Rafiki na adui nani anafaa katika mafanikio?

Rafiki na adui nani anafaa katika mafanikio?

Jackson94

JF-Expert Member
Joined
Sep 14, 2016
Posts
502
Reaction score
591
Habari rafiki, karibu tena katika wasaa mzuri kwenye mtandao huu wa Falsafa za Mafanikio. Leo tunaenda kujifunza mtu muhimu katika mafanikio kati ya rafiki na adui. Bila shaka umeshaanza kupata picha na una majibu tayari kichwani kwako lakini naomba uungane nami ili nipate kukushirikisha kitu kizuri ili uweze kujifunza Falsafa nzuri katika Mafanikio yako.

Rafiki ni mtu wa karibu ambae huwa unashirikiana nae katika mambo mbali mbali kuhusiana na maisha na hali zingine kwa vyovyote vile. Rafiki yupo tayari kukusaidia ufanikiwe. Pia yupo tayari usiwe mbali nae kwani mu wamoja! Cha zaidi hata fikra zenu zaweza kuwa sawa ndio maana ni marafiki. Aidha adui ni mtu ambae ni mpinzani katika Nyanja zako za maisha, hayuko tayari kukuona wewe unafanikiwa katika maisha yako. Nia yake wewe ushindwe na yeye afanikiwe katika azima yake.



Swali linakuja ili ufanikiwe je, unamuhitaji nani? Je, unaukumbuka msemo wa Profesa Jay ‘Nahitaji marafiki ili nifanikiwe, lakini nahitaji maadui ili nifanikiwe zaidi’?

Msemo huu una maana kubwa sana, kumbuka nimekwambia mtu ili awe rafiki yako kwa kiasi Fulani lazima muwe mnalingana mitazamo. Sasa wakati ukifika wewe ukawa na mtazamo tofauti na yeye tayari mtaanza kuwa na ukinzani kati yenu, wewe utaanza kuwa msaliti huenda umekataa ushauri wake ambao kiuhalisia hauna faida kwako, hivyo huyo rafiki ataanza taratibu kuwa adui na atakupinga vikali. Usikate tama kwani wanaofanikiwa hawafanyi mambo yanayofanana na wengine bali mambo yao huwa ya kipekee. Ukifanya mambo ya kawaida nawe unakuwa wa kawaida.

Rafiki hatakupa changamoto ambazo ndio mtaji wa mafanikio kwani mtakuwa nae katika hatua moja inayofanana nae hivyo huna jipya kwake ila adui atakupa changamoto ambazo zitakufanya kuwa mshindi endapo utazitatua na siku moja atakupongeza adui huyo huyo, wala usiweke kinyongo nae songa mbele mpaka kieleweke.

Rafiki atakupaka mafuta tu pale unapokosea lakini hatakupa njia sahihi ya kurekebisha makosa yako. Adui yeye atakupa njia ya kurekebisha mahali ulipokosea na hatimae utafanikiwa katika mipango yako. Mfano kama wewe ni mtumiaji mzuri wa mitandao ya kijamii na una smartphone nazani unaijua playstore ambako huwa zinapatikana software ambazo unatumia, huko kabla au baada ya kupakua izo software huwa wanaomba uwape mrejesho juu ya hizo software (kui-rate) sasa hapa kuna watu huwa wanatoa hata matusi juu ya hizo software, je, ulishawahi kuona wamezitoa hizo software? Bila shaka ni hapana, kwa nini? Jibu ni kwamba huwa wanafanyia kazi mambo hayo ambayo wateja wao au watumiaji wamerejesha na hatimae kuboresha huduma ndio maana unaona kuna matoleo mengi mengi ambayo kila toleo jipya ni zuri zaidi. Jifunze kitu hapo, laiti wale watoa matusi wasingekuwepo software zingekuwa mbaya lakini huwa zinakuwa bora zaidi kutokana na mchango wa adui asie na staha.

Hivyo basi rafiki yangu hii ni moja ya Falsafa ambayo unatakiwa kuijua katika maisha yako ya Mafanikio unayotaka kuishi. Ili ufanikiwe unahitaji zaidi adui ambae atakusaidia kukupa changamoto ambazo ni mtaji katika mafanikio. Aidha usiogope changamoto au kukosolewa katika maisha kwa kazi uzifanyazo kwani hapo ndipo utakapopata maarifa ya jinsi ya kuwa bora na hatimae watakupongeza ukifanikiwa badala ya kukushambulia kwa maneno mabaya kama walivyokuwa wakifanya kabla.

Karibu tuendelee kujifunza Falsafa za Mafanikio na pia kama umeipenda makala hii wasambazie na marafiki zako nao wapate maarifa haya.

Ni mimi rafiki na Mwana Falsafa za Mafanikio,
Jackson94
 
Back
Top Bottom