OFFICIAL: CHADEMA yawavua uanachama Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba...

CHADEMA

JF-Expert Member
Apr 13, 2013
488
2,468
Ndugu Wanachama wote pamoja na Watanzania wote kwa ujumla tupo hapa live kuwaletea mkutano na Waandishi wa habari ambao utaanza hivi pindi kuwajilisha maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama iliyokutana tarehe 03-04/01/2014 katika Ukumbi wa Mbezi Garden jijini Dar es Salaam. Karibu sana.

Tunaendelea kuwasubiri Viongozi watoke ofisini kwa Katibu Mkuu kuja mbele ya Waandishi wa Habari. Waandishi ni wengi sana hapa Makao Makuu wakitaka kujua nini kitazungumzwa mahali hapa. Tuendelee kuvuta subira muda si mrefu mkutano huu na Waandishi wa Habari utaanza rasmi

Tunaomba mtuwie radhi ndugu nyote mnaotufuatilia bado viongozi wakuu wanaendelea na kikao katika ofisi ya Katibu Mkuu na tunatarajia muda si mrefu kuanzia hivi sasa watatoka kuja kuzungumza na Watanzania kupitia kwa Waandishi wa Habari waliopo hapa Makao Makuu. Waandishi wanazidi kumiminika na ulinzi umeimarishwa kwelikweli. Tafadhali endelea kutufuatilia

Bado tunaendelea kuwasubiri Viongozi ndugu wananchi. Naona watu waliofika hapa wakiwa wamekaa vikundi vikundi wakibadilishana mawazo na kuwa mijadala midogo midogo ya hapa na pale. Nawaona pia Maofisifa kadhaa wa Chama nao wakiwa wanabadilishana mawazo na kuendelea kuvuta subira kuwasubiri Viongozi wetu waje wazungumze na Waandishi wa Habari.

DSC_2136.JPG

M/Kiti wa Chama Taifa ndio ameingia maeneo haya ya Ofisini akitokea Viwanja vya Karimjee muda wowote kuanzia hivi sasa Mkutano huu na Waandishi wa Habari utaanza rasmi ndugu Wananchi.

Ikumbukwe kuwa M/Kiti wa Chama Taifa ndie ambae amekuwa akizungumza na Waandishi wa Habari mara zote juu ya Maazimio ya Kamati Kuu baada ya Vikao hivyo. M/Kiti Taifa ndie Msemaji Mkuu wa Chama.

M/Kiti Taifa ameingia ofisini kwa Katibu Mkuu na muda wowote kuanzia hivi sasa M/Kiti atakuja kuzungumza na Waandishi wa Habari akiambatana na Ujumbe wa Wakurugenzi na Maofisa wa Chama.

Viongozi Wakuu akiwemo Katibu Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Chama, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Wajumbe wa Kamati Kuu na Viongozi wameshawasili hapa na sasa Mh. John Mnyika ndio anawakaribisha Waandishi wa Habari na Kutoa salamu za utangulizi

Mnyika anaanza kwa kuomba radhi kwa press kuchelewa anasema ni kwasababu ya uzito wa hoja zenyewe kwasababu Kamati Kuu iliiagiza Sekretarieti kuandaa tamko la leo. Pia Mnyika amewatambulisha Viongozi wa Kanda waliopo mahali. M/Kiti hayupo hapa mbele na badala yake Katibu Mkuu Dr. Wilbrod Slaa ndie anazungumza na Waandishi wa Habari na tayari ameshaanza kuzungumza

Katibu Mkuu nae anaanza kwa kuomba radhi kwa kuchelewa kuanza press akiungana na John Mnyika pia Katibu Mkuu anasema kuwa atasoma neno kwa neno kutokana na umuhimu wa hoja yenyewe! Ameanza kusoma na kusema kamati kuu ilikuwa ni ya dharura iliyokuwa na lengo la kuwajadili Wanachama watatu Dr. Kitila Mkumbo, Zitto Kabwe na Samsoni Mwigamba.

Dr Slaa anaonyesha kabrasha lenye nyaraka mbalimbali ikiwemo mkakati wa mabadiliko 2013, mashtka ya watuhumiwa na nyaraka nyingine muhimu. Sasa Dr. Slaa anasoma mashtaka yote 11 ya Watuhumiwa kama walivyokabidhiwa kwa maandishi

Katibu Mkuu anasema Watuhumiwa wawili yaani Dr. Kitila Mkumbo na Samsoni Mwigamba waliitikia wito wa Kamati Kuu lakini aliyehojiwa na Kamati Kuu ni Dr. Kitila Mkumbo pekee ambaye katika utetezi wao walikana kuvunja katiba ya Chama na Kanuni zake.

Katibu Mkuu anasema Dr Kitila Mkumbo alikiri kumfahamu M2 na anamjua fika lakini hawezi kumtaja mpaka awasiliane nae kwanza. Pia Dr Kitila Mkumbo alisema yeye na Mwandishi wa waraka ule walimpa briefing Mh. Zitto Kabwe kwa hiyo alikuwa anaufahamu waraka huo.

Dr. Kitila Mkumbo alikataa kuzungumzia vifungu vya katiba walivyodai vimevunjwa kwa madai kuwa tayari wana malalamiko kwa msajili tayari. Aidha Dr. Kitila Mkumbo alishindwa kuithibitishia Kamati Kuu kwa ushahidi kuhusu madai ya taarifa ya fedha ambazo yeye na Zitto walishiriki, pia alishindwa kuonyesha ushiriki wa M/Kiti katika manunuzi ya vifaa mbalimbali vya Chama zikiwemo pikipiki za Chama.

Hivyo Kamati Kuu imeamua kuwavua Uanachama ndugu Samsoni Mwigamba na Dr. Kitila Mkumbo kuanzia tarehe ya jana baada ya maamuzi ya kikao cha Kamati Kuu. Maamuzi hayo ni baada ya kunasa mawasiliano mbalimbali ya Zitto Kabwe na washirika wake akiwemo anayejulikana kwa jina la Chadema Mpya.

Dr. Slaa anasema malengo ya waraka wa mabadiliko hayakuwa ya kisiasa tu bali yalikuwa na lengo la kuimaliza chadema na kuwabomoa Viongozi wa Chama.

Mwisho

Chama kinawatangazia Wanachama wote na wapenzi wote kutokushiriki mikutano ama shughuli zozote za kisiasa zitakazoandaliwa na Zitto Kabwe na Washirika wake kwa jina la Chama.

Kuhusu madai ya Mwigamba juu ya kipengele cha Katiba Dr Slaa anaonyesha baraua ya tarehe 13 July 2006 iliyosainiwa na Ndugu Shaibu Akwilombe aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wakati huo kwenda kwa Viongozi wa Mikoa nchi nzima ambayo ilionyesha mabadiliko ya kipengele hicho pamoja na kipengele kilichomruhusu M/Kiti kuteua Manaibu Katibu Wakuu na Katibu Mkuu ambacho kwa makusudi hawakilalamikii kwasababu kilimnufaisha Zitto Kabwe.

Dr. Slaa anaongeza kuwa lengo la wakina Kitila lilikuwa ni kuonyesha kuwa CHADEMA na CCM ni walewale wote ni Mafisadi ili kukiharibia Chama sifa yake mbele ya Jamii.

Dr. Slaa anasema Kamati Kuu imechukua maamuzi haya kwa uchungu kwasababu CHADEMA haina lengo la kupunguza wanachama bali kuongeza Wanachama hata wanaCCM katika kuharikisha ukombozi wa Taifa letu.

Dr. Slaa anamkaribisha Mh. Tundu Lissu ili kuongezea taarifa. Lissu anasema kuwa mkakati wa kuwachafua viongozi ni wa siku nyingi ambapo Chama kimefanikiwa kunasa mawasiliano ya Zitto tangu mwaka 2009 alipokuwa akiwasiliana akina Denis Msack wa Mwananchi. Lissu anasema njama hizi ndio zilizopelekea mpaka mashtaka ya ugaidi ambapo katika mahojiano yake ya Star Tv akiwa na akina Mwigulu Nchemba zitto hakukanusha, pia aliandika kwenye mitandao kuwa Chadema imtose Wilfred Lwakatare.

Lissu anaongeza kuwa Zitto mpaka sasa ana magari mawili ya Nimrod Mkono na Mkono mwenyewe ndie amewaambia taarifa hizo. Mkono amewaambia kuwa amempa Zitto hela nyingi sana na Zitto alishiriki moja kwa moja kumzuia mgombea wa Chadema katika Jimbo la Nimrod Mkono wakati Nimrod Mkono alikuwa ni namba sita katika orodha ya Mafisadi iliyotajwa pale Mwembeyanga.

Lissu anasisitiza kuwa washirika wa usaliti huu na uhaini huu hawakupenda kutangazwa kuwa wao ni Wasaliti na wahaini lakini yeye anasema wale ni Wahaini na Wasaliti. Lissu anasema kuwa Zitto anaendelea kuwa Mwanachama na Mbunge wa CHADEMA kwasababu ya Mahakama tu na sio kwasababu ya mapenzi ya CHADEMA.

Dr. Slaa anasoma mawasiliano kati ya Zitto na Mtu anayejiita Chadema Mpya. ambapo anasisitiza kuwa Mkakati ulianza kutekelezwa mapema kwa hiyo hoja kuwa Zitto alikuwa hajui Mkakati ni ya Uongo.

Mnyika anamalizia kwa kusema kuwa tuko katika vita dhidi ya maadui wa Chama walioko nje na ndani ya Chama. Hivyo falsafa yetu ya Nguvu ya Umma ndio itakayotusaidia kwa hiyo anatoa wito kwa Wanachama nchi nzima kuitumia falsafa hiyo katika hatua zote ili kushinda vita hii.

Pia anawaomba Wanachama wote kujitokeza kwa wingi mahakamani siku ya kesho katika kusikiliza maamuzi ya Mahakama. Press imeisha Asantheni kwa Kutufuatilia.

FULL TEXT....


MAAZIMIO YA KIKAO CHA DHARURA CHA KAMATI KUU YA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) KUHUSU HATUA ZA KINIDHAMU DHIDI YA WANACHAMA ZITTO ZUBERI KABWE, DR. KITILA MKUMBO NA SAMSON MWIGAMBA

UTANGULIZI


Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ilikaa kikao cha dharura ili kupokea, kujadili na kuamua juu ya utetezi wa mashtaka ya ukiukaji wa Katiba, Kanuni na Mwongozo wa Chama yaliyokuwa yanawakabili aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zitto Zuberi Kabwe, aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu Dr. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba. Kikao hicho cha dharura kilifanyika Dar es Salaam kati ya tarehe 3-4 Januari, 2014.

Kabla ya kuanza kwa kikao, Kamati Kuu ilipokea taarifa kwamba Zitto Zuberi Kabwe amefungua mashtaka dhidi ya CHADEMA katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam. Aidha, Kamati Kuu ilijulishwa kwamba Mahakama Kuu imetoa amri ya zuio la muda ya kuizuia Kamati Kuu au chombo kingine cha Chama kutokukaa, kujadili na kuamua suala la uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe. Kutokana na amri hiyo ya Mahakama Kuu, Kamati Kuu haikujadili na kuamua juu ya mashtaka dhidi yake.


MASHTAKA

Watuhumiwa wote watatu walishtakiwa jumla ya mashtaka 11 yanayohusu ukiukaji wa vifungu mbali mbali vya Katiba ya Chama, Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama, Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na Maadili ya Wabunge wa Chama na Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali. Mashtaka yote yalitokana na watuhumiwa kuandaa kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko, 2013 kama ifuatavyo:

1. Kukashifu Viongozi Wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa Mh. Freeman A. Mbowe, na Katibu Mkuu Dr. Wilbrod P. Slaa;

2. Kutokuwa wakweli na wawazi kwa kushirikiana na vikundi vya majungu kwa kuanzisha na kuratibu mtandao wa siri ulioitwa ‘Mtandao wa Ushindi' nje ya utaratibu wa Chama ili kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa;

3. Kutoa tuhuma za uongo dhidi ya viongozi wa Chama na bila kupitia vikao halali vya Chama;


4. Kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini na ukanda vyenye makusudi ya kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa jamii;


5. Kujihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa Chama na wanachama wake;


6. Kuandaa na kutekeleza mpango wa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa bila kutangaza kusudio la kufanya hivyo kwa mujibu wa Mwongozo wa Chama;


7. Kutengeneza makundi na mitandao haramu ya kuwania uongozi ndani ya Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;


8. Kuwachafua viongozi na wanachama wenye nia au kusudio la kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;


9. Kujihusisha na upinzani dhidi ya Chama na makundi ya majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa uchaguzi wa Chama;


10. Kukashifu Chama na viongozi wa Chama nje ya Bunge kinyume cha Kanuni za Maadili ya Wabunge; na


11. Kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama kinyume cha Kanuni za Maadili ya Wabunge.

UTETEZI WA WATUHUMIWA

Watuhumiwa wote walijitetea kwa maandishi. Zaidi ya utetezi huo wa maandishi, Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba waliitikia wito wa Kamati Kuu wa kujitetea kwa mdomo mbele yake. Hata hivyo, siku ya utetezi wao, ni Dr. Kitila Mkumbo peke yake aliyejitokeza kwenye Kamati Kuu na kujitetea kwa mdomo. Katika utetezi wake wa maandishi, licha ya kukiri kushiriki katika maandalizi ya kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013, Dr. Kitila Mkumbo – kama ilivyokuwa kwa Samson Mwigamba – alikanusha na kukataa tuhuma zote za kukiuka Katiba ya Chama, Kanuni zake na Mwongozo wa Chama. Kwa maneno yake mwenyewe, Dr. Mkumbo alikanusha "kila tuhuma mojamoja na kwa ujumla wake dhidi ya[ke]", na kwamba mashtaka hayo sio ya kweli na hakuvunja Katiba, Kanuni wala Mwongozo wa Chama.

Aidha, licha ya kukiri kwake katika kikao cha Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana kwamba walioshiriki kuandaa Mkakati huo ni pamoja na mtu anayejulikana kama M2, mara hii Dr. Kitila Mkumbo aliiambia Kamati Kuu kwamba "waraka husika ulikuwa ni wa siri na haukuwahi kusambazwa wala kushirikisha … wanachama au viongozi wa CHADEMA isipokuwa mimi binafsi na Samson Mwigamba…." Vile vile, ijapokuwa katika Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana Dr. Mkumbo alidai kutokumfahamu kabisa M2, mara hii aliiambia Kamati Kuu kwamba anamfahamu fika M2 lakini hayuko tayari kumtaja mbele ya Kamati Kuu hadi atakapowasiliana naye!

USHIRIKI WA ZITTO ZUBERI KABWE KATIKA MKAKATI WA MABADILIKO

Itakumbukwa kwamba katika kikao cha Novemba 2013, Dr. Kitila Mkumbo na Zitto Zuberi Kabwe walikataa kata kata kuhusika kwa Zitto Zuberi Kabwe katika maandalizi ya Mkakati wa Mabadiliko. Aidha, Zitto Zuberi Kabwe alidai mbele ya Kamati Kuu kwamba alikuwa ameusikia Mkakati huo kwa mara ya kwanza kwenye Kamati Kuu, na amerudia kauli hiyo mara nyingi na hadharani tangu avuliwe nafasi zake za uongozi.

Hata hivyo, wakati wa mahojiano na wajumbe wa Kamati Kuu, Dr. Kitila Mkumbo alikiri kwamba yeye na waandishi wenzake wa Mkakati walimpa Zitto Zuberi Kabwe briefing juu ya Mkakati na kwamba alikuwa anaufahamu. Ukweli huu pia umethibitishwa na mawasiliano ya baruapepe iliyotumwa na Zitto Zuberi Kabwe mwenyewe kwa mtu anayeitwa ‘CHADEMA Mpya 2014' tarehe 27 Oktoba, 2013, karibu mwezi mmoja kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya Novemba iliyowavua madaraka.

Zaidi ya hayo, baada ya kuonyeshwa waraka wa Chama juu ya mabadiliko ya Katiba ya Chama uliotumwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama wakati huo Shaibu Akwilombe Julai 2006 unaothibitisha kwamba mabadiliko ya Katiba yaliyoondoa ukomo wa uongozi yalifanywa kwa uwazi na kwa kushirikisha ngazi zote za Chama, Dr. Kitila Mkumbo alikataa kata kata kujadili suala hilo kwa madai kwamba tayari walishapeleka malalamiko yao kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Kuhusu tuhuma zao kwamba kuna ufisadi na ubadhirifu wa fedha za Chama unaofanywa na Mwenyekiti wa Chama, Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Fedha Anthony Komu na kwamba taarifa za matumizi ya fedha ni siri ya viongozi hao watatu, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa mbali mbali za fedha zilizowasilishwa mbele ya vikao vya Kamati Kuu a Chama ambavyo yeye mwenyewe na Zitto Zuberi Kabwe walishiriki kama wajumbe wa Kamati Kuu. Aidha, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa za kibenki zinazoonyesha jinsi michango ya Mzee Jaffer Sabodo na michango mingine ya watu binafsi zilivyopokelewa na kutumiwa na taarifa zake kuwasilishwa kwenye vikao vya Kamati Kuu walivyohudhuria yeye na Zitto Zuberi Kabwe.

Zaidi ya hayo, Dr. Mkumbo alionyeshwa nyaraka za manunuzi ya vifaa vya Chama kama vile vile pikipiki, kadi, bendera, n.k, na jinsi ambavyo uamuzi wa manunuzi hayo yalifanywa na Kamati Kuu ambayo wao wenyewe ni wajumbe na walihudhuria vikao husika. Vile vile, Dr. Mkumbo alionyeshwa ushahidi wa maandishi kwamba Mwenyekiti wa Chama hakuhusika kwa namna yoyote ile katika manunuzi hayo na hakuna karatasi yoyote inayoonyesha saini ya Mwenyekiti katika manunuzi ya vifaa hivyo. Aidha, Dr. Mkumbo hakuweza kuthibitisha kwa namna yoyote kwamba CHADEMA ina mkataba wowote na watu binafsi wanaouza vifaa vya uenezi vya Chama kwa vile Kamati Kuu ya Chama katika vikao ambavyo vilihudhuriwa na Dr. Mkumbo na Zitto Zuberi Kabwe ilikwisharuhusu wafanya biashara binafsi kuagiza vifaa hivyo na kuviuza kwa wanachama wanaotaka kuvinunua. Kwenye yote haya, Dr. Kitila Mkumbo hakuwa na lolote la maana la kuiambia Kamati Kuu.

MAAMUZI YA KAMATI KUU

Baada ya kusikiliza utetezi wa Dr. Kitila Mkumbo na baada ya kumhoji kwa kirefu, Kamati Kuu imeridhika bila mashaka yoyote kwamba Mkakati wa Mabadiliko 2013 haukuwa na lengo la kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama peke yake. Mkakati huo ulikuwa na malengo makubwa zaidi ya kukibomoa Chama kwa kukichafua kwa wananchi na kuwachafua viongozi wake wa juu kwa kutumia tuhuma za uongo za ufisadi. Hii ni kwa sababu, kwa maoni ya Kamati Kuu, Chama cha siasa ambacho viongozi wake wa juu wanatuhumiwa kwa ufisadi hakiwezi kuaminiwa na wananchi kama tumaini lao la ukombozi.

Kamati Kuu imeridhika kwa ushahidi wa nyaraka mbali mbali zilizoandaliwa na Zitto Zuberi Kabwe mwenyewe ama na mawakala wake wakitumia vitambulisho bandia katika mitandao ya mawasiliano ya kijamii kwamba mkakati wa kukibomoa Chama umeandaliwa na kutekelezwa kwa muda mrefu. Mkakati huo ulihusisha pia hujuma dhidi ya Chama kwa kuwaengua wagombea wake katika chaguzi mbali mbali kama ilivyotokea katika majimbo ya Mpanda Mashariki, Musoma Vijijini na Singida Mjini ambapo Zitto Zuberi Kabwe alishiriki moja kwa moja.


Kwa sababu zote hizo, Kamati Kuu imeazimia ifuatavyo:


1. Kwamba kuanzia tarehe ya uamuzi wake, Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba wafukuzwe uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA); na

2. Kwamba, kwa vile Zitto Zuberi Kabwe amekishtaki Chama kinyume na matakwa ya Katiba ya Chama na Kanuni zake, na kwa vile Mahakama Kuu imeamuru vikao vyote vya Chama visijadili wala kuamua suala lolote linalohusu uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe, viongozi wa ngazi zote za Chama, wanachama, washabiki na wapenzi wa CHADEMA popote walipo katika nchi yetu na nje ya Tanzania wasishiriki wala kusaidia kwa namna yoyote mikutano yoyote ya nje au ya ndani au shughuli nyingine yoyote ya kisiasa itakayofanywa na Zitto Zuberi Kabwe na mawakala wake kwa jina la CHADEMA.

--------------------------------
Dr. Wilbrod P. Slaa
KATIBU MKUU
 
Ndugu Wanachama wote pamoja na Watanzania wote kwa ujumla tupo hapa live kuwaletea mkutano na Waandishi wa habari ambao utaanza hivi pindi kuwajilisha maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama iliyokutana tarehe 03-04/01/2014 katika Ukumbi wa Mbezi Garden jijini Dar es Salaam. Karibu sana.

Sisi tunataka kuona tu magamba yanaondolewa,,,, zzk na wenzake ili tusonge mbele kwa nguvu zaidi.
 
Tunaomba sana kurugenzi ya habari kuwa fasta ktk kutujuza sie tulio nje ya mkutano huo. Tu update kile kinachoendelea kila angalau baada ya dakika 5.
Ahsante.
 
Tunasubiri kwa hamu. Ila Kama hamkuzungumzia Hali ya sasa ya sasa ya wananchi hasa kuhusu pandisho la umeme ili kulipa gharama Za Richmond na ma tatizo mengine lukuki yaongezekayo kila uchwao mtapoteza uhalali wa kututetea sisi wananchi wanyonge.
 
Dr kitila mkumbo amevuliwa uanachama kwa kusimamia kauli yake ya kusema kweli daima
 
Back
Top Bottom