Wasanii wa Opera ya Wu, wakiwa wamevalia mavazi ya kuvutia na ya rangi angavu, walihuisha mila za kale za opera ya China mjini Harare, nchini Zimbabwe. Waliwavutia watazamaji kwa ishara, sauti za kuvutia, na kungfu.
Onyesho hilo lilihusisha kazi maridadi za asili za Opera ya Wu, zikiwemo "Mungu wa Kike wa Mbinguni Anatawanya Maua", "Safari ya kwenye Kiti cha Kubebwa" pamoja na "Mapigano Matatu dhidi ya Pepo wa Mifupa" na hadithi maarufu kutoka katika kazi ya fasihi ya kale ya China, "Safari ya Kuelekea Magharibi"
Opera ya Wu, ambayo pia inajulikana kama Opera ya Jinhua yenye asili yake katika Mkoa wa Zhejiang mashariki mwa China, ni sanaa ya maonyesho ya jadi inayounganisha uimbaji, sarakasi, na miondoko maalum ili kusimulia hadithi zisizopitwa na wakati, zenye mizizi katika historia na hadithi za China.
Mbali na mavazi yake ya kuvutia na mpangilio mgumu wa miondoko, sanaa hii inachunguza mada za kibinadamu za ulimwenguni kote kama vile mapenzi, ujasiri, haki, na kujitolea, ikiwapa watazamaji wa eneo hilo fursa ya kipekee ya kuona utajiri wa utamaduni wa China.
Onyesho hilo la "Opera ya Wu barani Afrika," lililoandaliwa na Kituo cha Utafiti wa Opera ya Wu cha Zhejiang, liliwezeshwa na Ubalozi wa China nchini Zimbabwe, Idara ya Utamaduni, Redio, Televisheni na Utalii ya Mkoa wa Zhejiang, pamoja na serikali ya manispaa ya Jinhua.
Maonyesho haya ni sehemu ya matukio mfululizo ya kitamaduni yanayofanyika kote Zimbabwe mwaka huu, kwa ajili ya kusherehekea "Mwaka wa China na Afrika wa Mawasiliano baina ya Watu," mpango unaolenga kuimarisha uhusiano wa kitamaduni na kukuza uelewa wa pamoja kati ya pande zote mbili.
Tang Xiaoping, Afisa Mshauri na Kaimu Mkuu wa Ubalozi wa China nchini Zimbabwe, alielezea onyesho hilo kama tukio muhimu katika mawasiliano kati ya nchi hizo mbili.
"Kupitia mawasiliano ya karibu zaidi ya kitamaduni na kati ya watu, tunaweza kuzidi kuelewana, na kuongeza nguvu mpya katika amani na maendeleo ya dunia," alisema Tang.
Tsitsi Gezi, Naibu Spika wa Bunge la Zimbabwe, aliunga mkono kauli ya Tang, akisema onyesho la sanaa linaweza kuelezea mambo ambayo wakati mwingine maneno hayawezi, na hivyo kuruhusu uhusiano wa kina zaidi kati ya watu.
Gong Jianjun, mkurugenzi wa Kituo cha Usimamizi katika Ukumbi wa Opera ya Wu nchini China, alisema anajivunia kuutangaza urithi wa utamaduni wa China kwa watazamaji wa Zimbabwe. Kupitia daraja la Opera ya Wu, anatumai kuacha sanaa yao bora zaidi nchini Zimbabwe na kuwezesha watazamaji kuhisi mvuto wa kina wa utamaduni wa jadi wa China.
Kwa Inaty Sibanda, ambaye alishuhudia opera ya Kichina kwa mara ya kwanza, mavazi ya kuvutia na miondoko ya waigizaji iliyobeba hisia nzito ilifanya hadithi iliyokuwa ikiwasilishwa jukwaani kuwa hai na yenye kugusa hisia.
Sibanda aliongeza kuwa kushuhudia opera hiyo kulitoa fursa ya kipekee ya kujifunza kuhusu urithi wa China, huku akitamani matukio kama haya ya kitamaduni yaweze kufanyika mara kwa mara ili kuongeza uelewa kwa jamii ya hapa.
Mtazamaji mwingine, Vheneka Roy, alisema alivutiwa na utajiri wa urithi wa utamaduni wa China pamoja na ustadi wa wasanii hao na namna walivyojitolea. Alisema onyesho hilo lilimfanya kuthamini zaidi namna watu wa Zimbabwe na China wanavyoweza kujieleza kwa njia zinazofanana.
Kwa Roy, uzoefu huo wa kuzama kikamilifu katika sanaa hiyo ulionyesha uwezo mkubwa wa diplomasia ya kitamaduni katika kuimarisha uhusiano wa kweli kati ya watu wa China na Zimbabwe.
"Katika kitu nilichojifunza leo, ni kujivunia asili yetu huku tukiwathamini wengine kwa asili yao pia," alisema Roy. "Tunaweza kuthaminiana katika nyanja zote bila kuhisi kuwa mmoja ni bora kuliko mwingine."