Ileje
JF-Expert Member
- Dec 20, 2011
- 9,335
- 13,293
ARODIA PETER NA MAULI MUYENJWA
-DAR ES SALAAM
ALIYEKUWA Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, ameufananisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuwa ni kama ‘ndoa ya jinsia moja’, kwa kuwa pande zote mbili zina haki sawa, hata kama ukweli utapindishwa.
Akitoa mada ya maslahi ya Zanzibar katika Katiba mpya wakati wa Mkutano Mkuu wa Kikatiba Dar es Salaam jana, Othman alisema kukwama kupatikana kwa Katiba mpya Tanzania ni hofu ya kuvunjika kwa Muungano, baada ya walio wengi kupendekeza mfumo wa Serikali tatu.
Pia aliponda hisia hizo kwa kusema zinajengwa kinadharia ili kuwatia hofu wananchi.
Othman, aliyejiuzulu wadhifa huo wakati wa Bunge Maalumu la Katiba la mwaka 2014, alisema ndoa za jinsia moja ni falsafa tu, lakini haziwezi kubadili ukweli wa maumbile halisi ya wahusika.
“Ukweli ndoa ya jinsia moja ni kwa falsafa tu, haibadilishi ukweli kuwa yule mwanamume anayejifanya mwanamke atabaki kuwa mwanamume, hata yule mwanamke atabakia mwanamke tu na ipo siku mmoja akiudhiwa anaweza kumwambia mwenzake hata mimi mwanamke, mwanamume kama wewe usinifuatilie,” alisema Othuman.
Katika mada yake hiyo, Othman alizungumzia kwa undani historia ya kero za Muungano tangu utawala wa marehemu Aboud Jumbe na alisema kilio chake juu ya kero hizo kiligharimu wadhifa wake.
Pia alisema ingawa mambo ya Muungano kwa idadi ni 22 kama yalivyoainishwa na Katiba ya mwaka 1977, lakini ukweli ni kwamba mambo ya Muungano hayajulikani ni mangapi.
“Dalili ya kwanza inayoonesha kwamba baadhi ya mambo yanafanywa kuwa ya Muungano lakini si kweli, ikiwamo masuala ya bima yanayosimamiwa na Kamishna wa Bima.
“Lakini pia Bunge limekuwa likitunga sheria na kuzifanya za Muungano, hata kwa mambo ambayo hayamo katika orodha ya Muungano, kwa mfano sheria ya proceeds Crimes Act ya 1991,” alisema.
Pia alisema Serikali tatu hazina tatizo lolote na hofu inayojengwa si halisi, bali ni ya kupandikizwa kwa sababu si kweli kwamba Serikali tatu zitavunja Muungano.
Othman alisisitiza kuwa, Muungano uliopo wa Serikali mbili ni kama mmoja ameamua kukubaliana na hali hiyo ili mambo yaende, lakini ukweli hata Zanzibar yenyewe ilihitaji kuwa na mamlaka yake huru.
Wakati huo huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. James Jesse, alisema ili mchakato wa Katiba mpya uweze kuendelea, ni lazima iundwe sheria ya amri ya rais na kupelekwa bungeni kuruhusu mchakato huo.
Alisema vifungu vipya vya sheria vinatakiwa kutengenezwa ambavyo vitatoa mwongozo mpya wa nini cha kufanya, kwa kuwa vile vya awali vimepitwa na wakati na haviwezi kutekelezeka.
Source:Mtanzania