Namtetea Profesa Joseph Mbele
Niliona humu ukumbini yametundikwa mawazo ya Profesa Mbele. " Wengi Waanza Kuona Ubora Wa JK". Yalikuwa ni maoni binafsi ya Profesa Mbele. Wengi wamechangia na wanaendelea kuchangia. Nami nitachangia pia. Nimepata bahati ya kukutana na kuongea na Profesa Mbele kwa simu na ana kwa ana . Ni pale aliporudi nyumbani Tanzania mwaka jana.
Naweza kusema nimemfahamu Profesa Mbele kupitia maandiko yake kwa maana ya makala zake anazozituma KWANZA JAMII na pia nilipoongea nae na kumsikia anavyoelezea mitazamo yake juu ya masuala mbali mbali ya nchi aliyozaliwa, Tanzania. Kwamba Profesa Mbele ni mtaalamu wa lugha ya Kiingereza haina maana hana anachokijua kuhusiana na nchi yake Tanzania na ulimwengu kwa ujumla.
Ni dhahiri kuna wanaotishika wanaposikia mtu anaitwa ' Profesa fulani'. Na kuna anayejisikia raha anaporudi nyumbani na kumwambia mumewe au mkewe; " Kuna jamaa kule JF anaitwa Profesa Mbele, kaja na hoja zake za kipumbavu, nimempa maneno yake, mpuuzi mkubwa!"
Aliyempa Profesa Mbele ‘maneno yake' huenda ana hitaji la kupunguza hasira zake, msongo wake wa mawazo. Kama hilo linamsaidia ni jambo la heri. Lakini bahati mbaya si wengi wako kama Profesa Mbele. Yeye atasoma na atalifahamu hilo, wala hutamwona akirudi na kujibu kwa hasira.
Ukikutana na Profesa Mbele huwezi kumsikia akitamka neno ‘Profesa'. Kwa Profesa Mbele ' sina hata ya kujisikia kuwa mimi ni sawa na ‘Mwalimu wa Zamu' Shule ya Sekondari Changanyikeni. Profesa Mbele hana makuu. Ni mwalimu na bado ana kiu ya kujifunza. Anajiamini. Si mwanachama wa chama cha siasa hapa Tanzania. Anaipenda Tanzania na anajisikia huru kuchangia fikra zake. Hana sababu za kuficha jina lake. Na katika hilo, Profesa Mbele na mimi tuna mitazamo sawa. Binafsi sioni tatizo kuandika maoni yangu. Naandika kwa uhuru . Sina chama na sina sababu ya kuficha jina langu kwa fikra zangu ninazozitoa hadharani. Mwenye kuzipinga, ruksa, azipinge kwa hoja, ni muhimu. Na mengine niandikayo yaweza kuwa ya kipuuzi, najua, maana mimi si malaika. Kuna watakayekubaliana na hoja zangu, na kuna watakaosema; " Sasa mshenzi huyu atakiona cha mtema kuni". Watanishambulia mimi binafsi hata kwa matusi ya nguoni. Nimeshazoea. Ukichagua mchezo wa masumbwi, usiogope ngumi za usoni!
Tujitahidi kujenga mazoea ya kuikabili hoja inayowasilishwa na si kumkabili mwasilisha hoja. Mathalan, Profesa Mbele yeye kwa mtazamo wake anaona kuwa JK ameonyesha ubora kama kiongozi. Ni mtazamo wake. Wengine tuje na mitazamo yetu kwa kupinga au kuunga mkono hoja zake. Si busara kuanza kumvamia Profesa Mbele na kwa kutumia lugha zisizo za kiungwana . Na wanaofanya hivyo baadhi yao ni waoga kwa vile hawatumii hata majina yao halisi.
Daima tupiganie ' Neno huru'. Uhuru wa kila mmoja wetu kutoa maoni yake. Tujiadhari tusije tukatumia majukwaa haya kukandamiza fikra huru. Si kwa bastola na pingu, bali kwa kalamu zetu. Tujiulize; ni Maprofesa wangapi wa Kitanzania wanaojitokeza kwa majina yao kuchangia fikra zao katika majukwaa ya wazi ya kijamii?
Na kama asememavyo Profesa Mbele Mwenyewe; "
Kuona mazuri ya JK kama kiongozi, kwa upande wangu, si sawa na kuipigia debe CCM. Tangu CCM ianze, nimekuwa nikiishutumu kwa namna mbali mbali, tena kimaandishi, ili kila mtu asome. Nimechapisha hata kitabu, wiki chache zilizopita, ambamo nimeendelea kuishutumu CCM.
Tatizo la waTanzania wengi ni ufinyu wa mawazo. Kwa vile wamezama mno katika siasa za vyama, wanayachukulia masuala kwa mtazamo wa kichama. Ukisema hivi, wanaangalia unaunga mkono chama gani. Ukisema vile, wanaangalia kwa mtazamo wa chama fulani. Ukweli ni kuwa mimi si mwanachama wa chama chochote. Nina uhuru wa kusema chochote ninachofikiri, hata kama kinawaudhi watu wa chama fulani. Shauri lao na siasa zao za ufinyu na ukandamizaji wa fikra kwa maslahi ya chama." Profesa Mbele.
Nawasilisha.
Maggid
' Mwalimu Wa Zamu'.
Tembelea:
http://mjengwa.blogspot.com