Mbowe atamba kuibuka na ushindi leo
na Mwandishi Wetu, Arusha
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ametamba kuwa chama chake kitaibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi mdogo wa kiti cha udiwani wa Kata ya Kati, katika Manispaa ya Arusha.
Mbowe ambaye aliwasili mjini hapa juzi, aliweza kubadilisha hali ya upepo wa kisiasa, tofauti na siku zote ambazo kampeni hizo zimekuwa zikifanyika katika Manispaa ya Arusha.
Akihutubia mamia ya wananchi wa mji huo kwenye mkutano mkubwa wa hadhara, juzi na jana katika kata hiyo, Mbowe alisema chama chake kitaibuka na ushindi kwenye uchaguzi huo na chaguzi nyingine nne zinazofanyika kata nyingine hapa nchini.
Nimekuwa hapa tangu jana, nimefarijika mno na mapokezi na jinsi watu mnavyojitokeza katika mikutano yangu naomba hali hii iwepo hadi kesho (leo) sote tujitokeze na kumpa kura mgombea wetu wa CHADEMA, Self Simba, alisema Mbowe.
Alisema wakati umefika kwa wakazi wa Manispaa ya Arusha kubadilika sasa na kuelewa kuwa nchi yao inaliwa na wajanja huku hakuna hatua zozote zinazochukuliwa na wahusika.
Mbowe alisema CCM inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete inapaswa kuondolewa madarakani, imekuwa haionyeshi nia njema huku baadhi ya viongozi wamelenga kujinufaisha kwa kujiuzia nyumba za serikali kwa bei poa.
Aliwataka Watanzania bila kujali itikadi za vyama vyao kuelewa kuwa umefika wakati wa kuungana ili kutetea masilahi ya taifa na kwamba jambo hilo linawezekana na kuwa njia pekee ya kuingoa CCM madarakani.
Nawaambia bila kujali vyama vyetu vya CUF, CCM, TLP, CHADEMA na hata UDP na vingine, Watanzania wenzangu tuungane tukombowe nchi yetu inamalizwa na mafisadi ambao wamewasahau ninyi wavuja jasho, alisema Mbowe.
Mbowe alitarajiwa jana jioni kufunga kampeni za udiwani Kata ya Kati, huku CHADEMA ikichuana vikali na mgombea wa CCM, Abdul Tojo.