49) kukamatwa na kufikishwa kituo
cha polisi na kati yao, thelathini na moja (31) kusomewa mashtaka
mahakamani.Hii ni kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kamanda wa
Polisi mkoa wa Arusha wakati wa mahojiano na ujumbe wa Tume katika
nyumba ya mapuziko (Police rest house) Arusha tarehe 10 January, 2011.

Taarifa hizo ziliendelea kueleza kuwa, kumetokea uharibifu wa mali,
nyumba kuchomwa moto vituo vya polisi, kutishiwa, kuvamiwa ofisi za
chama tawala, kupigwa mawe, uharibifu wa magari ya polisi na ya raia
na pia mali za watu kuibiwa.




2.0 UFUATILIAJI:
Kwa mujibu wa sheria iliyounda Tume ya Haki za Binadamu, sheria namba
7 ya mwaka
2001 iliyoanza kufanya kazi rasmi 2002, sura ya pili II, kifungu cha 6
(c) kimetoa mamlaka kwa Tume kufanya uchunguzi katika jambo lolote
linaloashiria au kuthibitisha uvunjwaji wa haki za binadamu na utawala
bora.

Aidha kwa mujibu wa sheria hii, sura ya tatu III, kifungu namba 15 (1)
(a), kwa ridhaa yake binafsi, Tume iliona umuhimu wa kufuatilia na
kuchunguza tukio hili.

Tume ilizingatia pia mamlaka iliyopewa katika Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Ibara ya mia na thelathini 130 (1) kifungu
kidogo cha (c) kinachosisitiza uwezo na mamlaka ya Tume kufanya yote
haya.

Tume ilimteua Mhe. Kamishna Joaquine De-Mello akiandamana na afisa
uchunguzi Philipo Sungu kutoka idara ya elimu kwa umma na mafunzo
kufuatilia tukio hilo kwa muda wa siku tatu (3) kuanzia Januari 10
hadi 13, 2011 ili kupata picha halisi. Lengo kuu lilikuwa kubaini
chanzo cha vurugu hiyo, uvunjwaji wa haki za binadamu kama ulikuwepo
ili kutoa maoni na mapendekezo kwa mamlaka husika.

Tume ilifanya mahojiano na wadau mbalimbali zikiwemo mamlaka ya Jeshi
la Polisi Tanzania, hususani uongozi wa juu mkoani Arusha, uongozi wa
Chama Cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA), madaktari na majeruhi
katika hospitali ya mkoa wa Arusha (Mount Meru) na ile ya kanisa la
KKKT (Seliani) na baadhi ya wananchi kwenye sehemu yalipotokea matukio
(site visit/site scene). (KIAMBATISHO II)

2.1 Maelezo kutoka Jeshi la Polisi:
Kwa ujumla maelezo ya jeshi la polisi yalielekeza shutuma kwa CHADEMA
kukaidi agizo halali la mamlaka ya juu ya Polisi lililozuia
maandamano.

Walidai kuwa licha ya mtiririko mzima wa majadiliano na makubaliano,
utata uliojitokeza ulikuwa ni zipi ziwe barabara/njia zitakazotumika
kwa ajili ya maandamano hayo. CHADEMA hadi inakwenda kwenye maandamano
haikuafikiana na badala yake kuja na idai zaidi ya ile
zilizopendekezwa. Askari walidai kuwa taarifa za ‘kiintelijensia’
ziliashiria uvunjifu wa amani na hivyo kutumia nguvu pale amri hiyo
ilipokiukwa.

Viongozi hawa walidai licha ya kuyasindikiza maandamano haya kwa
utulivu kutoka eneo la Phillips hadi Sanawari kupitia hoteli ya Mt.
Meru, utata ulijitokeza pale walipofika njia panda ya Sanawari ambapo
makundi makubwa ya watu yalijitokeza kutokea Kaloleni na Mianzini.

Askari wanadai hakukuwa na namna nyingine isipokuwa kutumia nguvu
kuwatawanya waandamanaji kwa kutumia mabomu ya machozi, risasi za
mpira na maji ya kuwasha kutawanya umati mkubwa wa waandamanaji.

Askari waliwakamata na kuwapiga viongozi ambao tayari walionyesha
kupandisha hasira na pamoja na wafuasi (40) waliwekwa rumande kituo
kikuu cha polisi cha mjini Arusha.

Wakati haya yakiendelea , baadhi ya viongozi wengine wakuu wa CHADEMA akiwemo
Katibu wa chama Taifa bwana Wilbroad Slaa na mbunge wa Moshi mjini mheshimiwa

Ndesamburo Kiwelu waliponyoka na kuwahi uwanjani NMC ili kuwahutubia
wananchi waliokuwa tayari wamewasili huko.

Askari wanasema walitishika pale viongozi hao waliokuwa jukwaani
wakichochea wananchi kuvamia kituo cha polisi kwa mustakabali wa
kuwakomboa viongozi waliokuwa wamekamatwa na kuwekwa rumande katika
kituo kikuu cha Polisi (KIAMBATANISHO I A).

Yote haya ni kwa mujibu wa mkuu wa polisi mkoani Arusha ( RPC )
Thobias Andengenye na Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai ( DCI
) Robert Manumba walioridhia kukutana na msafara wa Tume siku
tuliyowasili Arusha Jumatatu ya tarehe 10 mwezi Januari 2011.
Mazungumzo haya yalifanyika katika nyumba ya wageni ya Jeshi la Polisi
(rest house) mjini Arusha.
2.2 Maelezo kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA):
Jioni ya saa kumi na mbili (12:00) siku hiyo hiyo ya tarehe 10 mwezi
wa Januari, ujumbe wa Tume ukapata fursa ya kukutana na ujumbe wa
uongozi wa CHADEMA katika ofisi za wakili na diwani wa chama hicho
kata ya Moshi mjini, wakili Albert Msando.

Kwa upande wake CHADEMA ilidai kuonewa na kuburuzwa na jeshi la polisi
tangu majadiliano ya awali ya nia ya kufanya maandamano hayo tarehe
31/12/2011. Walishangazwa na kigezo cha kupata ruhusa kutoka katika
jeshi kinyume na sheria ya Polisi na ile ya vyama vya siasa
inayozungumzia kutoa taarifa (notice) tu.

Walisisitiza kuwa kazi ya jeshi katika matukio haya ni kulinda amani
na kuhakikisha utulivu unakuwepo katika shughuli nzima. Wanasema ni
dhahiri kulikuwa na njama za kuibana na kuifadhaisha CHADEMA kwa
sababu za kisiasa na ubinafsi. Kwao, tathmini nzima ya majadiliano
ilikuwa ni ya ubabaishaji

Waliendelea kusisitiza kuwa, uvumilivu ulipotea pale ambapo wakiwa
katika maandalizi ya mwisho siku ya tarehe 4 Januari usiku walipopata
habari kupitia wadau kwamba mkuu

wa jeshi ameyafuta maandamano hayo bila hata ya kutumia njia za
kimaandishi na kwa wakati muafaka.

Kubwa zaidi wanadai viongozi hao, ni utulivu na amani uliyoshamiri
tangu maandamano yaanze pale Phillips kupitia hoteli ya Mount Meru
hadi njia panda ya Sanawari ambapo askari walianza kwa kuwapiga na
kuwapeleka viongozi mahabusu. (KIAMBATISHO I B)

Walisisitiza kuingiliwa uhuru huo wa kikatiba na uongozi wa juu wa
Chama cha Mapinduzi ambao tangu kupatikana kwa ushindi wa kiti cha
ubunge kwa jimbo hilo na mengine machache wamekuwa wakitumia mbinu
mbali mbali kuwadhoofisha na kuwaadabisha tena kwa matumizi mabaya ya,
nguvu ya dola.

Waliohudhuria kikao hiki kilichoisha saa tatu usiku ni pamoja na
mbunge wa jimbo la Arusha Mjini Mheshimiwa Godbless Lema, katibu wa
chama mkoa bwana Amani Golugwa na diwani wa chama hicho bwana Albert
Msando


2.3 Maelezo kutoka kwa Madaktari na Wagonjwa Majeruhi katika Hospitali
Ujumbe huu uliendelea na safari Januari, 11 asubuhi ukianza kuonana na
madaktari na wagonjwa majeruhi waliolazwa katika hospitali mbili (2)
za Mount Meru na ile ya Seliani.

Taarifa zilizopatikana katika hospitali hizi ni kupokelewa kwa
majeruhi ishirini na sita (26) katika hospitali ya Mount Meru na
wawili (2) Seliani. Majeruhi watatu (3) walipoteza maisha wakati
wakipatiwa matibabu ya awali hapo hospitali ya Mount Meru, ishirini na
mbili (22) walilazwa katika hospitali ya Mount Meru na watatu
walipatiwa matibabu na kuruhusiwa kuondoka hospitalini( moja (1)
kutoka hospitali ya Mount Meru, wawili (2) kutoka hospitali ya
Seliani).

Madaktari walithibitisha kuwa vifo hivyo vilitokana na majeraha ya
risasi za moto. Kwa upande mwingine majeruhi walithibitisha kupigwa
risasi za moto huku wakionyesha majeraha hayo kwenye miili yao
(KIAMBATISHO I C)
2.4 Maelezo ya Wananchi katika sehemu za Matukio (site visit/ site scene)
Tarehe 12 ujumbe wa Tume ulipata fursa ya kuzipitia barabara ambazo
maandano yalipita na pia sehemu muhimu zilizokuwa na vurugu kubwa,
Katika hali ya kutatanisha wananchi wengi waliohojiwa hawakuwa tayari
kutoa majina yao kwa madai ya kuhofia ukatili wa askari.

Sehemu zilizopitiwa ni maeneo ya Sanawari, Kaloleni na uwanja wa NMC
ulikofanyika mkutano wa hadhara. Wengi walioulizwa walionyesha
kushangazwa na kusikitishwa na jinsi askari walivyokuwa na jazba
wakiwatawanya waandamanaji waliokuwa watulivu. Walishangaa kuona jinsi
virungu, risasi za mpira na moto, mabomu ya machozi, na maji ya
kuwasha yalivyokuwa yakimiminwa kwa chuki na hasira.

Walisema kuwa vitendo hivi viliamsha ari na hasira ya wananchi na
kuanza kurudisha mapigo kwa kutumia mawe. Wananchi walivunja vioo vya
ofisi ya CCM mkoa wa Arusha, wakati nyumba ya mwananchi moja
mfanyabiashara wa Yemen bwana Salum Ally iliyoko jirani na eneo la
Metropol mjini Arusha ikiungua kwa moto uliosababishwa na bomu
lililoruka kutoka katika gari la polisi.

Kwa upande wake mfanyabiashara bwana.Salum Ally alisikitishwa na hali
yote ya tukio hilo ambalo yeye aliliona ni la kiuchumi zaidi kupitia
njia za siasa. Alieleza kuwa kwa muda mrefu akiwa mfanyabiashara
katika eneo hili ameshuhudia hali duni za maisha zinavyoongezeka na
hasa kwa kundi la vijana.

Hata hivyo aliporejeshwa kuzungumzia tukio la uharibifu wa nyumba yake
alikiri kuwa lilitokana na bomu la moto la kurushwa na kwenda juu
kiasi kile hadi ghorofa ya pili. Alikiri isingekuwa rahisi kwa
wananchi kuchoma nyumba sehemu ya juu na kuacha chini. Aliendelea
kueleza kuwa amekuwa akifuatwa na mkuu wa Upelelezi wa Mkoa

(RCO) ili atoe tathmini ya uharibifu ili jeshi limfidie, dhana ambayo
yeye binafsi hayuko tayari kuiridhia na hapa amenukuliwa akisema, “ni
gharama ndogo tu isiyozidi shilingi milioni tatu, na sioni sababu
nilipwe kwani naamini bomu hili lililipuka kwa bahati mbaya tu”.
(KIAMBATISHO I D)
3.0 MFUMO WA SHERIA:
Wakati yote yakitokea ni vema kuangalia mfumo wa sheria ili kufikia
maoni na mapendekezo ya kitaalamu yatakayosaidia kurekebisha hali hii.
Ni vema pia kuangalia ni jinsi gani mifumo ya sheria invyochangia
katika kujenga au kudhoofisha haki katika jamii yetu.

Tukio hili limetokea wakati nchi yetu iko mstari wa mbele katika
kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ya haki za
binadamu na utawala bora. Mikataba hii ina maridhiano na vipengele
vizuri kwa madhumuni ya kuheshimu, kulinda, kutekeleza, kutetea na
kukuza haki za binadamu. Nchi inajivunia Katiba nzuri inayoainisha
vipengele mbali mbali vinavyotambua na kulinda haki za msingi za
binadamu.

Jumuiya ya kimataifa kwa pamoja inawajibika kwa Azimio la Ulimwengu la
Haki za Binadamu la mwaka 1948 (UDHR) ambalo ni mama wa matamko,
makubaliano na mikataba ya vizazi vyote vya haki. Vizazi hivi
vinahusisha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na
kiutamaduni 1966 (ESCR), Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na
Kisiasa 1966 (CCPR), Mkataba wa Kimataifa Kuhusu Haki za Watu Wenye
Ulemavu (UNCPRD), Mkataba wa Kimataifa Dhidi ya Ukatili na Unyanyasaji
dhidi ya Binadamu na mingine mingi.

Nchi wanachama, Tanzania ikiwa miongoni mwao, zilizoweka sahihi na
kuridhia mikataba hii zinawajibika moja kwa moja “kuheshimu, kulinda,
kutetea na kutekeleza” haki zilizoainishwa kwenye mikataba husika.
Pamoja na kutokuwa na msukumo wa kisheria nchi wanachama wanapaswa
kuzingatia zaidi utashi na weledi ili kufanikisha na kutimiza azma
hizi.

Azimio la ulimwengu juu ya haki za binadamu 1948, kifungu cha kumi na
tisa (19 ) kinaeleza kuwa “Kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake na
kujieleza, haki hii inajumuisha uhuru wa kusimamia maoni yake bila
kuingiliwa na kutafuta, kupokea na kutoa habari na mawazo kupitia
vyombo vya habari vya aina yoyote bila kujali mipaka”.

Nao Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa 1966, Ibara
ya 19.-(1) unaainisha kuwa, “Kila mtu ana haki ya kutoa mawazo yake
pasipo kubugudhiwa, (2) Kila mtu atakuwa na uhuru wa kujieleza; haki
hii inajumuisha uhuru wa kuuliza, kupokea, na kutoa taarifa na mawazo
ya aina yeyote pasipokujalisha, aidha kwa kuongea au kwa kuandika au
kupiga chapa ama kwa njia ya usanii ama kwa njia ya chombo cho chote
cha habari alichokichagua”.

Azimio hili pia katika, kifungu chake cha 20 (1) linabainisha kuwa
kila mtu anayo haki ya kushiriki katika mkutano na chama kwa hali ya
amani na kama inavyosisitizwa pia katika Mkataba wa Kimataifa wa Haki
za Kiraia na Kisiasa wa 1966 katika ibara yake ya 21.


Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, imebeba kwa upana
kwa kuzingatia haki ya kuishi, uhuru wa mtu na vikundi vya watu, haki
ya faragha na usalama wa mtu, uhuru wa kwenda utakako, haki ya uhuru
wa kutoa maoni, kuamini dini utakayo, uhuru wa kushirikiana na wengine
na uhuru wa kushiriki shughuli za umma. Ibara ya 12 hadi ya 21 ya
Katiba inajieleza vema.

Kuendana na mazingira ya tukio hili inabidi pia kuangalia sheria
nyingine za ndani ya nchi zinazohusu mikutano ya hadhara na maandamano
katika nchi yetu. Tukiangalia kanuni za jumla za jeshi la polisi namba
403 kifungu cha kwanza inasema;

(a) “Any person who is desirous of convening, collecting, forming or
organising any assembly or procession in any public place shall, not
less than forty eight hours before the time when the assembly or
procession is scheduled to take place submit ‘ a written notification’
of his impending assembly or procession to the police officer in
charge of

the area”,. Hivyo hitaji hapa kwa anayetaka kufanya maandamano au
mkutano wa hadhara kwa mujibu wa sheria hii ni kutoa ‘TAARIFA’ tu tena
katika kipindi kisichopungua saa arobaini na nane (48).


b) ‘ where a person submits a notification in accordance with the
preceeding paragraph, he may proceed to convene, collect, form, or
organise the assembly or procession in question as scheduled unless
and until he receives an order from the Police Officer in charge of
the area directing that the assembly or procession shall not be held
as notified. Hii inasisitiza kuwa Polisi “Officer in charge” wa eneo,
ambalo katika eneo hilo la Arusha mjini ni OCD wa Arusha Mjini – ndiye
anayeweza kutoa maelekezo ya kuzuia maandamano na sio RPC au IGP. Kwa
mantiki hii, taarifa ya CHADEMA kwa Polisi ilitosha kwa wao kuendelea
na mipango yao ya maandamano na mkutano kama inavyoelezwa katika
kifungu (b)





Sheria Na. tano (5) ya mwaka 1992 ya vyama vya siasa kifungu cha 11
vifungu vidogo vya (4) na (6). na sheria Na. 1 ya 1939 ya polisi na
huduma za mgambo kifungu 43.-(1), (2), zimekidhi pia hitaji la CHADEMA
kuendelea na mipango yao ya maandamano na mkutano wa hadhara kama
ilivyopangwa.



Sheria Na.5, 1992 ya vyama vya siasa kifungu 11. — (8) inasema; ‘A
stop order given under subsection (6) shall be in writing and, in such
form as is able to easily disclose the reasons for its issuance and,
state whether or not the political party concerned may hold the
meeting at the venue at another time or date convenient to it in the
same area’. CHADEMA wanasisitiza kwamba hawakupata taarifa ya
kimaandishi nao Polisi kudai kutoa barua hiyo kupitia kwa mwakilikishi
wa Chadema Estomihi Mala.Mala hakuweza kupatikana kuthibitisha madai
ya polisi na hadi ujumbe wa Tume unaondoka Arusha polisi hawakuwezesha
kuwasilisha nakala ya barua hiyo kwa ujumbe wa Tume kama walivyotakiwa
kuthibitisha madai yao.



Sheria ya Police - General Order No. 294 inasema;
1. ‘The following officers ONLY are authorized to release information
on police matters to the Press: - a) The Inspector General - on all
matters affecting Force policy and security.
b) Director of Criminal Investigation - Crime reports, wanted person
notices and appeals to the public in connection with crime, accidents
etc c) Chief of Public relations Police Headquarters - Routine Press
notices affecting the whole Force. d) Regional Commanders - Routine
Press Notices affecting particular Region.


2. All Press and radio releases shall normally be typed or written.
Verbal releases are only permissible in emergency and shall always be
confirmed, in writing, at the earliest opportunity”.Jeshi la polisi
halikukidhi matakwa ya sheria hii kwa kushindwa kutoa taarifa ya zuio
la maandamano na mkutano wa hadhara kwa taratibu zinazokubalika
kisheria.

Sheria Na. 1 ya 1939 ya polisi na huduma za mgambo kifungu 45 na 46. -
(4) inasema,

‘Any assembly or procession in which three or more persons attending
or taking part, neglect or refuse to obey any order for dispersal
given under the provisions of subsection (4) of section 43 or section
44, shall be deemed to be an unlawful assembly, within the meaning of
section 74 of the Penal Code’.Hata hivyo, kwa sababu kulikuwa hakuna
taarifa ya OCD ya kuzuia maandamano, polisi hawawezi kutumia kifungu
hiki cha (Penal code). Hivyo maandamano hayo yalikuwa halali.


Taarifa za ufuatiliaji zinaonyesha kuwa hata kama maandamano
yalizuiliwa CHADEMA
bado walikuwa na nafasi ya kudai haki hiyo kisheria kama kifungu
43.-(6) cha Sheria Na.
1, 1939 ya polisi na huduma za mgambo inavyosema,
“Any person who is aggrieved by the terms of a stop order issued under
subsection
(3) or, any order given by a police officer under subsection (4), may
appeal to the

Minister whose decision on the matter shall be final.” Hili Chadema
hawakulifanya kwa madai kuwa hawakupata barua ya zuio la maandamano na
mkutano wa hadhara kutoka polisi.

4.0 TATHIMINI YA UVUNJWAJI WA HAKI ZA BINADAMU:


· Taarifa ya kufanyika maandamano na mkutano wa hadhara tarehe 5
Januari,2011 ilitolewa kwa mkuu wa Jeshi la polisi wilaya ya Arusha
Mjini tarehe 31 Desemba, 2010. Maandamano na mkutano wa hadhara
uliridhiwa na serikali tarehe 4

Januari,2011.



· Maandamano yalizuiliwa katika dakika za mwisho kwa tangazo la Mkuu
wa jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema kupitia vyombo vya habari usiku wa
tarehe 4 Januari 2011.CHADEMA walifanya maandamano tarehe 5 Januari,
2011 kama ilivyopangwa licha ya kuepo kwa Tangazo la zuio.


· Ujumbe wa Tume umebaini kuna utata wa kutolewa taarifa ya zuio la
maandamano kimaandishi na kupokelewa na CHADEMA kupitia mwanachama
wake aitwae bwana Estomihi Mala.Ujumbe wa Tume haukupata nakala ya
barua ya zuio la maandamano kutoka pande zote mbili.

· Maandamano yalifanyika kwa utulivu na amani kuanzia eneo la Phillips
kupitia hoteli ya Mount Meru hadi njia panda ya Sanawari. Askari
waliyasindikiza wakati huohuo wakisihi viongozi na waandamanaji kuacha
kuandamana na kutawanyika. Ilielezwa kuwa, katika hali isiyokuwa ya
kawaida askari walitawanya maandamano ya amani kwa kutumia silaha
mbalimbali ikiwemo mabomu ya machozi, risasi baridi na moto, maji ya
kuwasha na virungu.

· Askari walifanya vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya
viongozi na waandamanaji hasa wanawake bila kujali hali zao; kwa
mfano, mbunge Lucy Owenya na Josephine Mushumbusi walipigwa na
kujeruhiwa vibaya sehemu

mbalimbali za miili yao. Viongozi wa CHADEMA na wanainchi wengi
walikamatwa na kuwekwa rumande katika kituo kikuu cha polisi kati
mjini Arusha.

· Askari waliwapiga waandishi wa habari,waliwanyang’anya vifaa vyao
vya kazi na kufuta picha na kazi walizokuwa wanazifanya kwenye
maandamano. Askari na waandamanaji walisababisha uharibifu wa magari
na mali za umma na wanainchi. Aidha walisababisha upotevu wa mali za
wanaichi zikiwemo simu mbili za mkononi za Mheshimiwa mbunge wa viti
maalumu Lucy Owenya na fedha tasilimu shilingi milioni mbili na laki
saba (TZSH.2,700,000/=) za majeruhi Ally John Ogaga walizodai
kunyang’anywa na askari, wakati Ofisi ya CCM Mkoa wa Arusha ilivunjwa
vioo kwa mawe na waandamanaji na nyumba ya mwanainchi bwana Salum Ally
iliungua kwa moto uliosababishwa na mlipuko wa bomu lililoruka kutoka
kwenye gari la polisi.



· Mkutano wahadhara ulifanyika na viongozi walitoa hotuba kwa
wanainchi.Wakati wa mkutano askari walishambulia wanainchi kwa kutumia
mabomu ya machozi.Wakati wa hotuba viongozi wa CHADEMA walitoa maneno
ya uchochezi yaliyowashawishi wanainchi kuelekea kituo cha polisi
kuwatoa viongozi waliokuwa wakishikiliwa na polisi.Hii ilisababisha
vurugu kubwa iliyopelekea watu watatu(3) kupoteza maisha, ishirini na
mbili(22) kuumia na kulazwa hospitalini,watatu (3)waliumia wakatibiwa
bila kulazwa na wengine wengi kujeruhiwa wakiwemo polisi.

· Madaktari wlithibitisha kuwa chanzo cha vifo na majeraha
vilisababishwa na risasi za moto na vipigo.Ujumbe wa Tume ulielezwa
kuwa huduma za kisheria, dhamana,matibabu na faragha havikutolewa
wakati muafaka kama Sheria inavyotaka, Kwenye kituo cha polisi askari
walitumia lugha chafu, matusi na kejeli ambavyo viliwadhalilisha na
kuwaumiza watuhumiwa kisaikolojia.

· Ujumbe wa Tume ulielezwa kuwa kulikuwa na msongamano mkubwa wa
mahabusu waliowekwa kwenye chumba kidogo kwa muda mrefu kwenye kituo
cha polisi bila kufanyika jitihada za haraka kuwahamishia walioumia
kupelekwa hospitalini na wengine katika vituo vingine vya polisi
vyenye nafasi.

· Askari walituimia ‘nguvu za ziada’ zisizokuwa na ulazima kuzuia
maandamano ya amani bila kuweka bayana sababu za msingi kuthibitisha
matumizi hayo. Kitendo hiki kilipelekea uvunjwaji wa haki za binadamu
kwa kiwango cha hali ya juu, kitu ambacho hakiwezi kuvumiliwa mbele ya
macho ya jamii na kuachwa kiendelee. Ni lazima hatua madhubuti
zichukuliwe kukomesha hali hii.
· Pande zote zinabeba lawama kufuatia tukio hili, ni ukweli
usiopingika kuwa polisi wanabeba lawama kubwa zaidi kwa kusababisha
mauaji, majeraha na vurugu kwa kuzuia maandamano halali ya amani
kinyume cha sheria. Viongozi wa CHADEMA kwa upande wao wanalaumiwa
kushindwa kuwa wavumilivu na kuwashawishi wafuasi wao kutoandamana ili
hali kulikuwa na zuio. Aidha kitendo cha kutumia maneno ya uchochezi
kuhamasisha wananchi kwenda kituo cha polisi kuwatoa viongozi wao na
wananchi waliokamatwa ni kinyume cha Sheria.
5.0 MAJUMUISHO:
Katika tukio hili askari walitumia nguvu nyingi kupita kiasi baada ya
kupata maelekezo kutoka kwa viongozi wao wa ngazi za juu kwa madai
mepesi ya sababu za ‘ki intelijensia’,badala ya kupima na kufanya kazi
kwa kufuata Sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza maadili ya kazi
zao.Amri zilitawala zaidi ya weledi katika kufanya maamuzi.

Maamuzi ya mkuu wa jeshi la polisi (IGP) ambaye hana mamlaka ya moja
kwa moja katika eneo husika kama sheria inavyotaka hayakuwa halali,
pia hakuwa na uhalali kuingilia na kutoa tamko katika ngazi ile na kwa
wakati mfupi hivyo wakati mwenye mamlaka na eneo husika alikuepo na
hakuzuia maandamano.Ujumbe wa Tume uliridhika kuwa hakukua na sababu
za msingi za kuzuia maandamano, sababu za kuzuia

maandamano kwa kigezo cha ‘intelijensia’ hazikutumika vizuri na
hazikupata nguvu za kuhalalisha (vague, speculative) zuio la
maandamano ya amani.

Kwa upande wa CHADEMA, viongozi waligubikwa na ukaidi na jazba. Utashi
wa uongozi na dira ya uvumilivu havikuzingatiwa wala kupewa nafasi
hasa pale walipotoa maelekezo kwa wafuasi wao kwenda kituo cha polisi
kuwatoa viongozi wao waliowekwa ndani. Kwa mtazamo wa haki za Binadamu
tunaamini maandamano sio njia pekee ya kuleta suluhu katika jamii pale
kunapotokea kutoelewana kwa pande mbili au zaidi.Njia za kidiplomasia
kama vile majadiliano ya pamoja zimeonekana kuwa na nguvu kubwa kuleta
suluhu kwa pande zilizotofautiana bila kusababisha madhara kwa jamii.

Umasikini, ukosefu wa ajira na upatikanaji wa huduma za kijamii (maji,
elimu na afya), tofauti za hali ya kipato, ubinafsi na udikteta,
matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na uvivu vimejenga chuki na hasira
miongoni mwa jamii. Ubadhirifu wa rasilimali za nchi kwa manufaa ya
wachache, ni tatizo linaloshamiri na kutishia amani ya nchi.

Ufahamu na, uelewa wa viongozi na jamii kuhusu haki za msingi za
binadamu pamoja na wajibu unaoendana nao, bado ni changamoto kubwa.
Dhana ya polisi jamii inadhoofishwa kutokana na vitendo vya mabavu na
ukatili vinavyofanywa na vyombo vya kutekeleza sheria hususani jeshi
la polisi. Lawama hizi hazikwepeki kwa wananchi ambao nao hawazingatii
wajibu walio nao mbele sheria.

Ukomavu na utashi wa vyama vya siasa bado ni changamoto katika jamii
zetu kutokana na mazingira ya mfumo wa chama kimoja, Visasi na chuki
vinaonekana kushamiri katika harakati mbali mbali za kudai haki. Hali
hii isiporekebishwa itahatarisha amani na utulivu uliojengeka kwa
miaka mingi. Hatima yake ni uvunjifu wa amani na mara zote
anaeathirika ni mwananchi wa kawaida.
Ni vizuri Jeshi la Polisi likaelewa kuwa nchi hii ni ya demokrasia ya
vyama vingi, na pale chama kimoja kinapohitilafiana na chama kingine,
kazi yao kubwa ni ile ya kulinda amani na sio kufanya vitendo
vinavyoonyesha hisia kuwa wanapendelea chama fulani.

Jeshi kama ilivyo serikali na wananchi ni vema wakubali dhana ya
‘kukosolewa na kuwajibishwa’ tena kwa mtazamo chanya. Dhana hii ina
nia ya kujitafakari, kujitambua na hatimaye kuchukua hatua madhubuti
za kujirekebisha na kuboresha demokrasia na utawala wa sheria.
6.0 MAONI YA BAADHI YA WANANCHI KUHUSU MAANDAMANO
Kwa kuwa vurugu za Arusha zilitokana na maandamano, Tume inaona ni
vema kukumbuka maoni ya watu mbalimbali kuhusu maandamano kwa
ujumla.Mhadhiri mmoja mwathirika wa migomo ya wanafunzi na wahadhiri
katika chuo kikuu cha Dodoma alibainisha maoni yake na, tunapenda
kumnukuu;

“Tabia inayojengeka na kuendekezwa na serikali kukumbatia na kuagiza
jeshi la polisi kutuliza hali si dalili nzuri kamwe, na ninasisitiza
tabia hii ikome kwani haina mwisho mzuri. Kwa kawaida mwanadamu
huchukua uamuzi wa kuandamana pale inapothibitika njia nyingine zote
za muafaka zimeshindikana. Jukumu la askari katika hali hii ni lile la
kulinda na kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa na si vinginevyo”

Tanzania kama nchi nyingine duniani bado inakabiliwa na changamoto za
kimageuzi,utandawazi umeifanya dunia kuwa kama kijiji,wananhi wetu
wanaona na kushuhudia yanayotendeka kila siku duniani kote,na wameanza
kuwa na uelewa mkubwa wa maswala ya demokrasia na haki za
binadamu,hivyo ni vizuri serikali kusoma alama za nyakati ili
kujipanga ipasavyo kukabiliana na hali hii badala ya kutumia amri na
vitisho kutatua migogoro ya maandamano. Pamoja na changamoto nyingi za
kiuchumi na kijamii ni vema kuweka vizuri misingi ya utawala bora na
uwazi katika utekelezaji wa majukumu mbali mbali katika utendaji wa
shughuli za umma.



Wengine waliotoa maoni ni Askofu mkuu wa jimbo kuu la Dar Es Salaam,
Mwadhama Kardinal Polycarp Pengo ambaye alisema, “Kitendo cha watu
kutegemea nguvu ya silaha wakifikiri kwamba njia hiyo ndiyo italeta
amani au wataweza kuleta ushindi wao. Huko ni kujidanganya na
kumtukana Mungu, kwa vile hayo ni maandalizi ya

maafa makubwa kwa ajili ya taifa la Tanzania’. Aliongeza kusema,
‘Mwenyezi atuepushe na laana hiyo’. Gazeti Majira.

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha,
katika mkutano na waandishi wa habari alisema “government intends to a
lasting solution to the political unrest in Arusha region between
wrangling CCM and, Chadema parties”. Aliendelea kusema, ‘ Since this
dispute is of a political nature, the government will take all
necessary measures to bring the disputing parties together such that
they sit on one table and, resolve their differences by having a
reconcillition team”.

Msajili wa vyama vya siasa bwana John Tendwa alinukuliwa kwenye gazeti
la Daily News akisema, “Chadema were initially allowed to stage a demo
and, hold a public rally, but the decision was reversed on Tuesday. A
letter to that effect was written to Chadema secretary and, on Tuesday
evening Inspector General of Police Saidi Mwema appeared on national
TV announcing cancellation of the demo”.
Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba aliwaeleza wanahabari kuwa
“his party was saddened by what happened to Chadema supporters and,
the people following police’s efforts to scatter their demonstration”,
aliendelea kusema, “Such acts by police makes us even stronger and,
bold us to continue fighting for our democratic rights and, we would
like to assure Chadema supporters and, people of Arusha that we will
always support them”.
7.0 MAONI NA MAPENDEKEZO YA TUME

· Tume imeona kuwa, kitendo cha polisi kuzuia maandamano ya amani na
halali ilikuwa ni uvunjwaji wa haki za Binadamu na ukiukwaji wa
Mikataba ya Kimataifa, Kikanda na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania.Pia ilikuwa ni kinyume na Sheria, Kanuni na taratibu
mbalimbali za nchi.Ukiukwaji huo ulipelekea maafa makubwa ikiwemo vifo
vya watu watatu (3) na wengine wengi kujeruhiwa, uharibifu wa mali na
wananhi kukosa imani na polisi (serikali).Hivyo ni vema serikali
kuchukua hatua stahiki kwa waliohusika na

mauaji na uharibifu wa mali ili haki itendeke na wananchi kurudisha
imani kwa serikali yao.




· Ni vema kushirikiana na vyombo vinavyohusika na kurekebisha sheria
kupitia na kurekebisha sheria kandamizi na zinazokinzana ili kuondoa
migongano katika sheria hizo.

· Kuelimisha jamii, viongozi, wadau na wataalam mbalimbali, kuheshimu
maamuzi na mitazamo mbali mbali ya kisiasa, kiitikadi, kidini na
kitamaduni kwa utashi, kuvumiliana na kuheshimiana. Kuna haja ya
kuweka mikakati mahususi ya kuhakikisha kuwa jamii inaufahamu wa kina
wa Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania, elimu ya Haki za
Binadamu, sheria za nchi, na mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa nchini
inaeleweka na kuzingatiwa, kuheshimiwa, kulindwa na kutekelezwa.

· Serikali iangalie kwa undani kero za watumishi wa umma hasa jeshi la
polisi ambalo limegubikwa na changamoto nyingi za kiutendaji na
kimaadili ikiwemo rushwa ili kuboresha hali za kimaisha kwa askari na
kufuata maadili ya kazi zao.



· Kuandamana ni haki ya kikatiba na Katiba ya nchi inatamka wazi kuwa
Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamii (civilian). Kama nchi
inayozingatia demokrasia serikali haipaswi kuzuia haki ya kuandamana
bali kuhakikisha haki hii inatekelezwa bila kuathiri amani na utulivu
wa nchi.

· Kwamba, kazi kubwa ya jeshi la polisi ni kulinda usalama wa raia na
mali zao, hakuna namna jeshi hili litatimiza malengo haya bila
ushirikishwaji wa wananchi, kwani makundi haya yanategemeana. Hivyo ni
vema serikali kuhakikisha inatimiza wajibu wa kuheshimu, kulinda na
kutekeleza haki za wananchi ili wananchi nao wawajibike kuheshimu,
kutii na kutekeleza sheria za nchi.Hii

itajenga uhusiano mwema baina ya polisi(serikali) na wananchi na
kupunguza uhasama na chuki iliyojengeka kati ya makundi haya.




8.0 VIAMBATANISHO:

Kiambatanisho Na. I: Maelezo kutoka kwa wadau mbalimbali

Kiambatanisho Na. II: Orodha ya Majina ya wadau na sehemu
zilizotembelewa Kiambatanisho Na. III: Barua zilizotumika kufanya
mawasiliano ya tukio kutoka CHADEMA
Kiambatanisho Na. IV: CD mbili (2) zinazoonyesha baadhi ya picha na
video za tukio kutoka CHADEMA


Mhe. Jaji (Mstaafu) Amiri Ramadhani Manento
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora

Machi 1, 2011
 
Back
Top Bottom