Prof. Lipumba ajitosa urais UKAWA

Magazetini

JF-Expert Member
Aug 16, 2014
588
1,698
lipumba+picha.jpg

Profesa Ibrahimu Lipumba akihutubia moja ya mikutano


Mei 30 2015

KWA UFUPI
Profesa Lipumba, ambaye anakuwa mwanasiasa wa tatu kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutangaza nia hiyo baada ya mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi na Dk George Kahangwa wa NCCR-Mageuzi kujitokeza kutaka kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano.
Tabora
Mbio za urais zimezidi kupamba moto kwa upande wa upinzani baada ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza nia ya kugombea nafasi hiyo ya juu kisiasa nchini, akisema ana sifa zote lakini hatakuwa na kinyongo iwapo hatapitishwa na umoja wa vyama vya upinzani.


Profesa Lipumba, ambaye anakuwa mwanasiasa wa tatu kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutangaza nia hiyo baada ya mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi na Dk George Kahangwa wa NCCR-Mageuzi kujitokeza kutaka kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano.

Mwanasiasa mwingine aliyejitokeza kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano ni Maxmillan Lyimbo wa TLP, wakati Hamad Rashid wa Alliance for Democratic Change (ADC na Maalim Sharrif Hamad wa CUF wametangaza kuwania urais wa Zanzibar.

Lipumba, ambaye atakuwa akiwania urais kwa mara ya tano, iwapo atapitishwa na Ukawa ambayo imeamua kusimamia mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama vinne, alitangaza nia yake juzi mjini Tabora wakati wa mikutano yake ya hadhara ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kupiga kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25.

"Ninachoomba ni ushirikiano wenu katika safari yangu hii ya kuwania tena urais," alisema Profesa Lipumba alipokuwa akihutubia wananchi kwenye uwanja wa mpira wa Shule ya Msingi ya Town School mjini hapa.

"Ninajua safari hii, urais (kwa upande wa upinzani) utasimamiwa na Ukawa, lakini naamini mimi ni mwadilifu na nina uwezo wa kuongoza nchi," alisema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba aliwaomba wapenzi na wanachama wa CUF pamoja na Watanzania kwa ujumla, kumuunga mkono katika safari yake hiyo ya kuelekea Ikulu.

Mwenyekiti huyo wa CUF ambaye kitaaluma ni mchumi, alisema ana uwezo na sifa za kuwa rais na kwamba madhumuni makuu ya kutaka kushika madaraka ni kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi na kupambana na ufisadi.

"Dhumuni kuu si cheo, bali ni kushirikiana na wananchi kuondoa kero zao," alisema mshauri huyo wa zamani wa uchumi wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

Lakini alikuwa makini na azimio la umoja huo wa wapinzani unaoundwa na CUF, NLD, NCCR-Mageuzi na Chadema, kuhusu kusimamisha mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama hivyo.

"Ingawa Ukawa itakuwa na mgombea mmoja wa urais, naamini kuwa mimi ni miongoni mwa wanaofaa kupeperusha bendera hiyo kwa kuwa najijua kuwa ni mwadilifu na nina uwezo wa kuliongoza Taifa changa kiuchumi kama Tanzania," alisema Profesa.

"Mimi naweka nia ya kugombea urais nikiwa na malengo mengi, ikiwamo kutaka kumaliza kero ya umaskini kwa Watanzania, lakini kikubwa ni ushirikiano wenu katika safari hii.

"Natangaza kuwa naingia kwenye kinyang'anyiro cha urais nikijua kuwa kuna ushindani, lakini kwa umoja wenu (CUF), wananchi na Ukawa, yote yanawezekana."

Profesa Lipumba aligombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 1995, wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi tangu siasa za ushindani kurejeshwa nchini mwaka 1992 na kushika nafasi ya tatu nyuma ya mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa na wa NCCR-Mageuzi, Augustine Mrema (sasa yuko TLP), akiwa amechukua asilimia 6.43 ya kura zote.

Mwaka 2000 alirejea tena ulingoni na kushika nafasi ya pili nyuma ya Mkapa akinyakua asilimia 16.26 ya kura zote na mwaka 2005 alishika nafasi ya pili akizidiwa na Rais Jakaya Kikwete baada ya kunyakua asilimia 11.63 na mwaka 2010 alishika tena nafasi ya tatu nyuma ya Kikwete na Dk Willibrod Slaa wa Chadema, akiwa amevuna asilimia 8.3 ya kura zote.

Vipi akitoswa na Ukawa
Hata hivyo Profesa Lipumba alisema kuwa lengo la Ukawa ni kujipanga ili kuiondoa CCM madarakani, hivyo hata ikitokea Umoja huo unadhani kuna mtu mwingine mzuri kuliko yeye, yuko tayari kumwachia mwenzake, ili mradi lengo hilo litimie.

"Sitakuwa na kinyongo kama ikitokea mwenzangu amechaguliwa kupeperusha bendera ya Ukawa kwa sababu naamini wote tuna nia moja tu; kuindoa CCM madarakani, hivyo akija mwingine naahidi kumuunga mkono," alisema.

Profesa Lipumba alieleza kuwa Ukawa ndiyo suluhisho la matatizo ya Watanzania kwa kuwa ndani ya umoja huo, kuna misingi na mikakati madhubuti wa kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

"Lengo la Ukawa ni kuwa na Serikali inayotenda haki. Sasa yeyote atakayepitishwa kuuwakilisha umoja huu, ataongozwa na misingi hiyo, ndiyo maana nasema sisi hatuna haja ya kugombania nafasi ya urais, ila demokrasia lazima itumike katika kumpata mgombea," alisema Profesa Lipumba.

Msomi huyo wa Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani, alibainisha kuwa ugumu wa maisha unaoendelea kwa wananchi wa hali ya chini, unatokana na Serikali ya CCM kukosa dira ya maendeleo, hivyo njia pekee ni kuhakikisha inaondolewa kwa kutumia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Profesa Lipumba alisema viongozi wa chama hicho tawala wameua viwanda na kuwafanya vijana wakose kazi za kufanya. Vijana wamekata tamaa na wanaishi kwa manyanyaso makubwa ndani ya nchi yao.

"Hapa (Tabora) palikuwa na viwanda vya maziwa, mbao na vingine vingi ambavyo vilikuwa vinatoa ajira kwa vijana. Ajira hizo ziliwafanya vijana wapate mishahara na hivyo waliweza kuongeza mzunguko wa fedha nchini na kuchangia katika kukuza uchumi. Lakini sasa hali ni tofauti, hakuna kazi na vijana wamekata tamaa," alisema Lipumba ambaye alizaliwa na kupata elimu ya msingi na sekondari mkoani hapa.

"Usafiri wa reli mkoani Tabora ulikuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa wananchi. Usafiri huo uliufanya mji wa Tabora uchangamke na kuwa sehemu madhubuti kwa mzunguko wa fedha, lakini kufa kwa reli leo kumewaacha wananchi yatima."
Profesa Lipumba amebobea kwenye Uchumi wa Maendeleo na Uchumi wa Kilimo pamoja na Biashara ya Kimataifa na Fedha, na ameshaandika machapisho mengi kuhusu kilimo, biashara, matatizo ya kiuchumi na mahitaji ya kimsingi.

Lipumba alieleza chanzo cha nchi kukosa maendeleo kuwa ni viongozi kuwa na matumizi mabaya ya fedha za umma na kukosa moyo wa uzalendo kwa Taifa lao.

"Baadhi ya viongozi wa Serikali ya CCM hawana uzalendo, hawawajibiki na wanadiriki hata kuwaibia wananchi. "Viongozi hao hawaoni aibu hata kutumia vibaya madaraka yao, matendo hayo yanawafanya wananchi wawe maskini wa kutupwa," alisema.

Kwa sasa Profesa Lipumba na wanachama 32 wa CUF wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama na kufanya maandamano bila ya kibali baada ya kukamatwa mwisho mwa Januari, wakati chama hicho kilipokuwa kikikumbuka wanachama wake waliouawa na polisi wakati hali ya kisiasa ilipochafuka kutokana na kutokubaliana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Zanzibar.

Nini kifanyike?
Profesa Lipumba alibainisha suluhisho la matatizo hayo kuwa ni jitihada za pamoja za kuiondoa madarakani Serikali ya CCM kwa kuwa imeshindwa kuongoza na kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

"Hatua ya mwanzo kabisa ya safari ya kuiondoa CCM madarakani ni kujiandikisha katika Daftari la Wapigakura na baadaye kujitokeza na kupigakura wakati wa Uchaguzi Mkuu," alisema.


Watu hawana taarifa ya BVR
Katika hatua nyingine Profesa Lipumba alilalamika kwamba wananchi wengi katika manispaa ya Tabora hawana taarifa kuhusu shughuli ya uandikishaji wapigakura inayofanywa kwa njia ya teknolojia ya utambuzi wa alama na taswira za mpigakura (Biometric Voter's Registraton (BVR)).

Aliwatupia lawama wakurugenzi wa halmashauri akisema kuwa ndio waliopaswa kuwapa wananchi hao taarifa hizo, lakini hawakufanya hivyo na kusababisha usumbufu usiokuwa wa lazima.

Awali, akizungumzia uandikishaji wapigakura kwa BVR, naibu mkurugenzi wa mipango na uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo, alisema CCM wamechakachua Katiba Inayopendekezwa na ndiyo maana wananchi wanaikataa.

Alitaka wananchi hao wajitokeza na kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura ili waiondoe CCM madarakani na kuweka uongozi mpya utakaoshughulikia matatizo yao kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.

Lipumba ni nani?

Ibrahim Haruna Lipumba alizaliwa Juni 6 mwaka 1952, katika kijiji cha Ilolangulu mkoani Tabora. Alisoma Shule ya Msingi Ilolanguru iliyoko Tabora na baadaye akajiunga na masomo ya sekondari katika Shule ya Wavulana Tabora (Tabora Boys) pia ya mkoani hapa kabla ya kwenda kusoma elimu ya juu ya sekondari kwenye shule maarufu ya Pugu. Kati ya mwaka 1973 na mwaka 1976, Lipumba alijiunga na masomo ya shahada ya kwanza ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Dares Salaam. Baadaye aliendelea na masomo ya shahada ya uzamili ya uchumi (M.A Economics), kati ya mwaka 1976 na mwaka 1978 katika Chuo hicho cha Dar es Salaam na baadaye Chuo Kikuu cha Stanford cha nchini Marekani.

Mwaka 1978 hadi mwaka 1983, Profesa Lipumba alisoma shahada ya uzamivu (PhD) ya masuala ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Stanford.

Tangu amalize masomo yake, Profesa Lipumba amekuwa akishika nyadhifa mbalimbali katika masuala ya elimu, ikiwamo mhadhiri wa vyuo vikuu kadhaa nchini na Marekani. Amewahi pia kuitumia taaluma yake ya uchumi kuishauri Serikali ya Uganda kuhusu masuala ya uchumi kati ya mwaka 1980 na miaka ya 1990 na kwa sasa anafanya shughuli zake za kiuchumi ingawa siasa inakula muda wake.

Historia yake kwenye siasa
Katika siasa, Profesa Lipumba amekuwa mwenyekiti wa CUF tangu mwaka 1995 na amekuwa akigombea kiti cha urais kila mwaka wa uchaguzi tangu wakati huo nchi ilipoingia kwenye Mfumo wa vyama vingi.

Mbali na shughuli hizo za kisiasa, Profesa Lipumba alikuwa mwanasoka nyota enzi zake akiwa shuleni Tabora na alitundika daruga baada ya kuumia goti.

CHANZO: Mwananchi
 
Hahahahahaha lipumba anataka kuitwa msaliti sasa,hajui kuwa ni kosa la jinai kutangaza nia ukiwa na ushirikiano na Chadema?Amuulize Zitto ndo atajua kuwa mbowe na slaa ni shida pale sakosini.
 
Hahahahahaha lipumba anataka kuitwa msaliti sasa,hajui kuwa ni kosa la jinai kutangaza nia ukiwa na ushirikiano na Chadema?Amuulize Zitto ndo atajua kuwa mbowe na slaa ni shida pale sakosini.
akili ya mjinga huwaza ujinga.
 
UKAWA tunaangalia anayekubalika ndani ya Ukawa na kwa wananchi .
 
Safi Prof japo nahisi Kama hakuna jipya kutangaza kwako maana ni Kama zaman,nakerwa na vyama kutoandaa sura mpya!
 
sometime nacheka tu. LIPUMBA WILL NEVER NE A PRESIDENT OF THIS COUNTRY AS WELL AS SLAA... hivininyi mafikria ni mchezo tu? well angalau Dr SLaa Lipumba kiukweli tumeshachoka naye jaman miaka 25 yote unataka urais unazidi kuporomoka tu bado hujiwazii? hawa wasomi wetu mbona hawawazi kama wasomi? msomi angekuwa ameshajua kuwa wananchi hawamtaki.
 
Back
Top Bottom