Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa amewaambia wakazi hawa wa Karagwe kwamba hata viongozi wapya wa sekretarieti ya CCM wakizunguka nchi nzima, hawana cha kuwambia wananchi kwa sababu ndio waliosababisha matatizo makubwa yanayowasumbua wananchi.
Akizungumza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kayanga, Karagwe Mkoani Kagera juzi, Dk. Slaa alisema CCM hawana majibu kwa Maswali Magumu yanayowakabili WATANZANIA.
Alisema Tanzania inahitaji Mabadiliko makubwa ya kimfumo na usimamizi makini wa raslimali zetu, na kwamba mambo haya hayawezi kufanyika chini ya utawala wa CCM.
Dk. Slaa alikuwa Mkoani Kagera kuhudhuria Mkutano wa Baraza la Mashauriano la Mkoa, ambalo pia lilialika viongozi wa mikoa yote ya Tanzania. Wakiwa Karagwe, viongozi hao walisajili wanachama wapya na kufungua Matawi katika Kila kijiji kwenye kata za Majimbo ya Karagwe na Kyerwa.