Waziri Dkt. Kijaji Aielekeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Kuwalea Wafanyabiashara

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,903
945
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imeelekezwa kuwalea wafanyabiashara nchini kwa kurahisisha jinsi ya kuifikia, kuwa mbunifu wa namna ya kuwahudumia na kuifanya Taasisi kuwa ya watanzania ili kufikia malengo ya uanzishwaji wake.

Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji(Mb) alipokuwa akifungua mkutano wa kwanza wa BRELA na wadau wake leo tarehe 27 Oktoba, 2023 kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kukabidhi uchumi wa taifa kwa sekta binafsi na amefungua mipaka yote, hivyo taasisi ya kwanza inayoshughulikia sekta binafsi ni BRELA kwakuwa uchumi wa nchi unakua kupitia ukuaji wa sekta ya viwanda na biashara nchini.

Ameongeza kwa kusema kuwa kuanzia mwaka 2019 hadi Juni, 2023 Serikali imeeendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara MKUMBI) na kuondoa tozo na kodi mbalimbali zaidi ya 374 zilizosumbua wafanyabiashara ambapo Serikali imefikia zaidi ya asilimia 75 ya dhamira yake.

“Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kupitia Sheria ya Fedha jumla ya Sheria na Kanuni 13 na pia Sheria ya Fedha ya mwaka 2023 zimeweza kupunguza na kufuta tozo, ada na faini 67 ikiwa na lengo la Serikali ya awamu ya sita la kuhakikisha mazingira ya biashara kuwa bora zaidi”, ameeleza Mhe. Dkt. Kijaji.

Mhe. Dkt Kijaji amesisitiza kuwa hakuna uchumi wa nchi unaokua kama hakuna maendeleo katika sekta ya viwanda na ya biashara iliyo imara, Serikali inahakikisha inaboresha mazingira ya ufanyaji biashara ndani na nje ya Tanzania na taasisi za udhibiti hazitumii mamlaka zao kufungia biashara yoyote lengo ni kuhakikisha kuwa sekta ya biashara inalea uchumi wa nchi.

“Tunaangalia uwekezano wa kutoa leseni zote za biashara katika mfumo mmoja wa BRELA kuliko kuwa na mifumo mingi inayotoa huduma za leseni za biashara hii itasaidia uratibu mzuri wa leseni za biashara na Serikali kuwa na kanzi data moja ya taarifa za biashara, tunawaomba mtupe ushirikiano katika hatua hii ili kuwahudumia kwa ufanisi mzuri", ameongeza Mhe. Dkt Kijaji.
 
Back
Top Bottom