OUT sasa tegemeo kuu elimu ya juu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

OUT sasa tegemeo kuu elimu ya juu

Discussion in 'Jukwaa la Elimu (Education Forum)' started by Pdidy, Nov 9, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Nov 9, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,521
  Likes Received: 5,752
  Trophy Points: 280
  Hussein Kauli na Salim Said

  KILIPOANZISHWA Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) ilionekana kama vile kimewalenga watu wachache tena wa umri mkubwa ambao hawakupata elimu ya juu. Baada ya jamii kuona faida zake na ubora wa elimu, hivi sasa OUT ni kimbilio pia la wahitimu wa kidato na mwelekeo wa chuo ni kufikia idadi ya wanafunzi kama nchi za Ulaya, India nk.

  "Kwa mfano, Chuo Kikuu Huria cha Uingereza na cha Afrika Kusini (UNISA) vina zaidi ya wanafunzi 250,000, wakati Chuo cha India (University of the Air) kina wanafunzi 1.5 milioni," anasema Makamu Mkuu wa OUT, Prof Tolly Mbwette wakati wa mahafali ya 21 yaliyofanyika kwenye makao makuu mapya eneo la Bungo, Kibaha mkoa wa Pwani.

  Prof Mbwete alitoa takwimu hizo ili kuonyesha namna watu wengi wanavyohitimu kupitia vyuo huria na akasema asilimia 70 ya wananchi wanaozipa mafanikio nchi za Mashariki ya Mbali wanasoma katika vyuo vikuu huria hivyo amewataka Watanzania wasipuuze.

  Wito kama huo alioutoa pia Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipozungumzia mtazamo potofu juu ya elimu masafa na huria (ODL) kwamba si elimu nzuri na inafananishwa na elimu isiyo rasmi, elimu linganifu na elimu ya watu wazima.

  Lakini anasema mtazamo huo si sahihi hata kidogo kwa sababu ODL imeanzishwa kwa ajili ya kuwapatia fursa ya kusoma watu ambao wako katika familia au kazini.

  "Ndugu zangu ODL ni elimu nzuri na bora kama elimu ya kukaa darasani, tatizo hili la mtazamo potofu juu ya ODL linatokana na mtazamo wa mtu kiakili. Ikiwa tutaweza kubadili mitazamo yetu na ya watu wetu, jamii inaweza kukubali na kuthamini elimu inayotolewa na OUT," anasema Pinda ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa OUT uliofanyika Oktoba 30, mwaka huu Dar es Salaam.

  "Msikate tamaa wala kuvunjika moyo OUT ni chuo kikubwa nchini tena kizuri na kinachotoa elimu bora, jitahidini na mimi nitazidi kuwashawishi watu mbalimbali kusoma hapa."

  Ili kuhakikisha OUT inathaminiwa, Prof Mbwette anasema lengo la OUT si kutoa wahitimu tu bali wenye ubora unaofanana na vyuo vingine vya kawaida. Makamu mkuu wa taaluma, Prof Elifas Bisanda anasisitiza kwamba kwa sasa chuo hicho kipo kwenye mabadiliko ya kimapinduzi ili kuifanya elimu huria kutoa mchango mkubwa kama ilivyo katika vyuo hivyo duniani.

  Baadhi ya hatua ambazo wameanza kuzifikia ni kuongeza idadi ya wahitimu wake katika ngazi mbalimbali ambayo haikuwahi kufukiwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho miaka 15 iliyopita.

  "Kwa kuboresha zaidi elimu tunayoitoa idadi ya wahitimu 30,000 tunaweza kuifikia kwa kudahili wahitimu wengi zaidi wa kidato cha sita wa shule za kata ambao kutokana na uwezo mdogo wa vyuo vilivyopo nchini wataweza kupata nafasi hapa," anasema Prof Mbwette.

  Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa kuna ongezeko la wanafunzi katika ngazi ya sekondari kutoka 524,325 mwaka 2005 wakiwemo wasichana 244,571 hadi wanafunzi 1,222,403 mwaka 2008 wakiwemo wasichana 543,279. Wavulana mwaka 2005 walikuwa 279754 na mwaka 2008 walikuwa 679,124.

  Pia kumekuwa na ongezeko la walioingia kidato cha tano kutoka 18,893 mwaka 2005 wakiwemo wasichana 7,147 hadi wanafunzi 37,816 mwaka 2008 wakiwemo wasichana 15,867. Mwaka 2005 wavulana walikuwa 11746 na mwaka 2008 walikuwa 21,949.

  Hao ndio wanaolengwa na vyuo vyote vya elimu ya juu kikiwemo OUT. Prof Mbwete anasema uwezo wa vyuo vikuu vilivyopo nchini ni kudahili wanafunzi chini ya nusu ya wanafunzi wanaohitimu elimu ya sekondari, hivyo changamoto hiyo itatoa fursa kwao kupata wanafunzi wa kutosha.

  Prof Mbwette anasema watu wengi wamekuwa wakidhani kuwa chuo hicho hudahili tu wanafunzi ambao ni watu wazima walioajiriwa katika taasisi za kiserikali na binafsi. Lakini chuo hicho pia hupata wanafnzi wanaohitimu kidato cha sita wanahitimu kwa muda mfupi na kupata kiwango bora cha elimu sawa na vyuo vingine.

  Mabadiliko

  Marekebisho mengine yaliyopitishwa hadi sasa ni wa mitihani kwamba chu kimefuta utaratibu wa zamani wa kufanya mitihani miwili ya majaribio na kazi mbili za mazoezi na mitihani wa mwisho mmoja.

  Badala yake kutakuwa na mtihani mmoja wa majaribio na mtihani mmoja wa mwisho ili kutoa muda mwingi kwa wanafunzi kumakinika na maudhui ya masomo yao badala ya kutumia muda mwingi kufanya kazi na majaribio hayo.

  "Ili kupata wanafunzi weledi wa masomo wanayojifunza kuanzia mwaka huu kutakuwa na mfumo mpya wa kwa kutumia 'student progress portfolio' katika kutathmini uwezo wa mwanafunzi," anasema Prof. Mbwette.

  Anaongeza kuwa, kwa kutumia utaratibu huo, kabla ya mtihani wa mwisho mwanafunzi atatakiwa kujibu maswali ya ana kwa ana ambayo majibu yake yataingizwa katika tiketi ya kuingilia kwenye chumba cha kufanyia mitihani huo.

  Ujenzi

  Mafanikio mengine ambayo OUT inajivunia kwa sasa ni uzinduzi wa ujenzi wa makao makuu ya kudumu ya chuo hicho, Bungo Kibaha. Makao hayo yanayotarajiwa kukamiliaka mwaka 2014, yametangewa eneo la uwekezaji wa kampuni itakayoingia ubia wa muda mrefu na OUT kuchapisha vitabu.

  Lengo la ubia huo ni kupunguza gharama za uchapishaji na kutoa vitabu kwa wanafunzi wa chuo hicho na vyuo vingine vinavyotumia vitabu hivyo katika masomo yao.

  Bisanda anasema "ukweli ni kwamba chuo kina kazi kubwa ya kufanya ili kiwe ni chuo kikuu huria kweli, kwa sababu baadhi ya taratibu zake zimefungwa"

  Anasema udhaifu wa mfumo wa tathmini, ambao ulikuwa kikwazo katika miaka ya nyuma, unapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili kuboresha ubora wa elimu inayotolewa.

  Anafafanua kuwa mfumo huo ulitumika kutathmini masomo ya shahada ya kwanza katika mazoezi na mitihani ya majaribio, lakini baadhi ya wanafunzi waliitumia kufanya udanyanyifu.

  Kwa upande wa mikoani OUT ina sera ya kununua majengo ili kuhakikisha inapata majengo ya kudumu ya chuo hicho katika mikio yote nchini.

  "Sera hii tuliianzisha baada ya juhudi zetu za kupata majengo kupitia wizara ya miundombinu kushindwa, hivyo kwa sasa tumefanikiwa kupata majengo hayo katika baadhi ya mikoa,"anasema.

  Kilio kikubwa kwa OUT ni pesa. "Ukosefu mkubwa wa fedha unaokikabili chuo unatokana na kutoza ada ndogo ukilinganisha na gharama za uendeshaji wa chuo, tunahitaji msaada mkubwa wa serikali katika hili” anasema Mbwette.

  Anaongeza kuwa, kasumba za viongozi wa kisiasa kuwa elimu huria ni rahisi na hafifu, kwa sababu tu wao walisoma katika vyuo vya kawaida.

  “Viongozi hawa huiweka elimu yetu katika daraja la pili ikitanguliwa na elimu ya vyuo vikuu vya kawaida, lakini katika vyuo vyao wanafunzi wengi wanafeli ukilinganisha na OUT”, ansema Mbwette.

  Prof Mbwette anaomba ushirikiano na vyuo vingine ambavyo muundo wake hautaweza kuwafikia walengwa wote wa elimu ya juu ili kuviwezesha kudahili wanafunzi wengi.

  "Tuko tayari kushirikiana na vyuo hivyo kwa kutumia miundombinu na walimu wetu kutoa elimu kwa wanafunzi wao kwa kutumia mitaala yao" anasema Mbwette na kuongeza: "Katika kuhakikisha nchi yetu inawawezesha wanafunzi wengi kupata elimu ya chuo kikuu ushindani wetu na vyuo vikuu vya kawaida hauna nafasi, waje tushirikiane kulijenga taifa letu," anasema.
   
Loading...