Posta Tantrade watoa mafunzo ya mifumo ya biashara mtandaoni Zanzibar

PendoLyimo

JF-Expert Member
Sep 30, 2014
879
956
Shirika la Posta Tanzania kwa kushirikiana na TanTrade wametoa Mafunzo ya Mifumo ya Biashara mtandaoni kwa Wafanya Biashara pamoja na Viongozi wa Taasisi mbalimbali za Kibiashara Visiwani Zanzibar.

Mifumo iliyofundishwa ni Mfumo wa Duka mtandao (Shirika la Posta), Mfumo wa Information Portal Market Access Map pamoja na Mfumo wa E-malalamiko. (TanTrade)

Mgeni Rasmi katika tukio Hilo alikuwa Dkt. Islam Salum Seif, Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Dkt. Islam ametoa pongezi kwa Shirika la Posta pamoja na TanTrade kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatakwenda kuwasaidia maafisa wote wanao simamia biashara pamoja na Wafanya Biashara wa Zanzibar.

Aidha,Katibu Mkuu huyo amesema mifumo hiyo ya biashara itawasaidia wafanya biashara wa Zanzibar kutangaza biashara zao hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa Ugonjwa wa Corona." Katika kipindi hiki ambapo dunia imekumbwa na ugonjwa wa Covid-19 wafanya biashara wameendelea kufanya biashara kupitia maduka ya mtandaoni, na wanafanya biashara bila ya kukutana ana kwa ana, hivyo mifumo hii itakwenda kuwasaidia wafanya biashara wa Zanzibar." Alisema Dkt Islam.

Naye Kaimu Postamasta Mkuu Ndugu Macrice Daniel Mbodo ameeleza namna ambavyo Shirika la Posta limejipanga katika kutoa huduma kwa Wananchi wa Zanzibar pamoja na Tanzania bara. "Shirika la Posta tumefanya maboresho makubwa katika kutoa huduma sasa tumetoa fursa kwa wafanya biashara kutangaza biashara zao kupitia mfumo wa duka mtandao" Alisema Bwana Mbodo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania Balozi Mteule Edwin Rutageruka amesema Mifumo hiyo inaenda kutekeleza azma ya Serikali ya kukuza Uchumi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

" Mifumo hii itaenda kutekeleza azma ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza Uchumi wetu" Alisema Balozi Edwin Rutageruka.


IMG-20210723-WA0101.jpg

 
Back
Top Bottom