Richmond; Tumejenga nyumba mchangani


Josh Michael

Josh Michael

JF-Expert Member
Joined
Jun 12, 2009
Messages
2,525
Likes
8
Points
135
Josh Michael

Josh Michael

JF-Expert Member
Joined Jun 12, 2009
2,525 8 135
NIANZE makala hii kwa kukiri udhaifu wangu binafsi kwamba, wiki iliyopita nilishindwa kuandika chochote katika safu hii si kwa sababu ya kutingwa au kwa kile ambacho tumekuwa tukikiita kila mara; ‘sababu zilizo nje ya uwezo wangu’ bali mshtuko nilioupata kutokana na kile kilichotokea ndani ya Bunge wiki mbili zilizopita.
Niandike mapema kwamba, mshtuko nilioupata kutokana na Bunge kutangaza rasmi kuufunga mjadala wa Richmond na kuiacha serikali ikikamilisha utekelezaji wa maazimio yote 23 haufanani hata kidogo na kwa namna yoyote ile na ule uliowakuta wanaharakati walio ndani ya vyumba vya habari, kwenye vyama vya siasa na katika taasisi za kijamii, ambao kwa takriban miaka mitatu sasa waliwekeza fikra zao katika hoja hiyo ambayo hakuna shaka imeitikisa serikali ya awamu ya nne.
Ni jambo dhahiri kwamba, kashfa ya Richmond itabakia kuwa moja ya matukio makubwa ya kisiasa hapa nchini kutokana na ukweli kwamba, matokeo yake kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hili yalisababisha Waziri Mkuu na mawaziri wengine wawili wajiuzulu na kumlazimisha rais kuvunja Baraza la Mawaziri na kuliunda upya.
Mwangwi wa anguko hilo la serikali la Februari mwaka 2008 lililomuacha rais akiwa kiongozi pekee wa kisiasa katika ngazi ya taifa aliyekuwa amebakia madarakani, ndiyo ambao hatimaye ulihitimishwa kwa kishindo kikubwa na tamko la Spika Samuel Sitta la kuufunga rasmi mjadala wa Richmond ndani ya Bunge.
Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, wakati Sitta akitangaza uamuzi huo ambao hakuna shaka ulitokana na sababu zile zile zilizokuwa nyuma ya kuanzishwa na kukuzwa kwa kashfa hiyo, majeraha ya kitaifa yaliyotokana na kashfa hiyo yalikuwa yangali yakiutesa umma wa Watanzania na kwa uhakika yangalipo.
Leo hii wiki mbili tangu suala hilo litangazwe kufungwa ndani ya Bunge, hoja zinazozingira uamuzi huo wa Bunge kuufunga mjadala huo zingali zikilizonga taifa kwa namna ambayo imesababisha spika mwenyewe na kundi moja la wabunge ambalo kwa kiwango kikubwa lilijijengea uhalali mkubwa nyuma ya ajenda hiyo, wajikute wakilazimika kutoa kauli za kujisafisha na kujitakasa ili kukwepa kile kinachoonekana kuwa ni hasira ya wananchi dhidi yao.
Wakati Spika Sitta akiwaongoza wabunge wa kundi la watu waliojipambanua kuwa makamanda wa vita dhidi ya ufisadi wa kariba ya Fred Mpendazoe na James Lembeli kujitetea na kuonyesha kauli za kuendeleza mapambano, ni wazi kwamba wanafanya hivyo leo baada ya wao wenyewe kusoma alama za nyakati na kubaini kwamba, ile taswira ya ushujaa waliyojijengea katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita imeanza kwa kiwango kikubwa kutiliwa shaka na kuwekwa katika mizani.
Hata hivyo, wakati akina Sitta wakionekana kufanya kila linalowezekana kupambana na dhambi ya usaliti dhidi ya mashabiki wao waliokuwa wamesambaa ndani ya vyumba vya habari, bungeni, serikalini na katika jamii ya wananchi wa kawaida, maadui zao kisiasa hususan wale walio ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaonekana kidogo kidogo wakianza kushangilia ushindi kimya kimya na wakati huo huo wakipanga mikakati mingine zaidi ya kujiimarisha.
Hali ya mambo nje ya CCM na nje ya kundi la makamanda wa ufisadi na maswahiba wao, hali inaonekana kuwa ni yenye kuleta mikanganyiko mingi, baada ya makundi tofauti ya watu kuonekana yakiwa na majibu tofauti kuhusu sababu hasa zilizosababisha Bunge lilazimike kuufunga mjadala huo.
Pamoja na ukweli kwamba maswali yanaonekana kuwa ni mengi kuliko majibu katika vichwa vya watu wa makundi hayo mengine mawili, bado jambo moja kubwa linaonekana kuwaunganisha takriban wale wote ambao kwa namna moja au nyingine wamekerwa au kuumizwa na uamuzi wa Bunge kuufunga mjadala huo ambao katika kipindi kirefu uliwajengea baadhi ya watu uhalali mkubwa katika jamii.
Kwa hakika jambo hilo si jingine bali shinikizo lisilohitaji mjadala ambalo linamtaka kila kiongozi anayetokana na CCM kwa nafasi yake kuhakikisha anashiriki kikamilifu katika kukijengea mazingira bora ya ushindi chama chake chini ya mwavuli wa urithi wa umoja na mshikamano, hususan wakati huu taifa linapojiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Hauhitaji kuwa na akili nyingi kubaini kwamba, ni shinikizo hili la shuruti, ndilo ambalo hatimaye lilisababisha Sitta na kundi lake wasalimu amri na kimsingi ndilo ambalo liliilazimisha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iunde kamati ya maridhiano inayoundwa na watu watatu ikiongozwa na Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.
Kikubwa kinachosikitisha katika hili ni ukweli wa wazi kwamba, wakati Sitta na kundi lake wakibeba lawama za usaliti kutoka kwa maswahiba na maadui zao, kundi kubwa la Watanzania linaonekana kushindwa kutambua nini hasa kilikuwa nyuma ya ajenda nzima ya Richmond ndani ya Bunge kabla na baada ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe.
Ni jambo la kufedhehesha sana kwamba, miongoni mwa wanahabari na wanaharakati ambao leo hii wanaonekana kuwanyoshea vidole makamanda wa ufisadi wakiwatwisha kila aina ya sifa na majina mabaya, ndio hao hao waliotusuta baadhi yetu wakati tulipoeleza bayana tangu mwanzo kwamba, kashfa ya Richmond ilifinyangwa lengo likiwa moja la kuinusuru CCM kwa njia za kisanii kwa namna ile ile ilivyofanyika bungeni wiki mbili zilizopita wakati spika alipotangaza kuufunga mjadala huo.
Ili kuweka rekodi sahihi nawaomba wasomaji wa safu hii niwakumbushe kuhusu kile ambacho safu hii ya Tuendako ilikiandika miaka miwili iliyopita, siku chache tu baada ya Kamati ya Mwakyembe kutoa ripoti yake bungeni chini ya kichwa cha habari kilichosema; ‘Kwa nini Edward Lowassa?; Nanukuu:
‘‘TAIFA limepita kipindi kigumu katika historia ya uhai wake unaoelekea kufikia miaka 47 tangu kupatikana kwa uhuru wetu. Kwa mara ya kwanza tumepoteza Waziri Mkuu aliyekuwa madarakani si kwa kifo kama ilivyokuwa kwa Edward Moringe Sokoine bali katika mazingira yanayohusishwa na uchafu ambao haujapata kuwekwa hadharani huko nyuma...
‘‘...Kwa namna yoyote ile, tukio la hivi karibuni la kuanguka kwa Lowassa kwa namna ile ilivyotokea ndani ya Bunge, akining’inizwa kwa namna na njia ile, lina dalili za wazi wazi kwamba, baadhi ya maswahiba wake, wenzi wake wa kundi la mtandao na/au wana CCM wenzake waliongoza harakati za kumuangusha miezi mingi kabla ya tukio lenyewe kutokea.
‘‘Leo hii, wana CCM wakiongozwa na kivuli cha baraka za Rais Kikwete, uratibu na usimamizi wa moja kwa moja na wa wazi wa Spika Sitta, jeuri ya kimamlaka ya Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Harrison Mwakyembe, munkari wa hoja za wabunge wa pande zote mbili na ushabiki wa jadi wa Kitanzania, wameanza kuvuna kile walichokuwa wakikitafuta kwa miaka miwili na ushee iliyopita. Kukirejeshea chama chao heshima bila kujali gharama za kufanya hivyo.
‘‘Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, kashfa moja tu ya Richmond ndiyo iliyoweza kutuingiza sisi wengine wote katika mtego haramu wa jitihada za kundi la wajanja lenye dhamira ya kujiokoa kutokana na makosa ya kimaamuzi waliyoyafanya wakiwa madarakani, huku likijua kuwa bado lina deni kubwa la kutufichulia mafisadi wengine walioliingiza taifa katika kashfa za ununuzi wa ndege ya rais, ununuzi wa rada na katika mikataba mibaya kuliko ya Richmond kama ile ya IPTL.
‘‘Huku tukifurahia wazi wazi matokeo ya kazi iliyofinyangwafinyangwa katika misingi ya kichochezi, wote kwa ujumla wetu tumejikuta tukibaki palepale tulipokuwa siku, miezi na mwaka mmoja na ushee kabla Kamati ya Mwakyembe haijatoa ripoti yake iliyosababisha Lowassa, Karamagi na Msabaha wajiuzulu.
‘‘Ninaweza nikadiriki kusema pasipo hofu kwamba, kwa mara nyingine tena, Watanzania tumejikuta tukilishwa ujinga na genge la wahuni ambao kwa kiasi kikubwa limechangia kuifanya nchi yetu hii iendelee kuwa masikini eti kwa sababu tu genge hilo limeamua kwa namna ya ufundi kuwatoa kafara wachache miongoni mwao.
‘‘Leo hii baada ya ripoti ya Mwakyembe kutoka, Watanzania bado tunaendelea kubakia gizani tukishindwa kubaini tena kwa uhakika Richmond ni kampuni ya nani na ni kiongozi gani hasa aliyekuwa nyuma ya mgongo wa wahuni hao ambao hatimaye waliweza kuwa washindi wa zabuni ya dola za Marekani milioni 172 ya kuzalisha umeme wa dharura na kabla Lowassa hajawa Waziri Mkuu wakashinda zabuni ya kujenga bomba la mafuta kutoka Dar hadi Mwanza ilhali wakiwa hawana kampuni.
‘‘Ni jambo gumu kuingia akilini kwamba Watanzania tumeingizwa mjini na Kamati ya Mwakyembe ambayo awali ilituaminisha kishabiki kuwa, Richmond ilikuwa kampuni iliyobebwa na ‘Bwana Mkubwa’ ambaye tafsiri yao alikuwa ni Lowassa (na si Shein, Kikwete, Mkapa au Sumaye) kabla ya kutugeuka na kutuambia kwamba yule ‘Bwana Mkubwa’ aliyewajibika hakuhusika bali alifanya hivyo kwa sababu tu ya makosa ya watu wa chini na yasiyo yake. Huu ni mzaha mbaya.
‘‘...Fedheha hii ya kiserikali imetufanya leo hii, hukumu ya Richmond ambayo kimsingi imemgusa kila mkubwa serikalini iishie kuwatoa kafara wanasiasa wachache tena huku ukijengwa ushahidi ambao kwa watu wenye akili au wale waliopata kusoma kashfa kubwa kubwa za kisiasa za kimataifa kama zile za Watergate au ile ya Clinton na Monica Lewinsky wanaweza wakashangazwa.
‘‘Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, wabunge wa upinzani nao, pasipo kujua kile kilichokuwa kikiendelea ndani ya CCM na miongoni mwa wahuni wa genge la mtandao waliokuwa wakitafuta kujitakasa kuchinjana wenyewe kwa wenyewe wameingia katika mtego wa kushangilia kung’oka kwa Lowassa huku CCM na serikali ikiendelea kubakia na kutembea kifua mbele. Hili ni tukio la bahati mbaya.
‘‘Naomba historia inihukumu katika hili nitakaloandika. Kafara ya damu ya kisiasa ya akina Lowassa, Daudi Ballali, Rostam, Karamagi, Msabaha na wenzao wengine watakaowafuata katika Kashfa ya Richmond au ile ya EPA na pengine nyingine zitakazokarabatiwa kati ya hivi sasa na mwaka 2010 ndizo zitakazojenga misingi mipya ya ushindi wa kimbunga au kishindo wa chama hicho tawala ambao kambi ya upinzani ikifanya mzaha unaweza ukawa zaidi ya ule wa mwaka 2005.
‘‘Watanzania wenzangu tuna kila sababu ya kuamini, tena kwa dhati kwamba, hulka tuliyoijenga miaka nenda miaka rudi, ya kujifanya mashabiki badala ya wadadisi wa mambo hata katika masuala mazito ya kitaifa kama hili la Richmond na EPA ndiyo itakayoendelea kututafuna na kuiacha CCM ikiendelea kubakia madarakani miaka nenda miaka rudi. Huko ndiko TUENDAKO.”
Naamini wasomaji wa safu hii watakubaliana nami kwamba, kazi iliyoanzishwa na kuhitimishwa na Sitta na genge lake kwa namna na kwa njia za kikachero pamoja na kuwatoa kafara wenzao na kulihadaa taifa zima kwamba wao walikuwa wapigania haki, ndiyo ambayo leo hii imeliacha taifa likibakia kushangaa pasipo kujua nini cha kufanya. Matokeo ya kazi hiyo haramu iliyoratibiwa na makachero akina Mwakyembe na genge lao imeficha moto wa kambi ya upinzani na kwa kiwango kikubwa imemhakikishia Kikwete na chama chake uhalali wasiostahili wa kuendelea kuliongoza taifa hili hata baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba kwa gharama za kutoaana kafara, kuchafuana, kusafishana na kuwaacha Watanzania tusiojibidiisha kufikiri na kuchukua maamuzi magumu tukiachwa njia panda. Kwa hakika tumejenga nyumba mchangani. 
Jayfour_King

Jayfour_King

JF-Expert Member
Joined
Nov 15, 2009
Messages
1,141
Likes
12
Points
0
Jayfour_King

Jayfour_King

JF-Expert Member
Joined Nov 15, 2009
1,141 12 0
Time will tell, tumechagua kuongozwa na waigizaji tuendelee kuangalia hizi movies zao.
 
Josh Michael

Josh Michael

JF-Expert Member
Joined
Jun 12, 2009
Messages
2,525
Likes
8
Points
135
Josh Michael

Josh Michael

JF-Expert Member
Joined Jun 12, 2009
2,525 8 135
Inauma sana ukiangalia Taifa linakokwenda maana watu wote wanajifanya hawahusiki kabisa na mambo haya yote
 

Forum statistics

Threads 1,251,234
Members 481,615
Posts 29,763,493