Pongezi Mheshimiwa Spika..!!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,475
39,988
WATANZANIA hatuna budi kupiga vigelegele, makofi na hoihoi za shangwe! Hatuna budi kucheza mdundiko, lizombe, gita, mganda, na mdumange! Hatuna budi kutunga tenzi, ngonjera na nyimbo za sifa kwani Spika wetu, amevaa vazi lenye michirizi ya dhahabu lililochirizwa Ulaya!

Kuna wakati hatuna budi kuondoa tofauti zetu za kisiasa, na hasa wivu usio na msingi, hasa tunapoona mwenzetu amefanikiwa. Si tu kuziondoa na kuziweka pembeni tofauti hizo, bali hata kuzizika na kuzisahau kabisa hasa inapotokea kiongozi wa Bunge letu amepata bahati ya kuvaa joho limeremetalo lenye picha za mabibo, korosho na mahindi ambapo limenakshiwa kitaalamu na mafundi maalumu huko London, Uingereza.

La mgambo limelia, likilia lina jambo, Mhe. Samuel John Sitta MB (Urambo Mashariki-CCM) amepata vazi jipya lililoshonwa Ulaya!

Bila ya shaka unajiuliza “mwanakijiji imekuwaje leo?” Wakati kikao cha Bunge kinachoendelea sasa kilipoanza siku chache zilizopita, Spika wa Bunge hilo, Sitta, baada ya kutoa maelekezo na taarifa mbalimbali aliamua pia kuwapa taarifa wabunge ambayo bila ya shaka ilikuwa ni muhimu kwao kupata.

Sitta alisema: “Kwa wale ambao hawajagundua, Spika leo amevalia joho jipya. Lile la zamani lilikuwa limechakaa” na akawaeleza wabunge kuwa joho hilo jipya limeshonwa na mafundi maalumu huko London. Wabunge wakafurahia joho hilo jipya la spika. Tulioangalia kwenye luninga tukabakia kutabasamu.

Hata hivyo kwa hakika, sidhani kama ipo haja ya kumpa pongezi za kuturingishia joho lake hilo kama watoto wachezao “doli doli” ili na sisi tusiojua kuwa Spika kapata joho jipya na tujue.

Sioni sababu hata chembe kwa ndugu yetu huyo ambaye kwa hakika anapaswa kuwa miongoni mwa wazalendo vinara kusimama na kututambia kana kwamba vazi lake hilo limeshonwa toka mbinguni.

Binafsi ninajihisi aibu, hasira, na kisirani kuona Spika wa Bunge letu akikejeli mafundi wetu wa nguo, na wabunifu kuwa vazi “la kispika” lazima lipigiwe debe mbele ya wWabunge wetu kuwa vazi hilo limetoka ‘majuu’. Kwa hakika ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni!

Hivi ni kweli katika Tanzania huru, Tanzania ambayo kiongozi mwingine aliwahi kutamba huko huko Bungeni kuwa “inapaa”, hivi kweli katika Tanzania hiyo hakuna mtu yeyote mwenye cherehani (ya umeme au ya kusuma na miguu) ambaye ana uwezo wa kuchiriza vazi la Spika, kwa michirizi ya dhahabu?

Hivi ndugu Hassanali na timu yake wangeshindwa kufanya kazi hiyo kabisa? Kama majibu yaliyotolewa Bungeni mwaka 2005 na Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa vazi la Spika. “litakuwa ni joho lenye kuonesha rangi za Bendera ya Taifa, Nembo ya Taifa na baadhi ya mazao makuu nchini.” Basi nina mashaka yawezekana tukafika mahali tukawa na vazi la spika lenye nembo za wazungu, bendera za nchi za Ulaya na mazao makuu ya Uingereza!

Kwa hakika si lengo langu hata kidogo kuzungumzia vazi la Spika. Ninachotaka kuzungumzia haswa ni kile kinachotokana na mawazo ya kitwana ambayo yameonekana katika wazo zima la Spika Sitta kututangazia ujio wa vazi hili jipya kutoka Ulaya. Watanzania bado tusipojichunguza vizuri tutashindwa kujigundua kuwa bado tuna mawazo ya kutawaliwa ambayo ndani yake kuna masalio ya fikra za kuwa duni na watu dhaifu mbele ya Wazungu.

Vinginevyo, tunaweza kuelezea vipi kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano kwenda kuwatangazia wazungu huko Ulaya na kuomba misaada ya watu kutuandikia mikataba ya madini kwa vile wataalamu wetu “hawana uwezo wa kutosha”? Hivi kweli katika Chuo Kikuu cha Dar es Saalam, Chuo Kikuu cha Mzumbe, na vinginevyo vyote hakuna wataalamu wanaoweza kufikiri kuwa mikataba lazima itunufaishe sisi kama nchi badala ya kuyanufaisha makampuni makubwa ya kimataifa? Hili la kuomba wataalamu kutoka nje kutufanyia mambo tunayoyaweza kwa hakika ni suala la joho la spika!

Kama hilo halitoshi, inakuwaje leo hii wanaochunguza suala la rada wawe ni wazungu na inakuwaje wao wawe na uchungu zaidi na suala hili kuliko sisi. Tulipopiga kelele tulichunguze tuliambiwa tuwaache wao serikali ya Uingereza ichunguze kwanza na hata sisi wenyewe hatukujua ni nini tunachochunguza. Nimefarijika kidogo kusikia kwamba hatimaye Takukuru nayo imefikia mahali sasa wanamsaka yule mwenye dili la rada.

Leo hii tunaambiwa kuwa ati kuna mtuhumiwa ambaye amefunguliwa kesi ya rushwa kuhusu suala hili. Hivi kama wasingekuwa hao wazungu kuanzisha uchunguzi wao na kumtaja huyo mtuhumiwa katika uchunguzi wao mapema mwaka huu, hivi kweli Watanzania tungejua kuwa tumeingizwa mjini? Kwanini Bunge la Uingereza litumie muda mrefu kuzungumzia suala la rada “yetu” wakati Bunge letu linapigwa mkwara na hawataki kuliangalia jambo hilo kwa karibu!?

Leo hii nimesoma mahali fulani kuwa wakandarasi wetu wana uwezo wa asilimia 30 tu ya kufanya shughuli zao za ukandarasi kiasi cha kwamba kimsingi Watanzania atuna uwezo wa kutengeneza barabara zetu na majengo etu kwa kiwango cha kimataifa bila kushirikisha Wazungu.

Sitashangaa kabisa kuwa hata samani zilizoko Ikulu, Bungeni na kwenye maofisi ya wizara zetu nyingi (kama si zote) zinatoka majuu, kwani katika Tanzania hatuna maseremala wanaoweza kukidhi mahitaji ya kifahari ya watawala wetu. Tusije kuambiwa kuwa hata mapazia yenye michirizi ya rangi rangi yanayopamba kuta za ofisi zetu za umma nayo yametoka kwa mjomba!

Ni mjomba gani huyu tuliyenaye Watanzania basi? Swali hili lilimsumbua hata Mwalimu na aliuliza na katika ile hotuba yake maarufu ya Mei Mosi, 1995 na kusema “Watanzania nionesheni mjomba wenu aliyeko Ulaya, na mkinionesha nitacheeeeka”.

Jambo ambalo bila ya shaka Baba wa Taifa hakujua ni kuwa si tu tuna mjomba Ulaya, bali pia tuna shangazi na binamu ambao wanafuatilia sana maslahi yetu hadi kutushonea vazi la spika wetu.

Ni mawazo gani haya ya kitwana na tena ya kitumwa? Hivi tulipoamua kuacha sera ya kujitegemea tulisema tumeacha hata mawazo ya kujitegemea au tumeacha kujitegemea kimawazo pia? Watanzania ni lazima tukatae mawazo na fikra zinazoturudisha nyuma hasa kutukuza vitu vya “Wazungu” alimradi tu vimetoka majuu.

Na hapa sizungumzii kwamba tuache vitu vya Wazungu au kutaka kuonesha kuwa kila walichonacho wazungu sisi tayari tunacho, nitakuwa muongo. Ninachosema ni kuwa, kile kinachoweza kufanywa na Watanzania na kinachoweza kufanywa Tanzania kwanini kisifanywe na Watanzania au kufanyika Tanzania?

Tunapofika mahali kuwa hata joho la Spika inabidi lifumwe Uingereza na kutangazwa kwa fahari Bungeni mjue tuna matatizo. Leo hii naona waandishi wetu hasa watangazaji wa luninga wanaozungumza kwa lafudhi ya Kizungu huku lafudhi zao za Kisukuma, Kichagga, na Kimang’ati wakizificha. Kwa hili nampongeza rafiki yangu Stephen Chuwa.

Nilimsikiliza Spika alipotamka majina ya baadhi ya wajumbe kwenye Mkutano Mkuu wa CCM (akitangaza matokeo) na nilijisikia kichefu chefu kuwa hata matamshi yamekuwa ya Kizungu!

Mtangazaji anasema “habari zenu”, hiyo “ri” inavyolembwa na kunatishwa utadhani mtu kashuka juzi kuwa Birmingham ni jambo la kusikitisha. Wale tulioishi na wageni au tunaishi na wageni tunaona jinsi gani wanavyohusudu lafudhi zetu za Kiafrika kwani ni tofauti, na inachangia katika kupamba matumizi ya lugha ya Kiingereza au lugha nyingine yoyote.

Sikatai kuwa unapozungumza lugha ya “wenyewe” si dhambi kuiga lafudhi zao kidogo, lakini unapozungumza Kigogo kwa lafudhi ya kizungu, na kidigo kwa lafudhi ya Mwingereza basi siyo utumwa wa mawazo tu uliotukumba bali utumwa wa lugha tunaoung’ang’ania!

Sasa unapokuwa na viongozi waliotawaliwa kifikra namna hiyo, hivi kweli tunategemea watoto wetu na vijana wetu watatukuza vitu vya Kiafrika kweli? Kulikuwa na onesho moja kwenye mojawapo ya vipindi vya Luninga ambapo walikuwa wanaonesha jinsi ya kutengeneza kofia za jadi kwa kutumia majani ya migomba. Ni wachache wetu watakurupuka kununua hizo kujikinga na jua, ikilinganishwa na kofia za nailoni zenye nembo ya NY au Miami!

Leo hii hata kwenye misiba mabinti zetu wanaona haya kujifunga khanga na badala yake wanatinga pamba za majeans na tshirt zenye kuchombeza. Kisa na mkasa, wawe kama Ulaya (kwa taarifa huko ugenini watu wakifikwa hawavai majeans isipokuwa wachache mashabiki wa hip hop).

Ndugu zangu, kitendo cha Spika kuturingishia joho lake la michirizi ya dhahabu kutoka Ulaya, ni kitendo cha aibu, cha kukatisha tamaa, na kwa hakika kinachopaswa kulaaniwa na wale wote wenye kuamini kuwa vile vinavyoweza kufanyika Tanzania vifanyike Tanzania.

Isipokuwa kama Spika anaweza kutuambia ni kwa nini joho lake lisingewezekana kabisa kuchirizwa Tanzania (nafahamu pale Zanzibar kuna mafundi wazuri sana wa mambo haya ya kuchiriza). Ni matumaini yangu, hii itakuwa ni mara ya mwisho kwa joho la Spika kutengenezwa Ulaya, hata kama hilo lina ujiko wa aina fulani.

Vinginevyo, huko tunakokwenda tutafikiria tunasonga mbele kumbe pole pole tunarudi nyuma. Na tusipoangalia haya mambo ya kutukuza vya majuu hayataishia kwenye joho la Spika na samani za mawaziri. Mungu aepushie mbali, tusije kujikuta siku moja tunaamka tukiwa na Rais kutoka Tanzania ambaye baraza lake la Mawaziri linatoka Marekani, Jaji Mkuu anatoka Ujerumani na Spika wa Jamhuri ya Muungano anatoka Uingereza huku joho lake limetengenezwa Ujapani. Labda haitakuwa mbaya kiasi hicho, lakini kwa mtindo huu, lolote linawezekana Tanzania.

niandikie: mwanakijiji-at-jamboforums.com
 
Mhhhh Thats what I call deep and critical analysis of issues. Jambo la kukumbuka hapa ni kuwa UKOLONI haujaisha. Ulianza na sura nyingi. Kisiasa, kiuchumi na kila nyanja ya maisha yetu. Jinsi tunavyojitahidi kuondokana nao ndivyo wanavyojitahidi kubadilisha sura ili waendelee kufaidi kufyonza kwa mabomba na sio mirija ya kila chetu chema tulichonacho.
Wazungu wanakandya kila kitu cha Africa na nchi maskini. wanatukuza vya kwao. Hata shule. Hata kama umesoma Mlimani ukifika kwao watakuambia umefanya TOEFIL AU EALT. Wakati ukweli ni kuwa tuliowengi kama umefika sekondari na kufaulu basi kingereza chako gramatically ni kizuri hata kuliko mtoto aliyezaliwa Brixton. Ila still kimawazo tumedumazwa mno na haya majamaa. Wanahusudu mashono ya kiafrika hasa darizi zetu. Ningetegemea Spika kusema kuwa ana vazi liliodariziwa na designer mtanzania na limeshonwa na mtanzania. Jamani hakuna uniform ya maspika ulimwenguni. Kwa hiyo kwa heshima na Taadhima nadhubutu kusema kuwa ni ufujaji na ubadhirifu wa mali ya umma kuedndelea kuagiza mavazi y spika au mameya ili hali yanweza kushonwa Tanzania. Tuagize vitu vile tu ambavyo technology yetu haitupi nafasi kuvitengeneza. SPIKA ZIIIIIIIIIIIIII. NAOMBA KUTOA HOJA.
 
Hivi hawa viongozi wamekukosea nini wewe, mara Lowassa, mara Makamba, sasa Spika Sitta. Hivi unafikiri you can do a better job than them? unaboa kaka, andika mambo mengine basi.

asante.
 
thats our country..watu walioko juuu wanakshindilia matumbo yaooo mpaka yapasuke...sie tulio chini twaaambiwa tuwangojeee huku huku chini na njaa zetu,wakubwa tuliowachagua watuletee misosi..(maendeleo) watarudi na vyakula tule woote...tutangoja milele
 
Du, Bi senti 50 na mwanakijiji!! utafikiri paka na panya hamkai mkaelewana?

M/kijiji
Au inawezekana hatuna aina ya material iliyotumika kwa hiyo ili kupunguza gharama wakaona ni vema lishonwe huko huko kunakotoka kitambaa? Just to gues
 
Du, Bi senti 50 na mwanakijiji!! utafikiri paka na panya hamkai mkaelewana?

M/kijiji
Au inawezekana hatuna aina ya material iliyotumika kwa hiyo ili kupunguza gharama wakaona ni vema lishonwe huko huko kunakotoka kitambaa? Just to gues


sahara, hivi kweli kuna material ya nguo ambayo inapatikana sehemu yoyote duniani na isingiweza kuletwa Tanzania? Ningefurahi kama watatuambia ni material gani, halafu walichukue hilo vazi walipeleke kwa mafundi wetu watuambie kama hawawezi kutarizi kitu kama hicho...
 
sahara, hivi kweli kuna material ya nguo ambayo inapatikana sehemu yoyote duniani na isingiweza kuletwa Tanzania? Ningefurahi kama watatuambia ni material gani, halafu walichukue hilo vazi walipeleke kwa mafundi wetu watuambie kama hawawezi kutarizi kitu kama hicho...

Good Mkijiji,
tunahitaji vichwa kama hivi siyo kidumuuuuuu kila jambo hata kama limepinda!

Kwa mwendo huu nadhani itabidi wawe wanafikiria mara mbili kabla ya kutenda na kuropoka kwa kutaka misifa!
 
Hivi hawa viongozi wamekukosea nini wewe, mara Lowassa, mara Makamba, sasa Spika Sitta. Hivi unafikiri you can do a better job than them? unaboa kaka, andika mambo mengine basi.

asante.


Just give him that mandate and see
 
mzee hunitakii mema... waache wao wahangaike nalo sisi tutaendelea kuwapigia kelele. Si unajua tena mashabiki wanapiga kelele utadhani ndio wanajua kucheza?
 
Back
Top Bottom