R.O.M.A MKATOLIKI

Oct 5, 2015
88
476
R.O.M.A MKATOLIKI, ALIVYOZAMISHWA NA KUIBUKIA ZIMBABWE.

Mtu mmoja, mtaalamu wa elimu ya fizikia, Hisabati na elimu ya anga, Bw. Archimedes wa Syracuse aliyeishi kati ya mwaka 287 - 212 Kabla ya Kristu, aliwahi kutoa kanuni aliyoiita kanuni ya Archimedes (Archimedes' principle) akielezea namna chombo kinavyoweza kuelea juu ya uso wa maji, na yanayotokea hadi chombo hiko kiweze kuelea. Kwa lugha rahisi kanuni ya Archimedes' inasema; "chombo chochote kinapozamishwa chote au kwa sehemu fulani, chini ya maji/kimiminika tulivu, kuna nguvu inayokisukuma kitu hiko juu, nguvu hiyo inakuwa kubwa zaidi katikati ya uzito wa hiko chombo...."

Mfano wa maelezo ya kanuni hii; unapoweka mpira wa soka juu ya maji yaliyotulia, mpira utaelea, kwa kuwa kuna nguvu inayosukuma mpira huo juu, na nguvu hiyo ni kubwa zaidi katikati ya uso wa mpira. Mathalani, mpira huo ukizamishwa, bado nguvu ile ipo, na ikiwa nguvu ya kuuzamisha mpira itaondolewa, mpira utarudi juu ya uso wa maji. Na kwa hiyo, ili mpira uendelee kuzama, lazima nguvu ya kuuzamisha iendelee kuwapo. La sivyo mpira utaibuka na kuendelea kuelea.

Falsafa hiyo, ya 'The Floating balloon' ndio falsafa inayotumika kuelezea upinzani wa kiitikadi. Tangu kale jamii imekuwa na watu wanaopinga itikadi za kiutawala. Kuna misukumo kadhaa inayopelekea kuwepo kwa upinzani, ingawa sababu kubwa na rahisi kuelezea ni kwamba binadamu hawawezi kamwe kufikiri sawasawa, tofauti za kifikra ni tunda la asili, tamu kwa watu werevu, lakini chungu kwa wajinga.

Misukumo mingine ya kuwapo kwa fikra kinzani, zinazozaa upinzani wa kiitikadi, siasa nk, ni hamu ya kutaka kuongoza au kutawala kwa kuwa labda mtawala hawezi, au anaonekana kutoweza, au utawala uliopo unakiuka miiko iliyowekwa na jamii husika. Misukumo mingine inaweza kutokana na tamaa za kutawala kwa lengo la kufaidi tunu za jamii. Misukumo hiyo wanaweza kuwa nayo watawala, na ikiwa hivyo basi watawala hufanya matendo yanayopelekea upinzani kuongezeka.
Ndio vile, unapogandamiza mpira chini ya maji, nguvu ya kuurudisha juu inaongezeka. Kadiri unavyoongeza nguvu ya kuuzamisha, ndivyo nguvu ya mpira kurudishwa juu inavyoongezeka. Tofauti ya nguvu hizo mbili ni kwamba, ile ya kuuzamisha mpira chini, mara zote ni ya kutengeneza, lakini nguvu ya kurudisha mpira juu ya uso wa maji ni nguvu za asili. Fikra kinzani ni jambo la asili.

Ndio maana, kwa kutambua hili, R.O.M.A MKATOLIKI katika wimbo wake wa Zimbabwe, mwishoni mwa shairi la kwanza anawaambia walengwa wake; "kutekana tekana huu ni uhuni wa kishamba, weka bunduki chini si tushindane kwa hoja".

Kwa kuwa kutekwa kwa R.O.M.A MKATOLIKI kunahusishwa na msimamo wake wa kupinga watawala, na kwa kuwa watawala hawajatoa taarifa zozote zinazoshawishi kutokuhusika na uhuni huo, basi jamii inabaki na imani thabiti kwamba watawala walihusika. Na kama hivyo ndivyo basi falsafa ya mpira unaolea, inakubali hasa.
Kwamba, nguvu ilitumika kutaka kumzamisha R.O.M.A MKATOLIKI ili asionekane, lakini baada ya nguvu hiyo kuondoka, R.O.M.A MKATOLIKI anaibuka. Na ieleweke wazi, kwamba nguvu inayomuibua R.O.M.A ni ya asili. Wakati ile ya kumzamisha ni ya kuazima. Pia, si kila mtu anayeonekana kuwa mpizani ni mpinzani. Mfano halisi upo kwa madiwani wa Chadema wa Kaskazini wanaodaiwa kupokea pesa ili kuhama chama na kusaliti itikadi ya mabadiliko, hao ni cowards, wanaoingia kwenye siasa kwa ajili ya kipato, wakishapata kipato wanayasahau mahubiri yote waliotangaza kwenye mimbari ya siasa.

Lakini alichoonesha R.O.M.A ni ile nguvu ya asili ya kuonesha fikra kinzani, halisi na za asili dhidi ya mambo yasiyompendeza.

FUNZO.
Kuna jitihada za makusudi za kutaka kudhulumu utu wa mtu mwenye mawazo kinzani dhidi ya utawala wa Tanzania. Serikali kupitia jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola imehusishwa moja kwa moja na vitendo hivi ambavyo R.O.M.A anaviita uhuni wa kishamba. Rafiki na kamarade Ben-Rabiu WaSaanane hajulikani alipo hadi leo. Ile nguvu ya kukandamiza mpira chini ya maji, imeendelea kudumu katika suala la Ben Saanane, lakini kwa kuwa ni nguvu ya kuazima haiwezi kukandamiza milele yote. Akina Ben wataendelea kuwapo vizazi na vizazi. Na huo ni ujumbe wa kweli unawatia jazba, na aibu wanaofanya 'uhuni wa kishamba'. Kwamba, watahitaji nguvu hizo milele yote, kwa maana ingine, watakosa kufanya mambo mengine ya msingi kwa kuelekeza nguvu kubwa dhidi ya fikra kinzani, ambazo haziishi, hazichoki, hazina 'expire date'.
"Ni mtu mdogo tu wa kichwa anayedhani bunduki ya mwanadamu inaweza kubadili ubongo wa Mungu. Mungu wa Paulo, Mungu wa Daudi, ndio huyo Mungu wa John wanaomuita Yohane wayahudi.

MWISHO.
R.O.M.A MKATOLIKI, namfananisha na mpira uliozamishwa lakini nguvu ya kuuzamisha ikashindwa na nguvu ya asili, ambayo R.O.M.A ameibatiza na kuiita nguvu ya umma kama anavyoimba,

"Nimechapwa mijeredi, nimevunjwa bila huruma, asante mliopaza sauti nimeiona NGUVU YA UMMA".

Nguvu ya Umma aliyoiona R.O.M.A ndio hiyo hiyo iliyomfanya aimbe kwa namna ya kufunguka kwa kile kilichomsibu, ni nguvu inayojidhihirisha kwa namna tofauti tofauti. Kwa kuimba, kwa kukemea majukwaani, kwa kuandika na wakati mwingine kwa uasi. Ndio, uasi! Sio mara zote waasi ni watu waovu, uasi dhidi ya uasi ni wema unatukuka machoni kwa Mungu. isipokuwa, maana halisi ya uasi inaweza kupotoshwa. Wapo waasi wanoishi ikulu, kuamuru majeshi na taasisi za kiserikali, nao wanastahili adhabu ileile wanayostahili waasi wengine. Lakini nirudie, tafsiri ya uasi inaweza kupotoshwa.

Tuendelee, kunakili vipande vya mashairi ya R.O.M.A MKATOLIKI huku tukijiuliza kama tunafanana na falsafa ya mpira wa soka juu ya maji, au pengine nguvu kidogo inahitajika kututoboa na kutuzamisha kusipo na jua, ambapo hujui hii saa nne au saa nane?
Nawakumbusha pia, mtakao comment kwenye makala hii; R.O.M.A anawaambia; Kunijadili mtanzania, kuwa makini pia, Makinikia...."
 
KAMA ASIPOTAJA WAZIWAZI WALIOMTEKA KAMA ALIVYOKUWA ANAFANYA ZAMANI KWENYE NYIMBO ZAKE,BASI NACHUKULIA KAMA MUOGA TU HIVI SASA KESHAKUWA MPOLE UANAHARAKATI UMEFICHWA KWA KIGEZO CHA FASIHI.
 
Back
Top Bottom