Polisi North Mara wananyanyasa raia


MziziMkavu

MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Messages
40,069
Points
2,000
MziziMkavu

MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined Feb 3, 2009
40,069 2,000
ILIKUWA siku ya Jumapili, Septemba 9, mwaka huu, siku ambayo Mariam Chacha Samuel Magita (50) wa Kijiji cha Magoto, akiwa na watoto wake, Ester Chacha (10), Baraka Chacha (7) na Daniel Chacha (4) walipopatwa na mkasa wa mkubwa.

Mariam ambaye ni mama ntilie katika eneo la Mrwambo, akiwa na watoto wake, akiwa anajitayarisha kwa shughuli zake za kila siku alishtukia bomu lililotupwa na askari polisi wa ABG North Mara, na kukisambaratisha kibanda chake cha biashara.

“Polisi walikuwa wamekusudia kuwalipua watu wanaoingia mgodini kusomba mchanga bila ruhusa ya wenyewe, bahati mbaya bomu hilo likaangukia kwenye kibanda changu. Baada ya hapo sijui kilichotokea , mimi nikajikuta niko kwenye zahanati ya ABG. Watoto wangu ambao pia waliiathirika na bomu hilo la moshi walikuwa wanalia kwa maumivu,” anaeleza Mariam.

“ Muuguzi wa ABG alitupa vidonge vya kupunguza maumivu na akawashauri maofisa wa polisi watupeleke kwenye hospitali ya Wilaya ya Tarime. Lakini kitu hicho hakikufanyika, ofisa mmoja wa ABG alifahamisha kwamba majeruhi hao walipewa huduma ya kwanza, lakini mtoto mdogo Ester alikuwa akitapika mfululizo”

“Waliletwa hapa na polisi baada ya kuumizwa na bomu la kutoa machozi, mama yao alikuwa kazimia, watoto wengine wawili wa kiume walikuwa wakilia kwa maumivu,”

“Nililazimishwa kwenda polisi kwa amri ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), kwenda kutoa maelezo ambayo wao walitaka, ili mimi nionekane nilipigwa bomu nikiwa ndani ya eneo la mgodi kama mvamizi na kufunguliwa mashitaka. Nilikuja kuwekewa dhamana na wifi yangu Zuhura Ally, ambaye pia ni mjane kama mimi ,” alieleza Mariam kwa huzuni.

“ Mtoto wangu Daniel Chacha alilia hadi sauti ikamkauka kutokana na maumivu na njaa. Watoto walikalishwa nje ya kituo cha polisi siku nzima hadi nilipowekewa dhamana,” anasema Mariam.

“Huku nikiwa na maumivu makali, nilielekea nyumbani na wanangu, sio tu kama mhanga wa bomu na kutoa machozi, bali pia nikiwa na kesi ya kujibu kama mhalifu,” anaeleza huku akitokwa na machozi.

Zuhura Ally (37), alithibitisha kwamba alikwenda kituo cha Polisi Nyamongo kumuwekea dhamana Mariam, baada ya kupata habari ya mkasa uliomfika.

“ Ilibidi kufanya hivyo ili wifi yangu wamwachie. Walitaka nitoe Sh 20,000, sikuwa nazo, waliambulia shilingi 2,000 huku nikitakiwa kupeleka kiasi kilichobaki siku iliyofuata. Askari huyo aliyekuwa akiandika maelezo ya Mariam alidai kwamba wifi yangu alikamatwa mgodini akiiba udongo wa dhahabu,” alisema Zuhura.

“Ninavyofahamu mimi, Mariam amekuwa akijishughulisha na uuzaji wa vyakula toka alipokuja kutoka kijijini kwao. Lakini swali ambalo kwa akili ya kawaida inakataa kwamba hakukamatwa kwenye mgodi. Je,mtu mwenye akili timamu, atakwenda yeye na watoto wake kuiba udongo kama polisi wanavyodai? anauliza.

Mwanakijiji mwingine, Kichere Nyagoto (71), anasema anamfahamu Mariam Chacha na kwamba Mariam hajawahi kuvamia eneo la mgodi hata mara moja.

“ Nimeishi hapa Nyamongo tangua 1941, mwanamke huyu hajawahi kuingia mgodini kama mvamizi kama ilivyo kwa baadhi ya vijana wa hapa Nyamongo. Polisi wanatabia ya kuwabambikiza watu kesi, lakini wahalifu wanawaacha huru. Wanamhangaisha mwanawake huyu ili kuwanyamazisha. Inasikitisha kwamba hapa Nyamongo, wanyonge hawana sauti,” anaeleza.

“Tulijaribu kupinga uonevu huu wa askari polisi, tulichoambulia ni vitisho kutoka kwa OCD. Binafsi alinionya kwamba kwa nini naingilia wakati mimi sio Mkurya,” anasema Petro Mashala (33).

Mashala anasema alijaribu kumwuliza OCD kwamba kwanini wanamshilikia mama na watoto wake ambao walikuwa wameathirika kutokana na vitendo vya polisi.

“ Wewe ni kabila gani? Kumbuka kwamba wewe si Mkurya na nashangaa wewe Msukuma unaingilia mambo yasiyokuhusu, ” Mashala anasema.

“Siku iliyofuata, nikwenda kumwona Mwenyekiti wa Kijiji cha Mrwambo, Vincent Charles, ambaye aliwapigia simu polisi. Siku iliyofuata, gari la ABG lilikuja na kunichukua, mimi na wanangu na kutupeleka Kituo cha Polisi Nyamwaga. Tulikaa kituoni hapo hadi saa tano usiku. Gari la polisi lilitubeba na kutupeleka Hospitali ya Wilaya, Tarime,” anasimulia Mariam.

“Ni kweli kwamba mama huyo na watoto wake walijeruhiwa na bomu lililotupwa na polisi wakati wakipambana na wavamizi,” alisema kiongozi huyo wa kijiji.

“Inasikitisha kwamba vyombo vya usalama hapa havitaki kuwajibika pale mambo yanapoharibika, lakini ni wepesi wa kuwatisha wananchi. Nililazimika kuingilia kati ndio wakalazimika kumpeleka hospitali, lakini sijapata taarifa yoyote toka hospitalini tangu wakati huo” anasema.

“Nakumbuka kumpokea mama huyo na watoto wake usiku wakiwa chini ya ulinzi wa polisi Septemba 11, 2012,” anasema Lucas Antony Chacha, ambaye ni Ofisa Usalama wa hospitali ya Tarime.

Jitihada za kumpata Mganga Mkuu wa Wilaya zilishindikana kwa kile kilichoelezwa kwamba yuko nje ya ofisi. Lakini Daktari Michael Seda, ambaye alikubali kuzungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu, alisema kwamba hakuwa na habari juu ya tukio hilo.

“Naona hawa watoto wako katika hali mbaya sana kutokana na kuathiriwa na gesi, mama yao atafute faili ili tuweze kuwatibia watoto hawa. Wakati faili likitafutwa, nashauri mama akaonane na Ofisa Ustawi wa Jamii, ambaye atatoa ushauri kwamba mama huyu hana uwezo wa kulipia matibabu.

Mwandishi alipokwenda kwenye ofisi za Ustawi wa Jamii, alikuta zimefungwa.

Mkuu wa Kituo cha Polisi Nyamongo pamoja na OCD, wote walikataa kuzungumza na Mwandishi.

“Suala hilo nalijua, lakini sina cha kusema. Kwakuwa limeshafika kwa Mkuu wa Wilaya, ni vizuri likaishia huko.” Anasema OCD wa Nyamongo ambaye ndiye alikuwa akiongoza kikosi kilichokuwa kinapambana na wavamizi wa mgodi.

Mkuu wa Wilaya, John Henjewele alimwelekeza Mwandishi kumuona Ofisa Utawala wa Wilaya, Ernest Kaboholo.

Hata hivyo Mwandishi alipokwenda kumuona Ofisa Tawala, hali ilibadilika na ofisa huyo kusema “Ilikuwaje ukaenda Nyamongo bila kutuarifu? Hivi unajua ni hatua gani naweza kukuchukulia hivi sasa? Huu ni upumbavu kwa kuwa najua nyie mnapenda kuandika habari za kichochezi ili kuleta vurugu hapa,” anafoka ofisa huyo.

“Ninyi ni waandishi wa namna gani? Mnawezaje kuingia wilayani kimya kimya bila kuutaarifu uongozi husika kabla hamjaanza kufanya kazi zenu,” anasema Ofisa Usalama wa Wilaya, ambaye alikataa kutaja jina lake.

OCS na OCD walikataa kwamba hati ya PF3 kwa ajili ya matibabu ya Mariam na watoto wake, iliandikwa na askari wa Kituo cha Nyamongo.

“Huyu mwanamke ni mwongo na tunaweza kumfungulia mashitaka kwa kusema uongo na kuchafua jina la Jeshi la Polisi,” alisema ofisa usalama huyo.

Wenyeji wa eneo hilo wanadai kwamba vyombo vya ulinzi na usalama katika eneo hilo, walikuwa wakilipwa na African Barrick Gold kiasi cha shilingi 25,000 kwa siku, licha ya kupewa chakula kila siku.

“Hawapo hapa kwa ajili ya usalama wetu, bali kutunyanyasa kila wakati. Ulishuhudia wakati vijana wa hapa Nyamongo walipopambana na vijana wa Nyabasi, na katika ugomvi huo kijana mmoja alikufa na polisi walikaa wakiangalia,” anasema Victor Marwa, ambaye ni mwanakijiji wa Kiwanjani.

“Naibu Waziri wa Nishati na Madini alikuwapo siku ya tukio. Polisi walikuwa wametanda kila mahali, lakini hawakusaidia kutuliza ghasia hiyo,” anasema Eliya Vincent (23) wa Kiwanjani.

Mariam Chacha na watoto wake wanatangatanga wakiomba msaada wa kujikimu na wa matibabu yake na watoto.

Hata ofisi ya Tume ya Haki za Binadamu haikuweza kumsaidia, pamoja na kwamba alikuwa na barua kutoka Ustawi wa Jamii, Tarime.

chanzo.
http://www.rai.co.tz/index.php?option=com_content&view=article&id=161:polisi-north-mara-wananyanyasa-raia-&catid=28:jamii&Itemid=39
 

Forum statistics

Threads 1,285,940
Members 494,834
Posts 30,879,791
Top