Ocean Road: Wagonjwa wengi wanaacha tiba na kukimbia kwa waganga na kwenye ibada

Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), imesema maboresho makubwa yanayoendelea katika huduma zake, yanakwazwa na tatizo kubwa la wagonjwa kukatisha tiba na kuhamia mbadala wa waganga wa kienyeji na nyumba za ibada.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dk. Julius Mwaiselage, amelalamika kuwa mwenendo huo unaowahusisha wastani wa wagonjwa 500 hadi 600 kutoka idadi ya wagonjwa 7,000 wanaofika kupata huduma za saratani kwa mwaka.

Ametaja sababu kuu ni kurubuniwa na matangazo mbalimbali yasiyo rasmi kuhusu dawa na maudhui yaliyomo katika mitandao ya kijamii.

Dk. Mwaiselage alitoa ufafanuzi huo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kuihamasisha jamii uelewa kuhusu saratani na hususan ya matiti, akisema ukiuaji huo ni mwenendo potofu.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, inakadiriwa kuwa asilimia 10 ya wagonjwa wa saratani, ndiyo wanaokatisha matibabu na kukimbilia tiba za asili na huduma za maombezi.

“Hatujafanya utafiti isipokuwa wanaondoka kwa njia zisizo rasmi kwenda kwenye tiba za asili na maombi ni kama asilimia 10 ya wagonjwa wote.

“Imani potofu zilizozagaa mitandaoni na ndani ya jamii ambako watu wanadanganyana kuwa wanaweza kupona saratani kwa njia ya maombi au dawa za kienyeji, zinawafanya wagonjwa kushindwa kuendelea na matibabu," alisema.

Dk. Mwaiselage aliendelea kusema kuwa tatizo hilo ni kubwa kwa sababu wagonjwa hawaagi kuwa wanaenda kupatiwa matibabu kwa njia mbadala isipokuwa wanaondoka kimyakimya.

"Anakuwa ametibiwa 'stage' (hatua) ya kwanza na ya pili anaacha na kwenda kwenye maombi na kwa waganga wa kienyeji kwa miezi mitatu, anapakwa dawa sijui ni chokaa, akirudi tena hospitali yupo katika hatua mbaya ya ugonjwa kusambaa zaidi na inakuwa ngumu kumtibu na kupona," alisema.

Alisema hospitali hufanya juhudi za kuwafuatilia kwa kuwapigia simu ili kuulizia sababu za kutoendelea na matibabu na hivyo kueleza sababu hizo na wakati mwingine wanapata taarifa kuwa mgonjwa husika ameshapoteza maisha.
“Kwa sababu wanaandika namba zao za simu, tukikaa miezi sita hatujamwona mgonjwa akirudi kuendelea na matibabu, tunalazimika kumpigia simu ili kujua sababu.

"Iwe ni sehemu za maombi au za tiba mbadala, waendelee nazo lakini hao wanaowapa huduma, wasiwazuie wakaacha dawa zetu na kuja kliniki kufanyiwa uchunguzi wa afya zao," alionya.
Mkurugenzi huo pia aliwataka wagonjwa kuzingatia kanuni na ushauri wa madaktari wakati wa matibabu ili kuondokana na madhara yatokanayo na kutozingatia maelekezo wakati wa matibabu.

Dk. Mwaisalege pia alisema taasisi hiyo ya saratani imeongeza idadi ya wagonjwa inaowatibu baada ya kupata mashine za kisasa na dawa mahususi, akibainisha mabadiliko ya kitakwimu kwamba kabla ya mwaka 2015 walikuwa jumla ya wagonjwa 30,000 wanaowatibu kwa mwaka, lakini maboresho yamewafikisha 55,000.

Alisema juhudi hizo za serikali na hospitali zinafifishwa na wagonjwa hao wanaorubuniwa na mitandao ya kijamii na jamii inayowashauri kwenda kwenye nyumba za ibada kufanyiwa maombi au kwa waganga wa kienyeji kupewa dawa za asili.

Akizungumzia elimu ya kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa uchunguzi wa mapema wa saratani ya matiti iliyohusisha wanawake waliopona ugonjwa huo wanaofahamika kama mashujaa, Dk. Mwaiselage aliwataka wanawake nchini kujitokeza kupatiwa matibabu kwa sababu ugonjwa huo unatibika.

Alisema nchini wagonjwa wapya wa saratani 42,000 hupatikana kila mwaka na kati yao asilimia 12 ni wagonjwa wa saratani ya matiti.

Oktoba ya kila mwaka ni mwezi maalum uliochaguliwa kueneza elimu na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa uchunguzi wa mapema na njia bora za kuzuia maradhi ya saratani ya matiti.
Kuna jamaa yangu alikufa hapo ocean road hosp. Tatizo kubwa rushwa huduma mbovu na ilivyo ukipelekwa hapo unaenda kufa so acha watu watafute tiba mbadala, aache uzuzu wa kudharau alternative, mbona corona tumepona?
 
Back
Top Bottom