comrade igwe
JF-Expert Member
- Jan 12, 2015
- 7,295
- 3,945
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Museveni kwa pamoja wamekubaliana kutosaini mkataba wa mahusiano ya kiuchumi na kibiashara kati ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ulaya (EPA).
Makubaliano hayo yamefanyika jana Ikulu, Jijini Dar es Salaam ambapo Rais Yoweri Museveni yuko nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 25 – 26 Februari, 2017.
Akiongea na waandishi wa habari Rais Magufuli amesema kuwa mkataba wa EPA hauna faida bali ni aina nyingine ya ukoloni ambao unataka kurejeshwa kwa nchi za Afrika.
“Nimeongea na Rais Yoweri Museveni amekubali kutosaini mkataba wa EPA, nitawaagiza wataalamu waliosaidia kutupa maelezo juu ya madhara ya mkataba huo kwenda pia Uganda kuwapa maelezo ambao waliyatoa kwa Tanzania,” alifafanua Dkt. Magufuli.
Kwa upande wake, Rais Yoweri Museveni amesema kuwa ameongea na Rais Magufuli na wamekubaliana kutosaini mkataba huo na kuongeza kuwa suala la EPA ni lazima lijadiliwe na nchi zote za Afrika Mashariki ili kuwepo na msimamo wa pamoja kwa nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha Rais Museni amempongeza Rais Magufuli kwa kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya Sita, hivyo amekaribisha shirika hilo kutoa huduma za usafiri wa anga nchini Uganda kutokana na nchi hiyo kuwa na uhitaji wa huduma hiyo.
Vilevile amempongeza Rais Magufuli kwa ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway) kutoka Dar es Salaa mpaka Mwanza na Isaka mpaka Rwanda ambapo itapelekea ujenzi wa bandari kavu katika mkoa wa Mwanza hivyo wafanyabiashara wa Uganda kunufaika na bandari hiyo ambayo itakuwa karibu zaidi kuliko ilivyo kwa Dar es Salaam.
Wakati huohuo Mawaziri wa Nje kutoka Tanzania na Uganda Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Oryem Henry Okello wamesaini makubaliano ya uhusiano katika mambo ya Diplomasia baina ya nchi hizo mbili.
Museveni yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo atatembelea baadhi ya maeneo kadhaa ikiwemo kiwanda cha Juice cha mfanyabiashara Mtanzania Said Bakhressa ambaye pia amewekeza nchini Uganda.