Pinda akanusha hoja ya Mbowe
Imeandikwa na Basil Msongo, Dodoma; Tarehe: 14th April 2011 @ 11:39 Imesomwa na watu: 156; Jumla ya maoni: 0
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amelieleza Bunge kuwa hakuna sababu kwa wananchi kuwa na hofu kuhusu maendeleo ya ukusanyaji maoni kuhusu muswada wa sheria itakayosimamia muswada wa mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.
Pinda amewaeleza wabunge mjini Dodoma kuwa, yeye haoni kama kuna hofu na akahoji hofu ya nini?
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, kinachoendelea sasa ni ukusanyaji wa maoni kwamba ni namna gani tutaendelaea na mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Pinda ameyasema hayo wakati anajibu maswali ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ambaye pamoja na mambo mengine alimuuliza Waziri Mkuu kwamba ni kwa nini asitangaze kusitisha mchakato wa muswada uliowasilishwa bungeni wa sheria itakayotumika kusimamia mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Wakati anauliza swali, Mbowe alisema, wananchi wana hofu kubwa kuhusu muswada huo na kwa kuzingatia waliyosema wadau, Wazanzibari na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Serikali haioni kuwa ni busara kukubaliana na utashi wa wananchi kutoa tamko la kuusitisha mchakato unaoendelea.
Pinda amemjibu kwamba, kwa sasa jambo hilo lipo katika ofisi ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, hivyo anasubiri ushauri wake ili serikali itoe uamuzi.
Makinda amekiri kuwa suala hilo lipo kwenye ofisi yake na ana wataalamu.
Waziri Mkuu amesema, hawezi kuupuuza ushauri wa Spika wa Bunge kuhusu suala hilo na akifanya hivyo wananchi watamshangaa.
Kwa hiyo mwenzangu Mbowe mbona una haraka, we poa tu amesema Pinda wakati anajibu maswali ya Mbowe kwenye kipindi cha maswali ya papo hapo kwa Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa Pinda, muswada huo uliwasilishwa bungeni kwa utaratibu wa hati ya dharura na kwamba, kinachoendelea ni utaratibu ndani ya Bunge.
Kwa mujibu wa Pinda, Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ilikusanya maoni hya wananchi kuhusu muswada huo, imeshawasilisha taarifa yake kwa Spika wa Bunge.
Amewaeleza wabunge kuwa, Spika akiona inafaa atashauriana na Serikali kwa kuzingatia yaliyotokea wakati wa ukusanyaji maoni kulingana na uzito wa jambo lenyewe.
Pinda amesema, hadi sasa hana taarifa yoyote kuhusu maendeleo ya suala hilo na kwamba Serikali ilikuwa na nia njema kuwasilisha muswada huo ili taifa lisonge mbele katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Serikali imetoa kauli hiyo ikiwa imebaki siku moja kabla ya wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuandamana katika mikoa 10 ya Tanzania bara kukusanya maoni ya wananchi kuhusu muswada huo.
Chadema hawataki mchakato wa muswada huo uendelee kwa madai kuwa unahitajika muda wa kutosha na hakuna sababu ya kuuharakisha.
source:
HabariLeo | Pinda akanusha hoja ya Mbowe
Makinda: Sikumzuia Zitto kuuliza swali
Imeandikwa na Basil Msongo, Dodoma; Tarehe: 14th April 2011 @ 12:21 Imesomwa na watu: 88; Jumla ya maoni: 0
SPIKA wa Bunge Anne Makinda, amesema, hakumzuia Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto, kumuuliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, swali la nyongeza ila alizingatia hoja ya kiongozi huyo wa shughuli za Serikali bungeni.
Makinda ametoa msimamo huo wakati anamjibu Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, aliyetaka mwongozo wa Spika kuhusu uamuzi huo wa Spika wakati wabunge wanamuuliza Waziri Mkuu maswali ya papo hapo.
Lissu alimuuliza Makinda kama uamuzi wake ulizingatia sheria na kanuni za Bunge zinazohusu maswali ya papo hapo kwa Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa Makinda, hakumzuia Zitto kuuliza swali ila alizingatia hoja ya Waziri Mkuu kuwa hana taarifa kuhusu ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwa hakupata uthibitisho wa matumizi ya sh bilioni 48 kati y ash. Trilioni 1.7 zilizotolewa kwa ajili ya kuhuisha uchumi.
Zitto amesema, fedha hizo zilitengwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2009/10.
Baada ya Makinda kumjibu Zitto, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, aliomba mwongozo wa Spika na kuhoji kwa nini yeye hakupata fursa ya kumuuliza swali Pinda lakini Zitto aliuliza wakati katika orodha ya wabunge, jina lake lilikuwa namba nane, na Mbunge huyo Ubungo, John Mnyima alikuwa takribani namba 16.
Makinda alimjibu Lema kuwa, anapokuwa kwenye kiti cha Spika anatazama wanaouliza maswali na wanaojibu na haongozi Bunge kama mtu aliyezibwa na kitambaa usoni.
Spika amesema, anazingatia jinsi, vyama, vijana, na maeneo wakati anawaruhusu wabunge wamuulize maswali Waziri Mkuu na kwamba, maamuzi anayoyafanya ndiyo maana ya kiti cha Spika wa Bunge.
source:
HabariLeo | Makinda: Sikumzuia Zitto kuuliza swali